Saturday, December 5, 2009

Usafi na Utunzaji wa Meno ya Watoto ....sehemu ya kwanza


Utunzaji wa meno ya watoto unahitaji uangalizi mkubwa kama ilivyo kwa watu wazima, na upuuzaji wa suala hilo unaweza kuwa na madhara ya muda mrefu maishani. Hii ndio maana madaktari wa meno wanashauri kuwa, ni vyema meno ya watoto yakaanza kusafishwa tangu pale linapochomoza au kuota jino la awali kinywani na ikiwezekana hata kabla ya hapo. Baadhi ya wataalamu wanashauri wazazi kutumia kitambaa na maji safi kusafishia meno ya mtoto, huku akiwa ameketi katika hali ya utulivu. Itafahamika kuwa bacteria au vijidudu maradhi huishi kwenye sehemu ile ya jino iliyofunikwa na utando wa vyakula uliong'ang'ania kwenye jino. Bacteria hao hukutana na chakula na kusababisha asidi na hatimaye hutengeneza tundu au mmomonyoko katika meno. Utando huo unapaswa kuondolewa kila siku wakati unapopiga mswaki ili kuhakikisha kuwa meno na fizi zako ni safi na salama. Wazazi wanapaswa kuzingatia usafi wao wa kinywa pamoja na wa watoto wao. Vijidudu hivyo maradhi vinapatikana ndani ya mate na kwa hivyo ni rahisi kuenezwa kutoka kwa mzazi hadi kwa moto wakati wa kubusiana au kushumiana na kupitia uchangiaji wa vyombo vya chakula. Wazazi au walezi wanapaswa kubeba jukumu la kusimamia afya ya vinywa cha watoto wao hadi hapo watakapofikia umri wa kati ya mia minane au tisa. Kwani wataalamu wanasema kuwa katika kipindi hicho, watoto huwa hawana uwezo wa kujisimamia katika kuboresha usafi wa meno unaotakikana. Mtoto anaweza kuanza kusafisha meno yake kwa kutumia mswaki vile inavyotakikana chini ya usimamizi wa wazazi au walezi akiwa na umri wa miaka saba.
Usafi wa kinywa na meno unapaswa kuanzishwa hata kabla ya mtoto hajaanza kuota meno. Fizi za watoto wachanga na wale wa chekechekea zinaweza kusafishwa kwa kufutwa kwa utaratibu kwa kutumia shashi au gauze, au hata kitambaa kisafi chenye unyevunyevu. Kitendo hicho huchangamsha pia fizi za mtoto na kusaidia kupunguza baadhi ya maumivu ambayo huwapata watoto wakianza kuota meno. Madaktari wa meno wanasema kuwa, mara meno ya mtoto yanapochomoza, yanapaswa kusafishwa kwa mpangilio angalau mara mbili kwa siku, baada ya kifungua kinywa na kabla ya kulala, yaani usiku, bila ya kusahau ulimi.

No comments: