Saturday, October 31, 2009

Maumivu ya Tumbo la Hedhi... Sehemu ya Pili


kukasababisha mtu kupatwa na maumivu ya tumbo la hedhi. Miongoni mwa magonjwa hayo ni:
• Endometriosis. Hii ni hali ambayo seli za ndani ya mfuko wa uzazi huanza kuoka nje ya fuko hilo, au hta sehemu nyinginezo.
• Adenomyosis: Huu ni ugonjwa wa wanawake ambapo tezi au uvimbe (tumors) zinaoota katika mfuko wa uzazi.
• PID au Ugonjwa wa uvimbe katika nyonga.
• Magonjwa ya zinaa yanayotokana na bakteria au magonjwa ya kuambukiza ya zinaa.
• Mlango wa uzazi unapokuwa mdogo kiasi kwamba unazuia damu ya hedhi isitoke kwa urahisi.
Baada ya kujua baadhi ya matatizo ya wanawake yanayoweza kusabibisha hedhi inayoambatana na maumivu ya tumbo, hebu sasa na tuzijue tumbo la mwezi linaumaje?
1. Maumivu mara nyingi si makali.
2. Muumivu huja na kuondoka, na kwa kiwango tofauti (spasmodic).
3. Maumivu zaidi huhisiwa sehemu ya chini ya tumbo.
4. Huchanganyika na maumivu ya sehemu ya chini ya mgongoni ambayo husambaa mpaka mapajani.
5. Kujihisi kutapika, kichefuchefu na wakati mwingine hata kutokwa jasho.
6. Kupata choo kilaini au hata kuharisha.
7. Kufunga choo.
8. Tumbo kuwa kubwa au kuwa gumu.
9. Kuhisi maumivu ya kichwa.
10. Kutojihisi vizuri au kujisikia kuchoka.
Inapasa kujua kuwa, kiwango cha maumivu ya tumbo la hedhi na mchanganyiko wa dalili inategemea mtu na mtu, mtu mwingine anaweza akawa anapata karibu dalili zote nilizozitaja hapo juu na mwingine ni baadhi tu au hata dalili moja. Wanawake wengi hutambua wanapopata tumbo la hedhi bila hata msaada wa daktari. Wanawake wanashauri iwapo watapata maumivu makali sana ni bora wakamuone daktari ili wafanye vipimo kama vile Ultrasound, CT na CT-Scan, MRI na vinginevyo ili kufahamu iwapo kuma matatizo mengine ya kitiba yanayosababisha maumivu hayo kuwa makali.
Matibabu ya maumivu ya tumbo la hedhi kwa kawaida huweza kutibika kwa urahisi kwa kutumia vidonge vya kupunguza maumivu, kama vile Ibuprofen, naproxen au aina nyinginezo za vidonge visivyokuwa na steroids (NSAIDS). Pia kuna wakati madaktari wanaweza kumshauri mgonjwa kutumia vidonge vya kuzuia mimba, Vidonge hivyo huzuia mzunguko wa yai au Ovulation na kupunguza ukali wa maumivu ya tumbo la hedhi.
Kuna baadhi ya tiba za mitishamba pia ambazo husadia kupunguza muamivu ya tumbo la hedhi. Hapa namaanisha herbal, wenzetu Wachina ni watalamu wazuri katika ujuzi huo. Vilevile wanawake washauriwa kufanya baadhi ya vitendo ambavyo hupunguza maumivu hayo, baadhi ya hivyo vimetaja kama kuoga maji moto, kutumia hot bottle na hata kuweka kitambaa chenye joto katika sehemu ya chini ya tumbo. Kuna baadhi husaidia kwa kufanya mazoezi kama yoga, meditation, kusuliwa, tiba ya sindano (Acupunture), TENS au kushituliwa mishipa ya fahamu ( Transcitaneous Electric Nerve Stimulation na hata wengine husaidiwa kwa tendo la kujamiiana. Vilevile kutumia vidonge vya vitamin E, Thiamine na Omega 3 kumetajwa kuwa husaidia katika suala hilo. Wanawake wanaopatwa na matatizo kama hayo ni bora wapumzike vyema na kupata usingizi wa kutosha.
Tunaelezwa kuwa tunaweza kujiepusha na kupatwa na maumivu ya tumbo la mwezi kwa kufanya yafuatayo:
 Kujitahidi kula matunda, mbogamboga na kupunguza kula vyakula vyenye mafuta mengi, pombe, cofeini, Sodium na sukari.
 Kufanya mazoezi.
 Kujiepusha na wasiwasi na mawazo.
 Kuepuka kufuta sigara.
… Haya kina mama na kina dada, tukumbuke kuwa afya ni zetu na inabidi tuzitunze!

Obama aondoa marufuku ya kuingia nchini Marekani walioathiriwa HIV


Marekani imeondoa marufuku ya kuingia nchini humo watu walioathiriwa HIV, sheria ambayo imetumiwa kwa miaka 22. Rais Barack Obama amethibitisha kuondoalewa marufuku hiyo wakati akiongeza fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma za magonjwa yanayoambatana na ugonjwa wa Ukimwi na HIV. Akibatilisha sheria hiyo Obama amesema kuwa, iwapo nchi hiyo inataka kuwa kiongozi katika kukabilina na Ukimwi basi wanapaswa kufanya vitendo kama hivyo. Ameongeza kuwa kuwapiga marufuku kuingia Marekani watu wenye Ukimwi kumetokana na woga badala ya kukubali ukweli wa suala hilo.
Marekani ilikuwa miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zinazuia watu wenye Ukimwi kuingia katika nchi hizo. Sheria hiyo mpya inatarajiwa kuanz akutumika mwanzoni mw amwaka 2010.

Monday, October 26, 2009

Wanawake wana dalili sawa za mshituko wa moyo na wanaume


Imekuwa ikiaminiwa kuwa wanawake wanapatwa na mshituko wa moyo tofauti na wanaume lakini wataalamu wamegundua kuwa fikra hiyo haina ukweli wowote. Wataalamu wa Magonjwa ya Moyo wa Canada wamesema hayo baada ya baada ya kuchunguza wanawake 305 waliokuwa wakifanyiwa operesheni ya angioplasty. Wataalamu hao wamesema kuwa, ugonjwa wa moyo huwapata kwa dalili sawa wanawake na wanaume. Mwaka 2003 Taasisi ya Kitaifa ya Marekani ilitangaza kwamba, wanawake wengi hawapatwi na maumivu ya kifua wakati wanapopatwa na mshituko wa moyo, na dalili za ugonjwa huo kwa wanawake hutofautiana. Lakini wataalamu wa Canada wamegundua kuwa, wanawake pia kama wanaume huhisi dalili za kawaida za mshituko wa moyo kama vile maumivu ya kifua pamoja na mauamivu katika koo, taya na shingo. Wamesema kuwa, taarifa zilizo sahihi zinapaswa kufikishiwa jamii ili kuhakikisha kwamba wanawake pamoja na wataalamu wa vituo vya afya wanatambua kuwa dalili muhimu za mshituko wa moyo ziko sawa kwa wanawake na wanaume.
Inafaa kujua kuwa dalili za tahadhari za kupatwa na mashituko wa moyo ni:
 Kuhisi maumivu kifuani
 Kushindwa kupumua
 Kuhisi kichefuchefu
 Kutokwa jasho
 Kuhisi wasiwasi

Sunday, October 25, 2009

Marekani yatangaza homa ya mafua ya nguruwe kuwa janga la kitaifa


Rais Barack Obama wa Marekani ametangaza kuwa homa ya mafua ya Nguruwe ni janga la kitaifa. Taarifa kutoka ikulu ya White House imesema kuwa Rais Obama alitia saini hati ya tangazo hilo usiku wa Ijumaa. Tangazo hilo litapelekea kuongezwa mikakati ya kupambana na homa hiyo aliogunduliwa mapema mwezi Aprili mwaka huu nchini Mexico. Duru za habari zinaarifu kuwa takriban majimbo 46 ya Marekani yameathiriwa na homa hiyo huku zaidi ya Wamarekani 1000 wakiripotiwa kuaga dunia kutokana na virusi vya H1N1 vinavyosababisha homa ya mafua ya nguruwe. Rais Obama amesema kuwa ugonjwa huo unasambaa kwa kazi na hivyo pana haja ya kuongeza juhudi za kukabiliana nao. Kutiwa saini hati ya tangazo hilo kunaipa serikali idhini ya kuepuka masuala ya kiitifaki katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Saturday, October 24, 2009

Kuumwa tumbo wakati wa hedhi- sehemu ya kwanza


Tumbo la hedhi au maumivu wakati wa hedhi (period pains) au kitaalamu dismenorrhea, ni maumivu yanayojitokeza sehemu ya chini ya tumbo au kiunoni wakati mwanamke anapoanza kupata siku zake au kabla ya hapo. Maumivu hayo huweza kuwa madogo au ya wastani huku baadhi ya wanawake wakipata maumivu makali sana. Maumivu ya tumbo wakati wa hedhi huanza pale mayai yanapotoka katika mirija (fallopian tubes) na kuteremka chini ya mirija hiyo wakati wa Ovulation.
Maumivu ya tumbo la hedhi yapo ya aina mbili. Aina ya kwanza au (Primary Dysmenorrhea) ni maumivu yasiyokuwa na sababu zozote za kimsingi za kitiba. Katika aina hii maumivu ni ya kawaida na huhisiwa sehemu ya chini ya tumbo na kiunoni. Maumivu hayo huanza siku moja au mbili kabla ya hedhi na humalizika baada ya siku mbili au nne.
Aina ya pili au (Secondary Dysmenorrhea) ni yale maumivu yanayojumuisha maumivu yanayosababishwa na sababu nyinginezo za kitiba kama vile matatizo katika kizazi, ugonjwa wa nyonga (PID) na matatizo katika mirija ya mayai.
Karibu nusu ya wasichana na wanawake hupata maumivu wakati wa hedhi na karibu asilimia 15 wanasema kuwa hupata maumivu makali. Uchunguzi unaonyesha kuwa kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuongeza uwezekano wa kuumwa tumbo wakati wa hedhi.
• Kuwa na umri wa chini ya miaka 20.
• Kuvunja ungo wakati wa miaka 11 au chini ya miaka hiyo.
• Kutoka na damu nyingi wakati wa hedhi. (suala hilo linaweza kusababishwa na matatizo mbalimbali ya kitiba).
• Wanawake ambao hawajawahi kuzaa.

…..Inaendelea… usikose kufuatilia semu ya pili ili kujua namna ya kutibu maumivu hayo.

Wednesday, October 21, 2009

Ngozi zenye mafuta na jinsi ya kuzitunza


Ngozi yenye mafuta kwa kawaida huwa inang'ara, nene na yenye rangi iliyotitia. Mara nyingi ngozi yenye mafuta mengi sana huwa na chunusi nyingi na vipelepele na mara nyingine huwa na chunusi zenye vichwa vyeusi. Katika aina hizi za ngozi mafuta hutokana na tezi za sebaceous na kuzalisha mafuta zaidi ya kiwango kinachotakiwa. Mafuta hayo husambaa katika ngozi na kuifanya iwe na mafuta mafuta.
Sababu zinazosababisha ngozi kuwa na mafuta:
• Kuridhi.
• Lishe.
• Kiwango cha homoni mbalimbali mwilini.
• Ujauzito.
• Vidonge vya kuzuia mimba.
• Baadhi ya vipodozi .
• Hali ya unyevu (humidity) na hali ya hewa ya joto.

Namna ya kutunza ngozi zenye mafuta
Faida kubwa ya kuwa na ngozi yenye mafuta ni kuwa haizeeki kwa haraka ikilinganishwa na aina nyinginezo za ngozi. Miongoni mwa mambo yanayosaidia ili kuitunza ngozi yenye mafuta na kuiepusha na chunusi na hali isiyopendeza ni:-
1. Ngozi yenye mafuta inahitajia kusafishwa vyema kwa maji ya moto na sabuni ili kuzuia vinyweleo visizibwe na mafuta.
2. Epusha vifaa vigumu visikwaruze uso wako na kupelekea ngozi kubanduka, kwani suala hilo husababisha tezi za mafuta kufanya kazi zaidi ili kujaza sehemu iliyopotea ya mafuta.
3. Epuka kutumia vipodozi ambavyo huifanya ngozi yako ipotze maji au kukauka. Kwani husababisha sehemu ya juu ya ngozi inyauke, na hivyo kusababisha mafuta kuziba vinyweleo na kupelekea kutokea vichwa vyeusi.
4. Jitahidi kuitunza vyema ngozi yako na kuisafisha vizuri. Jaribu kuosha uso mara mbili au tatu kwa siku. Usioshe mara nyingi kwani kufanya hivyo huufanya uso kutoa mafuta zaidi.
5. Chagua kile unachosafishia kwa makini, jiepushe kutumia cream nzito nzito au vifaa vugumu wakati wa kuosha uso wako. Ni bora utumie sabuni za kawaida zisizokuwa na madawa. Unaweza kutumia lotion ya kuua bacteria au sabuni zisizo na dawa nyingi (lightly medicated), au sabuni zenye madini mbalimbali. Ni bora usioshe au kutumia lotion au michanganyiko yenye alkoholi.
6. Tumia maji ya moto au ya vuguvugu wakati unaosha uso wako.
7. Wakati unapoosha uso wako, ukande kwa kutumia ncha za vidole, jiepushe kupaka sabuni moja kwa moja usoni, inaweza kuganda na kuzuia vinyweleo kuziba.
8. Kutumia mask za udongo (clay) na tope (mud) husaidia katika ngozi za aina hii. Ni bora utumie mask mara moja au mbili kwa wiki.
9. Jitahidi kutumia vipodozi vya uso ambavyo vimetengenezwa kwa ajili ya ngozi yenye mafuta.

Monday, October 19, 2009

Je wajua vyakula unavyokula kila kimoja kina umuhimu gain? Part1



Pengine methali hii kuwa "tunakula ili tuishi" si ngeni masikioni mwa wengi. Chakula kimekuwa na nafasi hai katika maisha yetu ya kila siku, kiasi kwamba tumelizoea jambo hilo na kuona kuwa ni mfululizo tu wa kila siku, bila kujali tunachokula au kutaka kujua vyakula tunavyokula vina umuhimu gani kwa afya zetu. Kwa kutambua umuhimu wa vyakula mbalimbali kwa miili yetu na afya zetu, kutasaidia tuweze kuchagua tule vyakula gani, na sufuria na sahani zetu kila siku zijae vyakula vya aina gani zinapokuwa mezani. Ama pale tunapoelekea sokoni, tuchague na kununua nini ili kuyajaza makapu yetu kabla ya kuelekea nyumbani kutayarisha chakula.
Katika sehemu hii ya kwanza tutaelezea baadhi ya faida zinazotokana na ndizi kwa ajili ya Afya zetu.
Ndizi:
Ndizi ni chakula kinachujulikana kama tiba asilia kwa matatizo mengi ya kiafya. Ukifananisha ndizi na tufaha (apple), ndizi zina protini mara nne zaidi, sukari mara mbili, potassium mara tatu vitamini A na chuma mara tano zaidi. Vile vile vitamini na madini nyinginezo hupatikana pia katika tunda hilo. Ndizi zina sukari asilia ya sucrose, fructose na glucose iliyochanganyika na ufumwele (fibre). Kwa kula ndizi unaupatia mwili nishati na nguvu ya haraka. Pia uchunguzi umeonyesha kuwa, kula ndizi mbili huweza kuupatia mwili nguvu za kutosha kwa ajili ya kujitayarisha kufanya mazoezi kwa dakika 90! Pengine ndio sababu, ndizi zikawa ni tunda la kwanza linalotumiwa zaidi kwa ajili ya wanamichezo hasa wanaokimbia mbio ndefu. Nishati sio kitu pekee chenye faida kinachoweza kupatikana kwenye ndizi kwa ajili ya miili yetu, bali pia huweza kusaidia miili kuzuia magonjwa na matatizo kadhaa.
Ndizi kwa kuwa na kiasi kikubwa cha chuma, husaidia kushajiisha uzalishwaji wa hemoglobin katika damu. na hivyo kusaidi kuondoa upungufu wa damu wa Anemia.
Ndizi kwa kuwa na kiwango cha juu sana cha potassium na kiasi kidogo cha chumvi, hulifanya tunda hilo lifae katika kupambana na shinikizo la damu (blood pressure).
Ndizi huweza kusaidia mwili katika kuimarisha uwezo wake wa kufyonza calcium, na hivyo kuifanya mifupa kuwa imara.
Imeonekana kwamba ndizi husaidia ubongo na kuongeza uwezo wa kujifunza na kufahamu mambo. Hivyo wataalamu wanashauri kuwa tunaweza kuwapa ndizi watoto washule wakati wa mitihani katika kipindi cha mapumziko, wakati wa chakula cha mchana au staftahi (breakfast).
Kwa kuwa na kiasi kikubwa ha ufumwele, ndizi husaidia tumbo kufanya kazi vyema na kupambana na matatizo ya choo au constipation.]
Kwa wale wanaosumbuliwa na ulevi na pale wanapotaka kuondokana na hali ya hangover, basi suluhisho lao ni ndizi. Kwa kunywa mchanganyiko wa ndizi, maziwa na asali (banana milkshake) wanaweza kuondokana haraka na hali ya ulevi.
Pale unapong'atwa na mdudu, kabla ya kutumia krimu ya kuua sumu ya wadudu, jaribu kusugua sehemu ya ndani ya ganda la ndizi pale ulipong'atwa. Kufanya hivyo husaidia kupunguza maumivu, uvimbe na kuwasha.
Ndizi zina kiasi kikubwa cha vitamin B, hivyo husaidia mfumo wa fahamu.
Kwa wanawake na wasichama wanashauriwa kula ndizi kabla ya siku zao za mwezi, kwani husaidia kukabilina na PMS au kutojisikia vyema kabla ya hedhi.
Ndizi zinaweza kuwasaidia wale wanaotaka kuacha kuvuta sigara.
Na kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya MIND, watu wenye matatizo ya msononeko wa mawazo na fikra, (depression) hujisikia vyema pale wanapokula ndizi. Hii ni kwa sababu ndizi zina tryptophan, ambayo ni aina ya protini inayobadilishwa mwilini na kuwa serotonini, mada ambayo huufanya mwili ujisikie vyema na kwa ujumla humfanya mtu asikie furaha.
Basi kwa kujua baadhi tu ya faida za ndizi, mtakubaliana na mimi kuwa ni muhimu tule ndizi kwa ajili ya afya zetu.
Lakini kumbuka kuwa, haushauriwi kula ndizi iwapo una ugonjwa wa kisukari na haifai kuhifadhi ndizi katika jokovu au friji kwani kufanya hivyo hupelekea ndizi kupoteza uwezo wake huo wa kitiba.
Haya shime na tusikose ndizi katika vyakula vyetu.

Saturday, October 17, 2009

Utafiti mpya washauri kuwa, watoto wasipewe Paracetamol baada ya chanjo!


Wataalamu wanasema kuwa, kuwapa watoto paracetamol baada ya kupata chanjo ili kuuzia homa, kunaweza kupunguza athari ya chanjo. Utafiti uliofanywa kwa watoto 450 waliopatiwa chanjo umeonyesha kwamba, ni kweli dozi ya paracetamol inapunguza homa kwa masaa 24 baada ya kupewa mtoto, lakini uchunguzi huo umeonyesha pia kuwa, dawa za kupunguza maumivu zina changia kwa kiasi kikubwa kupunguza athari ya chanjo.
Vilevile Madaktari wa Uingereza wameunga mkono uchauri kwamba, haifai kuwapa dawa watoto bila sababu maalum. Kwa hivyo wameshauri kuwa, ni bora wazazi wasiwape watoto paracetamol kabla ya chanjo, kwa kuhofia kuwa huenda wakapatwa na homa baada ya kupatiwa chanjo. Hii ni mara ya kwanza kuonekana athari hiyo na wataalamu wanasema kuwa huenda paracetamol ikawa inaaingilia kati radiamali (response) za seli za kulinda mwili kwa kinga.

Friday, October 16, 2009

Wanawake 70 elfu hufariki dunia kila mwaka kutokana na utoaji mimba usio salama


Ingawa njia za kuzuia mimba hupunguza utoaji mimba holela kwa kiasi kikubwa, lakini ulimwengu unashuhudia wanawake 70 elfu wakipoteza maisha yao kila mwaka kutokana na kutumia njia zisizo salama kutoa mimba. Ripoti zinasema kuwa hata hivyo kiwango cha utoaji mimba kimepungua duniani ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Katika nchi ambazo kumekuwa na sheria kali za kuzuia utoaji mimba, kumeshuhudiwa utoaji mimba wa kutumia njia siziso salama kwa afya ya mama ukiongezeka zaidi.
Hata hivyo bado takwimu zinaonyesha kuwa, utoaji mimba holela umeendelea kuwa tatizo sugu linalogharimu maisha ya wanawake 70,000 kila mwaka duniani. La kusikitisha zaidi ni kuwa vifo hivyo hutokea zaidi katika nchi zilizoko Afrika chini ya jangwa la Sahara.
Wakinamama na wanawake wanapaswa kujua kuwa, utoaji mimba holela na kwa kutumia njia zisizo salama zaidi ya kuhataraisha maisha ya mwanamke, humsababishia pia matatizo mbalimbali ya kiafya na pengine hata kupelekea asiweze tena kubeba mimba baadaye.
Ni muhimu kwa baba na mama kupanga uzazi ili kuboresha maisha ya familia zao na pia kulinda maisha ya mama. Chambelecho waswahili : kukinga siku zote ni bora zaidi kuliko kuponya"!

Monday, October 12, 2009

Mask ya ndizi na asali kwa ajili ya ngozi zenye mafuta


Baada ya kuelezea namna ya kutengeneza mask ya Avocado ambayo ni kwa ajili ya ngozi za kawaida na zilizo kavu, hebu sasa na tuangalie namna ya kutengeneza mask ya ndizi na asali kwa ajili ya ngozi zenye mafuta na kutoka chunusi.
Vinavyohitajika
• Ndizi moja iliyoiva vyema.
• Asali kijiko kimoja cha chakula.
• Limau, ndimu au chungwa moja.

Namna ya kutengenza:
1. Menya ndizi na uiponde vizuri, kisha changanya katika kibakuli safi pamoja na asali.
2. Kamua limau, ndimu au chungwa, toa kokwa na maji yake changanya kwenye mchanganyiko wa ndizi na asali.
3. Chanyanya vizuri hadi upate mchanganyiko sawia.
4. Paka mchanganyiko huo usoni na shingoni bila kuweka machoni.
5. Wacha kwa muda wa dakika 15 na osha kwa maji ya uvuguvugu.

Saturday, October 10, 2009

Kujitayarisha kabla ya Ujauzito


Kina mama na wanawake wanashauriwa kufanya matayarisho kabla ya kushika mimba. Imeonekana kuwa kufanya matayarisho kabla ya mimba haijatunga kuna faida kubwa kwa mama mwenyewe na mtoto anayezaliwa. Kuutayarisha mwili wa mama kabla hajabeba mimba, huifadhi afya ya mama wakati wa ujauzito hata baada ya kujifungua uwe na faya bora zaidi. Miongoni mwa matayarisho anayotakiwa kufanya mwanamke kabla ya kushika ujauzito ni pamoja na kupima magonjwa mbalimbali kama vile kisukari, presha na ugonjwa wa moyo ili kuona kama ana magonjwa hayo au la. Vilevile mama anashauriwa kujitahidi kuwa na uzito unaotakiwa kwa kuzingatia kimo chake. Yaani asiwe mnene au mwembamba sana kabla ya kubeba mimba bali awe na uzito wa wastani.
Suala hilo linaweza kutekelezwa kwa mwanamke anayetaka kubeba mimba kuhudhuria hospitalini au kuonana daktari mtaalamu wa masuala ya uzazi au mkunga. Daktari wa kawaida pia anaweza kutoa ushauri kuhusiana na suala hilo.
Mimba nyingi hutungwa bila kupangwa, suala ambalo mara nyingi hupelekea mama na hata mtoto aliye tumboni akabiliwe na hatari mbalimbali hasa wakati wa wiki 8 ya mwanzo ya ujauzito. Kwani wakati huo kina mama wajawazito huwa hawafahamu kuwa wana mimba, na wakati wanapotambua na kwenda hospitalini au kumuona daktari au mkunga, muda mwingi unakuwa umeshapita. Mwanamke anapokwenda hospitalini au kumuona daktari kwa matayarisho kabla ya kubeba mimba, huchunguzwa mambo mablimbali. Baadhi ya mambo hayo ni.
 Uzito aliokuwa nao, kama ni mnene sana hushauriwa kupunguza unene wake kwa kufanya mazoezi na kula vyakula vinavyotakiwa na kama ni mwembamba sana pia hushauriwa kuongeza uzito ili kufikia kiwango kinachotakiwa.
 Hupimwa magonjwa mbalimbali kama vile kisukari na kuangaliwa iwapo ana kisukari aina ya kwanza au ya pili.
 Hupimwa kama ana shinikizo la damu au la.
 Hushauriwa kutumia vidonge vya Vitamini E na C, kula vyakula vyenye Calcium, ufumwele, Magnesium na chuma (Iron).
 Hushauriwa kuanza kutumia vidonge vya Folic Acid na kula vyakula vinavyoweza kuupatia mwili wake mada hiyo. Imeonekana kuwa, Foic Acid humzuia mtoto aliyeko tumboni asipatwe na matatizo ya ubongo na mfumo wa fahamu. Mama mjamzito anashauriwa kuanza kutumia vidonge vyenye faida kubwa vya Folic Acid miezi mitatu kabla ya kutunga mimba.
 Kujiepusha au kupunguza kula vyakula vyenye Kafeini kama vile chai, kahawa, hot chocolate na vinywaji vyenye kafeini kama Coca Cola.
 Kujiepusha au kuacha uvutaji sigara.
 Kupima baadhi ya magonjwa ya kurithi na magonjwa mengineyo kama vile Talasemia, HIV na kadhalika.
 Kufanya mazoezi ili kuutayarisha mwili na kubeba ujauzito. Imeonekana kuwa kufanya mazoezi kabla ya kubeba mimba kuna faida nyingi kwa mama na mtoto anayezaliwa.

Thursday, October 8, 2009

Namna ya Kutengeneza Mask ya Avocado


Vinavyohitajika:
1.Avocado moja lililoiva vyema.
2.Mtindi kijiko kimoja cha chakula.
3.Asali asilia (natural honey).
4.Maji ya ndimu/limao.

Namna ya kutayarisha:
Kata Avocado katika vipande viwili, ondoa kokwa na menya.
Changanya avocado ulomenya na mtindi, asali na maji ya ndimu au limao. Koroga mapaka upate mchanganyiko wa hali moja halafu weka pembeni.
Chukua maganda ya avocado na kwa upande wa ndani ya maganda hayo sugulia uso na shingo. Kufanya hivyo husaidia kuondoa seli zilizokufa na ngozi zilizoharibika. Pia huutayarisha uso kwa ajili ya mask.
Kisha paka mchanganyiko uliotayarisha usoni na shingoni (sio machoni).
Subiri kwa dakika 15 na kisha osha kwa maji vuguvugu.

Wednesday, October 7, 2009

Nani kasema Maharagwe si Mboga?


Mie naamini maharagwe ni mboga tena yanaweza kuwa ni mboga zaidi
kuliko hata mboga nyinginezo zinazoliwa kama mboga. Hii inatokana na ukweli unaotokana na faida tele na muhimu zinazotokana na chakula hicho. Wataalamu wanatuambia kuwa katika kila gramu 100 za maharagwe tunaweza kupata gramu 22 za protini, gramu 6 za madini ya chuma, miligramu 1370 za Potassium na mikrogramu 130 za Folic Acid.
Si vibaya pia ukijua kwamba, kuzoea kula maharagwe kila mara kunazuia hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo kwani husaidia kupunguza kiwango cha mafuta aina ya Colestrole mwilini. Kwani maharagwe yamejaa protini na ufumwele (Fibres) ambazo husaidi sana katika suala hilo.
Halikadhalika kwa wale wanaotaka kupunguza uzito maharagwe ni miongoni mwa vyakula wanavyoshauriwa kula.
Pia ni miongoni mwa vyakula vinavyosaidia katika kupunguza uwezekano wa kupata kisukari.Bila kusahau kuwa maharagwe huongeza kiwango cha mada iitwayo Leptin mwilini, ambayo hukufanya usitamani kula (appetite reducer), kinyume na vyakula vyenye sukari ambavyo kila unapokula leptin huzalishwa kwa kiwango kidogo mwilini na kukufanya utake kula zaidi.
… ndio sababu basi nikasisitiza tena na tena kuwa….Maharagwe ni mboga, tena mboga iliyo bora!

Tuesday, October 6, 2009

Sababu 18 zinazokulazimu upunguze uzito wako na uuogope unene!


