Friday, December 18, 2009

Mmh!... watafiti wasema ukoma unaweza ukawa ugonjwa wa kumbukiza!


Watafiti wamegundua geni ambazo zinahusiana na ugonjwa wa ukoma, suala ambalo linaondoa fikra ya huko nyuma kwamba ukoma si ugonjwa wa kuzaliwa au wa kuridhi. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa huko China na kuchafishwa katika Jarida la Tiba la Uingereza, mabadiliko ya geni 7 mwilini yanaweza kuwa ndio chanzo cha uwezekano wa baadhi ya watu kupatwa na ukoma. Wataalamu hao wamesema kuwa, tangu kale imekuwa ikifikiriwa kuwa ukoma ulikuwa ukisababishwa tu na vijidudu lakini uchunguzi wao umeonyesha kuwa maambukizo ya ugonjwa huo yansababishwa pia na genetiki. Wamesema kwamba, iwapo mzazi ana ugonjwa huo, basi kuna uwezekano mkubwa mwanaye naye akapatwa na ugonjwa huo. Hata hivyo wataalamu hao wamesema, cha kushangaza ni kuwa, iwapo mmoja kati ya mke na mume wana ukoma, mwingine hawezi kuambukizwa ugonjwa huo kwa miaka mingi. Geni 5 kati ya hizo 7 zinazosababisha ugonjwa huo, inaaminiwa kuwa zinauhusiano wa karibu na mfumo wa kulinda mwili.
Uchunguzi huo unaleta matumaini ya kuweza kukingwa mapema wale wanaodhaniwa kuwa wana uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huo. Vilevile utafiti huo unaweza kutumika kuchunguza zaidi vijidudu vya magonjwa mengine ambavyo vinakaribiana na vijidudu vinayosababisha ukoma, kama vile vijidudu vya kufua kikuu ugonjwa ambao husababisha vifo vya watu milioni 1.8 duniani.
Sio vibaya kujua kuwa, ugonjwa wa ukoma au Leprosy kwa kiingereza na kitaalamu Hansen's disease, unaosabaishwa na bacteria waitwao Mycobacterium Lapracea na Mycobacterium Lepromatosis huathiri ngozi, utando telezi (mucous membranes), neva za ukingoni (peripheral nerve) pamoja na macho.
Kuharibika daima neva au mishipa ya fahamu kunakosababishwa na ugonjwa wa ukoma, humzuia mtu anayepona ugonjwa huo kuhisi maumivu, suala ambalo huwafanya wagonjwa wa ukoma kuwa wenye kupata kwa urahisi majeraha madogo madogo na vidonda ambayo baadaye huwa makovu ya kudumu.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa, kuna kesi 254,525 mpya za ugonjwa wa ukoma katika nchi za tropiki na zilizo chini ya jangwa la sahara.
Kumbuka kuwa ugonjwa wa ukoma unatibika na unapotibiwa mapema huweza kumuepusha mgonjwa kupata madhara makubwa ya kukatika viungo na kuwa mkoma!

No comments: