Sunday, August 15, 2010

Swaumu na Siha


Kwanza nawatakiwa wadau Waislamu wa Kona ya Afya swaumu njema na kw amanasaba wa mwezi mtukufu wa Ramadhani nimeandika makala hii kuhusiana na umuhimu wa kufunga. natumaini mtafaidika nayo.
Kufunga kumeamriswa katika dini mbalimbali ikiwepo dini tukufu ya Uislamu, Uyahudi na Ukiristo. Mbali na dini mbalimbali kuamuru wafuasi wao wafunge kama moja ya ibada muhimu, wataalamu wengi wa masuala ya tiba wamekuwa wakiamini kuwa kufunga ni miongoni mwa tiba asilia na inaleta faida kubwa kiafya. Kufunga kuna faida tele kwa afya na kwa siha ya mwili. Uislamu unawataka wafuasi wake wawe wenye afya njema, wasafi, walio imara kiimani na kimwili na mwenye nguvu. Bwana Mtume Mtukufu Muhammad (S.A.W) ametilia nguvu hoja hiyo pale aliposema kwamba: "Fungeni mpate siha".
Hii leo pia wataalamu wa masuala ya afya wamethibitisha faida kemkem mtu anazoweza kuzipata mtu kwa kufunga, zinazouinufaisha mwili na akili. Kuna baadhi ya madaktari wanasema kuwa kufunga kunamfaidisha mtu kisaikolojia na kimwili. Mbali na swaumu kumfanya anayefunga awe na stamina ya njaa na aweze kuvumulia matatizo na awe na subra, pia husaidia kupunguza mafuta ya zaida mwilini. Faida za kufunga haziishiii hapo bali pia swaumu ni njia ya kuponya magonjwa mbalimbali yakiwemo yale yanayohusiana na mfumo wa chakula kama vile maumivu ya tumbo sugu, kuvimba utumbo mkubwa, ugonjwa wa ini, kukosa choo na matatizo mengineyo kama vile unene wa kupindulia, kuziba mishipa ya moyo (arteriosclerosis), shinikizo la damu, asthma, diphtheria na kadhalika.
Lakini kabla hajujaendelea na mada yetu hii hebu sasa tueelezee kwa undani kitaalamu jinsi kitendo cha kufunga kinavyoufaidisha mwili.
Kufunga kitaalamu huanza pale mwili unapokosa chakula kwa masaa 12 hadi 24. Kikemia kufunga hakuanzi hadi pale sukari aina ya carbohydrate iliyohifadhiwa mwilini inapoanza kutumiwa kama chanzo cha kuzalisha nguvu. Kufunga huko huendelea madam tu mafuta na carbohydrate iliyohifadhiwa iendelee kunyofolewa na badilishwa kuwa nguvu, bila kutumiwa protini iliyohifadhiwa. Pale protini inapoanza kutumiwa na kubadilishwa kuwa nguvu (suala ambalo hupelekea misuli kupungua) kitaalamu tunasema kuwa mtu ameanza kukabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula mwilini au kwa kimbombo starving.
Faida za kufunga zinaweza kufahamika kwa kujua jinsi mwili unavyofanya kazi wakati chakula kinapokosekana.
 Wakati mwili unapoishiwa na nguvu inayotokana na chakula, huanza kutegemea hazina yake ya chakula kilichohifadhi na kitendo hicho huitwa Autolysis. Autolysis ni kuvunja vunja mafuta yaliyohifadhiwa mwilini ili kutengeneza nguvu, kitendo ambacho hufanywa na ini. Hali hiyo hupunguza mafuta ya ziada mwilini ambayo ndio sababu kuu ya magonjwa mengi kama vile shinikizo la damu, mshituko wa moyo na kadhalika.
 Kufunga pia husaidi kuondoa sumu mwilini. Suala hilo hurahisishwa na kufunga kwani chakula kisipoingia mwilini, mwili hubadilisha mafuta yaliyohifadhiwa kuwa nishati na kupitia kitendo hicho kemikali nyinginezo na sumu zenye madhara kwa mwili pia hutoka katika utumbo, ini, figo, mapafu na ngozi. Hizi ni sumu ambazo hutokana na vyakula tunavyokula na mazingira yetu, na huingia mwilini na kuhifadhiwa pamoja na mafuta.
 Faida nyingine ya swaumu kitiba ni kuupumzisha mfumo wa chakula. Wakati mtu anapokuwa hali, nguvu inayotumiwa na mfumo wa chakula ambao huwa umepumzika huelekezwa kwenye metabolism na mfumo wa kulinda mwili. Kitendo hicho husaidia mfumo wa kulinda mwili uweze kufanya kazi zake vyema zaidi na kupambana na mgonjwa au vile visivyotakiwa mwilini. Pengine hii ndio babu wanyama wanapopata jeraha huacha kula, na wanadamu hupoteza hamu ya kula wanapopatwa na magonjwa kama vile mafua. Kwa sababu mwili huielekeza nguvu yake yote kwenye mfumo wa ulinzi wa mwili ili kupambana na vijidudu. Faida hiyo mtu huipata pia anapofunga.
 Wakati wa kufunga vilevile joto la mwili hupungua kwa kiasi kikubwa. Hii hutokana na kupungua kasi ya metabolism na kusimama kazi nyingi zinazofanywa na mwili. Kwa kupungua kiwango cha sukari au glukosi katika damu, mwili hutumia glukosi inayohifadhiwa kwenye ini. BMR (basal metabolis rate) hupungua ili kuhifadhi nishati mwilini. Pia homoni mbalimbali huzalishwa wakati mtu anapokuwa amefunga zikiwemo homoni za kukua na za kuzuia seli zisizeeke. Hivyo njia mojawapo ya kuzuia uzee na kuwa na maisha marefu ni kufunga.
Kwa kuzingatia maelezo hayo yote tunaweza kusema kuwa, swaumu ina faida kubwa kiafya kwa mwanadamu.

Thursday, August 12, 2010

Ni vipi ubebe mimba ya mtoto wa kike?Napenda kuchukua nafasi hii kujibu swali la pili la mdau mmojawapo wa Kona ya Afya ambaye ameuliza kuwa, ni vipi anaweza kubeba mimba ya mtoto wa kike. Katika kujibu swali hilo naweza kusema kwamba, ndugu mdau ulimwengu hivi sasa umeendelea sana kiasi kwamba matatizo mengi katika jamii yanatatuliwa kwa msaada wa wataalamu mbalimbali. Mojawapo ni suala la mtu kuzaa mtoto wa kike au wa kiume. Ingawa njia hizo nitakazoziandika hapa pengine hazina uhakika mia kwa mia, lakini wapo watu wengi wamejaribu na zimewasaidia. Hivyo nina matumaini kwa kufuata maelekezo haya ukaweza kupanga na kuzaa mtoto wa kike kama unavyokusudia. Ninachotaka kusisitiza hapa ni kuwa, maendeleo ya elimu hasa katika uwanja wa sayansi na tiba yamekuwa na taathira nyingi katika kupunguza matatizo ya familia kama vile ugumba, kuzaa mtoto wa jinsia inayotakiwa na wazazi, magonjwa ya wanawake, vifo vya wajawazito na kadhalika. Ni ukweli usiopingika kwamba ingawa watu wengi wanazingatia kuzaa mtoto aliye mzima wa mwili na afya bila kujali jinsia ya mtoto huyo, lakini uchunguzi unaonyesha kwamba kuna baadhi ya watu au wazazi wanaopenda kuwa na watoto wa jinsia fulani zaidi. Vilevile imeonekana kuwa wanawake hupendelea kuwa na watoto wa kike huku wanaume wakipenda kuwa na watoto wa kiume. Hata hivyo wazazi ambao tayari wana watoto wa jinsia ya kike au ya kiume hupendelea kuwa na mtoto wa njinsia nyingineyo ili kuwa na watoto wa kiume na wa kike.

Je, ni vipi jinsia ya mtoto huainishwa?
Kinyume na wengi wanavyofikiria kwamba mwanamke au mwili wa mwanamke ndio mwenye jukumu la kuainisha jinsia ya mtoto kwa kuwa yeye ndiye anayebeba mimba, uhakika wa mambo ni kuwa mwanamume ndie mwenye uwezo wa kuainisha jinsia. Kila yai la mwanamke lina chromozu mbili za X. Iwapo manii ya mwanamume au spemu (ambayo in chromozomu X na Y) itakuwa na X na kurutubisha yai la mwanamke lenye X tupu, basi mtoto atakayezaliwa atakuwa mwanamke. Vilevile iwapo spemu ya mwanamume itakuwa na Y na kurutubisha yai la mwanamke, basi mtoto atakayezaliwa atakuwa mwanamume. Hivyo kwa kufahamu suala hilo, ni matumaini yetu kuwa vile visa vya kinamama kuachwa eti kwa kuwa hawakuzaa watoto wa kiume au wa kike vitapungua katika jamii zetu. Mke wako asipozaa mtoto wa jinsia uitakayo, usifikiri kuwa yeye ndio mwenye makosa.
Wakati mwanamume anapomwaga shahawa, spemu kati ya milioni 200 hadi 400 humwagwa katika uke wa mwanamke. Baadhi ya spemu hizo huwa zina chromozomu X na baadhi zina chromozomu Y. Hata hivyo, ni spemu moja tu ambayo hutakiwa kwa ajili ya kurutubisha yai la mwanamke na kuunda mimba. Nadharia mbalimbali zinazotolewa kwa ajili ya kusaidia kuchagua ni jinsia gani unaitaka awe nayo mwanao, zinategemea suala la kuandaa mazingira katika uke na mwili wa mwanamume na mwanamke, yatakayosaidia spemu ya baba yenye chromozomu inayotakiwa irutubishe yai la mama, na hivyo kutungwa mimba ya jinsia inayotakiwa.
Njia ya Dr. Shettles ya kuzaa mtoto wa kike
Njia hii imekuwa ikitumiwa na watu wengi kwa miaka mingi sana na imewasaidia kuweza kuzaa mtoto wa kike. Wengi wanasema kuwa uwezekano wa kufanikiwa njia hii ni asilimia 90. Njia ya Dr. Shettles inategemea msingi kwamba, chromozomu Y (yenye kuwezesha kutungwa mimba ya mtoto wa kiume) ni ndogo na yenye kwenda kwa kasi zaidi ikilinganishwa na chromozomu X (yenye kuwezesha kutungwa mimba ya mtoto wa kike) ambayo ni kubwa na huenda polepole. Pia kwa kutegemea kuwa chromozomu X inaishi muda mrefu zaidi kuliko ile ya Y. Hivyo Dr. Shettles anashauri kuwa iwapo unataka kuzaa mtoto wa kike uhakikishe kuwa:
• Unajamiiana siku 2 au 3 kabla ya Ovulation. Kinadharia spemu za kiume zitakuwa zimeshakufa hadi kufikia siku hasa ya Ovulation na kuziacha spemu za kike zikiwa hai tayari kurutubisha yai na kuunda mtoto wa kike.
• Anashauri pia wanawake wajizuie kufikia kileleni (orgasm) kwani hali hiyo itaufanya uke uwe na hali ya asidi ambayo ni kwa faida ya spemu ya kike yenye chromozomu X.
• Pia anawashauri wazazi wanapojamiina wawe katika hali ya mwanamke kulala chini na mwanamume juu au missionary position. Kwani anasema kuwa mtindo huo huziwezesha spemu zenye chromozamu X zimwagike karibu na mlango wa uke na kuwa na uwezekano mkubwa wa kuingia ukeni na kutungwa mimba.
Njia ya O+12
Njia hii inayomaanisha Ovulation jumlisha siku 12 ilivumbuliwa na mama mmoja wa Australia aliyekuwa akihangaika kupata mtoto wa kike baada ya kuzaa watoto 6 wa kiume. Mama huyo anawahusia wale wanaotaka kubeba mimba ya mtoto wa kike wajamiiane masaa 12 baada ya Ovulation. Mama huyo alifuata njia ya Dr. Shettles bila mafanikio katika mimba zake za nyuma. Lakini baada ya kugundua njia yake hii mwenyewe mwishowe alibeba mimba na kujifungua mtoto wa kike.Kuna wengine wanaamini kwamba baadhi ya lishe na vyakula vya aina mbalimbali husaidia kutunga mimba ya mtoto wa kike. Kwa mfano kuna wanaoamini kuwa kula baadhi ya vyakula huufanya uke uwe na hali ya asidi ambayo husaidia Chromozomu Y ife katika uke. Nadharia nyingineyo inayotumiwa katika kuchagua jinsia ya mtoto inasema kwamba, mwanamke anayetaka kubeba mimba ya mtoto wa kike ale vidonge vya virutubisho (supplements) vya Calcium na Magnessium mwezi mmoja kabla ya kubebea mimba. Iwapo unataka kutumia vidonge vya virutubisho ili uweze beba mimba ya mtoto wa kike, ni bora ushauriane na daktari wako kwanza. Hii ni kwa sababu dawa hizo huweza kuingiliana na dawa nyinginezo za magonjwa mbalimbali.
Baadhi ya vyakula vinavyotajwa kuwa vinasaidia katika kutunga mimba ya mtoto wa kike ni.
• Mahindi, nyama, maharagwe, samaki, tunda damu, mayai na maini.

