Saturday, December 26, 2009

Kujiingiza katika mapenzi kwenye umri mdogo husababisha kensa ya mlango wa kizazi


Huko nyuma iliaminiwa kuwa, virusi aina ya papiloma au (HPV) pamoja na vipimo duni ndio sababu kuu inayopelekea ugonjwa wa kensa ya mlango wa kizazi, lakini uchunguzi mpya umeonyesha kuwa kuna sababu nyinginezo muhimu zinzosababisha ugonjwa huo. Kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa katika jarida la Kensa la Uingereza, mahusiano ya kijinsia yanayofanywa katika umri mdogo huongeza uwezekano wa kupata kensa ya mlango wa kizazi mara dufu. Suala jingine lililohesabiwa kuchangia maambukizo hayo, ni muda mwanamke anapopata mtoto wake wa kwanza.
Katika uchunguzi huo, imeonekana kuwa wanawake wanaoishi maisha ya kimasikini, huanza kujiingiza katika masuala ya kimapenzi miaka minne mapema kuliko wengineo. Hivyo kuna uwezekano wa kupata maambukizo ya virusi vya HPV mapema zaidi, na hivyo kuvipa muda zaidi virusi hivyo kuzaliana kwa muda mrefu na baadaye kusababisha kensa ya kizazi. Wanasayansi waliofanya uchunguzi huo wamependekeza kwamba ni bora chanjo dhidi ya virusi vya HVP itolewe mapema, hasa kwa wasichana wanaoishi katika jamii masikini, ili kuwakinga na ugonjwa wa kensa ya mlango wa kizazi.
Inafaa kujua kuwa, kensa ya mlango wa kizazi au kwa kimombo cervical cancer, ni saratani inayoshambulie lango la uzazi, sehemu ya chini kabisa na nyembamba ya kizazi. Ugonjwa huo unaweza kugunduliwa kirahisi kwa kufanya kipimo cha Pap smear. Ni muhimu kufahamu kwamba ugonjwa wa kensa ya kizazi ni ugonjwa hatari lakini unaweza kuzuiwa na kutibiwa kwa urahisi. Naahidi kuelezea kwa undani juu ya ugonjwa huo hapo baadaye.

No comments: