Monday, December 21, 2009

Ujuwe ugonjwa wa Kifua Kikuu au TB ....sehemu ya kwanzaKaribuni wapenzi wadau wa Kona ya Afya katika mfululizo mwingine wa
kujadili magonjwa mbalimbali. Leo tumepata fursa ya kuzungumzia ugonjwa wa kifua kikuu, ambacho maambukizo yake yanaongezeka kwa kasi kubwa ulimwenguni, khususan katika nchi zinazoendelea. Kwa kuzingatia kuwa ugonjwa wa kifua kikuu huathiri watu wa rika zote na hasa vijana kati ya miaka 15 hadi 45 ambayo ndiyo nguvu kazi katika nchi nyingi za dunia, kunapaswa kufanyika jitihada kubwa za kudhibiti maambukizo ya ugonjwa huo. Kifua Kikuu ambao kitaalamu hujulikana kama Tuberculosis ni ugonjwa wa kuambukiza ambao huenezwa kwa njia ya hewa. Kifua kikuu husababishwa na bacteria au kimelea aina ya Mycobacterium tuberculosis au (tubercle bacterium). Ugonjwa huu kwa kawaida huathiri mapafu, lakini pia huweza kushambulia viuongo vingine vya mwili kama vile tezi za limfu, ubongo na mifupa.
Tb inambukizwa kwa namna gani? :
Mtu mwenye kifua kikuu au Tb ambaye hajatibiwa, anapokohoa, kupiga chafya, kutema mate au makozi husambaza bacteria au vimelea hivyo vya ugonwja huo hewani. Kwa hivyo mtu mwingine akivuta hewa yenye vimelea hivyo anaweza kuambukizwa kifua kikuu. Kwa mfano takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa nchini Tanzania ugonjwa wa Kifua Kikuu umekuwa ukiongezeka kwa kasi kubwa ambapo watu elfu 65,000 hivi sasa wanaugua kifua kikuu nchini humo. Kati yao asilimia 50 pia wana ukimwi. Hapa linajitokeza swali kwamba dalili za Kifua Kikuu ni zipi?
Mtu ambaye amepatwa na ugonjwa wa Tb au Kifua Kikuu huwa na dalili au husumbuliwa na hali zifuatazo:
Kukohoa kwa muda usiopungua wiki mbili na mara nyingine kukohoa damu, homa za jioni za mara kwa mara, kutokwa na jasho usiku, kukosa hamu ya kula, kupungua uzito kwa kiasi kikubwa na kadhalika.
Kundi ambalo liko kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa Tb au kifua kikuu ni la wale wanaoishi kwa karibu na kwa muda mrefu na mtu yule aliyekwisha ambukizwa ugonjwa huo. Kwa hiyo hapa nitaorodhesha makundi ambayo yako kwenye hatari na ya uwezekano mkubwa wa kuambukizwa Tb iwapo watakuwa karibu na mgonjwa. Watu hawa ni rahisi kupatwa na kifua kikuu kwa sababu kinga zao za mwili huwa ni za kiwango chini: Watoto wadogo na wazee, wale wote wanaougua kisukari, watu wnaotumia dawa aina ya steroids au dawa nyinginezo zinazoathiri mfumo wa kinga ya mwili, waathirika wa ukimwi na HIV, wale wote wanaoishi maeneo yenye msongamano mkubwa watu yaliyoduni kiafya, wanaoishi kwenye sehemu zisizokuwa na hewa ya kutosha, watu wanaotumia dawa mbalimbali, au pombe na mwisho wale wenye lishe duni.
Usikuko muendelezo wa makala hii, na daima linda afya yako.

No comments: