Wednesday, October 19, 2011
Majaribio ya chanjo ya kwanza ya malaria duniani yaonyesha mafanikio
Majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa malaria yameonyesha mafanikio na hivyo kuleta matumaini kuwa huenda gonjwa hilo sugu linalohatarisha maisha ya mamilioni ya watoto barani Afrika likapatiwa chanjo kwa mara ya kwanza duniani. Taarifa kuhusu awamu za mwisho za majaribio ya chanjo hiyo inayotengenezwa na shirika la GlaxoSmithKline zilitangaza Jumanne ya wiki hii na kuonyesha kwamba ina uwezo wa kuulinda mwili dhidi ya malaria kwa watoto wenye umri wa miezi mitano hadi 17. Andrew Witty Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la kutengeza dawa la Uingereza ambalo limetengeneza chanjo hiyo amesema kwamba, mafanikio hayo yanaonyesha kuwa hivi karibuni dunia kwa mara ya kwanza itaweza kupata chanjo ya ugonjwa wa Malaria. Hata hivyo sambamba na kusifu mafanikio hayo Bw. Witty amesisitiza kwamba wanasayansi wanaoshulighulia ugonjwa huo na wataalamu wa masuala ya afya ulimwenguni kote bado wanasisitiza kwamba chanjo hiyo inayojulikana kana RTS,S au Mosquirix bado sio njia ya haraka ya kutokomeza malaria. Licha ya hayo inaelezwa kuwa chanjo hiyo ya aina ya sindano haina athari sana katika kuzuia ugonjwa wa malaria ikilinganishwa na chanjo nyingine kama vile za ugonjwa wa polio na ndui.
Gonjwa la malaria bado ni janga kubwa kwa nchi nyingi duniani hasa za Afrika zilizo chini ya Jangwa la Sahara na kila mwaka hupelekea vifo vya watu wengi kwenye nchi hizo hasa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. Chanjo sio changamoto pekee inayowakabili wataalamu wa masuala ya afya na tiba duniani katika kupambana na malaria bali tiba ya ugonjwa huo pia imekuwa ikibadilika mara kwa mara kutokana na vidudu vya ugonjwa huo kujibadili na kuzishinda nguvu dawa zinazotengeneza za kutibu ugonjwa huo. Kwa ajili hiyo madaktari na wataalamu wamekuwa wakishauri kutumiwa zaidi tiba ya dawa mseto katika kutibu malaria kuliko dawa moja pekee. Njia nyingine za kujilinda na malaria ni pamoja na kutumia chandarua, kupiga dawa za kuua mbu na kuyaweka mazingira tuishiyo katika hali ya usafi bila kuwepo vindimbwi vya maji na kuzungukwa na vichaka suala ambalo husababisha mbu wazaane.
Ingawa habari hii ni mafanikio makubwa yanayopaswa kupigiwa makofi na wadau wote wa masuala ya afya na tiba lakini, shaka yangu mie ni kuwa, hata kama chanjo hiyo ikianza kufanya kazi kesho lakini je, watoto wote wa bara Afrika wataweza kupatiwa chanjo hiyo na kuepusha na vifo vya holela vinavyosababishwa na malaria? Au isije ikawa hadithi zile zile za chanjo ya polio na ndui ambazo zimekuwepo kwa miongo mingi lakini mpaka leo bado kuna watoto wa Kiafrika wasiopatiwa chanjo hizo kutokana na sababu mbalimbali.
Sunday, October 16, 2011
Kila siku faida za Folic Acid zazidi kugunduliwa
Katika hali ambayo muda mrefu imekuwa ikifahamika kwamba dawa za folic acid zinazotakiwa kuliwa na mama wajawazito zina faida kemkem kwa watoto wanozaliwa, wataalamu hivi karibuni wameendelea kufahamu umuhimu wake zaidi. Siku zote kina mama wajawazito wamekuwa wakishauriwa kula folic acid miezi mitatu kabla ya kushika mimba, na pia kwa miezi kadhaa wakati wa ujauzito. Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kwamba watoto ambao mama zao walikula folic acid kabla na wakati wa ujauzito kwa kiasi kikubwa huwa hawachelewi kuzungumza. Uchunguzi huo uliofanywa huko Norway kwa kuwashirikisha wanawake 40,000 umebainisha kwamba wale ambao hawakula folic acid kabla na wakati walipokuwa na mimba wana uwezekano mara dufu wa kuzaa watoto wenye matatizo ya kuchelewa kuongea kuliko waliokula. Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapisha kwenye Jarida la Marekani la Taasisis ya Tiba (JAMA) kula folic acidi wiki 4 kabla ya ujauzito na kuendelea hadi wiki 8 baada ya kutungwa mimba husaidia kupunguza hatari ya watoto kushindwa kuongea hata wanapofikia miaka mitatu. Ingawa wataalamu wamekiri hawajui ni namna gani folic acid inazuia watoto kuchelewa kuongea lakini wanasema, kuna uwezekano dawa hizo zikawa zinataathira katika mfumo wa neva na kuzuia tatizo hilo lisitokee.
Folic acid ni miongoni mwa tembe zinazohusiwa sana mama wajawazito kula, kwani inajulikana kuwa zinazuia watoto wachanga kuzaliwa wakiwa na ugonjwa unaoitwa 'neural tube defects' ambao ni matatizo katika sehemu ya chini ya ute wa mgongo ambapo mtoto mchanga huzaliwa huku ubongo wake ukiwa haukukua kabisa. Lakini ingawa hayo yote yanajuliakana shaka yangu ni kuwa je, mama wajawazito katika nchi zetu wanajua hilo au je, wanaelimusha juu ya umuhimu wa kula folic acid? Nadhani ni jukumu langu mie na wewe kuielimisha jamii.
Subscribe to:
Posts (Atom)