Vyakula hivyo ni vya asidi hivyo huifanya PH ya mwili wako hupungua na kuwa ya acidi. Hali hiyo husaidia kuua spemu za Y na hivyo kusaidia kuzifanya spemu za X ziwe na uwezekano mkubwa wa kurutubisha yai. Hivyo mwanamke anayependelea kubebea mimba ya mtoto wa kike anashauriwa kutokula vyakula vyenye alikali ambavyo ni kama, ndizi, chokleti, juisi ya machungwa, viazi, tikiti maji na vinginevyo.
Pia sio mbaya kutaja baadhi ya imani na itikadi wanazoamini baadhi ya watu kuwa zinasaidia katika kupata mtoto wa kike:
• Fanya mapenzi wakati wa mchana.
• Fanya mapenzi siku shufwa (even days) za mwezi.
• Fanya mapenzi wakati mwezi umekamilika ( full moon days).
• Kula samaki na mboga mboga kwa wingi, na baadaye kufuatiwa na kitinda mlo cha chokleti.
• M-surprise mwenzi wako, kuna wahenga wanaamini wanawake wanaoanzisha wao kufanya mapenzi huzaa watoto wa kike!]
Hivyo kila la kheri wadau, unaweza kuchagua moja ya njia kati ya zilizotajwa hapo juu na kwa kufuata maelekezo ukajaaliwa kuzaa mtoto wa kike.

Wednesday, August 11, 2010

Ni alama gani za mwili wako zitakufahamisha Ovulation imewadia?Wadau wa Kona ya Afya, niliahidi kuendeleza mada yetu ya namna ya kuzijua siku za kushika mimba kwa kuzungumzia baadhi ya alama za mwili zinazosaidia kutambua ni wakati gani Ovulation imewadia. Alama hizo za Ovulation si ngumu kuzitambua, iwapo utafahamu unatafuta alama gani. Kuna baadhi ya alama za mwili zinazokutahadharisha kwamba Ovulation iko njiani, hivyo kuweza kukusaidia kupanga vyema muda wa kujamiiana kwa ajili ya kupata mamba. Alama nyinginezo zinakufahamisha kwamba Ovulation imewadia au imeshapita. Ingawa alama hizo ziko nyingi na nitazungumzia baadhi ya hizo, lakini usifikiri kwamba unatakiwa utumie zote, kwani kufanya hivyo kunaweza kukuchanganya.
Iwapo hutoona alama zozote za Ovulation au iwapo siku zako za mwezi hazina mpangilio maalum, ni bora umuone daktari ambaye atakusaidia zaidi.
Mabadiliko ya joto lako la Mwili
Tunaweza kusema kuwa Joto lako la mwili au (Body Basal Temperature) ndio alama maarufu inayotumiwa na wanawake wengi ili kufahamisha kwamba Ovulation imewadia pale wanapotaka kubeba mimba. Hii ni kwa sababu joto lako la mwili huongezeka kwa kiasi kidogo na huendelea kuongezeka baada ya Ovulation. Ongezeko hilo la joto husababishwa na homoni ya progesterone, ambayo huongezeka sana punde baada ya Ovulation. Kwa kujipima joto lako la mwili na kuandika chati ya mabadiliko hayo unaweza kufahamu ongezeko hilo la joto lako la mwili. Unahitajia kipimamoto kwa ajili ya kufanikisha suala hilo. Zipo pimajoto maalum kwa ajili hiyo lakini unaweza kutumia pimajoto ya kawaida pia. Hakikisha unapima joto la mwili wako asubuhi baada ya kuamka na uhakikishe huna homa, hukukosa usingizi, hukunywa pombe, si mgonjwa wala huna wasiwasi na fikra nyingi. Ni bora ufanye hivyo kwa mizunguko kadhaa ya siku zako ili uweze kuijua vyema chati ya mabadiliko ya joto la mwili kwa mujibu wa mzunguko wako wa mwezi.Ingawa njia hii haianishi moja kwa moja kuwa Ovulation imewadia, lakini joto la mwili huongezeka kidogo kabla yakipindi hicho na huongezeka kwa kwa degree 0.4 hadi 0.6 baada tu ya kumalizika Ovulation. Kuongezeka joto kwa kiasi kikubwa baada ya Ovulation huendelea hadi siku utakayopata siku zako ambapo hupungua na mzunguko wako wa mwezi huanza tena. Iwapo utakuwa umepata mimba joto lako la mwili litaendelea hivyo hivyo kuwa juu. Kwa kuwa mabadiliko ya joto hutokea wakati wa Ovulation iwapo unajaribu kubeba mimba, kufuatilia mabadiliko hayo kwa muda usiopungua miezi miwili ni jambo la dharura ili uweze kujua wakati wa Ovulation ambapo una uwezekano mkubwa wa kubeba mimba.
Mabadiliko ya majimaji ya ukeni
Wakati Ovulation inakaribia majimaji ya ukeni hubadilika pia kwa kiasi na hali. Ikiwa hakuna Ovulation majimaji ya ukeni huwa yanayonata au kama kremu au hukosekana kabisa. Wakati Ovulation inakaribia majimaji ya ukeni huongezeka na huwa katika hali ya majimaji na wakati mwingine huwa rangi nyeupe kama ya yai bichi. Iwapo utapima kwa vidole vyako huvutika kwa inchi au zaidi kati ya vidole vyako.
Ni bora nikumbushe hapa kwamba, kuan wakati unaweza kuwa na majimaji ya ukeni yanayofanana na ya wakati wa Ovulation hali ya kuwa huko katika Ovulation. Hali hiyo ni ya kawaida kwa watu wenye PCOS. Kutumia dawa za Clomid au Antihistamin huweza kufanya majimaji ya ukeni yakauke na hivyo kuwa vigumu kutumia njia hii ili kujua ni zipi siku zennye uwezekano mkubwa wa mimba. Njia hii huhesabiwa kuwa yenye itibari zaidi.
Ongezeko la Matamanio
Inaonekana kuwa maumbile nayo hutusaidia kujua ni siku gani tunaweza kubeba mimba! Wataalamu wameonyesha (jambo ambalo pengine wengi wameshalihisi) kwamba wanawake wanapokuwa katika siku zenye uwezekano mkubwa wa kupata mimba, matamanio yao ya huongezeka. Hizo ni siku chache kabla ya kujiri Ovulation, ambapo ndio wakati unaofaa wa kujamiiana iwapo unataka kubeba mimba.
Hata hivyo njia hii si ya kutumainiwa sana kwani baadhi ya hali kama vile msongamano wa mawazo, fikra nyingi na wasiwasi huweza kupunguzaa matamanio. Au mtu anaweza akahisi matamanio katika muda wote wa mzunguko wa mwezi.
Mabadiliko ya Ukeni:
Kama ambavyo majimaji ya ukeni yanavyobadilika wakati wa Ovulation, uke nao (cervix) hubadilika wakati wa kukaribia Ovulation. Wakati huo uke husogea mbele, huwa laini na hufunguka zaidi.
Maumivu kidogo katika Matiti:
Baadhi ya wanawake wakati wanapokaribia Ovulation au baada ya hapo matiti yao huwa na maumivu kidogo. Suala hili huhusiana na mabadiliko ya homini mwili ambazo hujitayarisha kwa ajili ya mimba. Hata hivyo njia hii sio yenye kutegemewa sana kwani maumivu ya matiti huweza kusababishwa na masuala mengine. Pia maumivu ya matiti hutokea kabla ya hedhi au baada ya kutumia baadhi ya dawa za kusaidia uzazi.
Alama nyinginezo
Baadhi ya wanawake huhisi maumivu kidogo ya tumbo ambayo baadhi huyaita Middle Pain. Maumivu hayo kwa kawaida hutokea upande ule yai linapotoka yaani upande wa Ovulation. Maumivu hayo hutokana na mwendo wa yai wakati linapopenya kwenye mirija. Maumivu hayo si ya kuendelea na wala si makubwa na huisha haraka. Hali hiyo huweza kutokea mara kadhaa katika siku za Ovulation. Kuna baadhi ya alama kama vile baadhi ya wanawake huhisi kichefuchefu, gesi, kukojoa mara kwa mara na maumivu wakati wa kujamiina, hali ambayo haitokei kwa watu wengi. Pia kuna baadhi ya vifaa vinavyopaatikana katika madula ya dawa katika baadhi ya nchi ambavyo huweza kukusaidia kujua wakati wako wa Ovuation umewajia, vifaa hivyo hujulikana kama 'Ovulation Kit"
La muhimu ni kufahamu kuwa wanawake hutofautiana katika kupata alama hizi, kwani kuna baadhi wanaweza wakapata baadhi ya alama hizi na wengineo wakapata nyinginezo. Kuuelewa vyema mwili wako ni jambo zuri linaloweza kukusaidia kuzijua siku zako la Ovulation na hivyo kuweza kujua siku zako za kubeba mimba.

Saturday, August 7, 2010

Je, Poda zina madhara kwa watoto?


Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu, Kona ya Afya imeamua kuanza tena kutoa makala kwa ari mpya, ambapo kwanza tunaanzia kwa kuwajibu maswali wadau ambayo yaliulizwa huko nyuma. Hivyo napenda kuwaeleza wale waliouliza maswali yao kuwa, wasifikiri nimeyatupa kapuni bali nitayajibu moja baada ya jingine Mungu akijaalia.
Tukirudi katika swali la mdau aliyeuliza je Poda zina madhara kwa watoto, kwanza tujue poda ni nini?
Poda ya watoto ni unga unga unaotumika ili kuzuia vipele vya nepi kwa watoto na wakati mwingine hutumika kwa ajili ya kuondosha harufu kama deodorant na kwa matumizi mengine ya vipodozi. Poda inaweza kuwa imechanganywa na 'talc' ambapo poda ya aina hiyo huita talcum powder, na wakati mwingine huchanganywa na unga wa wanga. Poda ya Talcum ni hatari iwapo itamezwa na mtoto kwa sababu inaweza kusababisha pneumonia au ugonjwa wa granuloma. Hakuna maelekezo ya moja kwa moja ya madaktari au taasisi zinazohusika kwa mfano WHO kuhusiana na madhara ya poda kwa watoto au kupiga marufuku matumizi ya poda kwa watoto. Lakini kuhusiana na aina ya poda za Talcum baadhi wanasema kwamba, talc ni mada inayoweza kusababisha kensa na magonjwa mbalimbalia kama vile cysts. Pia wanasema kwamba poda aina ya talc ni hatari kwa mtoto iwapo ataimeza au itamwingia mtoto mdomoni. Lakini pia wako wengine wanaosema kuwa hata poda ya wanga nayo ikitumiwa kwa ajili ya kupunguza vipele vya nepi huweza kuzidisha maambukizo ya 'yeast' au fungus. Vilevile kuna wengine wanaosema kwamba kwa kuwa mwili wa mtoto bado ni mchanga na dhaifu, kujiepusha kutumia katika ngozi ya mtoto vitu vinginevyo kama poda au hata mafuta huweza kusababisha mtoto apate allergy hasa iwapo vifaa kama hivyo vitakuwa vimepitwa na wakati au havikuhifadhiwa katika hali nzuri. Lakini la muhimu kabisa ambalo madakatari, wauguzi na wakunga huwahusia wazazi hasa baada ya kuzaliwa mtoto ni kujihadhari iwapo wanatumia poda wahakikishe kuwa poda haingii kwenye kitovu cha mtoto kabla hakijaanguka.
Hivyo ndugu mdau uliyeuliza swali hili, sina jibu la moja kwa moja kwamba poda ina madhara au la, ispokuwa nakuachia mwenyewe baada ya kusoma makala hii uamue utumie poda kwa ajili ya mtoto wako au usitumie.
• Lakini iwapo utataka kutumia poda basi naweza kukushauri tu ni bora unaponunua poda basi na uangalie vyema kabla ya kununua na kuhakikisha kwamba si ya talcum. Na kama utatumia ya wanga basi iwapo mtoto atapata fungus kwa wakati huo usiendelee kutumia poda hadi atakapopona. Kwani kuendelea kutumia poda kunafanya fungus zizidi.
• Pia hakikisga poda haiingia katika kitovu cha mtoto hasa wakati kibichi na kabla yakijaanguka.
• Hakikisha mtoto hamezi poda au poda haimuuingia mdomoni, puani au masikioni.
• Hakikisha unanua aina za poda zinazojulikana vyema kutoka katika mashirika yenye itibari.
• Hakikisha hata kama unanua poda yenye jina linalojulikana lakini usinunue sehemu mbazo poda humwaga chini au huhifadhiwa katika sehemu zisizofaa ambapo huweza kusababisha hali ya awali ya poda ibadilike.
• Zingatia muda wa kuisha matumizi ya poda unayoitumia, expire date.

Thursday, August 5, 2010

Zijue siku zako za kushika MimbaNimeamua kuandika makala hii ili kujibu swali la moja wa mdau wa blogi hii ambaye ameuliza kwamba, anahitaji kushika mimba na je, kwa mfano mwezi huu alianza period yake tarehe 17 Juni, ni zipi siku zake za kushika mimba? Ndugu mdau kwanza kabisa nachukua nafasi hii kukuomba samahani kwa kuchelewa kujibu swali lako. Pengine ninapoandika makala hii utakuwa tayari umeshashika mimba, basi kama ni hivyo hakuna tabu bali natumaini swali lako litakuwa limewasaidia wengine ambao pengine wana tatizo kama halo. Pia umeualiza je, ukitaka mtoto wa kike ufanyeje?
Nachukua nafasi hii kwanza kujibu swali lako la kwanza kabla sijaenda kwenye swali lako la pili. Kwani kuelewa vyema swali la kwanza kutasaidia kuelewa swali la pili pia.
Inafaa tufahamu kuwa ili kuweza kujua ni siku zipi za mwezi mwanamke anaweza kushika mimba (to conceive) inabidi tujua kwanza kipindi ambacho mwili wa mwanamke uko tayari kushika mimba au Ovulation Period. Ovulation ni wakati ambao yai lililokua hutoka katika mirija ya ovari katika kizazi cha mwanamke na katika wakati huu uwezo wako wa kushika mimba ni mkubwa. Kwa kawaida mwanadamu huwa na mayai kadhaa katika ovari zake kwa wakati maalum wa mwenzi, ambapo yai kubwa kuliko yote huondoka na kueleka katika tumbo la uzazi kupitia mirija ya ovari. Ovulation haifuati mpangilio maalum kati ya ovari katika kila mwezi na haijulikani ni ovari gani itatoa yai kila mwezi. Wakati yai linapotoka huwa na uwezo wa kurutubishwa au kukutana na mbegu ya kiume na kuanza kutengeneza mtoto kwa muda wa masaa 12 hadi 24, kabla halijapoteza uwezo wake. Iwapo yai litafanikiwa kurutubishwa na mbegu ya kiume kwa wakati maalum na kujikita katika fuko la uzazi basi matokeo yake ni mimba. Na iwapo halitorutubisha yai hilo pamoja na kuta za kizazi huharibika na kutoka nje ya mwili kama damu ya hedhi.
Nimetangulia kueleza haya kama utangulizi kabla ya kuzieleza siku za kushika mimba kwani kuelewa suala hilo kutatusaida kujua umuhimu wa kujua idadi ya siku zetu za mzunguko wa mwezi (Menstrual Cycle) na umuhimu wake katika kushika mimba na hata katika magonjwa ya wanawake. Ili kuelewa vyema siku hizo inatubidi tujue kitu kinachoitwa Kalenda ya Ovulation au kalenda ya kubeba mimba na pia tujua mzunguko wetu wa hedhi una siku ngapi. Mzunguko wa mwezi ni siku ya kwanza unayopata damu yako ya hedhi hadi siku kabla ya kupata tena hedhi nyingine.Wataalamu wanatuambia kuwa ili kujua mzunguko huo vyema inatubidi tuchunguze hedhi yetu kwa miezi isiyopungua 6. Lakini kama una haraka na huwezi kuchunguza kwa miezi 6 chunguza kwa miezi mitatu. Unaweza kufanya hivyo kwa kutumia kalenda ya kawaida na kwa kuziwekea mduara kwa kalamu siku zako za mwezi, yaani siku ya kwanza ya kupata damu ya hedhi hadi siku ya mwisho kabla ya hedhi inayofuata. Mzunguko wako wa mwezi ni siku ya kwanza ya hedhi hadi siku ya kabla ya kuanza hedhi nyingine. Kwa mfano iwapo nimepata siku zangu tarehe Pili Julai na nimepata tena siku zangu tarehe 29 Julai, mzunguko wangu ni wa siku 28. Kwa kawaida mzunguko wa siku 28 ndio mzunguko wa kawaida kwa wanawake wengi. Lakini kuna baadhi ya wanawake huwa na mzunguko wa chini ya siku 28 na wengine huwa na mzunguko wa hadi siku 35.
Ni vipi utazijua siku zako za Ovulation
Wakati wa Ovulation katika mzunguko wa mwezi huainishwa na luteal phase, katika mzunguko wako. Unaweza kujua muda wa Ovulation katika mzunguko wako wa mwezi kwa kutoa idadi ya siku za luteal phase. Katika kuhesabu huko utapata mzunguko mfupi na mrefu. Chukua mzunguko mfupi wa mwezi na hesabu idadi ya siku katika mzunguko huo. Toa 18 katika mzunguko huo na utapata idadi fulani. Halafu anza kuhesabu siku yako ya kwanza ya mzunguko wa hedhi katika mwezi unaofuata kwenda mbele hadi kufikia namba ulioyopata, hivyo utaweza kupata siku ambayo una uwezekano mkubwa wa kubebea mimba.
Kwa mfano mzunguko wako mfupi ni siku 29, unatoa 18 katika 29 na unapata 11. Iwapo siku yako ya kuanza hedhi mwezi ujao ni Oktoba 3, ongeza siku 11 kuanzia siku hiyo. Hivyo siku ambayo una uwezekano mkubwa wa kubeba mimba itakuwa Oct. 14.
Halafu chungua idadi ya siku za mzunguko wako mrefu wa hedhi. Toa siku 11 kutoka katika idadi ya siku za mzunguko huo na utapata namba fulani. Halafu tena anza kuhesabu katika mzunguko wako ujao wa hedhi kwenda mbele hadi kufikia siku ambayo una uwezekano wa kupata mimba.
Kwa mfano iwapo mzunguko wako mrefu ni siku 31, toa 11 katika mzunguko huo na utapata 20. Iwapo hedhi yako ijayo inaanza tarehe 3 Oktoba, ongeza siku 20 kuanzia siku hiyo na tarehe 23 Oktoba itakuwa siku yako ambayo una uwezekano mkubwa wa kubeba mimba.
Kwa utaratibu huo utakuwa umepata kipindi cha kati ya Oktoba 14 hadi 23 ambacho ni siku ambazo una uwezekano mkubwa wa kubeba mimba au Ovulation window kwa kimombo.
Ovation huweza kubadilika kidogo katika mzunguko wako wa hedhi kwa sababu Ovulation huweza kucheleweshwa na sababu mbalimbali kama vile wasiwasi au fikra nyingi, ugonjwa, lishe au kufanya mazoezi.


