Sunday, August 15, 2010

Swaumu na Siha


Kwanza nawatakiwa wadau Waislamu wa Kona ya Afya swaumu njema na kw amanasaba wa mwezi mtukufu wa Ramadhani nimeandika makala hii kuhusiana na umuhimu wa kufunga. natumaini mtafaidika nayo.
Kufunga kumeamriswa katika dini mbalimbali ikiwepo dini tukufu ya Uislamu, Uyahudi na Ukiristo. Mbali na dini mbalimbali kuamuru wafuasi wao wafunge kama moja ya ibada muhimu, wataalamu wengi wa masuala ya tiba wamekuwa wakiamini kuwa kufunga ni miongoni mwa tiba asilia na inaleta faida kubwa kiafya. Kufunga kuna faida tele kwa afya na kwa siha ya mwili. Uislamu unawataka wafuasi wake wawe wenye afya njema, wasafi, walio imara kiimani na kimwili na mwenye nguvu. Bwana Mtume Mtukufu Muhammad (S.A.W) ametilia nguvu hoja hiyo pale aliposema kwamba: "Fungeni mpate siha".
Hii leo pia wataalamu wa masuala ya afya wamethibitisha faida kemkem mtu anazoweza kuzipata mtu kwa kufunga, zinazouinufaisha mwili na akili. Kuna baadhi ya madaktari wanasema kuwa kufunga kunamfaidisha mtu kisaikolojia na kimwili. Mbali na swaumu kumfanya anayefunga awe na stamina ya njaa na aweze kuvumulia matatizo na awe na subra, pia husaidia kupunguza mafuta ya zaida mwilini. Faida za kufunga haziishiii hapo bali pia swaumu ni njia ya kuponya magonjwa mbalimbali yakiwemo yale yanayohusiana na mfumo wa chakula kama vile maumivu ya tumbo sugu, kuvimba utumbo mkubwa, ugonjwa wa ini, kukosa choo na matatizo mengineyo kama vile unene wa kupindulia, kuziba mishipa ya moyo (arteriosclerosis), shinikizo la damu, asthma, diphtheria na kadhalika.
Lakini kabla hajujaendelea na mada yetu hii hebu sasa tueelezee kwa undani kitaalamu jinsi kitendo cha kufunga kinavyoufaidisha mwili.
Kufunga kitaalamu huanza pale mwili unapokosa chakula kwa masaa 12 hadi 24. Kikemia kufunga hakuanzi hadi pale sukari aina ya carbohydrate iliyohifadhiwa mwilini inapoanza kutumiwa kama chanzo cha kuzalisha nguvu. Kufunga huko huendelea madam tu mafuta na carbohydrate iliyohifadhiwa iendelee kunyofolewa na badilishwa kuwa nguvu, bila kutumiwa protini iliyohifadhiwa. Pale protini inapoanza kutumiwa na kubadilishwa kuwa nguvu (suala ambalo hupelekea misuli kupungua) kitaalamu tunasema kuwa mtu ameanza kukabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula mwilini au kwa kimbombo starving.
Faida za kufunga zinaweza kufahamika kwa kujua jinsi mwili unavyofanya kazi wakati chakula kinapokosekana.
 Wakati mwili unapoishiwa na nguvu inayotokana na chakula, huanza kutegemea hazina yake ya chakula kilichohifadhi na kitendo hicho huitwa Autolysis. Autolysis ni kuvunja vunja mafuta yaliyohifadhiwa mwilini ili kutengeneza nguvu, kitendo ambacho hufanywa na ini. Hali hiyo hupunguza mafuta ya ziada mwilini ambayo ndio sababu kuu ya magonjwa mengi kama vile shinikizo la damu, mshituko wa moyo na kadhalika.
 Kufunga pia husaidi kuondoa sumu mwilini. Suala hilo hurahisishwa na kufunga kwani chakula kisipoingia mwilini, mwili hubadilisha mafuta yaliyohifadhiwa kuwa nishati na kupitia kitendo hicho kemikali nyinginezo na sumu zenye madhara kwa mwili pia hutoka katika utumbo, ini, figo, mapafu na ngozi. Hizi ni sumu ambazo hutokana na vyakula tunavyokula na mazingira yetu, na huingia mwilini na kuhifadhiwa pamoja na mafuta.
 Faida nyingine ya swaumu kitiba ni kuupumzisha mfumo wa chakula. Wakati mtu anapokuwa hali, nguvu inayotumiwa na mfumo wa chakula ambao huwa umepumzika huelekezwa kwenye metabolism na mfumo wa kulinda mwili. Kitendo hicho husaidia mfumo wa kulinda mwili uweze kufanya kazi zake vyema zaidi na kupambana na mgonjwa au vile visivyotakiwa mwilini. Pengine hii ndio babu wanyama wanapopata jeraha huacha kula, na wanadamu hupoteza hamu ya kula wanapopatwa na magonjwa kama vile mafua. Kwa sababu mwili huielekeza nguvu yake yote kwenye mfumo wa ulinzi wa mwili ili kupambana na vijidudu. Faida hiyo mtu huipata pia anapofunga.
 Wakati wa kufunga vilevile joto la mwili hupungua kwa kiasi kikubwa. Hii hutokana na kupungua kasi ya metabolism na kusimama kazi nyingi zinazofanywa na mwili. Kwa kupungua kiwango cha sukari au glukosi katika damu, mwili hutumia glukosi inayohifadhiwa kwenye ini. BMR (basal metabolis rate) hupungua ili kuhifadhi nishati mwilini. Pia homoni mbalimbali huzalishwa wakati mtu anapokuwa amefunga zikiwemo homoni za kukua na za kuzuia seli zisizeeke. Hivyo njia mojawapo ya kuzuia uzee na kuwa na maisha marefu ni kufunga.
Kwa kuzingatia maelezo hayo yote tunaweza kusema kuwa, swaumu ina faida kubwa kiafya kwa mwanadamu.

3 comments:

Paul Akwilini said...

somo zuri sana. maana sisi tunaoishi mijini, tunakula vitu vingi vyenye sumu, kama mafuta ya kula, chips na vyakula vingi vya madukani.

Disminder orig baby said...

Mashallah Allah akuzidishie, asante sana, umetufungua sana

Anonymous said...

mamy jamani dawa ya kukoroma.