Wednesday, September 29, 2010

Samahanini Wadau

Tafadhalini sana wadau naomba kama mtu ana swali la haraka anitumie kupitia email yangu ambayo ni sthugs4j@yahoo.com . Hii ni kutokana na baadhi ya wadau kuuliza maswali yao yanayohitaji ufafanuzi wa haraka katika comments za makala zilizopita, sasa kuna baadhi ya wakati hata sipati muda wa kucheck comments za makala zilizopita, na hivyo kushidwa kujibu katika wakati unaotakiwa.
Samahani sana....Shally.

Saturday, September 18, 2010

Huraa! Maambukizo mapya ya Ukimwi yapungua Afrika!


Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba nchi zilizoko chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika zinaongoza kwa kupungua maambukizo mapya ya virusi vya Ukimwi. Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulia masuala ya Ukimwi (UNAids) kimesema kuwa nchi 22 ambazo ziko katika eneo hilo la chini ya Jangwa la Sahara lenye maambukizo makubwa zaidi ya Ukimwi duniani zimeshuhudia kupungua maambukizo ya ugonjwa huo kwa asilimia 25!. Kupungua maambukizo hayo kumetokana na watu kuelewe vizuri na kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo pamoja na kutumiwa vyema njia za kujikinga. Hata hivyo Umoja wa Mataifa umesema kwamba maambukizo mapya ya Ukimwi yameongezeka huko mashariki mwa Ulaya, katikati mwa bara Asia, na miongoni mwa wanaume mashoga katika nchi zilizoendelea. Mkurugenzi Mtendaji wa UNAids Michel Sibide amesema kwamba, dunia inapiga hatua kubwa katika kufikia utekelezwaji wa Malengo ya Sita ya Maendeleo ya Milenia (MDG6) ya kupambana na kupunguza maambukizo ya HIV/Aids hadi kufikia mwaka 2015. Shirika hilo aidha limesema kuwa, kuwa watu milioni 5.2 wanapatiwa matibabu ya Ukimwi duniani kote, suala ambalo limesaidia kuhakikisha kwamba watu wachache zaidi wanakufa kutokana na virusi vya ugonjwa huo hatari ikilinganishwa na huko nyuma.
Haya shime jamani tuendeleze kwa nguvu zote mapambano dhidi ya Ukimwi!

