Wednesday, October 19, 2011
Majaribio ya chanjo ya kwanza ya malaria duniani yaonyesha mafanikio
Majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa malaria yameonyesha mafanikio na hivyo kuleta matumaini kuwa huenda gonjwa hilo sugu linalohatarisha maisha ya mamilioni ya watoto barani Afrika likapatiwa chanjo kwa mara ya kwanza duniani. Taarifa kuhusu awamu za mwisho za majaribio ya chanjo hiyo inayotengenezwa na shirika la GlaxoSmithKline zilitangaza Jumanne ya wiki hii na kuonyesha kwamba ina uwezo wa kuulinda mwili dhidi ya malaria kwa watoto wenye umri wa miezi mitano hadi 17. Andrew Witty Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la kutengeza dawa la Uingereza ambalo limetengeneza chanjo hiyo amesema kwamba, mafanikio hayo yanaonyesha kuwa hivi karibuni dunia kwa mara ya kwanza itaweza kupata chanjo ya ugonjwa wa Malaria. Hata hivyo sambamba na kusifu mafanikio hayo Bw. Witty amesisitiza kwamba wanasayansi wanaoshulighulia ugonjwa huo na wataalamu wa masuala ya afya ulimwenguni kote bado wanasisitiza kwamba chanjo hiyo inayojulikana kana RTS,S au Mosquirix bado sio njia ya haraka ya kutokomeza malaria. Licha ya hayo inaelezwa kuwa chanjo hiyo ya aina ya sindano haina athari sana katika kuzuia ugonjwa wa malaria ikilinganishwa na chanjo nyingine kama vile za ugonjwa wa polio na ndui.
Gonjwa la malaria bado ni janga kubwa kwa nchi nyingi duniani hasa za Afrika zilizo chini ya Jangwa la Sahara na kila mwaka hupelekea vifo vya watu wengi kwenye nchi hizo hasa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. Chanjo sio changamoto pekee inayowakabili wataalamu wa masuala ya afya na tiba duniani katika kupambana na malaria bali tiba ya ugonjwa huo pia imekuwa ikibadilika mara kwa mara kutokana na vidudu vya ugonjwa huo kujibadili na kuzishinda nguvu dawa zinazotengeneza za kutibu ugonjwa huo. Kwa ajili hiyo madaktari na wataalamu wamekuwa wakishauri kutumiwa zaidi tiba ya dawa mseto katika kutibu malaria kuliko dawa moja pekee. Njia nyingine za kujilinda na malaria ni pamoja na kutumia chandarua, kupiga dawa za kuua mbu na kuyaweka mazingira tuishiyo katika hali ya usafi bila kuwepo vindimbwi vya maji na kuzungukwa na vichaka suala ambalo husababisha mbu wazaane.
Ingawa habari hii ni mafanikio makubwa yanayopaswa kupigiwa makofi na wadau wote wa masuala ya afya na tiba lakini, shaka yangu mie ni kuwa, hata kama chanjo hiyo ikianza kufanya kazi kesho lakini je, watoto wote wa bara Afrika wataweza kupatiwa chanjo hiyo na kuepusha na vifo vya holela vinavyosababishwa na malaria? Au isije ikawa hadithi zile zile za chanjo ya polio na ndui ambazo zimekuwepo kwa miongo mingi lakini mpaka leo bado kuna watoto wa Kiafrika wasiopatiwa chanjo hizo kutokana na sababu mbalimbali.
Sunday, October 16, 2011
Kila siku faida za Folic Acid zazidi kugunduliwa
Katika hali ambayo muda mrefu imekuwa ikifahamika kwamba dawa za folic acid zinazotakiwa kuliwa na mama wajawazito zina faida kemkem kwa watoto wanozaliwa, wataalamu hivi karibuni wameendelea kufahamu umuhimu wake zaidi. Siku zote kina mama wajawazito wamekuwa wakishauriwa kula folic acid miezi mitatu kabla ya kushika mimba, na pia kwa miezi kadhaa wakati wa ujauzito. Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kwamba watoto ambao mama zao walikula folic acid kabla na wakati wa ujauzito kwa kiasi kikubwa huwa hawachelewi kuzungumza. Uchunguzi huo uliofanywa huko Norway kwa kuwashirikisha wanawake 40,000 umebainisha kwamba wale ambao hawakula folic acid kabla na wakati walipokuwa na mimba wana uwezekano mara dufu wa kuzaa watoto wenye matatizo ya kuchelewa kuongea kuliko waliokula. Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapisha kwenye Jarida la Marekani la Taasisis ya Tiba (JAMA) kula folic acidi wiki 4 kabla ya ujauzito na kuendelea hadi wiki 8 baada ya kutungwa mimba husaidia kupunguza hatari ya watoto kushindwa kuongea hata wanapofikia miaka mitatu. Ingawa wataalamu wamekiri hawajui ni namna gani folic acid inazuia watoto kuchelewa kuongea lakini wanasema, kuna uwezekano dawa hizo zikawa zinataathira katika mfumo wa neva na kuzuia tatizo hilo lisitokee.
Folic acid ni miongoni mwa tembe zinazohusiwa sana mama wajawazito kula, kwani inajulikana kuwa zinazuia watoto wachanga kuzaliwa wakiwa na ugonjwa unaoitwa 'neural tube defects' ambao ni matatizo katika sehemu ya chini ya ute wa mgongo ambapo mtoto mchanga huzaliwa huku ubongo wake ukiwa haukukua kabisa. Lakini ingawa hayo yote yanajuliakana shaka yangu ni kuwa je, mama wajawazito katika nchi zetu wanajua hilo au je, wanaelimusha juu ya umuhimu wa kula folic acid? Nadhani ni jukumu langu mie na wewe kuielimisha jamii.
Saturday, January 22, 2011
Tatizo la kukosa choo watoto wadogo au kuwa na choo kigumu na jinsi ya kulitatua
Tatizo la kukosa choo watoto wadogo au kuwa na choo kigumu na jinsi ya kulitatua
Watoto wadogo hasa wale ambao bado wananyonya na ndio kwanza wamenzishwa vyakula vinginevyo zaidi ya maziwa, mara nyingi hupatwa na choo kigumu au kukosa choo kabisa hali tunayoiita kimombo, constipation. Hali hiyo huanza pale mtoto anapoachishwa maziwa ya mama na kuanza kunyweshwa maziwa ya kopo au mengineyo au pia anapoanzishwa kula vyakula vingine zaidi ya maziwa. Mara nyingi watoto wanaonyonya maziwa ya mama huwa hawasumbuliwa na tatizo hilo, bali tatizo hilo huanza kujitokeza pale wanapoanza kulishwa vyakula vingine zaidi ya maziwa ya mama. Pia mama ambaye tayari mwenyewe anasumbuliwa na tatizo la kukosa choo, huenda mwanae pia akasumbuliwa na tatizo hilo.
Mtoto mwenye tatizo la kukosa choo huwa anapata choo wa shida huku akisumbuliwa na tumbo na kupata choo kigumu. Wakati mwingine hulia wakati akipata choo huku akijiminya na kukunja uso. Muone daktari iwapo mtoto ana umri wa chini ya mwezi mmoja na hajapata choo kwa siku 4.
Iwapo mtoto wako mchanga au mdogo ana tatizo la kukosa choo au kupata choo kigumu kwanza wasiliana na daktari au mpeleke hospitalini ili upate ushari wa daktari. Pia unashauriwa kujaribu njia zifuatazo:
1. Jaribu kumpa mtoto wako maji safi na salama kuanzia mililita 60 hadi 120 kwa siku. Punguza au ongeza kiasi hicho kwa kuzingatia jinsi hali ya mwanao inavyokuwa. Ni bora maji ya mtoto yachemshwe na kufunikwa vyema.
2. Iwapo maji hayasaidii, jaribu pia kumpa juisi za matunda. Mpe mtoto wako juisi ya tufaha (apple), pea au prune iliyotengenezwa kwa kutumia maji salama na safi kila siku. Anza kwa mililita 60 hadi 120 kwa siku na punguza au ongeza kiasi hicho kwa kuzingatia jinsi hali ya mwanao inavyokuwa.
3. Jitahidi kumpa mwanao chakula chenye ufumwele au fiber. Iwapo mwanao ameanza kula vyakula vigumu, basi mpe vyakula vyenye ufumwele kuliko vyakula vyenye wanga, kama vile tumia unga wa shayiri au tunda la apple na pea lililopondwa pondwa vyema na kuwa kama uji. Epuka kumpa mtoto cereal ya mchele au uji wa mchele kama anatatizo la kukosa choo au kufunga choo.