Vipi kipindi cha Ovulation kinaainisha ziku za kubeba mimba?
Kipindi cha kubeba mimba huanza siku 4 hadi 5 kabla ya Ovulation, na humalizika masaa 24 hadi 48 baada ya hapo hii ni kwa sababu muda wa ovulation huweza kuchelewa au kuwahi kutokana na sababu mbalimbali. Pia kwa sababu mbegu ya kiume huwa na uhai kwa siku 4 hadi 5 na yai huweza kuishi kwa masaa 24 hadi 48 baada ya kuingia katika tumbo la uzazi. Hivyo kwa kujua siku hizo humsaidia mwanamke kufahamu kipindi chake cha Ovulation kimewadia na hivyo kuweza kukukutana na mumewe au mwenza wake wakati huo ili aweze kubeba mimba. Pia kujua kipindi hiki na masuala mengineyo kama hali ya joto la mwili ilivyo wakati wa Ovulation huweza kutumika kama njia ya kuzuia mimba. Yaani kutojamiiana katika kipindi hiki huweza kumzuia mtu asipate mimba.
Kwa kuwa kipindi cha Ovulation hakina tarehe maalum na ni siku kadhaa, katika makala ijayo nitaendelea kuzungumzia baadhi ya alama za mwili zinazosaidia kutambua ni wakati gani Ovulation imewadia.
Daima tuzilinde afya zetu!

Monday, August 2, 2010

Nimerudi blogini Wadau na samahani sana kwa kupotea!


Wapenzi wadau wangu wa Kona ya Afya,
Napenda kuchukua nafasi hii kuwajulisha kwamba nimerudi blogini. Pia kuwaomba samahani kwa kusokena kw amuda mrefu kutokana na majukumu, kazi na safari za hapa na pale. Nawaahidi kwamba nitajitahidi kujibu maswali yenu mliyoniuliza na kuirejesha tena blogi yetu katika hali yake ya kawaida.
Nawatakieni Afya Njema!
Shally!