Monday, September 13, 2010

Sababu ya kukoroma na jinsi ya kuzuia hali hiyo


Kukoroma ni tatizo linalowapata watu wengi wakati wanapolala ambalo linaweza kuwatokea watu wa kila umri ingawa hutokea mara nyingi kwa wanaume au watu wanene. Kukoroma huzidi kwa kadri umri unavyoongezeka na asilimia 54 ya watu wazima hukoroma baadhi ya wakati huku asilimia 25 ya wengine wakiwa na tabia ya kukoroma kila wakati. Kukoroma baadhi ya wakati kwa kawaida sio tatizo kubwa na mara nyingi huleta tu karaha kwa mtu anayelala karibu na mkoromaji. Hata hivyo kukoroma huko sio tu kwamba huharibu usingizi wa anayekoroma bali pia huwasumbua na kuwakeresha wanaolala karibu na mkoromaji. Wale wenye tabia ya kukoroma, hukoroma kila wanapolala na mara nyingi huchoka wanapoamka, na watu wa aina hii hushauriwa kumuona daktari na kushauriwa kuhusiana na tatizo hilo. Lakini kabla hatujaendela mbele ni bora tujue kukoroma hasa ni nini au hutokea vipi?
Mtu huwa anakoroma pale kunapokuwa na kitu au sababu yoyote itakayoziba kuingia au kutoka kwa hewa mdomoni na katika pua. Kuta za koo hutikisika wakati wa kupumua na matokeo yake ni sauti inayosikika ya kukoroma. Kuingia au kutoka kwa hewa huweza kuzuiwa na sababu mbalimbali kama vile:
• Kuziba tundu za pua kusiko kamili ambako husababisha nguvu zaidi zitumike katika kupitisha hewa kwenye pua wakati mtu akiwa amelala. Kitendo hicho hupelekea nyama laini za pua na koo zijikusanye na kusababisha mkoromo. Kuna baadhi ya watu wanakoroma tu kipindi cha allergy (allergy season) au wanapatwa na matatizo ya sinus. Baadhi ya matatizo kama vile kupinda pua (deviated septum) au ukuta unaotenganisha tundu za pua na polyps za pua pia huweza kufanya pua zizibe na kusababisha kukoroma. Watu wengi wanaofanya operesheni za pua pia hupatwa na tatizo la kukoroma.
• Kuwa na misuli dhaifu katika koo na ulimi. Misuli au nyama za koo na ulimi zinapokuwa dhaifu sana hulegea na kuanguka upande wa nyuma wa sehemu inayopita hewa. Suala hilo hutokea pale mtu anapolala fofofo au kuwa na usingizi mzito na kusababisha kukoroma.
• Kuwa na misuli minene ya koo. Hii ni kwa wale watu wanene ambao hata nyama zao za koo pia hunenepa na kupanuka na suala hilo husababisha kukoroma, Pia watoto wenye tonsesi kubwa na adenoids baadhi ya wakati hukoroma.
• Kuwa na kilimi kikubwa ni mojawapo ya sababu zinazosababisha kukoroma. Kilimi kirefu kinaweza kuzuia koo na pale kinapotikisika wakati hewa inapita kwa msukumo husababisha kukoroma.
• Sababu nyinginezo zinazoweza kumsababishia mtu akorome anapolala ni kuwa na umri mkubwa au uzee, imeshuhudiwa kuwa watu wa makamo na wazee hukoroma, kwani misuli na nyama za koo huanza kuzeeka na kulegea kadri umri unayoongezeka. Vilevile wanaume wanakoroma zaidi kuliko wanawake hii ni kutokana na wanaume kuwa na njia nyembamba zaidi ya hewa kuliko wanawake. Kukoroma pia kunaweza kuwa ni tatizo la kurithi. Pombe, kuvuta sigara na matumizi ya baadhi ya dawa pia husababisha misuli ya koo ilegee na hivyo hupelekea mtu akorome. Kulala vibaya pia husababisha kukoroka kama vile kulala kichalichali, kwani hufanya nyama za koo zilegee na kuziba hewa.



Je, Dawa ya kukoroma ni nini?
Swali hilo limeuliwa sana na mimi katika kulijibu ningependa kusema kuwa, kujua sababu inayosababisha mtu akorome na kuitatua au kuiondoa sababu hiyo ndiko kunakotibu kukoroma. Sote tunajua adha inayotokana na kukoroma, na sauti hiyo inavyosumbua hasa iwapo anayekoroma ni mtu wako wa karibu kama vile mumeo, mwenzi wako au yoyote yule inayekubidi ulale naye karibu au katika kitanda kimojana hata chumba kimoja. Kukoroma pia huathiri usingizi wa mkoromaji kwani anayekoroka humbidi aamke mara kadhaa usingizini akijua au bila kujua kutokana njia zake za hewa kufunga kwa sekunde kadhaa ambapo usingizi pia hukatika. Wanaokoroma pia hushindwa kulala vizuri suala linalopelekea asubuhi wawe wamechoka na kutofanya majukumu yao vyema, na pia wale wanaolala nao karibu hupatwa na matatizo kama hayo. Vilevile tunapaswa kujua kuwa kukoroma kuna athari za kiafya za muda mrefu kwa mtu anayekoroma hivyo si jambo la kufanyia mzaha na ni tatizo ambalo linapaswa kushughulikiwa na kutatuliwa.
Wataalamu wanatuambia kuwa ili kujua kukoroma kwako kunasababishwa na nini ni bora ushirikiane na mwenzi wako au yoyote unayelala naye ili akuchunguze pale unapolala na kujua jinsi mwili wako unavyokuwa pale unapokoroma. Ni bora aandae orodha na kuchunguza yafuatayo:
1. Kufunga mdomo na kukoroma kunaonyesha kuwa kuna matatizo ya ulimi.
2. Kufungua mdomo na kukoroma kunaonyesha unaweza kuwa na tatizo katika misuli au nyama za koo.
3. Kukoroma unapolala kichalichali kunaonyesha kuwa pengine kwa kubadilisha namna unavyolala kukoroma nako kunaweza kwisha.
4. Kukoroma wakati unapolala kwa kila mlalo kunaonyesha kwamba tatizo lako ni kubwa na pengine kunahitajia tiba kubwa zaidi.




Iwapo umebadilisha namna unavyolala na haikusaidia, unashauriwa ujaribu yafuatayo:
 Punguza uzito
 Safisha njia yako ya hewa. Kuwa na pua iliyoziba hufanya kupumua kuwe kugumu na kusababisha kukoroma. Unaweza kufanya hivyo kwa kutumia dawa za kusaidia kupumua kwa urahisi (nasal decongestants) zinazopatikana kwa urahisi katika maduka ya dawa.
 Wacha kuvuta sigara.
 Lala mapema na pata usingizi wa kutosha kila mara huku ukijiepusha na kuchoka sana. Kunyanyua kichwa kwa nchi 4 huweza kupunguza kasi ya kupumua na kusaidia ulimi na taya kwenda mbele hali ambayo hupunguza kukoroma. Fanya hilo kwa tumia mito maalum ya kupunguza kukoroma au lala bila mto.

Wataalamu pia wanasema kwamba unaweza kupunguza kukoroma kwa kutokula baadhi ya vyakula au dawa kabla ya kulala ambavyo huongeza kukoroma. Vitu hivyo ni kama vile
o Kutokula mlo mkubwa kabla ya kulala.
o Kutokula vyakula vinavyotokana na maziwa au maziwa ya soya.
o Kutokunywa pombe kabla ya kulala.
o Kutotumia dawa aina ya antihistamines.
o Kutotumia vyakula au vinjwaji venye kafeini.

Vilevile wanaokoroma wanashauriwa kufanya mazoezi ya koo ambayo ni pamoja na kuimba, kusoma kwa kurudia rudia voweli (a,e,i,o,u) kwa nguvu kwa dakika tatu mara kadhaa kwa siku, kuweka ncha ya ulimi chini ya meno ya mbele na kurudisha ulimi nyuma kwa dakika 3 kila siku au huku mdomo ukiwa wazi pelekea taya yako upande wa kulia na wacha ibakie katika hali hiyo kwa sekunde 30. Huku mdomo ukiwa wazi, kaza misuli ya nyuma ya koo na rudia kitendo hicho kwa sekunde thelathini. Unaweza kutizama kwenye kioo na kuona jinsi kilimi kinavyokwenda juu na chini.
Iwapo kukoroma hakutoisha kwa kutumia njia hizo tofauti zilizoelezwa, usife moyo jaribu kumuona daktari na akupe ushauri wa kitiba kuhusiana na tatizo hilo. Madakatari wataalamu wa magonjwa ya pua, masikio na koo au ENT wanaweza kukusaidia zaidi kutatua tatizo hilo. Siku hizi kuna vifaa mbalimbali vinavyotumiwa mahospitalini ili kuondoa kukoroma kama vile kifaa kinachowekwa kwenye meno, CPAP, kidude kinachowekwa mdomoni au hata kufanyiwa operesheni ili kuondoa tatizo hilo.

Wednesday, September 8, 2010

Mambo ya kuzingatia iwapo unataka kushika mimba


Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kumfanya mtu asishike mimba. Sababu hizo zinaweza zikawa zinamhusu mwanamke, mwanamume au wakati mwingine kutojulikana kabisa hali hiyo imesababishwa na nini. Wataalamu wanasema kwamba kwa miaka 20 iliyopita matatizo yanayohusu kushindwa kuzaa yameongezeka kwa kiwango kikubwa na asilimia 25 ya watu wanaotaka kubeba mimba na kuzaa mtoto wanakabiliwa na tatizo hilo. Ni kweli kuwa kwa kawaida watu wengi hubeba mimba na kujaaliwa mtoto pale tu wanapofanya tendo la ndoa. Lakini jambo hilo halitokeo kwa watu wote na ingawa kwa baadhi ya watu kila kitu huonekana kwenda sawa lakini pia hushindindwa kubeba mimba. Utafiti unaonyesha kwamba katika kila familia au 'couples' 5 zinazojamiiana katika wakati muafaka wa ovulation ni moja tu ndio hufanikiwa kupata mtoto, huku karibu wanawake 9 kati ya 10 wakifanikiwa kushika mimba baada ya kujaribu kutafuta mtoto kwa mwaka mmoja mzima bila kuzuia mimba. Hivyo basi nawaomba wale ambao wamekuwa wakifanya jitihada za kufuata maelekezo ili waweze kushika mimba lakini hawakufanikiwa, wasife moyo kwani ipo siku jitihada zao hizo zitazaa matunda.
Mambo ya kuzingatia iwapo unataka kushika mimba…
• Kwanza kabisa ni kuhakikisha kuwa kabla ya yote unamona dokta wako au unakwenda hospitalini na kufanyiwa vipimo ili kujua kama afya yako iko salama au la kwa ajili ya kushika mimba. Baadhi ya vipimo vinavyoshauriwa kufanywa ni pamoja na
1. General examination au uchunguzi wa jumla.
2. Kipimo cha kensa au Pap smear.
3. Kipimo cha magonjwa ya zinaa (STD) kama vile Chlamydia ambao wanaweza kuathiri uwezo wako wa kushika mimba.
4. Kipimo cha damu cha kuangalia kama una upungufu wa damu, Rh na kinga yako ya mwili dhidi ya ugonjwa wa Rubella.
5. Kipimo cha mkojo cha kuchunguza iwapo una ugonjwa wa kisukari. Ugonjwa wa kisukari huweza kumzuia mtu asishike mimba hata iwapo mzunguko wake wa mwezi uko sawa, anapata Ovulation na kidhahiri anaonekana hana tatizo lolote.
6. Kama una paka nyumbani au unakula sana nyuma (red meat) pengine si vibaya pia kupima kipimo cha Toxopmasmosis infection.
7. Kuyajua na kuzingatia baadhi ya mambo yanayoathiri kushika mimba ambayo ni pamoja na:-
• Ingawa unene unaweza kumzuia mtu asishike mimba lakini kufanya mazoezi sana na kuwa na uzito mdogo sana wa zaidi ya kilo 50 huweza pia kumsababisha mtu asishike mimba. Mazoezi ya kupindukia pia huathiri homoni mwiilini.
• Kuwa na fikra nyingi na msongo wa mawazo 'stress' huweza pia kauthairi uwezo wa mtu wa kushika mimba.
• Kutokula vizuri na kutopenda kula kwani humkosesha mwanamke au hata mwanamme baadhi ya virutubisho muhimu vinavyotakiwa kwa ajili ya kufanikisha suala la kushika mimba (nitazungumzia vyakula vinavyosaidia kushika mimba baadaye)
• Sigara, marijuana na pombe ni miongoni mwa vitu ambavyo vinaweza kuathiri uwezo wa kubeba mimba. Mwanamke anayetaka kubeba mimba anashauriwa aache kunywa pombe na kuvuta sigara. Mwanamume pia anashauriwa kuacha kuvuta sigara kwani sigara huathiri kiwango cha mbegu za kiume za mwanamme.
Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayomsaidia mwanamke kushika mimba:
• Anza kutumia vidonge vya Folic Acid, vidonge hivyo mbali ya faida nyinginezo humkinga mtoto atakayezaliwa na magonjwa ya ubongo. (Neural Tube Defect) kama vile Spinal Bifida na mengineyo. Dozi ni kwa uchache miligramu 0.4 za Folic acid kwa siku, miezi mitatu kabla ya kuanza hata kutafuta mtoto.
• Endelea tu na tendo la ndoa bila kuchoka au kukata tamaa, lakini ni bora nguvu zihifadhiwe kwa siku chache kabla ya Ovulation na siku kadhaa baada ya hapo ili mwanamume aweze kuboreshe na kuhifadhi mbegu zake kwa ajili ya siku hizo, Usikimbie chooni au bafuni baada tu ya kukutana kimwili na mwenzio. Kulala kwa dakika kadhaa baada ya tendo la ndoa huongeza uwezo wa mbegu ya kiume kuweza kuendelea kukutana na yai la kike na hivyo kuongeza uwezekano wa kubeba mimba.
• Jiepushe kunywa kahawa na binywaji vinginevyo venye caffeine. Waataalamu wanasema caffeine huweza kukuongezea matatizo ya kushindwa kushika mimba.
• Jiepushe na kutumia dawa za aina yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinazonunulika maduka ya dawa bila ulazima wa cheti cha daktari au Over-the-counter drugs inabidi zitumiwe baada ya kushauriana na daktari.
• Usitumie baadhi ya vitu vinavyoufanya uke uwe na hali itakayoua mbegu za kiume au kupunguza majimaji yake. Vitu hivi ni kama spray mbalimbali na tampons zinazotumiwa na wanawake ili kuufanya uke uwe na harufu nzuri. Mafuta ya aina mbalimbali na jeli kwa ajili ya kulainisha sehemu za siri, mafuta ya kula (vegetable oils) glycerin na mate. Vitu kama hivi kufanya Ph ya uke isiwe ya kawaida na huweza kuua mbegu ya kiume, kusababisha baadhi ya magonjwa ya wanawake au kupunguza majimaji ya ukeni ambayo yanatakiwa ili kusafirisha mbegu za kiume.
• Hakisha mwenzi wako hafanyi kazi au hawi katika mazingira yenye mada hatari ambazo hupunguza uwezo wa mbegu za kiume au kutungwa mimba. Kufanya kazi kwenye mazingira ya joto kali sana kama vile mwanaume wanaofanya kazi kwenye matanuri ya kupika mikate, viwanda vya mafuta na miale hatari baadhi ya wakati huwa na matatizo ya kutozaa. Hivyo kabla mwanamke hajaanza kujilaumu kwa nini hashiki mimba, mwanamme wake pia anapaswa kufanyiwa uchunguzi kamili kuhusiana na suala hilo. Pengine ni suala ambalo wengi hatulijui kwamba katika tiba iwapo mke na mume au mtu na mwenzi wake wana tatizo la kutopata mtoto, wawili hao kwa pamoja hupaswa hufanyiwa vipimo na wala sio mwanamke mwenyewe. Hivyo iwapo unashindwa kushika mimba, hakikisha pia mwenzi wako hana tatizo pia. Wanaume pia kama walivyo wanawake hukabiliwa na matatizo mengi tu yanayosababisha familia kukosa watoto. Matatizo kama vile upungufu wa mbegu za kiume, uchache wa mbegu, kutokuwa na kasi mbegu na mengineyo ni miongoni mwa matatizo kibao ambayo mwanamume anaweza kuwa nayo na kukosa mtoto. Hivyo tabia ya kuwatizama wanawake kwa jicho la lawama katika jamii na kuwanyooshe kidole pale mimba inaposhindikana kushika ni kinyume cha ukweli wa kitiba na uhalisia.
• Usichoke kufuata mzunguko wako wa Ovulation na kufanya tendo la ndoa katika wakati ambao mwili wako (ewe mwamamke) uko katika siku za kuweza kushika mimba.

Monday, September 6, 2010

Wataalamu karibu watakugundua dawa nyingine ya kutibu Malaria


Matokeo ya utafiti wa kimataifa yanaonyesha kwamba wanasayansi karibu watafanikiwa kutengenza dawa yenye athari zaidi ya kutibu ugonjwa wenye kuleta maafa mengi wa Malaria. Dawa hiyo inayoitwa "NITD609" ambavyo inatokana na mada ya 'spinoindolones' imeanza kutengenezwa kwa jitihada mbalimbali za wanasayansi wa Marekani, Singapore, Switzerland, Thailand na Uingereza. Wanasayansi hao wanasema kwamba, dawa hiyo ambayo ni ya kumeza inatofautiana na dawa nyinginezo za Malaria zilizopo madukani kwa kuponya ugonjwa huo haraka, kutokuwa na madhara kwa mtumiaji na kuweza kutibu Malaria kwa kutumiwa dozi moja tu.
Utafiti bado unaendelea kuhusiana na majaribio ya dawa hiyo na kwamba dawa hiyo imeonyesha mafanikio mazuri katika kutibu Malaria baada ya kujaribiwa kwa panya watano waliokuwa wagonjwa bila kuwa na madhara yoyote.
Wataalamu wanasema pia kwamba dawa hiyo ya NITD609 inatofautiana sana na dawa ziliopo za Malaria kwa umbo na kwa kikemia na kwamba ingawa dawa zilizopo zinaweza kutibu ugonjwa huo lakini zimeshindwa kufikia matarajio yanayotakiwa. Wataalamu sasa wanasubiri kuijaribu dawa hiyo kwa binadamu, suala ambalo litaanza baadaye mwakani.
Ingawa sote tunajua lakini si vibaya kukumbusha hapa kuwa watu karibu milioni 500 huugua ugonjwa wa Malaria kila mwaka duniani, ambapo vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo ni karibu milioni moja huku watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano ndio wanaoshambuliwa zaidi na Malaria. Ugonjwa huo umekuwa ukisababisha vifo na matatizo mengi katika nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika kuliko maeneo mengineyo duniani.