4. Jiepushe kumpa mtoto wako vyakula vyenye wanga na sukari na vyakula vinavyotengenezwa kwa unga uliokobolewa.
5. Mpake mwanao mafuta kidogo sehemu inayotoka choo kikubwa ili kurahisisha utokaji wa kinyesi. Usitumia mafuta ya madini (mineral oil) au dawa za kulainisha choo na za kuharishwa katika kutibu tatizo hilo la kukosa choo la mtoto.
6. Kukosa choo watoto wadogo mara chache huwa kunasababishwa na magonjwa kama vile Hirschsprung ugonjwa wa kumee neva katika utumbo, au Cystic Fibrosis. Muone daktari au mpeleke mtoto wako hospitalini kama tatizo hilo la kukosa choo linaendelea hata baada ya kubadilisha aina ya chakula cha mtoto au linaambatana na dalili nyingine kama vile kutapika au mtoto kukosa utulivu na kuhangaika.
7. Kuna baadhi ya watoto wanakosa choo au kuwa na choo kigumu kutokana na kutumia maziwa ya ng’ombe. Iwapo umetumia dawa na umefuata maelekezo ya kuondoa ukosefu wa choo na hukufanikiwa. Katisha kumpa mtoto maziwa ya ng’ombe kwa siku mbili au tatu, baada ya siku hizo iwapo bado hajaacha choo badi endelea kumpa maziwa hayo, na pengine tatizo hilo halisababishwi na maziwa ya ng’ombe.
8. Mwogeshe au mweke mwanao katika beseni la maji ya uvuguvugu na hakikisha maji yanafika hadi kifuani. Mkande mtoto tumbo lake wakati akiwa majini na njia hiyo husaidia kulegeza misuli ya mwili wa mtoto, na kumsaidia kupata chook wa urahisi.
N.B Ukosefu wa choo kwa watu wazima baadhi ya wakati huandamana na magonjwa kama vile Arthritis, Appendicitis, Cataract, saratani, shinikizo la damu, Rheumatism na kadhalika lakini kwa watoto huenda tatizo hilo likawa halisababishwi na maradhi hayo.
Utafiti unaonyesha kuwa hakuna uhusiano wowote kuhusu kukosa choo mtoto na kupewa nyongeza ya chuma au Iron Supplement. Hivyo usimkatishe kumpa mwanao chuma iwapo anakosa choo. Kwani chum ni muhimu sana katika kuzuia upungufu wa damu mwilini kwa mtoto wako mdogo.
Wednesday, January 19, 2011
Jibu la swali la Mdau
Kuna mdau ambaye aliniuliza muda mrefu uliopita iwapo mwanamke na mwanamume ambao wana Ukimwi wanaweza kupata mtoto kwa njia ya IVF au la. Kwa kuwa ni muda mrefu sikuwepo kuandika blog hii na kujibu maswali, nimeamua kulijibu swali hili hapa ili muulizaji aone jibu lake kwa urahisi na wengine pia waweze kufaidika nalo.
Jibu ni kuwa ni vigumu kusema kuwa njia hiyo inaweza ku-guarantee kuzaliwa mtoto asiyekuwa muathirika wa HIV, hasa kwa kuzingatia kuwa wote baba na mama ni wagonjwa. Ni kweli iwapo mmoja tu ndiye mgonjwa kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kufanyika IVF kwa njia inayoitwa Sperm wash ambayo hufanywa kabla ya mbegu ya kiume kutumbukizwa kwenye tumbo la mama na huweza kuzaliwa mtoto asiye mgonjwa wa Ukimwi. Lakini sikukatishi tamaa mdau, iwapo huna matatizo ya uzazi, kuna uwezekano wa mwanamke na mwanamume waathirika wa Ukimwi kuzaa mtoto asiyeathirika, iwapo watakuwa wakitumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo kabla na wakati wa ujazito, na hasa mama kuendelea kutumia dawa hizo wakati wote wa ujauzito.Kuzaliwa watoto wasioathirika kutoka kwa wazazi waathirika wa Ukimwi, kumeshuhudiwa mara nyingi nchini Tanzania na kwingineko.
