Saturday, January 5, 2013

Neno 'Afya' linamaanisha nini?



Kwa mujibu wa  ufafanuzi uliotolewa na kutangazwa na Shirika la Afya Duniani WHO katika mkutano wake wa tarehe 19-22 Juni 1946 na kusainiwa na wawakilishi wa nchi 61 duniani, 'afya ni hali ya mtu kuwa vizuri kimwili, kiakili na kijamii na sio tu kutokuwa na ugonjwa au udhaifu.' Ufafanuzi huo ulianza kutumika Aprili mwaka 1948 na hadi hii leo maana hiyo ya afya haijabadika. Ufafanuzi huo unamaanisha kwamba, tunaposema mtu ana afya sio tu tunakusudia kuwa mwili wake hauna maradhi, upungufu au udhaifu bali pia mtu huyo anatakiwa asiwe na matatizo ya kimwili, kiakili na hata kijamii. Kwa mujibu wa tafisri hiyo pana ya neno 'afya' tunaona kuwa watu wengi wanaamini kuwa afya imeganyika katika makundi mawili muhimu ambayo ni afya ya kimwili na afya ya kiakili. Afya ya mwili kwa binaadamu ina maana, kuwa na mwili wenye afya usiokuwa na maradhi, afya ambayo kwa kawaida hutokana na kuupa mwili mazoezi ya mara kwa mara, lishe bora na mapumziko ya kutosha. Katika nchi au maeneo ambayo watu wanapata lishe bora, huduma nzuri za afya na kuishi katika hali ya kimaisha inayoambatana na viwango vinavyotakiwa, kwa kawaida vimo na uzito wao huongezeka. Ukweli ni kuwa, ukiwauliza watu wengi afya ni nini, watasema kwamba inahusiana na  mwili kuwa salama bila ya kuathirika na ugonjwa. Lakini tukienda ndani zaidi, kitiba afya ya mwili inaamanisha ustawi wa mwili hali ambayo mtu anaipata kwa kutekeleza vipengee vyote vinavyohusiana na afya katika maisha yake. Uzima wa mwili unaakisi kufanya kazi vizuri moyo na mfumo wa kupumua, uwezo wa misuli, viungo pamoja na mwili kuweza kukubali mabadiliko tofauti na muundo wa mwili kwa ujumla. Masuala mengine ni pamoja na lishe bora, uzito wa mwili, kutokuwepo uraibu wa madawa ya kulevya, pombe, mahusiano salama ya kimwili, usafi kwa ujumla na pia kulala na kuamka kwa wakati unaotakiwa.

 Afya ya akili au uzima wa kiakili ni utambuzi wa mtu na uzima wake kisaikolojia. Mtu ambaye ana afya nzuri ya kiakili hana matatizo ya kiakili au kichaa. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO, 'afya ya akili ni pale mtu anapoweza kufahamu uwezo wake na kustahamili mfadhaiko (stress) unaotakana na dhiki au matatizo ya kawaida ya kimaisha. Aweze kufanya kazi yenye kuleta mafanikio na kuchangia masuala tofauti katika jamii yake.'

Ni rahisi watu kuelezea maana ya ugonjwa wa akili kuliko afya ya akili. Watu wengi wanakubali kwamba afya ya akili ni kutokuwepo ugonjwa wa akili lakini maana hiyo haitoshi. Hii ni kwa sababu kama tutachagua watu 100 ambao hawana kichaa au ugonjwa wa akili unaoweza kutambuliwa na daktari wa akili, lakini miongoni mwao tunaweza kuona kwamba afya ya baadhi yao kiakili imeimarika kuliko wengine.Tunaweza kusema kuwa, afya ya akili inajumuisha masuala kadhaa kama vile uwezo wa kuishi kwa furaha, uwezo wa kuvumilia shida na kurejea katika hali ya kawaida baada ya kupatwa na matitizo, uwezo wa kuwa na uwiano katika maisha,  uwezo wa kubadilika kwa urahisi na kuzoea mazingira mapya, kujihisi salama na kujitambua.