1. Unene unaongeza kiwango cha mafuta mwilini, ambayo huongeza uwezekano wa kupata kensa.

2. Unene unaongeza mafuta mwilini, ambayo hufanya matibabu ya kensa yawe magumu zaidi.

3. Unene huongeza mafuta mwilini ambayo huushinikiza nu kuubana moyo.

4. Mtu mnene huwa mvivu kufanya mazoezi, suala ambalo humuongezea zaidi unene.

5. Mafuta mengi mwilini yana madhara kwa ubongo.

6. Unene huathiri hata tabia na miamala ya mtu.

7. Unene huongeza uzito katika mifupa na viunga vya mifupa (bone joints).

8. Unene husababishwa kibofu cha mkojo kibanwe suala linalopelekea matatizo mbalimbali ya mkojo.

9. Unene hupunguza uwezo wa mtu wa kijinsia.

10. Unene hupunguza uwezo wa kuzaa na hata kupelekea utasa na ugumba.

11. Unene hupelekea mwili upatwe kwa wepesi na magonjwa mbalimbali kama vile kisukari na presha.

12. Watu wanene wanapohudhuria mahospitali upimaji wao pia huwa wa matatizo.

13. Unene husababisha ujauzito kuwa wenye matitizo mengi.

14. Unene huathiri pia afya ya mtoto mchanga anayezaliwa.

15. Unene hufanya matibabu ya athma yawe magumu.

16. Unene hupelekea mtu asilale vizuri, na wakati mwingine mtu mnene anapolala hupanwa na pumzi suala linalompelekea kuamka mara kwa mara.

17. Unene humfanya mtu ashindwe kuwajibika vizuri kazini, na hata huweza kuathiri ajira yake.

18. Unene hufanya matumizi ya fedha yawe makubwa.

……Je? Hata baada ya kujua hayo yote bado unaupenda unene?!

Monday, October 5, 2009

Hatimaye Wizara yaagiza vyumba vya 'leba' visafishwe



KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, amewaagiza wakunga katika hospitali za Serikali wahakikishe kwamba vyumba kwa ajili ya akinamama kujifungua ni visafi kila siku.

Nyoni amesema, kama chumba kwa ajili ya kujifungua ni kisafi hakutakuwa na maambukizi yoyote kwa mama au mtoto anayezaliwa.

Amewataka wakunga hao wahakikishe kwamba, suala hilo linakuwa sehemu ya kazi yao kila siku. Amesema, hospitali nyingi za Serikali hasa wodi wanazotumia akinamama kujifungua ni chafu.

“Usafi ni tiba kwa asilimia 60 hivyo hakikisheni kwamba sehemu mnazofanyia kazi zinakuwa safi ili kuwapa imani akinamama wanaokuja kupata huduma yenu,” amesema Nyoni.

Nyoni amesema, tabia ya wakunga wengi kutojali maeneo wanayofanyia kazi inasababisha hali hiyo. Ameyasema hayo leo wakati anafungua mkutano ulioandaliwa na Chama cha Wakunga Tawi la Muhimbili, Dar es Salaam kujadili kuhusu matumizi ya njia bora za uzazi wa mpango.

Nyoni amesema,katika ziara zake za kutembelea hospitali mbalimbali za Serikali nchini, amekuta uchafu wa kutisha.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Serikali, uchafu huo unaweza kusababisha maambukizi mapya kwa akinamama hao. Aliwataka wakunga hao waache visingizio kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Kwa mujibu wa Nyoni, Bohari Kuu ya Dawa (MSD), imenunua kila aina ya kifaa kinachohitajika katika hospitali za serikali.

“Jamani kwa hili naomba usafi kiwe kipau mbele chenu, nilienda pale Muhimbili hali niliyoikuta sikuifurahia; lakini wameniahidi kuwa nikirudi tena sitakuta ile hali ya uchafu,” amesema.

Nyoni pia aliwataka wakunga hao kuwa wawazi kwa wagonja wanaowahudumia ili kuweka ujirani kati yake na mgonjwa.

Amesema, kumekuwa na tabia ya wakunga kutokuwa wawazi kwa wagonjwa wao hivyo kumfanya mgonjwa kutokuwa na habari kamili kuhusu ugonjwa wake.