Sunday, January 16, 2011
Kuwaanzisha watoto chakula kigumu miezi 6 mapema kunawasaidia
Maneno haya si yangu, lakini nakumbuka kwa uzoefu wangu siku zote nilikuwa nikipingana na waalimu darasani na mahospitalini kuhusu muda wa kuanzishwa chakula kigumu watoto wanaonyonya au 'weaning'!. Siku zote walimu wangu chuo kikuu walikuwa wakisema kuwa watoto wachanga wanaonyesha waanzishwe vyakula vingine wanapokuwa na miezi minne, lakini mie nikipinga na kusisitiza kwamba muda huo utumike kwa watoto wenye asili ya kizungu au weupe, lakini kwa uzoefu wangu, watoto wetu wa Kiafrika tunawaanzisha chakula kigumu wanapokuwa na miezi minne, kwani ifikapo muda huo maziwa ya mama zao huwa hayawatoshi tena! Pia hata wadau wa Kona ya Afya pale waliponiomba ushauri niliwashauri hivyo.
Hoja yangu hiyo imethibitishwa hivi karibuni na timu moja ya Uingereza ambayo ilifanya utafiti na kuchapisha utafiti huo katika Makala ya Tiba ya Uingereza. Wanatimu hiyo wamesema, kutegemea tu maziwa ya mama pekee kwa watoto hadi miezi sita sio vizuri na hayatoshi. Wamesema maziwa ya mama yanaweza kuwa na faida iwapo watoto wataanzishwa vyakula vinginevyo mapema hasa baada ya miezi minne. Huko nyuma wataalamu walishauri kuwa mtoto apewe maziwa ya mama pekee hadi miezi sita lakini hivi sasa wamebadilisha msimamo huo na wanashauri mtoto aanze kupewa chakula kingine akiwa na miezi minne huku akiendelea kunyonyeshwa. Miaka 10 iliyopita Shirika la Afya Duniani lilitoa muongozo kwamba, watoto wachanga wanyonyeshwe maziwa ya mama pekee hadi miezi 6!
Utafiti mwingine umeonyesha kuwa, watoto wachanga wanaocheleweshwa kuanzishwa chakula kigumu hupatwa na upungufu wa damu au anemia kuliko wale wanaoanzishwa vyakula vingine wakiwa na miezi minne hadi 6. Hata hivyo wazazi na walezi wametakiwa kuzingatia aina ya vyakula wanavyowapa watoto wao wachanga pale wanapofikia muda wa kuanza kula, kwani baadhi ya vyakula huwasababishia allergies na pia kufanya wakose choo.
Sigara huharibu DNA mwilini na kuongeza hatari ya kupata kensa!
Kemikali za sumu zilizoko katika tumbaku ya sigara huharibu DNA za mwili wa binadamu dakika chache tu baada ya mtu kuanza kuvuta sigara. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni, kemikali hizo zinazoitwa Polycylic Aromatic Hydrocarbons (PAHs) husababisha DNA ziharibike na kuongeza uwezekano wa mtu kupata kensa. Katika uchunguzi huo watalamu walichukua kemikali hizo katika miili ya wavuta sigara na kuzifanyia uchunguzi, ambapo waligundua kuwa, kemikali za PHA hubadilika haraka mwilini na kuwa sumu ambayo huharibu DNA baada ya kupita dakika 15 hadi 30 tangu kuingia tumbaku katika mwili wa binadamu. Sumu hiyo hubadilisha seli mwilini au kufanya mutation, kitendo ambacho huweza kusababisha kensa. Wataalamu hao wanasema, kitendo hicho hufanyika kwa haraka sana kama vile inavyoingizwa mada ya sumu kwenye damu kwa sindano. Habari hii ni tahadhari kwa watu wanaotaka kuanza kuvuta sigara, kwani takwimu zinatuonyesha kwamba, watu 3,000 hufariki dunia kila siku umwenguni kutokana na kensa ya mapafu, maradhi ambayo husababishwa kwa asilimia 90 na uvutaji sigara. Madhara ya kuvuta sigara kwa muda mrefu yanajulikana na wengi, ambayo ni pamoja na magonjwa ya moyo na kensa mbalimbali, lakini wataalamu wanatuasa ya kuwa, madhara ya sigara huanza pale tu mtu anapoanza kupiga pafu ya kwanza na kuingiza moshi wa sigara mwilini. Hivyo bado hujachelewa na unaweza kuacha sigara hii leo!
Subscribe to:
Posts (Atom)