Sunday, December 20, 2009

Njia za kuondoa makovu


Kuna matatizo malimbali ya ngozi yanayoweza kuwapata watu ambapo makovu ni mojawapo ya matatizo hayo.Makovu baadhi ya wakati hajawezi kuepukika hasa iwapo makovu hayo yamesababishwa na magonjwa au ajali mbalimbali. Makovu katika sehemu mbalimbali za mwili huweza kufunikwa na kufichwa kwa urahisi iwapo hayapo katika sehemu zinazoonekena. Lakini iwapo makovu yatakuwa usoni, mikononi au kifuani, huwa si rahisi kuyaficha na mara nyingi huwakera wale walio na makovu. Watu wengi wangependa kujua ni njia gani ambazo mtu anaweza kutumia ili kuondoa makovu. Ili kulijibu swali hilo ni bora kwanza tujue kovu ni nini hasa. Kovu katika mwili hutokea pale tishu aina ya fibrous inapojikusanya juu ya ngozi ili kusaidia kukarabati seli na ngozi iliyoharibika. Wakati kunapotokea jeraha, ngozi kutoa seli ziitwazo fibroblasts ambazo hutoa kitu kiitwacho collagen na kujaza sehemu yenye jeraha. Collagen ni ngumu, iko kama ufumwele unaopatikana katika protini ambayo hujaza eneo lote le kovu. Collagen ipo pia katika ngozi ya kawaida lakini katika kovu huwa nyingi na iliyojipanga katika mpangilio holela. Hii ndio sababu kovu huwa na rangi iliyokolea na huonekana kwa urahisi. Baadhi ya makovu huondoka kwa urahisi, baadhi huchukua miezi na hata miaka, huku makovu mengine yakibadilika polepole rangi na muonekano wake. Kovu huenekana kirahisi juu ya ngozi kwa sababu seli zilizotumika kuunda kovu hutofautiana na seli za mwanzo za ngozi. Kwa mfano makovu yaliyo juu ya ngozi hayawezi kuota vinyeleo kwa kuwa seli zake hazina matundu ya vinyeleo. Pia makovu hayana uwezo wa kuzuia miale ya jua. Kwa bahati mbaya ni vigumu kidogo kuweza kuondoa baadhi ya makovu moja kwa moja katika ngozi. Ingawa kuna njia kama vile vipodozi vinavyoweza kuziba makofu na njia nyinginezo za kitiba, lakina hata hivyo njia zote hizo mara nyingi huwa haziwezi kuondoa baadhi ya makovu kabisa, hasa yale makovu yaliozama katika ngozi na kuharibu kwa ngozi kwa kiasi kikubwa. Njia za tiba zinazoweza kutumiwa kuondoa makovu ni kama vile operesheni ya Laser (laser sugery), sindano za steroid, kubandua ngozi ya juu (dermabrasion) na radio therapy.
Lakini hata hivyo kuna njia mbalimbali za tiba asilia ambazo zinaaminika kuweza kusaidia kuondosha makovu. Njia hizo ni kama
1. Majani ya Aloe Vera. Majani haya yanapatikana kila sehemu hasa kwetu Tanzania na kwingineko Afrika. Majani hayo pia ni dawa nzuri ya kutibu magonjwa mbalimbali ya ngozi kama vile kiba au kishilingi. Kata majani hayo na utumie utomvu wake kupaka katika makovu. Baada ya muda polepole itapunguza na kuondoa makovu. Aleo Vera ni majani ambayo yanasifika hivi sasa ulimwenguni kote kwa ajili ya ngozi na yanatumiwa katika vipondozi mbalimbali. Basi zaidi ya kukuondoa makovu, yatasaidia pia kuifanya ngozi yako iwe nyororo.
2. Njia nyingine ni kutumia tango. Twanga tango na tumia mchanganyiko wake kupaka juu ya kovu. Husaidia kulainisha makovu na unapotumia kwa muda mrefu huondoa makovu pia.
3. Kupaka asali juu ya kovu na kuiacha usiku kucha. Njia hii inaweza kurudiwa mara kwa mara hadi pale kovu litakapotoweka.
4. Kula vyakula vyenye vitamin E, ambavyo ni ni muhimu katika kusaidia ngozi kupona na kurudia katika hali yake ya kawaida. Vitamin E iko katika mayai, nyungu za aina mbalimbali kama karanga, mayai, mafuta ya nafaka na vinginevyo. Kama huwezi jitahidi utumie vidonge vya vitamin E lakini baada ya kupata ushauri wa daktari.
5. Kupaka baking soda kidogo na maji sehemu yenye kovu na kuikanda sehemu hiyo kwa dakika moja. Mara mbili kwa siku. Kisha safisha kwa maji ya vuguvugu halafu paka mafuta ya zaituni.
6. Kutumia cream zenye vitamini E nad C na upake moja kwa moja katika kovu. Husaidia ngozi kuota tena katika kovu. Unaweza kumuona mtaalamu wa magonjwa ya ngozi naye akakushauri ni cream gani utumie ili kuondoa makovu yako. Pia jitahidi kupata lishe nzuri bila kusahau matunda na mboga mboga ambayo ni muhimu kwa ajili ya afya ya ngozi. Kunywa maji ya kutosha kwani maji pia kulainisha ngozi yako na kufanya makovu kutoka kwa urahisi.

Inafaa kujua kuwa baadhi ya makovu kama vile yaliyosababishwa na kuungua au kuchanjwa ni vigumu kuyaondoa kwa kutumia njia hizo zilizotajwa.

1 comment:

Anonymous said...

Ni aina gani ya asali inayotumika,maana kuna asali mbichi na zingine sio mbichi.