Wednesday, December 30, 2009

WHO yasema, ni mapema mno kutangaza ushindi dhidi ya virusi vya H1N1


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO amesema kuwa ni mapema mno kuweza kutangaza ushindi dhidi ya virusi vya homa ya mafua ya nguruwe akiashiria uwezekano wa virusi hivyo kubadili sura yake na kuwa hatari kubwa zaidi kwa mwanadamu. Margaret Chan amesema kuwa virusi vya H1N1 bado vinaendelea kuzagaa na tayari vimewasibu mamilioni ya watu. Mkuu wa Shirika la Afya Duniani amesema habari njema ya kitiba kuhusu virusi hivyo ni kupungua kasi yake licha ya kwamba vimekwisha sababisha vifo vya watu 12 elfu wengi wao wakiwa wanawake waja wazito, watoto wadogo na watu wenye maradhi sugu. Chan amesema idadi hiyo rasmi ya watu waliofariki dunia kutokana na virusi vya mafua ya nguruwe haiakisi ukweli wa mambo na kwamba idadi kamili ya wahanga wa ugonjwa huo itajulikana baada ya kupita miaka miwili.

Sukari kupimwa kupitia lensi za macho



Wanasayansi wamegundua teknolojia mpya itakayowezesha kupimwa kiwango cha sukari katika damu bila ya kuhitajia mgonjwa kutolewa damu kila siku. Wataalamu hao wa Chuo Kikuu cha Ontario magharibi huko Hamilton, wamegundua teknolojia hiyo mpya ambapo sukari huweza kupimwa kwa kutumia lensi za macho za aina ya hudrogel zilizotengenezwa kwa vipendo vidogo vidogo vya nano. Wagonjwa wa kisukari watakaovaa lensi hizo wataweza kujua kuhusana na kiwango cha sukari mwilini mwao, kutokana na mabadiliko ya rangi ya lensi hizo za macho. Vipande vya nano vilivyotumika kutengeneza lensi hizo, hubadilika kwa kuzingatia molekuli za glukosi zilizoko kwenye machozi, suala ambalo husababisha mabadiliko ya kikemia na mabadiliko ya rangi. Wanasayansi wana matumaini kwamba, kwa kugunduliwa lensi hizo mpya na kuanza kutumika, katika siku zijazo kutakuwa hakuna tena haja ya wagonjwa wa kisukari kudungwa sindano na kuchukuliwa damu kila siku ili kujua kiwango cha sukari mwilini.

Saturday, December 26, 2009

Kujiingiza katika mapenzi kwenye umri mdogo husababisha kensa ya mlango wa kizazi


Huko nyuma iliaminiwa kuwa, virusi aina ya papiloma au (HPV) pamoja na vipimo duni ndio sababu kuu inayopelekea ugonjwa wa kensa ya mlango wa kizazi, lakini uchunguzi mpya umeonyesha kuwa kuna sababu nyinginezo muhimu zinzosababisha ugonjwa huo. Kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa katika jarida la Kensa la Uingereza, mahusiano ya kijinsia yanayofanywa katika umri mdogo huongeza uwezekano wa kupata kensa ya mlango wa kizazi mara dufu. Suala jingine lililohesabiwa kuchangia maambukizo hayo, ni muda mwanamke anapopata mtoto wake wa kwanza.
Katika uchunguzi huo, imeonekana kuwa wanawake wanaoishi maisha ya kimasikini, huanza kujiingiza katika masuala ya kimapenzi miaka minne mapema kuliko wengineo. Hivyo kuna uwezekano wa kupata maambukizo ya virusi vya HPV mapema zaidi, na hivyo kuvipa muda zaidi virusi hivyo kuzaliana kwa muda mrefu na baadaye kusababisha kensa ya kizazi. Wanasayansi waliofanya uchunguzi huo wamependekeza kwamba ni bora chanjo dhidi ya virusi vya HVP itolewe mapema, hasa kwa wasichana wanaoishi katika jamii masikini, ili kuwakinga na ugonjwa wa kensa ya mlango wa kizazi.
Inafaa kujua kuwa, kensa ya mlango wa kizazi au kwa kimombo cervical cancer, ni saratani inayoshambulie lango la uzazi, sehemu ya chini kabisa na nyembamba ya kizazi. Ugonjwa huo unaweza kugunduliwa kirahisi kwa kufanya kipimo cha Pap smear. Ni muhimu kufahamu kwamba ugonjwa wa kensa ya kizazi ni ugonjwa hatari lakini unaweza kuzuiwa na kutibiwa kwa urahisi. Naahidi kuelezea kwa undani juu ya ugonjwa huo hapo baadaye.

Friday, December 25, 2009

X-Mass Njema Wadau


Leo ni sikukuu ya Christmas, kwanza kabisa blogi ya Kona ya Afya inatoa mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa kuzaliwa masihi, Issa Bin Maryam, (Yesu Kristo) kwa wafuasi wote wa dini hiyo ya mwenyezi Mungu. Ni matumaini yetu kuwa katika wakati huu wa sikukuu ya X-mass wadau wote huku wakisherekea sikukuu na kuwa mapumzikoni, hawatazembea pia kuzitunza afya zao. Kwa ajili hiyo basi zifuatazo ni nukta kadhaa za kufuata ili kuepusha wasiwasi na mfadhaiko wa mawazo (stress) wakati huu wa mapunziko na sikukuu, na zinazosadia kuhakikisha kwamba tunabaki katika afya njema kimwili, kiakili na kihisia.
• Jitahidi kushikamana na ibada. Kushikamama na ibada za kiroho wakati huu wote wa sikukuu, na kuwa karibu na muumba ( kwa kutegemea imani na dini ya mtu) kwa kufanya ibada kama kusali, kwenda kanisani au msikitini husaidia kumfanya mtu ajisikie vizuri kiroho.
• Pata hewa nzuri. Kila unavyojitahidi kuwa nje ya nyumba na kufanya shughuli mbalimbali ndivyo mwili wako unavyopata nishati zaidi. Kuvuta hewa safi na salama kutaufanya ubongo wako upate oksijeni zaidi na kuupa mwili wako nishati. Hivyo wakati huu wa sikukuu jitahidi kufanya michezo kama vile kukimbia, kusketi, kupanda baiskeli, kutembea kando ya bahari au mto na kadhalika.
• Jishughulishe na masuala ya sikukuu kama vile kuwanunualia watu zawadi madukani, kuwatembela ndugu jamaa na marafiki na hata wagonjwa, kualika au kwenda katika mialiko mbalimbali na kadhalika. Vitendo hivyo ni bora kuliko kukaa tuu nyumbani na kula na kunywa peke yako huku akiangalia tv au filamu.
• Pata usingizi wa kutosha na pumzisha mwili wako. Unaweza ukalala kidogo mchana au kuamka kwa kushelewa kidogo wakati wa asubuhi.
• Tenda kile moyo wako inachopenda. Kuwa na afya njema wakati wa X-mass ni pamoja na kufanya kile kinachoburudisha moyo wako. Imba kama unapenda kuimba, cheza kama unapenda kucheza, andika, tembea, chora picha, pika nakadhalika, ilimradi utende chchote kili kinachofaurahisha moho wako.
• Kula na kunya kusizidi kiasi, na bila kusahau vyakula visivyo na mafuta mengi au sukari nyingi ambavyo ni salama kwa afya zetu. Wale wenye magonjwa mbalimbali sugu wasijisahau na kuvunja miiko ya vyakula wasivyotakiwa kula. Usisahau kuwa, sikukuu itapita lakini afya yako ni muhimu sana kwa maisha yako yote… Sikukuu njema wadau huku tukitunza afya zetu!

Wednesday, December 23, 2009

Jeli ya nyanya ni bora kuliko aspirini


Utafiti mpya uliofanywa kwa majaribio umegundua kuwa katika mbegu za nyanya kuna mada asilia, inayoweza kusadia mzungumzo wa kawaida wa damu na kuzuia damu isigande. Mada hiyo iliyoko kwenye mbegu za nyanya iligunduliwa mwaka 1999 na Profesa Adim Dutta-Roy. Jeli hiyo inayozunguka mbegu za nyanya, hunaweza kusaidia mzunguko wa damu.
Jeli hiyo isiyokuwa na rangi wala ladha, huzuia chembe za damu aina ya platelets zisishikane, suala ambalo hupunguza uwezekano wa damu kuganda, kama inavyofanya aspirini lakini bila kuwa na madhara.
Wachunguzi wa Uingereza wamesema kwamba, athari za geli hiyo huanza masaa matatu tangu inapoanza kutumiwa na kudumu kwa masaa 18, hivyo inahitaji kutumiwa kila siku.
Wataalamu hao wamependekeza kwamba, kuongeza jeli hiyo katika vyakula mbalimbali kunaweza kuepusha matumizi ya aspirini kwa ajili ya kuzuia hatari ya magonjwa ya mishipa ya moyo.

Mshituko wa moyo mara nyingi hutokea saa tatu asubuhi


Wataalamu wa magonjwa ya moyo wamesema kuwa hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo hutokea zaidi mapema asubuhi, hasa saa tatu asubuhi.
Utafiti huo uliotangazwa katika Kongress ya 4 magonjwa ya moyo ya Mashariki ya Kati imesema kuwa, watu wanaokabiliwa na hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo, hutokewa na ugonjwa huo mapema asubuhi kwa sababu ya mabadiliko ya homini ambayo huongeza hitajio la oksijeni la mishipa ya moyo katika wakati huo, na kusababisha mshituko wa moyo. Uchunguzi huo umeelezea pia kuwa, ripoti zinaonyesha ongezeko la matukio ya mshituko wa moyo katika siku za Jumatatu, suala ambalo huenda likawa linachangiwa na kiasi kikubwa na kula kupita kiasi siku za wikiendi. Wataalamu hao pia wamesema kuwa, mishipa ya juu ya mwili huwa inasinyaa msimu wa baridi, hali ambayo ni kinyume na utendaji wa mishipa ya moyo na husababisha kupungua kiwango cha oksijeni inayohitajiwa na misuli ya moyo. Wamesema hii ndio sababu, watu hupata mishtuko wa moyo kwa wingi wakati wa mapukutiko (fall) na baridi (winter).
Uchunguzi huo pia umeachiria kwamba, umri wa watu wanaopatwa ugonjwa huo imeshuka na hata kufikia chini ya miaka 55 katika baadhi ya nchi.

Monday, December 21, 2009

Ujuwe ugonjwa wa Kifua Kikuu au TB ....sehemu ya kwanza



Karibuni wapenzi wadau wa Kona ya Afya katika mfululizo mwingine wa
kujadili magonjwa mbalimbali. Leo tumepata fursa ya kuzungumzia ugonjwa wa kifua kikuu, ambacho maambukizo yake yanaongezeka kwa kasi kubwa ulimwenguni, khususan katika nchi zinazoendelea. Kwa kuzingatia kuwa ugonjwa wa kifua kikuu huathiri watu wa rika zote na hasa vijana kati ya miaka 15 hadi 45 ambayo ndiyo nguvu kazi katika nchi nyingi za dunia, kunapaswa kufanyika jitihada kubwa za kudhibiti maambukizo ya ugonjwa huo. Kifua Kikuu ambao kitaalamu hujulikana kama Tuberculosis ni ugonjwa wa kuambukiza ambao huenezwa kwa njia ya hewa. Kifua kikuu husababishwa na bacteria au kimelea aina ya Mycobacterium tuberculosis au (tubercle bacterium). Ugonjwa huu kwa kawaida huathiri mapafu, lakini pia huweza kushambulia viuongo vingine vya mwili kama vile tezi za limfu, ubongo na mifupa.
Tb inambukizwa kwa namna gani? :
Mtu mwenye kifua kikuu au Tb ambaye hajatibiwa, anapokohoa, kupiga chafya, kutema mate au makozi husambaza bacteria au vimelea hivyo vya ugonwja huo hewani. Kwa hivyo mtu mwingine akivuta hewa yenye vimelea hivyo anaweza kuambukizwa kifua kikuu. Kwa mfano takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa nchini Tanzania ugonjwa wa Kifua Kikuu umekuwa ukiongezeka kwa kasi kubwa ambapo watu elfu 65,000 hivi sasa wanaugua kifua kikuu nchini humo. Kati yao asilimia 50 pia wana ukimwi. Hapa linajitokeza swali kwamba dalili za Kifua Kikuu ni zipi?
Mtu ambaye amepatwa na ugonjwa wa Tb au Kifua Kikuu huwa na dalili au husumbuliwa na hali zifuatazo:
Kukohoa kwa muda usiopungua wiki mbili na mara nyingine kukohoa damu, homa za jioni za mara kwa mara, kutokwa na jasho usiku, kukosa hamu ya kula, kupungua uzito kwa kiasi kikubwa na kadhalika.
Kundi ambalo liko kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa Tb au kifua kikuu ni la wale wanaoishi kwa karibu na kwa muda mrefu na mtu yule aliyekwisha ambukizwa ugonjwa huo. Kwa hiyo hapa nitaorodhesha makundi ambayo yako kwenye hatari na ya uwezekano mkubwa wa kuambukizwa Tb iwapo watakuwa karibu na mgonjwa. Watu hawa ni rahisi kupatwa na kifua kikuu kwa sababu kinga zao za mwili huwa ni za kiwango chini: Watoto wadogo na wazee, wale wote wanaougua kisukari, watu wnaotumia dawa aina ya steroids au dawa nyinginezo zinazoathiri mfumo wa kinga ya mwili, waathirika wa ukimwi na HIV, wale wote wanaoishi maeneo yenye msongamano mkubwa watu yaliyoduni kiafya, wanaoishi kwenye sehemu zisizokuwa na hewa ya kutosha, watu wanaotumia dawa mbalimbali, au pombe na mwisho wale wenye lishe duni.
Usikuko muendelezo wa makala hii, na daima linda afya yako.

Sunday, December 20, 2009

Njia za kuondoa makovu


Kuna matatizo malimbali ya ngozi yanayoweza kuwapata watu ambapo makovu ni mojawapo ya matatizo hayo.Makovu baadhi ya wakati hajawezi kuepukika hasa iwapo makovu hayo yamesababishwa na magonjwa au ajali mbalimbali. Makovu katika sehemu mbalimbali za mwili huweza kufunikwa na kufichwa kwa urahisi iwapo hayapo katika sehemu zinazoonekena. Lakini iwapo makovu yatakuwa usoni, mikononi au kifuani, huwa si rahisi kuyaficha na mara nyingi huwakera wale walio na makovu. Watu wengi wangependa kujua ni njia gani ambazo mtu anaweza kutumia ili kuondoa makovu. Ili kulijibu swali hilo ni bora kwanza tujue kovu ni nini hasa. Kovu katika mwili hutokea pale tishu aina ya fibrous inapojikusanya juu ya ngozi ili kusaidia kukarabati seli na ngozi iliyoharibika. Wakati kunapotokea jeraha, ngozi kutoa seli ziitwazo fibroblasts ambazo hutoa kitu kiitwacho collagen na kujaza sehemu yenye jeraha. Collagen ni ngumu, iko kama ufumwele unaopatikana katika protini ambayo hujaza eneo lote le kovu. Collagen ipo pia katika ngozi ya kawaida lakini katika kovu huwa nyingi na iliyojipanga katika mpangilio holela. Hii ndio sababu kovu huwa na rangi iliyokolea na huonekana kwa urahisi. Baadhi ya makovu huondoka kwa urahisi, baadhi huchukua miezi na hata miaka, huku makovu mengine yakibadilika polepole rangi na muonekano wake. Kovu huenekana kirahisi juu ya ngozi kwa sababu seli zilizotumika kuunda kovu hutofautiana na seli za mwanzo za ngozi. Kwa mfano makovu yaliyo juu ya ngozi hayawezi kuota vinyeleo kwa kuwa seli zake hazina matundu ya vinyeleo. Pia makovu hayana uwezo wa kuzuia miale ya jua. Kwa bahati mbaya ni vigumu kidogo kuweza kuondoa baadhi ya makovu moja kwa moja katika ngozi. Ingawa kuna njia kama vile vipodozi vinavyoweza kuziba makofu na njia nyinginezo za kitiba, lakina hata hivyo njia zote hizo mara nyingi huwa haziwezi kuondoa baadhi ya makovu kabisa, hasa yale makovu yaliozama katika ngozi na kuharibu kwa ngozi kwa kiasi kikubwa. Njia za tiba zinazoweza kutumiwa kuondoa makovu ni kama vile operesheni ya Laser (laser sugery), sindano za steroid, kubandua ngozi ya juu (dermabrasion) na radio therapy.
Lakini hata hivyo kuna njia mbalimbali za tiba asilia ambazo zinaaminika kuweza kusaidia kuondosha makovu. Njia hizo ni kama
1. Majani ya Aloe Vera. Majani haya yanapatikana kila sehemu hasa kwetu Tanzania na kwingineko Afrika. Majani hayo pia ni dawa nzuri ya kutibu magonjwa mbalimbali ya ngozi kama vile kiba au kishilingi. Kata majani hayo na utumie utomvu wake kupaka katika makovu. Baada ya muda polepole itapunguza na kuondoa makovu. Aleo Vera ni majani ambayo yanasifika hivi sasa ulimwenguni kote kwa ajili ya ngozi na yanatumiwa katika vipondozi mbalimbali. Basi zaidi ya kukuondoa makovu, yatasaidia pia kuifanya ngozi yako iwe nyororo.
2. Njia nyingine ni kutumia tango. Twanga tango na tumia mchanganyiko wake kupaka juu ya kovu. Husaidia kulainisha makovu na unapotumia kwa muda mrefu huondoa makovu pia.
3. Kupaka asali juu ya kovu na kuiacha usiku kucha. Njia hii inaweza kurudiwa mara kwa mara hadi pale kovu litakapotoweka.
4. Kula vyakula vyenye vitamin E, ambavyo ni ni muhimu katika kusaidia ngozi kupona na kurudia katika hali yake ya kawaida. Vitamin E iko katika mayai, nyungu za aina mbalimbali kama karanga, mayai, mafuta ya nafaka na vinginevyo. Kama huwezi jitahidi utumie vidonge vya vitamin E lakini baada ya kupata ushauri wa daktari.
5. Kupaka baking soda kidogo na maji sehemu yenye kovu na kuikanda sehemu hiyo kwa dakika moja. Mara mbili kwa siku. Kisha safisha kwa maji ya vuguvugu halafu paka mafuta ya zaituni.
6. Kutumia cream zenye vitamini E nad C na upake moja kwa moja katika kovu. Husaidia ngozi kuota tena katika kovu. Unaweza kumuona mtaalamu wa magonjwa ya ngozi naye akakushauri ni cream gani utumie ili kuondoa makovu yako. Pia jitahidi kupata lishe nzuri bila kusahau matunda na mboga mboga ambayo ni muhimu kwa ajili ya afya ya ngozi. Kunywa maji ya kutosha kwani maji pia kulainisha ngozi yako na kufanya makovu kutoka kwa urahisi.

Inafaa kujua kuwa baadhi ya makovu kama vile yaliyosababishwa na kuungua au kuchanjwa ni vigumu kuyaondoa kwa kutumia njia hizo zilizotajwa.

Friday, December 18, 2009

Mmh!... watafiti wasema ukoma unaweza ukawa ugonjwa wa kumbukiza!


Watafiti wamegundua geni ambazo zinahusiana na ugonjwa wa ukoma, suala ambalo linaondoa fikra ya huko nyuma kwamba ukoma si ugonjwa wa kuzaliwa au wa kuridhi. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa huko China na kuchafishwa katika Jarida la Tiba la Uingereza, mabadiliko ya geni 7 mwilini yanaweza kuwa ndio chanzo cha uwezekano wa baadhi ya watu kupatwa na ukoma. Wataalamu hao wamesema kuwa, tangu kale imekuwa ikifikiriwa kuwa ukoma ulikuwa ukisababishwa tu na vijidudu lakini uchunguzi wao umeonyesha kuwa maambukizo ya ugonjwa huo yansababishwa pia na genetiki. Wamesema kwamba, iwapo mzazi ana ugonjwa huo, basi kuna uwezekano mkubwa mwanaye naye akapatwa na ugonjwa huo. Hata hivyo wataalamu hao wamesema, cha kushangaza ni kuwa, iwapo mmoja kati ya mke na mume wana ukoma, mwingine hawezi kuambukizwa ugonjwa huo kwa miaka mingi. Geni 5 kati ya hizo 7 zinazosababisha ugonjwa huo, inaaminiwa kuwa zinauhusiano wa karibu na mfumo wa kulinda mwili.
Uchunguzi huo unaleta matumaini ya kuweza kukingwa mapema wale wanaodhaniwa kuwa wana uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huo. Vilevile utafiti huo unaweza kutumika kuchunguza zaidi vijidudu vya magonjwa mengine ambavyo vinakaribiana na vijidudu vinayosababisha ukoma, kama vile vijidudu vya kufua kikuu ugonjwa ambao husababisha vifo vya watu milioni 1.8 duniani.
Sio vibaya kujua kuwa, ugonjwa wa ukoma au Leprosy kwa kiingereza na kitaalamu Hansen's disease, unaosabaishwa na bacteria waitwao Mycobacterium Lapracea na Mycobacterium Lepromatosis huathiri ngozi, utando telezi (mucous membranes), neva za ukingoni (peripheral nerve) pamoja na macho.
Kuharibika daima neva au mishipa ya fahamu kunakosababishwa na ugonjwa wa ukoma, humzuia mtu anayepona ugonjwa huo kuhisi maumivu, suala ambalo huwafanya wagonjwa wa ukoma kuwa wenye kupata kwa urahisi majeraha madogo madogo na vidonda ambayo baadaye huwa makovu ya kudumu.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa, kuna kesi 254,525 mpya za ugonjwa wa ukoma katika nchi za tropiki na zilizo chini ya jangwa la sahara.
Kumbuka kuwa ugonjwa wa ukoma unatibika na unapotibiwa mapema huweza kumuepusha mgonjwa kupata madhara makubwa ya kukatika viungo na kuwa mkoma!

Wednesday, December 16, 2009

Sumu ya Ndani ya Chakula au Food Poisoning…sehemu ya mwisho


Mambo mengi yanaweza kufanywa ili kuzuia vijidudi maradhi na sumu kuchafua chakula chetu. Mosi, safisha mikono yao kwa utaratibu, kabla na kila mara unapotayarishah chakula, funika kwa sashi au bandage sehemu yoyote ya yenye mchubuko au uliojikata katika mkono wako kabla ya kuanza kuandaa chakula,safisha sehemu zote utakazotumia wakati wa maandalizi ya chakula, brashi na sponji za kuoshea vyombo kwa kiasi kikubwa huwa na uwezekano wa kubeba bacteria. Kwa hivyo ni lazima zioeshwe mara kwa mara baada ya kutumia. Vyakula aina ya nyama na mayai vinapaswa kupikwa barabara na vipoti kupashwa moto vizuri kabla yakuliwa. Hakiisha jokofu au friji lako lina nyuzi joto 40 na freeza ikiwa nyuzi 0 au chini ya hapo, kiporo cha chakula kisikae ndani ya jokofu kwa zaidi ya siku nne, usiache ovyo nyama bila ya kuihifadhi, na vyema uichemshe kwa zaidi ya nyuzi joto 140, kuwa mwangalifu wakati wa kuhifadhi vyakula kama vile samaki, nyama mbichi na mayai, hivyo vyote vinaweza kuchafuliwa na bacteria wa maradhi. Usivue samaki kutoka kwenye maji yaliyochafuka, safisha mboga mbichi na matunda kabla ya kula au kupika, unanunuji vyakula vinavyouzwa ndani ya makopo, mikebe n.k unapaswa kwanza kuangalia muda wa matumizi yake unakwisha lini, usile uyoga wa mwituni, ambao haujaidhinishwa na mtaalamu kuwa ni salama kwa mwanadamu na mwisho hakikisha kuwa bidhaa zote zinazotokana na maziwa ambazo nyingi huuzwa madukani ni lazima ziwe zimeondolewa vijidudu hasa bacteria kwa njia ya kitaalamu ijulikanayo kama pasteurization. Maziwa ya ng'ombe ambayo hayajapitia katika njia hiyo ya pasteurization, yanapaswa kuchemshwa vizuri kabla ya kutumia.
Itakumbukwa kuwa watoto, wazee na wale wote wenye magonjwa ya muda mrefu au wenye kinga ya dhaifu ya mwili huwa na hali mbaya wakati wakila chakula kilichoharibika au kuchafuliwa na vimelea vya maradhi. Kwa hiyo ili kukabiliana na tatizo hili, watu wazima wanapaswa kubeba jukumu kuu la kuepukana na suala hilo na vile vile kuwaelekeza watoto pia nini cha kufanya.

Monday, December 14, 2009

Oooh! Jeli ya HIV ya kina mama imeshindwa kuzuia Ukimwi!


Jaribio kubwa la jeli ya ukeni ya kuzuia vijidudu limeonyesha kuwa, hakuna ushahidi kwamba inapotumiwa huuzuia hatari ya maambukizi ya Ukimwi kwa wanawake. Jeli jiyo inayoitwa PRO 2000, ilikuwa inakusudiwa kutumiwa kabla ya kujamiiana ili kusaidia kupunguza maambukizo ya Ukiewi. Jaribio hilo lilifanywa kwa kuwashirikisha wanawake 9,385 katika nchi 4 za Kiafrika. Ilikuwa inatarajiwa kuwa jeli hiyo ya kuzuia vijidudu ingeweza kuwa njia muhimu ya kupunguza kuenea kwa virusi vya HIV, huku wataalamu wakikiri kwamba kuenezwa kondom pekee hakujasaidia kupunguza maambukizo ya ugonjwa huo. Wataalamu wanasema kuwa bado njia mpya zinahitajika zaidi ili kupambana na gojwa hilo hatari, hasa katika nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara barani Afrika, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya wale walioambukizwa ugonjwa huo ni wanawake. Wanawake mara nyingi wamekuwa wakilazimika kufanya ngono zembe, na wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kupatwa na ugonjwa wa Ukimwi kuliko wanaume, hivyo inafikiriwa kuwa iwapo itapatikana jeli ambayo wataweza kutumia ili kuzuia maambukizo hayo, suala hilo litawalinda zaidi.
Huko nyuma jaribio dogo lilionyesha kwamba jeli aina ya PRO 2000 ingeweza kupunguza hatari ya mambukizo ya HIV kwa asilimia 30.

Haya tena…. kukoroma kuna uhusiano na kisukari!


Uchunguzi mpya umeonyesha kwamba, wale wanaokoroma wakati wakilala, wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari kuliko wale wanaolala kimya. Kwa mujibu wa uchunguzi huo uliofanywa kwenye chuo kikuu cha Yale, wale wanaokoroma sana wanapolala, wanakabiliwa na uwezekano wa kupata kisukari kwa asilimia 50. Wataalamu wanasema pia kuwa, kushindwa kupumua usingizini au kitaalamu kunahusiana na kisukari aina ya pili, bila kujali sababu nyinginezo kama vile umri, jinsia, uzito na hata asili anayotoka mtu.
Kukoroma sugu, au kitaalamu sleep apnea ni hali ambayo inasababishwa kushindwa kufanya kazi njia ya hewa, suala ambalo humfanya mtu aamke mara kadhaa usingizini wakati anapolala. Hali hiyo inahusiana na baadhi ya mabadiliko ya umetaboli au hali ya ujenzi wa seli na uvunjaji vunjaji wa kamikali mwilini, kwa kimombo ‘metabolism’.

Sunday, December 13, 2009

Afya njema inaongeza uwezo wa akili au IQ


Utafiti mpya umeonyesha kwamba kuna uhusiano kati ya afya njema ya mwili wa vijana na watu wazima pamoja na kufanya kazi vyema ubongo, na uwezo wa kupata maksi za juu katika vipimo vya akili au IQ test. Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Akademia la sayansi umeeleza kwamba, kuwa na afya nzuri ya mwili katika umri wa miaka 15 na 16 kunaongeza uwezekano wa kuwa na uwezo wa akili wa juu. Wataalamu wamesema vijana wa aina hiyo wana uwezo mkubwa wa kufanikiwa kusoma elimu ya juu na kupata kazi nzuri maishani. Kuwa fiti kimwili inaamisha pia kuwa na moyo unaofanya kazi vizuri na uwezo mkubwa wa mapafu, vilevile kuwa na ubongo wenye kupokea vyema hewa ya oxygen, suala ambalo wataalamu wanasema linatofautiana na kuwa na nguvu za misuli. Wanasayansi wanaamini kuwa, sababu za kimazingira zinaathiri zaidi afya ya mtu na kiwango cha akili kuliko sababu za kurithi.

Saturday, December 12, 2009

Sumu Ndani ya Chakula au Food Poisoning...sehemu ya kwanza


Neno food poisoning ni ugonjwa unaosababishwa na ulaji na unywaji wa chakula kilichochafuliwa au kuguswa na aidha sumu za bacteria au vimelea vya maradhi na kumsababishia mtu maumivu ya tumbo (tumbo kukata) kuhara, kutapika n.k. Nnnaposema unywaji ninamanisha vinywaji kama vile maji, maji ya matunda, maziwa n.k. Kesi nyingi za kuchafuliwa huko kwa chakula zinatokana na ulaji wa vyakula vilivyochafuliwa na bacteria wengi wanaosababisha madhara, hata hivyo food poisoning inaweza pia kusababishwa na virusi, kemikali, mimea na samaki wenye sumu. Ni wazi kuwa, tumezungukwa na bacteria kila upande, kwa hiyo kutokea kwa baadhi ya kesi za uchafuzi wa chakula ni jambo la kawaida. Vimelea hao wanaotuzunguka wanapatikana pia kwenye chakula na wakati mwingine wanaweza kuwa wa manufaa kwetu. Hata hivyo bacteria wale ambao wako katika vitu vilivyooza na mabaki ya vyakula, si wazuri kwetu. Mtu aliye kula chakula kilichochafuliwa au kugusana na vijidudu maradhi hao, huwa na dalili kuu zifuatazo: kutapika, kuhara na maumivu ya tumbo(kitaalamu hujulikana kama stomach flu). Aidha dalili hizo mara nyingi huambatana na maumivu ya misuli, homa, kutetemeka mwili na kuihisi kuchoka. Hatua ya kuhara na kutapika mtu, husaidia mwili kuondoa mada zenye sumu au athari katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula (digestive tract) na hivyo kuzizuia sumu au vijidudu maradhi hivyo kuingia katika mfumo wa damu. Vyakula vinavyotokana na wanyama, vyakula vibichi na vile vya jamii ya mboga ambavyo havioshwi, vyote vinaweza kuwa na vidudu maradhi au Germs na kuchafua chakula au kusababisha food poisoning. Vyakula hivyo ni kama vile nyama, kuku, mayai maziwa na samaki aina ya kama wadogo. Bacteria kama vile Salmonela na Listeria ni miongoni mwa vimelea vinavyopatikana katika vyakula vilivyoharibika au kuoza.
Wakati mwingine inakuwa vigumu kueleza iwapo umekumbwa na hali hiyo baada ya kula chakula kilichoharibika. Sasa iwapo mtu atakuwa na mojawapo ya dalili hizo zilizotajwa, kama vile tumbo kukatakata, ni vyema awaulize watu wengine wa familia iwapo kuna wengine walio na dalili kama hiyo na kama wamekula chakula kama hicho alichokula yeye. Na iwapo kutakuwa hakuna yeyote mwenye dalili kama yake, basi kwa kiasi kikubwa huwenda akawa amepatwa na maradhi hayo. Wakatimwingine mtu huanza kujisikia mgonjwa katika muda wa masaa machache baada ya kula chakula kilichochafuliwa na sumu za bacteria au na vimelea vya maradhi. Dalili huanza kujitokeza kuanzia muda wa saa moja hadi matatu baada ya kula chakula kisichofaa. Na wakati mwingine mtu hawezi kujisikia mgonjwa, hadi kupita siku kadhaa baadaye. Na iwapo mtu atakuwa amekula chakula chenye kiasi kidogo cha sumu au toxin, muda wake wa kuuugua utakuwa mfupi na mara moja ataanza kujisikia vizuri. Katika hali kama hiyo mtu anapoona ana dalili hizo nilizozitaja, ni vyema amuone daktari mapema kwa ajili ya matibabu. Iwapo utakwenda kwa tabibu au daktari, atakuuliza masuali mengi kama vile unajisikiaje, umeanza kuumwa lini, ulikula nini hapo kabla na je kuna mtu yoyote wa karibu yako au unaemfahamu aliye na dalili kama zako? Nk. Aidha daktari anaweza kukuandikia vipimo vya haja kubwa na ndogo ili kuona kama vijidudu hivyo maradhi ndivyo vimesababisha hali hiyo iliyokusibu. Na iwapo utaona damu ndani ya kinyesi, unashauriwa kumuona daktari mara moja pasina na kuchelewa……. Makala hii inaendelea.

Thursday, December 10, 2009

Watu milioni 5 hufariki dunia kila mwaka kutokana na tumbaku



Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kwamba kila mwaka watu milioni 5 hufariki dunia kutokana na kutumia tumbaku, na kusisitiza kuwa hatua muhimu zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na uvutaji wa sigara. Tumbaku inaongoza duniani katika kusababisha magonjwa mbayo yanawezekana kuzuilika. Kuwa karibu na mazingira ya wanaovuta sigara au uvutaji sigara usio wa moja kwa moja (second hand smoking) pia kunasababisha vifo vya watoto 600,000 wanaozaliwa bila kufikia muda wao kila mwaka, huku karibu asilimia 95 ya watu duniani wanaishi katika sehemu ambazo hazina sheria zozote zakupiga marufuku ufutaji sigara. Mkurugenzi wa WHO anayeshughulikia marufuku ya tumbaku Douglas Bettcher amesema kwamba, watu wanapaswa kuelemishwa zaidi juu ya madhara ya tumbaku ambayo ni mabaya kwa afya ya binadamu. Maafisa wa afya wanatabiri kwamba, ifikao mwaka 2030, tumbaku inaweza kusabbaisha vifo vya watu milioni 8 kwa mwaka, hasa katika nchi zilizoendelea, iwapo hatua muhimu hazitochukuliwa ili kupambana na suala hilo.
….Wapenzi wadau wa blogi ya Kona ya Afya, leo wakati nikiandika habari hii nimekuwa nikifikiria ni kwa nini binadamu baadhi ya wakati tushindwe kujizuia kufanya masuala ambayo tunajua fika kuwa ni hatari kwa afya zetu?. Pengine tumesikia mara nyingi kuwa uvutaji sigara una madhara makubwa na tumeshashuhudia hata watu wa karibu yetu wakipata madhara hayo. Labda pia kwa kuwa uvutaji sigara ni suala la kawaida katika nyumba zetu, ofisi zetu, majumba ya starehe, katika mitaa yetu na kote kulikotuzunguka basi tumelizoea suala hilo na kuliona ni la kawaida. Lakini ukweli usiopingika ni kwamba, ufutaji sigara una madhara, sio tu kwa wavutaji sigara peke yao, bali hata kwa sisi tulio karibu ya wavutaji hao. Nafikiri muda umewadia sasa wa kujiuliza kwa undani swali hili kuwa: Je? kama kuna magonjwa yenye madhara kwa afya na uzima wa miili yetu ambayo yanaweza kuepukika, basi kwa nini tusijiepushe nayo!??
Daima tuzitunze afya zetu!

Wednesday, December 9, 2009

Kunywa kawaha kunaweza kupunguza hatari ya kupatwa na kensa ya korodani


Utafiti uliofanywa nchini Marekani umeonyesha kuwa, kunywa kahawa kunaweza kusaidia kupunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kensa ya korodani au prostate cancer.
Uchunguzi huo umeonyesha kwamba, wanaume wanaokunywa kahawa kwa wingi, hunguza hatari hiyo kwa asilimia 60 ikilinganishwa na wanaume ambao hawanywi kahawa kabisa. Kahawa inaathiri jinsi ambavyo mwili unayeyusha sukari, pamoja na kiasi cha homoni za jinsia, masuala ambayo yanahusiana moja kwa moja na kensa ya korodani. Watalamu hao wamesema kuwa, kampaundi za kibayolojia zilizoko katika kahawa zinazuia tishu kuharibika na hivyo kupunguza uwezekano wa kensa ya korodani kukua.
Inafaa kufahamu kwamba, kensa ya korodani ni kensa ya pili inayowapata kwa wingi wanaume duniani na kusababisha vifo. Kati ya wanaume 6 mmoja kati yao hupatwa na saratani ya korodani.

Monday, December 7, 2009

Usafi na Utunzaji wa meno ya watoto…sehemu ya 2



Wapenzi wadau na leo tunaendelea kujadili usafi wa meno ya watoto. Imeelezwa kuwa kwa watoto wadogo yaani wale wa chekechea, wazazi wanashauriwa kutumia kiwango kidogo cha dawa ya meno yaani dawa hiyo iwekwe kwenye shashi au kitambaa na wasafishe meno ya watoto wao kwa utaratibu. Na ikiwa meno yote ya mbele ya mtoto wako yameota, unashauriwa kutumia mswaki mdogo wa watoto. Njia nyepesi ya kumsafisha mtoto ni kuhakikisha kuwa kichwa chake kimejiegemeza kwenye mapaja yako, ili uweze kuona vyema ndani ya kinywa chake na kuyasafisha kama inavyotakikana, huku mtoto akiwa katika hali ya utulivu. Na iwapo mtoto atakuwa mkubwa kuanzia miaka saba anaweza kusimama mkabala na mzazi wake huku ukikiinua kichwa chake ili kuweza kufikia na kuona vizuri meno yote. Mara nyingine wazazi wamekuwa akishuhudia watoto wao wakitokwa na damu kwenye fizi wakati wakipigwa mswaki. Jambo hili lisiwazuie wazazi kuwasafisha meno watoto wao. Kuvuja damu fizi ni ishara ya kuathiriwa na maradhi. Kwa hiyo uvujaji huo wa damu utatokomea iwapo utando unaong'ang'ania kwenye meno na bacteria au vijidudu maradhi vitaondolewa.
Kwa kuzingatia kuzagaa aina mbalimbali za dawa za kusafisha meno (au tooth paste) katika maduka mbalimbali hivi sasa, wazazi wanakabiliwa na hali ngumu katika kuchagua dawa ipi ni bora kwa usafi na utunzaji wa meno ya watoto. Lililo umuhimu hapa ni kufahamu kiasi kinachotakikana kutumika katika mswaki wa mtoto wako na si aina ya dawa. Kiasi kidogo tu cha dawa ya meno kinatakikana kwa mtoto wako na si kurundika lundo la dawa, hiyo haina faada yoyote ghairi ya kumletea madhara. Dawa ya meno haipaswi kumezwa. Hatua ya kumeza au kula kiasi kikubwa cha dawa ya kusafishia meno inazidisha hatari ya kuoza meno ya muda ya watoto yaani (permanent teeth) khususan kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano. Kwa sababu hiyo wataalamu wa meno hawashauri kutumia dawa za kusukutulia kinywa yenye kampaundi ya fluoride kwa watoto chini ya miaka sita, kwa sababu hawawezi kujizuia kumeza na hivyo huwa na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na maradhi ya fluorosis.
Je mnafahamu kuwa chakula kina athari kubwa katika afya ya kinywa na meno ya mtoto wako? Uchaguzi wa vyakula na mipangilio ya ulaji tangu kipindi cha utotoni huweza kuwa na taathira kwa afya ya uhai wa maisha yako yote. Mlo kamili unaojumuisha vyakula vya aina tatu kwa siku (Yaani protini,vitamini na wanga ) unapaswa kushajiishwa. Hatua ya kujumuisha mada za protini katika milo hiyo husaidia watoto kutohisi njaa haraka, na hivyo kumfanya mtoto kukosa hamu ya kukimbilia kula vyakula visivyo na manufaa kama vile vyenye sukari nyingi. Wataalamu wa meno wa watoto wanasema kuwa miendo bora ya ulaji chakula pamoja na usafi wa kinywa unaotakikana si tu kuwa humuepusha mtoto kuoza na kuharibika kwa meno yake, bali pia humfanya mtoto kimwili kuwa katika afya njema.

Watoto wanaozaliwa na uzito mdogo hubaleghe mapema


Kuna ushahidi kuwa watoto wanaozaliwa na uzito mdogo, hufikia baleghe mapema. Jarida la ripoti za lishe za Marekani limearifu kwamba, kuongezeka kwa haraka uzito wa mtoto katika umri wa miaka miwili ya mwanzo, pia kunapeleka kubaleghe mapema mtoto huyo. Kubaleghe mapema pia kumekuwa kukihusishwa na ongezeko la hatari ya kupatwa na kensa za matiti na korodani. Hii si mara ya kwanza utafiti kuonyesha kwamba uzito mdogo wakati wa kuzaliwa unaweza kusababishwa mtoto kukua mapema. Wataalamu wanasema kuwa, kueleweka vyema sababu zinazotokea mapema katika maisha na kupelekea hatari ya kupatwa mtu ugonjwa wa kensa, kunaweza kusaidia katika kuchukuliwa stratejia za kuzuia ugonjwa huo mapema.
Miongoni mwa sababu zinazosababisha mtoto kuzaliwa akiwa na umri mdogo ni:
• Matatizo ya fuko la uzazi
• Rubella
• Mama kuwa na ugonjwa wa Ukimwi
• Mama kutumia pombe kwa wingi wakati wa ujauzito
• Mama kuvuta sigara wakati wa ujauzito
• Mama mjamzito kuwa na magonjwa sugu
• Shinikizo la damu wakati wa ujauzito
• Mama mjamzito kukosa lishe bora
• Mama mjamzito kutumia madawa ya kulevya
• Kuwepo maji mengi kwenye fuko la uzazi.
• Mama mjamzito kuwa na kifafa cha mimba (Preeclampsia)
• Fuko la uzazi kuvunjika kabla ya muda wake
• Mama mjamzito kuwa na magonjwa ya mfumo wa mkojo (U.T.I)
• Matatizo ya urithi
• Mama mjamzito kuwa na matatizo ya figo

Sunday, December 6, 2009

Kuvuta sigara mara baada ya kuama kunaongeza hatari ya kensa ya mapafu


Wanaovuta sigara mara tu baada ya kuamka asubuhi, husababishwa kiwango cha juu cha nikotini kukusanyika katika damu zao, zaidi ya wale wanaofuta sigara baadaye, suala ambalo huwafanya wakabiliwe na hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kensa ya mapafu. Kuvuta sigara baada ya kupata kifungua kinywa, huunguza kiwango hicho cha nikotini katika damu. Uchunguzi umeonyesha kwamba, wafutaji sigara wa mapema asubuhi, huongeza kiwango kikubwa cha nikotini katika damu zao, bila kuzingatia kwamba wanavuta sigara ngapi kwa siku. Uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Tiba cha Penn State umeshauri kwamba, wanaovuta sigara mapema asubuhi wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kupata kensa ya mapafu, hivyo ni bora wasaidiwe kuacha kuvuta sigara. Ingawa sababu inayopelekea kiwango cha nikotini kiwe juu zaidi kwa wafuta sigara kabla ya kula stahtahi haijafahamika, lakini inaonekana kuwa wale wanaovuta sigara kabla ya kula kitu wamebobea zaidi katika uvutaji, ikilinganiswa na wale wanaosubiri na kuvuta sigara baadaye.
Inafaa kujua kuwa: Uvutaji sigara unasababisha kwa asilimia 90 vifo vinavyotokana na kensa ya mapafu. Idadi ya watu wanaopatwa na kensa ya mapafu inaongezeka kila siku duniani na kuzidisha vifo vinavyotokana na saratani nyinginezo.
Kwa kawaida kensa ya mapafu huwapata watu wanapokuwa na umri wa miaka 45, na wakati mtu anapopimwa na kukutwa na ugonjwa huo kwa kawaida huwa tayari umeshasambaa mwilini mwake. Saratani ya mapafu inahusiana moja kwa moja na uvutaji sigara. Hatari ya kupatwa na kensa ya mapafu inaambatana moja kwa moja na idadi ya sigara mtu anazovuta.

Kutumia simu ya mkono, hakuna uhusiano wowote na saratani ya ubongo


Japokuwa kumekuwa na imani kwamba kutumia simu ya mkono kwa muda mrefu kunaongeza hatari ya kupatwa na kensa ya ubongo, lakini utafiti mpya umekanusha madai hayo. Huko nyuma uchunguzi ulionyesha kwamba kukaririwa sumaku umeme za redio zinazotoka katika simu za mkono, kunasababisha hatari kubwa ya kupatwa na kensa. Lakini kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa katika Jarida la Taasisi ya Kensa, hakujakuwa na mabadiliko yoyote kuhusiana na ugonjwa wa kensa ya ubongo tangu simu za mkono zilizpogunduliwa katika muongo wa 1990.
Wataalamu wanasema kwamba, kuna ushahidi wa kisayansi unaosema kuwa, kutumia simu za mkono kwa miaka isiyozidi 10 hakuongezi uwezekano wa kupatwa na saratani, na utafiti huo unaunga mkono suala hilo. Hata hivyo wataalamu wameshauri kuwa, uchunguzi na ufuatiliaji wa muda mrefu unatakiwa kufanywa, kwani uvimbe wa ubongo kwa kawaida unachukua muda mrefu sana hadi unapotokea.
Si vibaya kujua kuwa, utafiti huo umetolewa baada ya kuchunguzwa kesi 59,684 za kensa ya ubongo zilizookea katika miaka 30 tangu mwaka 1974 hadi 2003 kati ya watu wazima milioni 16.

Saturday, December 5, 2009

Usafi na Utunzaji wa Meno ya Watoto ....sehemu ya kwanza


Utunzaji wa meno ya watoto unahitaji uangalizi mkubwa kama ilivyo kwa watu wazima, na upuuzaji wa suala hilo unaweza kuwa na madhara ya muda mrefu maishani. Hii ndio maana madaktari wa meno wanashauri kuwa, ni vyema meno ya watoto yakaanza kusafishwa tangu pale linapochomoza au kuota jino la awali kinywani na ikiwezekana hata kabla ya hapo. Baadhi ya wataalamu wanashauri wazazi kutumia kitambaa na maji safi kusafishia meno ya mtoto, huku akiwa ameketi katika hali ya utulivu. Itafahamika kuwa bacteria au vijidudu maradhi huishi kwenye sehemu ile ya jino iliyofunikwa na utando wa vyakula uliong'ang'ania kwenye jino. Bacteria hao hukutana na chakula na kusababisha asidi na hatimaye hutengeneza tundu au mmomonyoko katika meno. Utando huo unapaswa kuondolewa kila siku wakati unapopiga mswaki ili kuhakikisha kuwa meno na fizi zako ni safi na salama. Wazazi wanapaswa kuzingatia usafi wao wa kinywa pamoja na wa watoto wao. Vijidudu hivyo maradhi vinapatikana ndani ya mate na kwa hivyo ni rahisi kuenezwa kutoka kwa mzazi hadi kwa moto wakati wa kubusiana au kushumiana na kupitia uchangiaji wa vyombo vya chakula. Wazazi au walezi wanapaswa kubeba jukumu la kusimamia afya ya vinywa cha watoto wao hadi hapo watakapofikia umri wa kati ya mia minane au tisa. Kwani wataalamu wanasema kuwa katika kipindi hicho, watoto huwa hawana uwezo wa kujisimamia katika kuboresha usafi wa meno unaotakikana. Mtoto anaweza kuanza kusafisha meno yake kwa kutumia mswaki vile inavyotakikana chini ya usimamizi wa wazazi au walezi akiwa na umri wa miaka saba.
Usafi wa kinywa na meno unapaswa kuanzishwa hata kabla ya mtoto hajaanza kuota meno. Fizi za watoto wachanga na wale wa chekechekea zinaweza kusafishwa kwa kufutwa kwa utaratibu kwa kutumia shashi au gauze, au hata kitambaa kisafi chenye unyevunyevu. Kitendo hicho huchangamsha pia fizi za mtoto na kusaidia kupunguza baadhi ya maumivu ambayo huwapata watoto wakianza kuota meno. Madaktari wa meno wanasema kuwa, mara meno ya mtoto yanapochomoza, yanapaswa kusafishwa kwa mpangilio angalau mara mbili kwa siku, baada ya kifungua kinywa na kabla ya kulala, yaani usiku, bila ya kusahau ulimi.

Thursday, December 3, 2009

Dalili za mshituko wa moyo… sehemu ya mwisho


Leo tutazungumzia dalili za mshitiko wa moyo na hivyo kukamilisha mada ya mshituko wa moyo.
Baadhi ya wakati mshituko wa moyo hutokea kwa dalili zilizo wazi na kwa haraka sana. Lakini mara nyingi mshituko wa moyo hutekea polepole huku mtu akipata mauvimu ya wastani na kutokujisikia vyema. Mara nyingi watu wanaopatwa na hali kama hiyo huwa hawana uhakika na kile kinachotokea na husubiri kwa muda mrefu kabla ya kuomba msaada au kumuona daktari. Zifuatazo ni dalili ambazo hutekea pale mtu anapopatwa na mshituko wa moyo.
• Maumivu katika kifua: Mara nyingi mtu anapopatwa na mshituko wa moyo huhisi maumivu sehemu za kifua hasa sehemu za katikati ya kifua ambayo huweza kuisha baada ya dakika kadhaa au mara nyingine maumivu hayo huisha na kurudia tena. Mtu huhisi kana kwamba kifua kinabana, kimejaa na kinauma.
• Maumivu katika sehemu za juu za kiwiliwili: Mtu anaweza akajihisi maumivu sehemu za mikono, mgongo, shingo, taya na tumbo.
• Kukosa pumzi au kushindwa kupumua: Hali hii huweza kutokea ikichanganyika na maumivu ya kifua au bila maumivu hayo.
• Dalili nyinginezo: Dalili nyinginezo ni pamoja na kutoka kijacho chembemba (cha baridi), kujisikia kichefuchefu pamoja, kichwa kuwa chepesi na kizunguzungu.
• Moyo kwenda mbio. Kuhisi mapigo ya moyo yanapiga zaidi kuliko kawaida.
Unashauriwa iwapo utajiskia mumivu ya kifua, hasa pamoja na mchanganyiko wa moja wa dalili tilizotaja hapo huu, usisubiri zaidi ya dakika na haraka mpigie simu daktari au wasiliana na kituo cha afya ili upatiwe msaada. Au haraka elekea hospitali mwenyewe. Muda unaofaa wa kutibiwa mshituko wa moyo ni saa moja tangu wakati hali hiyo ilipotokea. Kutibiwa mapema dalili za mshituko wa myo hupunguza hatari ya kuharibika seli za moyo. Hata kama huna uhakika dalili unazohisi ni za mshituko wa moyo, ni bora umuone daktari na ufanyiwe uchunguzi.
Utafiti waliofanyiwa wanawake 515 ambao walipata mshituko wa moyo umeonyesha kuwa, wengi wao waliripotiwa kuwa na dalili za kujihisi kuchoka, kutokulala vyema, kushindwa kupumua, kujisikia maumivu baada ya kula na wasiwasi. Asilimia 70 ya wanawake hao walihisi dalili zisizopungua moja kabla ya kupatwa na mshituko wa moyo.