Saturday, June 19, 2010

Kunywa maji kwa mpangilio husaidia kurahisisha utendaji wa mwili



Kila mtu anajua umuhimu wa maji katika miili yetu. Sio kwamba tu mwili wenyewe umejengwa kwa asilimia kati ya 55 na 75 za maji (kwa kutegemea unene wa mtu ambapo watu wembemba wana kiasi kikubwa cha maji mwilini kuliko wanene) bali pia mwili unahitajia maji kwa kiasi kikubwa ili kufanya kazi zake vyema.
Je? Unajua mapafu yako yanahitajia vikombe wiwili vya maji hadi vinne kila siku ili kufanikisha kwa ufanisi kazi yake ya kupumua? Na kiasi hicho huhitajika ziadi wakati wa baridi.
Je, unajua wakati unapotoka jasho kikombe kimoja cha maji hupungua mwilini mwako. Na je, unatambua kwamba iwapo utaoga wakati wa mchana kwa mara karibu tatu kwa siku ni kana kwamba umekunywa vikombe 6 vya maji?
Kunywa maji kwa kiasi cha kutosha husaidia kupunguza uwezekano wa kutokea mawe katika figo, hulainisha viungo na huzuia mafua na kusaidia kupona haraka ugonjwa huo. Vilevile kunywa maji husaidia mtu kupata choo vyema.
Maji ni hitajio la dharura kwa afya zetu, kwani asilimia 60 ya uzito wako ni maji na kila mfumo wa mwili wako hutegemea maji ili kufanya kazi zake. Ukosefu wa maji mwilini humfanya mtu akaukiwe na maji au dehydration, hali ambayo hutokea pale mtu asipokuwa na maji ya kutosha mwilini ya kuuwezesha mwili wake kufanya kazi zake za kawaida. Hata katika upungufu mdogo wa maji mwilini, wakati ambapo asilimia 1 hadi 2 ya uzito wa mwili inapopungua, huweza kumfanya mtu akose nguvu na ajisike amechoka. Miongoni mwa dalili za upungufu wa maji mwilini ni:
• Kukihi kiu sana
• Uchovu
• Kichwa kuuma
• Mdomo kukauka
• Kukosa mkojo au kiasi cha mkojo kuwa kidogo.
• Udhaifu wa misuli
• Kuhisi kizunguzungu


Ni muhimu kujua kwamba mwili hupoteza maji kila siku kwa kutokwa na jasho, iwe jasho hilo umelihisi au haukulihisi, kutoa pumzi nje (exhaling), kukojoa na harakati ya tumbo. (bowel movement). Ili mwili wako uweze kufanya kazi vizuri unahitajia kurudisha maji hayo mwilini kwa kunywa vinywaji mbalimbali na vyakula vyenye maji.
Wataalamu wengi wanakubaliana kuwa mwanadamu anahitajia kunywa vikombe 8 vya maji kwa siku, ili kufidia maji yanayopotae mwilini. Hata hivyo wengine wanashauri kwamba, wanaume wanywe vikombe 13 vya maji kwa siku na wanawake vikombe 8 vya maji, na hiyo ni kutokana na tofauti ya miili yao. Tunashauriwa kuwa badala ya kunywa maji kiholela tunywe kwa mpangilio maalum kwa siku, ili kusaidia vyema katika kazi za mwili.
 Tunashauriwa kunywa vikombe viwili vya maji asubuhi pindi tunapoamka, kwani husaidia kuamsha viungo vya ndani ya mwili.
 Tunashauri tunywe kikombe kikoja cha maji dakika 30 kabla ya mlo, kwani husaidia kupata choo vizuri.
 Tunashuariwa tunywe kikombe kimoja cha maji kabla ya kwenda kuoga, husaisia kupunguza shikizo la damu.
 Na tunashauriwa kunywa kikombe kimoja cha maji kabla ya kulala kwani kufanya hivyo huzuia shinikizo la moyo.
Basi kunywa maji kwa afya yako mdau!

Sunday, June 6, 2010

Kensa kuua watu milioni 13.2 ifikapo mwaka 2030


Maafisa wa Umoja wa Mataifa wametangaza kwamba, watu zaidi ya milioni 13.2 watafariki dunia ifikapo mwaka 2030 kutokana na maradhi ya kensa, idadi ambayo ni mara mbili ya ile ya mwaka 2008. Takwimu hizo za hivi karibuni zinaonyesha pia kwamba, ugonjwa wa saratani mwaka 2008 ulisababisha watu milioni 7.6 waage dunia na kwamba kesi mpya milioni 12.7 za kensa mbalimbali zimegunduliwa mwaka huu. Nchi zinazoendelea zimeripotiwa kuwa na asilimia 56 ya kensa mpya na asilimia 63 ya kensa zote zilizoripotiwa mwaka 2008. Kensa ambazo zilitokea kwa kiasi kikubwa mwaka 2008 ni kensa za mapafu, matiti na kensa ya utumbo, rectum na apendeksi au colorectal cancer. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Kimataifa cha Utafiti wa Kensa( IARC) kesi za ugonjwa wa kensa zitaongezeka mara dufu katika miongo miwili ijayo iwapo hali ya sasa itaendelea hivyo hivyo. Christopher Wild Mkurugenzi wa IARC amesema kwamba, maradhi ya kensa hakuna sehemu yoyote duniani yasipokuwepo, hata katika nchi zilizoendelea na zenye utajiri mkubwa. Amesisitiza kwamba la kusikitisha ni kuwa maradhi ya kensa ambayo mwanzoni yalishudiwa kwa wingi katika nchi zinzoendelea hivi sasa yapo pia katika nchi masikini.

Wednesday, May 26, 2010

DAWA ZA KIUNGULIA ZINASABABISHA MPASUKO WA MIFUPA



Taarifa mpya zinasema kwamba, maafisa wa afya wametahadharisha juu ya kutumiwa kwa muda mrefu dozi kubwa ya dawa za kuondoa kiungulia, (heartburn) na kusisitiza kwamba zinasababisha mifupa kupasuka. Dawa hizo ni zile zinazojulakana kama Proton Pumping Inhibitors (PPI) zinazozuia kiungulia na ambazo hutumiwa kudhibiti kiwango cha asidi katika tumbo na pia kutibu ugonjwa wa GERD au gastroesophageal reflux disease. Taarifa hizo zilizotolewa na Kitengo cha Kusimamia Vyakula na Dawa cha Marekani (FDA) zinasema kwamba, dawa hizo za kingulia huongeza uwezekano wa kupasuka mifupa ya nyonga (hip), mikono na ute wa mgongo kwa watu wazima, hasa iwapo dawa hizo zitatumiwa kwa mwaka mmoja au zaidi, au kwa dozi kubwa.
Joyce Korvick Mkurugenzi wa masuala ya usalama wa kitengo cha FDA anasema kwamba, kwa kuwa dawa hizo zinatumiwa sana na watu wengi, ni muhimu kwa watu wote kufahamu madhara yanayoweza kusababishwa na dawa hizo. Maafisa hao pia wamewataka madaktari kuwaandikia tu dawa hizo wagonjwa ambao hali zao ni mbaya mno, na kusisitiza kuwa faida ya dawa hizo pale zinapotumiwa mara chache ni zaidi ya hatari inayozisababisha.
Huko nyuma pia wataalamu walisema kwamba, dawa hizo za kutibu kiungulia zinahusiana na ongezeko la hatari ya maambukizo ya bacteria aina ya C. difficile anayesababisha ugonjwa wa kuharisha.
Dawa hizo ni kama zile za Emsomeprazole, Dexlansoprazole, Lansoprazole, Emprazole/Sodium Bicarbonate, Pantoprazole, Rabeprazole na Rabeprazole.
Ndugu mdau kama wewe ni miongoni mwa wanaotumia dawa hizo, basi jihadhari kabla ya hatari!

Sunday, May 23, 2010

WHO YATAHADHARISHA JUU YA UNENE WA WATOTO


Mawaziri wa Afya Duniani huku wakitahadharisha juu ya ongezeko la idadi ya watoto wenye unene wa kupindukia, wamesema kwamba watajaribu kupunguza kutumiwa vyakula holela (junk food) kwa kupiga marufuku matangazo ya vyakula hivyo. Mawaziri hao wa nchi 193 duniani ambazo ni wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wametoa muongozi kwa ajili ya mashirika ya kuuza vyakula na vinywaji visivyokuwa na ulevi kwa ajili ya watoto.
Viwanda vya vyakula na vinjwaji vimetakiwa kuongeza udhibiti katika aina zote za mauzo ya vyakula kwa watoto, na wauzaji vyakula wadogo wadogo pia wametakiwa kuacha kuzalisha na kuuza vyakula ambavyo si vizuri kwa afya ya watoto. WHO imesema kwamba, vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta, sukari na chumvi vinachangia katika kuleta magonjwa sugu kama vile kisukari, maradhi ya moyo na kensa za aina mbalimbali, magonjwa ambayo yanasababisha vifo kwa asilimia 60 duniani kote.
Timoth Armstrong Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa Sugu na Ustawi wa Afya cha WHO amesema kwamba, unene wa kupindukia kwa watoto unaongezeka duniani. Kiwango cha ongezeko hilo katika nchi zilizoendelea ni kikubwa zaidi kwa sababu ya mabadiliko ya kasi ya lishe pamoja na jinsi mwili unavyoshughulishwa.
Yafaa kujua kuwa, tangu mwaka 1980, unene wa kupindukiwa umeongezeka mara dufu kwa watu wazima na mara tatu kwa watoto. Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa, watoto milioni 42 wenye umri wa chini ya miaka mitano wana uzito uliozidi, huku milioni 35 kati yao ni wale wanaoishi katika nchi zilizoendelea kiuchumi. Shirika hilo limeshauri kwamba, inabidi wazazi wapunguze kuwaachia watoto wao kuangalia televisheni, na mashuleni na katika sehemu za michezo za watoto kusiwe na vyakula holela na vinywaji vyenye sukari nyingi.

Thursday, May 20, 2010

Chanjo ya Ndui kuzaidia kupambana na virusi vya HIV


Kutotumiwa chanjo ya ndui katika baadhi ya nchi duniani kunaaminika kuwa kumesaidia katika kueneza maambukizo ya virusi vya HIV, hasa kwa kuzingatia kuwa ugonjwa huo umeongeza sasa siku hizi. Chanjo ya ndui polepole ilianza kutotolewa katika baadhi ya nchi duniani na ugonjwa wa ndui kutokomezwa katikati mwa karne ya 20. Utafiti uliochapishwa katika jarida la BMI Immunology umeonyesha kwamba, chanjo ya ndui ilikuwa ikipunguza maambukizo ya virusi vya HIV, hasa mwanzoni ugonjwa huo ulipogunduliwa duniani. Lakini kuacha kutolewa chanjo hiyo na wataalamu wa Afya, kunaweza kuwa ndio sababu iliyopelekea ongezeko la maambukizo ya ugonjwa wa Ukimwi yaongezeke. Wataalamu waliofanya utafiti huo wanasema kwamba, kuna sababu kadhaa zilinazoweza kutolewa kuhusiana na kasi ya ongezeko la Ukimwi barani Afrika, baadhi ya sababu hizo ni vita, kurudiwa kutumiwa sindano bila kuondolewa vijidudu (unstrelizized needles) pamoja na chanjo za ndui za mwanzo ambazo zilikuwa na vijidudu. Hata hivyo, wataalamu hao wamesema kuwa, sababu zote hizo zimekanushwa au hazitoshi kuelezea sababu ya ongezeko kubwa la maambukizo ya HIV duniani hasa barani Afrika.
Chanjo ya ndui inapunguza uwezekano wa virusi vya HIV kuzaana mara kadhaa katika seli za damu. Pia chanjo hiyo huleta mabadiliko ya muda mrefu katika mfumo wa kulinda mwili, hubadilisha tafsiri ya recepta ya CCR5, ambayo iko juu ya seli za chembechembe nyeupe za damu zinazotumiwa na virusi vya ndui pamoja na HIV.
Wataalamu wanamini kwamba chanjo ya ndui itaweza kutumiwa katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi katika miaka ijayo ya hivi karibuni, lakini pia wamesisitiza kwamba uchunguzi zaidi unapaswa kufanywa ili kuhdibitisha zaidi suala hilo.


Ugonjwa wa ndui ni miongoni mwa magonjwa ambayo yaliitikisa dunia katika miaka ya huko nyuma. Lakini kugunduliwa chanjo ya ndui ambapo kwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa huo mara moja mtu huweza kuwa na kinga dhidi ya ugonjwa huo kwa maisha yake yote, kulipunguza maambukizo ya ugonjwa huo na hatimaye ugonjwa huo ukang'olewa kabisa karibu katika nchi zote duniani. Ndugu mdau, kama huna uhakika kama umepatiwa chanjo ya ndui, basi angalia katika moja ya mabega yako na kama utakuta kovu dogo la duara, basi ujue kuwa una kinga ya ndui. Nawahusia wakina mama wanaowazaa watoto wao siku hizi wahakikishe kwamba wanapatiwa chanjo ya ndui, kwani kama inavyoelezwa mbali ya kumzuia mtoto wako asipate ugonjwa wa ndui maishani, pia hupunguza maambukizo ya ugonjwa wa Ukimwi. Haya tena wadau lakini wewe unafikiri ni sababu gani hasa inayopelekea ongozeko la maambukizo ya Ukimwi katika jamii zetu?..... tueleze maoni yako ili tusaiidiane katika kuifunza jamii na kupambana na ugonjwa hatari wa Ukimwi.

Sunday, May 16, 2010

Kupewa watoto sukari kabla ya chanjo kunapunguza maumivu


Watafiti wa Canada wamesema kuwa, kuwapa watoto sukari kabla ya kupewa chanjo kunapunguza maumivu. Watafiti wa Chuo Kikuu cha Toronto wamesema kwamba watoto wachanga wakipewa matone machache ya maji ya sukari, kabla ya chanjo hawatolia au watapunguza kulia. Hayo yamesemwa baada ya watoto 1,000 wachanga kupewa maji ya glukosi kabla ya kupigwa sindano na kupunguza kulia kwa asilimia 20. Utafiti huo umechapishwa katika jarida la Mafanikio ya Magonjwa ya watoto na umetokana na matokeo ya majaribio 14 yaliyofanywa kuhusiana na suala hilo. DaktaArme Ohlsson aliyeongoza timu ya utafiti huo amesema kwamba umefanywa kwa watoto wasiozidi mwaka mmoja. Pia watatifi hao wamesema kwamba, matone machache tu au nusu kijiko cha maji ya glukosi au sackrosi pia hupunguza muda wa mtoto kulia. Pia wamewashauri maafisa wa afya wawape watoto sakrosi na glukosi kabla ya kuwapatia chanjo. Wamesema kwa kuwa vyakula vitamu vina uwezo wa kupunguza maumivu ndio sababu watoto wanapopewa glukosi kabla ya chanzo huwa hawalii.

Wednesday, May 12, 2010

Kuchoka wakati wa ujauzito na namna ya kujiepusha

Wapenzi wadau natumaini hamjambo! kumekuwa na baadhi ya wadau wanaoniandikia na kuomba ushauri mbalimbali kutokana na matatizo waliyonayo. Nawashukuru sana kwa kuwa wanafuatilia yale yanayojiri katika blogi hii na kupata ingawa machache kuhusiana na afya zetu. Pia nawashukuru kwa kuniwezesha nami kuzungumzia mada mbalimbali kutokana na maswali yenu munayoyauliza. Kwa wale wenye maswali na matatizo mbalimbali tafadhali sana niandikieni kwa kupitia email yangu ambayo ni sthugs4j@gmail.com. Kwani wale wanaoandika maswali yao katika sehemu ya maoni, baadhi ya wakati huwa siyaoni katika muda unaotakiwa na hivyo hunifanya nichelewe kuwajibu. Wote mnashukuriwa. Leo tutazungumzia suala la kujihisi uchovu wakati wa ujauzito ambalo limeulizwa na mmoja wa wadau wanaofuatilia kwa karibu kona ya afya nami nalijibu swali lake kama ifuatavyo.

Wanawake wengi kwa kawaida huwa wanahisi uchovu wakati wa ujauzito. Uchovu, kulegea mwili na kuishiwa na nguvu ni jambo la kawaida katika kipindi hicho. Hii ni kwa sababu mwili katika kipindi hiki unatumia nguvu za kiada ili kuunda kiumbe kipya. Pia wakati huu mwili hutengeneza damu kwa wingi zaidi ili kufikisha chembechembe za chakula kwa mtoto, suala ambalo huufanya mwili ufanye kazi ya ziada na hata viungo vingine muhimu kama vile moyo na vinginevyo. Uzito wa mtoto nao unaoongezeka katika mwili wa mama mjamzito siku baada ya siku, ni sababu nyingine inayomfanya mama mjamzito ajihisi kuchoka. Kuchoka au kiushiwa na nguvu ni tatizo la kawaida hasa katika miezi mitatu ya mwanzo ya mimba. Katika miezi hiyo ya mwanzo ya mimba tatizo hilo husababishwa na mabadiliko ya homoni za mimba mwilini hasa progestrogen na wakati mwingine hali hiyo huongezwa na kichefuchefu na kutapika. Hali hiyo ya mchoko inatarajiwa kuisha inapoingia miezi mitatu ya pili ya mimba. Lakini pia kuna wengine ambao hali hiyo ya kuchoka huendelea nayo hadi wakati wa kujifungua. Kushindwa kulala vizuri kutokana na kwenda mara kwa mara msalani, au kukosa uzingizi kutokana na ongezeko la ukubwa wa tumbo mwishoni mwa ujauzito, ni miongoni mwa masuala ambayo humfanya mama mjazito ajisikie mchovu na akose nguvu siku nzima.
Vilevile mabadiliko ya kifizikia na kisaikolojia ya wakati wa ujauzito humfanya mama mjamzito awe na morali ya chini na kuhisi uchovu wa kimwili na hata kiakili. Sababu nyinginezo zinaweza kutokana na kazi mbalimbali anazofanya mama huyo au pia ukosefu wa lishe inayofaa na ya kutosha kwa ajili ya mwili wake, ambao unahitajia nguvu ya ziada hasa kwa ajili ya uumbaji wa ukamilifu wa mtoto aliye tumboni.
La muhimu analoshauriwa mama mjamzito ni kutoogopa na kutotishwa na hali hiyo, kwani inatokana na baadhi ya mabadiliko yanayotokea katika mwili wake. La muhimu ni mama mjamzito kufuata ushauri unaotakiwa ili kukabilina na hali hiyo.
Zifuatazo ni njia za kukabiliana na uchovu wakati wa ujauzito.
• Kwanza kabisa mama mjamzito anatakiwa ale vyema. Mama mjamzito anatakiwa ale chakula bora na kamili, chenye kalori 300 au 500 za ziada ikilinganishwa na mtu asiye mjamzito kwa siku. Lakini awe mwangalifu na ni bora akigawe chakula chake katika sehemu ndogo ndogo 5 au 6 (suala hili tumelizunguzia kwa undani katika makala iliyopita ya kiungulia wakati wa ujauzito, tafadhali pitia makala hizo). Anaweza akawa akibeba matunda na mboga mboga kama asusa (snacks) kwa ajili ya kula kila anapohisi njaa popote pale awapo. Lakini ni bora ajiepushe na vyakula vyenye sukari nyingi na caffeine, kwani vyakula hivyo huyeyuka haraka mwilini na kumfanya ahisi njaa mapema.
• Mama mjamzito ahakikishe kuwa hana upungufu wa damu. Na kama anao basi atumie dawa za kuongeza damu zinazotolewa na madaktari, au ale vyakula vinavyoongeza damu. Hii ni kwa sababu ukosefu wa madini ya chuma mwilini unaosababisha ukosefu wa damu, ni miongoni mwa sababu zinazomfanya mama mjamzito ahisi kuchoka. Mtu mwenye ukosefu wa damu (Anemia) huhisi kubanwa na pumzi, ongezeko la mapigo ya moyo, udhaifu, kupauka na kizunguzungu. Onana na daktari iwapo una dalili kama hizo.



• Mama wajawazito wanashauri kujipumzisha nyakati za mchana. Ni bora mama mjamzito apumzike kwa kadri anavyoweza wakati wa mchana, baada ya chakula cha mchana au hata kabla ya nyakati za magharibi. Ikiwa unafanya kazi, basi pumzika mara kwa mara japo kwa muda mfupi ili kufanya mwili upate nguvu.
• Mama wajawazito wanashauriwa kujitahidi kulala mapema, hasa kama ikiwa inakubidi uamke mara kadhaa usiku kutokana na sababu mbalimbali, kama vile kwenda msalani, kula au kutokana na maumivu.
• Kufanya mzoeni husaidia kupunguza uchovu na kuna faida kemkem wakati wa ujauzito. Kahusiana na suala hilo soma makala zilizotangulia.
• Mama mjamzito anatakiwa anywe maji ya kutosha. Ukosefu wa maji mwilini huchangia kumfanya mama mjamzito ahisi uchovu.
• Usifanye kazi nyingi kutwa nzima, na kama inawezekana ni bora usaidiwe kazi hizo hasa za nyumbani na watu wengine katika familia kama vile watoto, mume ndugu, jamaa na marafiki.
• Usikilize mwili wako. Pale unaposikia njaa basi kula na pale unapojisikia uchovu jitahidi upumzike.
• Pata ushauri wa daktari iwapo unahisi uchovu wa kupindukia au unachoka kila mara, ili uwe na uhakika kuwa hakuna tatizo au hatari inayoweza kuhatarisha maisha yako na ya mtoto.