Saturday, December 12, 2009

Sumu Ndani ya Chakula au Food Poisoning...sehemu ya kwanza


Neno food poisoning ni ugonjwa unaosababishwa na ulaji na unywaji wa chakula kilichochafuliwa au kuguswa na aidha sumu za bacteria au vimelea vya maradhi na kumsababishia mtu maumivu ya tumbo (tumbo kukata) kuhara, kutapika n.k. Nnnaposema unywaji ninamanisha vinywaji kama vile maji, maji ya matunda, maziwa n.k. Kesi nyingi za kuchafuliwa huko kwa chakula zinatokana na ulaji wa vyakula vilivyochafuliwa na bacteria wengi wanaosababisha madhara, hata hivyo food poisoning inaweza pia kusababishwa na virusi, kemikali, mimea na samaki wenye sumu. Ni wazi kuwa, tumezungukwa na bacteria kila upande, kwa hiyo kutokea kwa baadhi ya kesi za uchafuzi wa chakula ni jambo la kawaida. Vimelea hao wanaotuzunguka wanapatikana pia kwenye chakula na wakati mwingine wanaweza kuwa wa manufaa kwetu. Hata hivyo bacteria wale ambao wako katika vitu vilivyooza na mabaki ya vyakula, si wazuri kwetu. Mtu aliye kula chakula kilichochafuliwa au kugusana na vijidudu maradhi hao, huwa na dalili kuu zifuatazo: kutapika, kuhara na maumivu ya tumbo(kitaalamu hujulikana kama stomach flu). Aidha dalili hizo mara nyingi huambatana na maumivu ya misuli, homa, kutetemeka mwili na kuihisi kuchoka. Hatua ya kuhara na kutapika mtu, husaidia mwili kuondoa mada zenye sumu au athari katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula (digestive tract) na hivyo kuzizuia sumu au vijidudu maradhi hivyo kuingia katika mfumo wa damu. Vyakula vinavyotokana na wanyama, vyakula vibichi na vile vya jamii ya mboga ambavyo havioshwi, vyote vinaweza kuwa na vidudu maradhi au Germs na kuchafua chakula au kusababisha food poisoning. Vyakula hivyo ni kama vile nyama, kuku, mayai maziwa na samaki aina ya kama wadogo. Bacteria kama vile Salmonela na Listeria ni miongoni mwa vimelea vinavyopatikana katika vyakula vilivyoharibika au kuoza.
Wakati mwingine inakuwa vigumu kueleza iwapo umekumbwa na hali hiyo baada ya kula chakula kilichoharibika. Sasa iwapo mtu atakuwa na mojawapo ya dalili hizo zilizotajwa, kama vile tumbo kukatakata, ni vyema awaulize watu wengine wa familia iwapo kuna wengine walio na dalili kama hiyo na kama wamekula chakula kama hicho alichokula yeye. Na iwapo kutakuwa hakuna yeyote mwenye dalili kama yake, basi kwa kiasi kikubwa huwenda akawa amepatwa na maradhi hayo. Wakatimwingine mtu huanza kujisikia mgonjwa katika muda wa masaa machache baada ya kula chakula kilichochafuliwa na sumu za bacteria au na vimelea vya maradhi. Dalili huanza kujitokeza kuanzia muda wa saa moja hadi matatu baada ya kula chakula kisichofaa. Na wakati mwingine mtu hawezi kujisikia mgonjwa, hadi kupita siku kadhaa baadaye. Na iwapo mtu atakuwa amekula chakula chenye kiasi kidogo cha sumu au toxin, muda wake wa kuuugua utakuwa mfupi na mara moja ataanza kujisikia vizuri. Katika hali kama hiyo mtu anapoona ana dalili hizo nilizozitaja, ni vyema amuone daktari mapema kwa ajili ya matibabu. Iwapo utakwenda kwa tabibu au daktari, atakuuliza masuali mengi kama vile unajisikiaje, umeanza kuumwa lini, ulikula nini hapo kabla na je kuna mtu yoyote wa karibu yako au unaemfahamu aliye na dalili kama zako? Nk. Aidha daktari anaweza kukuandikia vipimo vya haja kubwa na ndogo ili kuona kama vijidudu hivyo maradhi ndivyo vimesababisha hali hiyo iliyokusibu. Na iwapo utaona damu ndani ya kinyesi, unashauriwa kumuona daktari mara moja pasina na kuchelewa……. Makala hii inaendelea.

No comments: