Monday, December 7, 2009

Usafi na Utunzaji wa meno ya watoto…sehemu ya 2



Wapenzi wadau na leo tunaendelea kujadili usafi wa meno ya watoto. Imeelezwa kuwa kwa watoto wadogo yaani wale wa chekechea, wazazi wanashauriwa kutumia kiwango kidogo cha dawa ya meno yaani dawa hiyo iwekwe kwenye shashi au kitambaa na wasafishe meno ya watoto wao kwa utaratibu. Na ikiwa meno yote ya mbele ya mtoto wako yameota, unashauriwa kutumia mswaki mdogo wa watoto. Njia nyepesi ya kumsafisha mtoto ni kuhakikisha kuwa kichwa chake kimejiegemeza kwenye mapaja yako, ili uweze kuona vyema ndani ya kinywa chake na kuyasafisha kama inavyotakikana, huku mtoto akiwa katika hali ya utulivu. Na iwapo mtoto atakuwa mkubwa kuanzia miaka saba anaweza kusimama mkabala na mzazi wake huku ukikiinua kichwa chake ili kuweza kufikia na kuona vizuri meno yote. Mara nyingine wazazi wamekuwa akishuhudia watoto wao wakitokwa na damu kwenye fizi wakati wakipigwa mswaki. Jambo hili lisiwazuie wazazi kuwasafisha meno watoto wao. Kuvuja damu fizi ni ishara ya kuathiriwa na maradhi. Kwa hiyo uvujaji huo wa damu utatokomea iwapo utando unaong'ang'ania kwenye meno na bacteria au vijidudu maradhi vitaondolewa.
Kwa kuzingatia kuzagaa aina mbalimbali za dawa za kusafisha meno (au tooth paste) katika maduka mbalimbali hivi sasa, wazazi wanakabiliwa na hali ngumu katika kuchagua dawa ipi ni bora kwa usafi na utunzaji wa meno ya watoto. Lililo umuhimu hapa ni kufahamu kiasi kinachotakikana kutumika katika mswaki wa mtoto wako na si aina ya dawa. Kiasi kidogo tu cha dawa ya meno kinatakikana kwa mtoto wako na si kurundika lundo la dawa, hiyo haina faada yoyote ghairi ya kumletea madhara. Dawa ya meno haipaswi kumezwa. Hatua ya kumeza au kula kiasi kikubwa cha dawa ya kusafishia meno inazidisha hatari ya kuoza meno ya muda ya watoto yaani (permanent teeth) khususan kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano. Kwa sababu hiyo wataalamu wa meno hawashauri kutumia dawa za kusukutulia kinywa yenye kampaundi ya fluoride kwa watoto chini ya miaka sita, kwa sababu hawawezi kujizuia kumeza na hivyo huwa na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na maradhi ya fluorosis.
Je mnafahamu kuwa chakula kina athari kubwa katika afya ya kinywa na meno ya mtoto wako? Uchaguzi wa vyakula na mipangilio ya ulaji tangu kipindi cha utotoni huweza kuwa na taathira kwa afya ya uhai wa maisha yako yote. Mlo kamili unaojumuisha vyakula vya aina tatu kwa siku (Yaani protini,vitamini na wanga ) unapaswa kushajiishwa. Hatua ya kujumuisha mada za protini katika milo hiyo husaidia watoto kutohisi njaa haraka, na hivyo kumfanya mtoto kukosa hamu ya kukimbilia kula vyakula visivyo na manufaa kama vile vyenye sukari nyingi. Wataalamu wa meno wa watoto wanasema kuwa miendo bora ya ulaji chakula pamoja na usafi wa kinywa unaotakikana si tu kuwa humuepusha mtoto kuoza na kuharibika kwa meno yake, bali pia humfanya mtoto kimwili kuwa katika afya njema.

No comments: