Wednesday, May 26, 2010

DAWA ZA KIUNGULIA ZINASABABISHA MPASUKO WA MIFUPA



Taarifa mpya zinasema kwamba, maafisa wa afya wametahadharisha juu ya kutumiwa kwa muda mrefu dozi kubwa ya dawa za kuondoa kiungulia, (heartburn) na kusisitiza kwamba zinasababisha mifupa kupasuka. Dawa hizo ni zile zinazojulakana kama Proton Pumping Inhibitors (PPI) zinazozuia kiungulia na ambazo hutumiwa kudhibiti kiwango cha asidi katika tumbo na pia kutibu ugonjwa wa GERD au gastroesophageal reflux disease. Taarifa hizo zilizotolewa na Kitengo cha Kusimamia Vyakula na Dawa cha Marekani (FDA) zinasema kwamba, dawa hizo za kingulia huongeza uwezekano wa kupasuka mifupa ya nyonga (hip), mikono na ute wa mgongo kwa watu wazima, hasa iwapo dawa hizo zitatumiwa kwa mwaka mmoja au zaidi, au kwa dozi kubwa.
Joyce Korvick Mkurugenzi wa masuala ya usalama wa kitengo cha FDA anasema kwamba, kwa kuwa dawa hizo zinatumiwa sana na watu wengi, ni muhimu kwa watu wote kufahamu madhara yanayoweza kusababishwa na dawa hizo. Maafisa hao pia wamewataka madaktari kuwaandikia tu dawa hizo wagonjwa ambao hali zao ni mbaya mno, na kusisitiza kuwa faida ya dawa hizo pale zinapotumiwa mara chache ni zaidi ya hatari inayozisababisha.
Huko nyuma pia wataalamu walisema kwamba, dawa hizo za kutibu kiungulia zinahusiana na ongezeko la hatari ya maambukizo ya bacteria aina ya C. difficile anayesababisha ugonjwa wa kuharisha.
Dawa hizo ni kama zile za Emsomeprazole, Dexlansoprazole, Lansoprazole, Emprazole/Sodium Bicarbonate, Pantoprazole, Rabeprazole na Rabeprazole.
Ndugu mdau kama wewe ni miongoni mwa wanaotumia dawa hizo, basi jihadhari kabla ya hatari!

Sunday, May 23, 2010

WHO YATAHADHARISHA JUU YA UNENE WA WATOTO


Mawaziri wa Afya Duniani huku wakitahadharisha juu ya ongezeko la idadi ya watoto wenye unene wa kupindukia, wamesema kwamba watajaribu kupunguza kutumiwa vyakula holela (junk food) kwa kupiga marufuku matangazo ya vyakula hivyo. Mawaziri hao wa nchi 193 duniani ambazo ni wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wametoa muongozi kwa ajili ya mashirika ya kuuza vyakula na vinywaji visivyokuwa na ulevi kwa ajili ya watoto.
Viwanda vya vyakula na vinjwaji vimetakiwa kuongeza udhibiti katika aina zote za mauzo ya vyakula kwa watoto, na wauzaji vyakula wadogo wadogo pia wametakiwa kuacha kuzalisha na kuuza vyakula ambavyo si vizuri kwa afya ya watoto. WHO imesema kwamba, vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta, sukari na chumvi vinachangia katika kuleta magonjwa sugu kama vile kisukari, maradhi ya moyo na kensa za aina mbalimbali, magonjwa ambayo yanasababisha vifo kwa asilimia 60 duniani kote.
Timoth Armstrong Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa Sugu na Ustawi wa Afya cha WHO amesema kwamba, unene wa kupindukia kwa watoto unaongezeka duniani. Kiwango cha ongezeko hilo katika nchi zilizoendelea ni kikubwa zaidi kwa sababu ya mabadiliko ya kasi ya lishe pamoja na jinsi mwili unavyoshughulishwa.
Yafaa kujua kuwa, tangu mwaka 1980, unene wa kupindukiwa umeongezeka mara dufu kwa watu wazima na mara tatu kwa watoto. Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa, watoto milioni 42 wenye umri wa chini ya miaka mitano wana uzito uliozidi, huku milioni 35 kati yao ni wale wanaoishi katika nchi zilizoendelea kiuchumi. Shirika hilo limeshauri kwamba, inabidi wazazi wapunguze kuwaachia watoto wao kuangalia televisheni, na mashuleni na katika sehemu za michezo za watoto kusiwe na vyakula holela na vinywaji vyenye sukari nyingi.

Thursday, May 20, 2010

Chanjo ya Ndui kuzaidia kupambana na virusi vya HIV


Kutotumiwa chanjo ya ndui katika baadhi ya nchi duniani kunaaminika kuwa kumesaidia katika kueneza maambukizo ya virusi vya HIV, hasa kwa kuzingatia kuwa ugonjwa huo umeongeza sasa siku hizi. Chanjo ya ndui polepole ilianza kutotolewa katika baadhi ya nchi duniani na ugonjwa wa ndui kutokomezwa katikati mwa karne ya 20. Utafiti uliochapishwa katika jarida la BMI Immunology umeonyesha kwamba, chanjo ya ndui ilikuwa ikipunguza maambukizo ya virusi vya HIV, hasa mwanzoni ugonjwa huo ulipogunduliwa duniani. Lakini kuacha kutolewa chanjo hiyo na wataalamu wa Afya, kunaweza kuwa ndio sababu iliyopelekea ongezeko la maambukizo ya ugonjwa wa Ukimwi yaongezeke. Wataalamu waliofanya utafiti huo wanasema kwamba, kuna sababu kadhaa zilinazoweza kutolewa kuhusiana na kasi ya ongezeko la Ukimwi barani Afrika, baadhi ya sababu hizo ni vita, kurudiwa kutumiwa sindano bila kuondolewa vijidudu (unstrelizized needles) pamoja na chanjo za ndui za mwanzo ambazo zilikuwa na vijidudu. Hata hivyo, wataalamu hao wamesema kuwa, sababu zote hizo zimekanushwa au hazitoshi kuelezea sababu ya ongezeko kubwa la maambukizo ya HIV duniani hasa barani Afrika.
Chanjo ya ndui inapunguza uwezekano wa virusi vya HIV kuzaana mara kadhaa katika seli za damu. Pia chanjo hiyo huleta mabadiliko ya muda mrefu katika mfumo wa kulinda mwili, hubadilisha tafsiri ya recepta ya CCR5, ambayo iko juu ya seli za chembechembe nyeupe za damu zinazotumiwa na virusi vya ndui pamoja na HIV.
Wataalamu wanamini kwamba chanjo ya ndui itaweza kutumiwa katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi katika miaka ijayo ya hivi karibuni, lakini pia wamesisitiza kwamba uchunguzi zaidi unapaswa kufanywa ili kuhdibitisha zaidi suala hilo.


Ugonjwa wa ndui ni miongoni mwa magonjwa ambayo yaliitikisa dunia katika miaka ya huko nyuma. Lakini kugunduliwa chanjo ya ndui ambapo kwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa huo mara moja mtu huweza kuwa na kinga dhidi ya ugonjwa huo kwa maisha yake yote, kulipunguza maambukizo ya ugonjwa huo na hatimaye ugonjwa huo ukang'olewa kabisa karibu katika nchi zote duniani. Ndugu mdau, kama huna uhakika kama umepatiwa chanjo ya ndui, basi angalia katika moja ya mabega yako na kama utakuta kovu dogo la duara, basi ujue kuwa una kinga ya ndui. Nawahusia wakina mama wanaowazaa watoto wao siku hizi wahakikishe kwamba wanapatiwa chanjo ya ndui, kwani kama inavyoelezwa mbali ya kumzuia mtoto wako asipate ugonjwa wa ndui maishani, pia hupunguza maambukizo ya ugonjwa wa Ukimwi. Haya tena wadau lakini wewe unafikiri ni sababu gani hasa inayopelekea ongozeko la maambukizo ya Ukimwi katika jamii zetu?..... tueleze maoni yako ili tusaiidiane katika kuifunza jamii na kupambana na ugonjwa hatari wa Ukimwi.

Sunday, May 16, 2010

Kupewa watoto sukari kabla ya chanjo kunapunguza maumivu


Watafiti wa Canada wamesema kuwa, kuwapa watoto sukari kabla ya kupewa chanjo kunapunguza maumivu. Watafiti wa Chuo Kikuu cha Toronto wamesema kwamba watoto wachanga wakipewa matone machache ya maji ya sukari, kabla ya chanjo hawatolia au watapunguza kulia. Hayo yamesemwa baada ya watoto 1,000 wachanga kupewa maji ya glukosi kabla ya kupigwa sindano na kupunguza kulia kwa asilimia 20. Utafiti huo umechapishwa katika jarida la Mafanikio ya Magonjwa ya watoto na umetokana na matokeo ya majaribio 14 yaliyofanywa kuhusiana na suala hilo. DaktaArme Ohlsson aliyeongoza timu ya utafiti huo amesema kwamba umefanywa kwa watoto wasiozidi mwaka mmoja. Pia watatifi hao wamesema kwamba, matone machache tu au nusu kijiko cha maji ya glukosi au sackrosi pia hupunguza muda wa mtoto kulia. Pia wamewashauri maafisa wa afya wawape watoto sakrosi na glukosi kabla ya kuwapatia chanjo. Wamesema kwa kuwa vyakula vitamu vina uwezo wa kupunguza maumivu ndio sababu watoto wanapopewa glukosi kabla ya chanzo huwa hawalii.

Wednesday, May 12, 2010

Kuchoka wakati wa ujauzito na namna ya kujiepusha

Wapenzi wadau natumaini hamjambo! kumekuwa na baadhi ya wadau wanaoniandikia na kuomba ushauri mbalimbali kutokana na matatizo waliyonayo. Nawashukuru sana kwa kuwa wanafuatilia yale yanayojiri katika blogi hii na kupata ingawa machache kuhusiana na afya zetu. Pia nawashukuru kwa kuniwezesha nami kuzungumzia mada mbalimbali kutokana na maswali yenu munayoyauliza. Kwa wale wenye maswali na matatizo mbalimbali tafadhali sana niandikieni kwa kupitia email yangu ambayo ni sthugs4j@gmail.com. Kwani wale wanaoandika maswali yao katika sehemu ya maoni, baadhi ya wakati huwa siyaoni katika muda unaotakiwa na hivyo hunifanya nichelewe kuwajibu. Wote mnashukuriwa. Leo tutazungumzia suala la kujihisi uchovu wakati wa ujauzito ambalo limeulizwa na mmoja wa wadau wanaofuatilia kwa karibu kona ya afya nami nalijibu swali lake kama ifuatavyo.

Wanawake wengi kwa kawaida huwa wanahisi uchovu wakati wa ujauzito. Uchovu, kulegea mwili na kuishiwa na nguvu ni jambo la kawaida katika kipindi hicho. Hii ni kwa sababu mwili katika kipindi hiki unatumia nguvu za kiada ili kuunda kiumbe kipya. Pia wakati huu mwili hutengeneza damu kwa wingi zaidi ili kufikisha chembechembe za chakula kwa mtoto, suala ambalo huufanya mwili ufanye kazi ya ziada na hata viungo vingine muhimu kama vile moyo na vinginevyo. Uzito wa mtoto nao unaoongezeka katika mwili wa mama mjamzito siku baada ya siku, ni sababu nyingine inayomfanya mama mjamzito ajihisi kuchoka. Kuchoka au kiushiwa na nguvu ni tatizo la kawaida hasa katika miezi mitatu ya mwanzo ya mimba. Katika miezi hiyo ya mwanzo ya mimba tatizo hilo husababishwa na mabadiliko ya homoni za mimba mwilini hasa progestrogen na wakati mwingine hali hiyo huongezwa na kichefuchefu na kutapika. Hali hiyo ya mchoko inatarajiwa kuisha inapoingia miezi mitatu ya pili ya mimba. Lakini pia kuna wengine ambao hali hiyo ya kuchoka huendelea nayo hadi wakati wa kujifungua. Kushindwa kulala vizuri kutokana na kwenda mara kwa mara msalani, au kukosa uzingizi kutokana na ongezeko la ukubwa wa tumbo mwishoni mwa ujauzito, ni miongoni mwa masuala ambayo humfanya mama mjazito ajisikie mchovu na akose nguvu siku nzima.
Vilevile mabadiliko ya kifizikia na kisaikolojia ya wakati wa ujauzito humfanya mama mjamzito awe na morali ya chini na kuhisi uchovu wa kimwili na hata kiakili. Sababu nyinginezo zinaweza kutokana na kazi mbalimbali anazofanya mama huyo au pia ukosefu wa lishe inayofaa na ya kutosha kwa ajili ya mwili wake, ambao unahitajia nguvu ya ziada hasa kwa ajili ya uumbaji wa ukamilifu wa mtoto aliye tumboni.
La muhimu analoshauriwa mama mjamzito ni kutoogopa na kutotishwa na hali hiyo, kwani inatokana na baadhi ya mabadiliko yanayotokea katika mwili wake. La muhimu ni mama mjamzito kufuata ushauri unaotakiwa ili kukabilina na hali hiyo.
Zifuatazo ni njia za kukabiliana na uchovu wakati wa ujauzito.
• Kwanza kabisa mama mjamzito anatakiwa ale vyema. Mama mjamzito anatakiwa ale chakula bora na kamili, chenye kalori 300 au 500 za ziada ikilinganishwa na mtu asiye mjamzito kwa siku. Lakini awe mwangalifu na ni bora akigawe chakula chake katika sehemu ndogo ndogo 5 au 6 (suala hili tumelizunguzia kwa undani katika makala iliyopita ya kiungulia wakati wa ujauzito, tafadhali pitia makala hizo). Anaweza akawa akibeba matunda na mboga mboga kama asusa (snacks) kwa ajili ya kula kila anapohisi njaa popote pale awapo. Lakini ni bora ajiepushe na vyakula vyenye sukari nyingi na caffeine, kwani vyakula hivyo huyeyuka haraka mwilini na kumfanya ahisi njaa mapema.
• Mama mjamzito ahakikishe kuwa hana upungufu wa damu. Na kama anao basi atumie dawa za kuongeza damu zinazotolewa na madaktari, au ale vyakula vinavyoongeza damu. Hii ni kwa sababu ukosefu wa madini ya chuma mwilini unaosababisha ukosefu wa damu, ni miongoni mwa sababu zinazomfanya mama mjamzito ahisi kuchoka. Mtu mwenye ukosefu wa damu (Anemia) huhisi kubanwa na pumzi, ongezeko la mapigo ya moyo, udhaifu, kupauka na kizunguzungu. Onana na daktari iwapo una dalili kama hizo.



• Mama wajawazito wanashauri kujipumzisha nyakati za mchana. Ni bora mama mjamzito apumzike kwa kadri anavyoweza wakati wa mchana, baada ya chakula cha mchana au hata kabla ya nyakati za magharibi. Ikiwa unafanya kazi, basi pumzika mara kwa mara japo kwa muda mfupi ili kufanya mwili upate nguvu.
• Mama wajawazito wanashauriwa kujitahidi kulala mapema, hasa kama ikiwa inakubidi uamke mara kadhaa usiku kutokana na sababu mbalimbali, kama vile kwenda msalani, kula au kutokana na maumivu.
• Kufanya mzoeni husaidia kupunguza uchovu na kuna faida kemkem wakati wa ujauzito. Kahusiana na suala hilo soma makala zilizotangulia.
• Mama mjamzito anatakiwa anywe maji ya kutosha. Ukosefu wa maji mwilini huchangia kumfanya mama mjamzito ahisi uchovu.
• Usifanye kazi nyingi kutwa nzima, na kama inawezekana ni bora usaidiwe kazi hizo hasa za nyumbani na watu wengine katika familia kama vile watoto, mume ndugu, jamaa na marafiki.
• Usikilize mwili wako. Pale unaposikia njaa basi kula na pale unapojisikia uchovu jitahidi upumzike.
• Pata ushauri wa daktari iwapo unahisi uchovu wa kupindukia au unachoka kila mara, ili uwe na uhakika kuwa hakuna tatizo au hatari inayoweza kuhatarisha maisha yako na ya mtoto.

Saturday, May 8, 2010

Kula zabibu usipatwe na ugonjwa wa moyo


Wadau msichoke na mimi kuzungumzia ugonjwa wa moyo, au nisiseme mimi, bali niseme wataalamu ambao kila siku wamekuwa wakifanya majaribio na kutuelewesha vyakula au njia zinazotuepusha na ugonjwa huu. Hii ni kwa sababu ugonjwa wa moyo kweli ni tishio duniani kote. Ni wiki iliyopita tu mfanyakazi mwenzangu ambaye nilikuwa naye kazini hadi nyakati za mwisho za kazi, siku ya pili nakuja kazini naambiwa kafariki dunia kwa mshituko wa moyo. Masikini baba wa watu!!, huku akiwa anayetegemewa na familia, akiacha mke na mtoto ameondoka kama utani tena kwa kufumba na kufumbua. Baada ya kutoka kazini alikaa juu ya kochi na kujiegemeza akisubiri atengewe msosi, lakini hapo hapo aliaga dunia. Msosi ulipotengwa na mkewe kumuamsha ale akidhani labda amepitiwa na usingizi, aliona haamki tena, na ndipo walipomkimbiza hospitalini. Huko waliambiwa ameshakufa zamaaani kutokana na mshituko wa moyo!.
Sasa hali ni hii, na hivi karibuni uchunguzi mpya umeonyesha kwamba kula zabibu au vyakula vyenye zabibu ndani yake kunapunguza shinikizo la damu, husaidia moyo kufanya kazi zake vyema na kupunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo uliotolewa kenye mkutano wa Majaribio ya Bayolojia huko California, zabibi zina uwezo wa kupunguza shinikio la damu, husaidia mwili uweze kuvumilia sukari (glucose tolorance) na kupunguza kiwango cha mafuta aina ya triglycerides mwilini ambayo ni chanzo cha matatizo ya moyo.

Wataalamu wanasema zabibu pia zinaweza kupunguza uvimbe, uharibivu unaotokana na free radicals zinazozalishwa mwilini na shinikizo la moyo.
Kwa ujumla zabibi zinazuia hali inayoitwa Metabolic Syndrome suala ambalo linatokana na mada za phytochemicals zilizoko kwenye matunda hayo.
Metabolic Syndrome ni mchanganyiko wa matatizo ya kitiba ambayo yanaongeza uwezekano wa kupatwa na maradhi ya mishipa ya damu pamoja na kisukari.
Hivyo wataalamu wanatushauri tule zabibi au kuongeza zabibu katika vyakula wanavyokula kila siku, ili tujikinge na ugonjwa wa Metabolic Syndrome, ugonjwa wa moyo na kisukari aina ya pili.
Haya shime tule zabibu kwa ajili ya afya zetu!.

Friday, May 7, 2010

Kweli lishe bora inaongeza umri…. Afa akiwa na miaka 114!


Mwanamke wa Kijapan aliyevunja rikodi ya Dunia ya Guinness kwa kuwa mtu mzee zaidi duniani amefariki dunia siku kadhaa zilizopita, akiwa na umri wa miaka 114 na siku 357. Mwanamke huyo aitwaye Kama Chinen alikuwa akiishi katika kisiwa cha Okinawa na alifariki dunia Mei 2, ambapo aliishi na kushuhudia karne tatu!. Inasemekana kuwa bibi huyo aliishi muda mrefu kwa kuwa lishe yake ilikuwa chai ya kijani, supu ya miso, mboga mboga, wali na samaki freshi. Bi. Chinen sio makazi pekee wa eneo hilo la Japan aliyeishi muda mrefu, kwani ripoti zinasema kuwa watu wengi wanaoishi eneo hilo huishi maisha marefu na ni kutokana na lishe yao. Japan ndio nchi inayoongoza kwa kuwa na kiwango kirefu zaidi cha maisha ya watu (Highest Life Expactancy) huku Okinawa ukiwa mji ulio na watu wengi wenye umri mrefu, suala ambalo linatokana na lishe bora na hali ya hewa ya kisiwa hicho.
Kwa mujibu wa utafiti, mji wa Okinawa una kiasi kidogo sana cha watu wenye magonjwa ya kensa, na hiyo inatokana na watu kula vyakula vyenye mafuta kidogo, kalori chache, ufumwele kwa wingi na mboga mboga na matunda kwa kiasi kikubwa. Pia suala lingine ni kujishughulisha kwao na wala sio kukaa tu.

Wednesday, May 5, 2010

Kukosa usingizi kunasababisha vifo vya mapema


Imetahadharishwa kwamba kulala usingizi wa chini ya masaa 6 kila usiku kunaweza kusababisha mtu apatwe na kifo cha mapema. Watafiti wamesema kuwa watu ambao kwa kawaida huwa wanalala masaa hayo machache wengi wao hupatwa na vifo vya mapema kwa asilimia 12 zaidi ya wale wanaolala kawaida kwa masaa 8. Vifo ambavyo hutokea katika umri wa baada ya miaka 25. Pia imeonyeshwa kwamba kulala zaidi ya masaa 9 pia kunapelekea vifo vya mapema ingawa kulala huko kunaweza kukawa na uhusiano na matatizo ya kiafya. Utafiti huo umetolewa kwa kuchunguzwa uhusiano uliopo kati ya kifo na usingizi kwa kutegemea chunguzi 16 zilizofanywa kwa kuwahusisha watu milioni 1 na nusu katika nchi za Uingereza, Marekani , Ulaya na Mashariki mwa Asia.
Profesa Francesco Cappiccio aliyeongeza utafiti huo wa chuo kikuu cha Warwick cha Uingereza anasema jamii za hivi sasa zilizoendelea zimekuwa taratibu zikipunguza muda wa kulala, na tatizo hili linawapata sana watu wanaofanya kazi masaa mengi. Amesema suala hili linaonyesha kwamba hayo yote yanatokana na mashinikizo ya kimaisha yanayowapelekea watu wafanye kazi masaa mengi na kuchukua shift nyingi za kazi. Amesema kwamba, kuporomoka kwa afya kunaambatana na kulala masaa mengi zaidi. Wataalamu wanasema kuwa, watu wanapaswa kufahamu kwa nini hasa usingizi ni suala muhimu sana kwa afya nzuri. Usingizi ni kama karatasi ya litmus inayoonyesha afya na hali ya mwili na akili ya mtu kwani usingizi unaathiriwa na magonjwa na hali mbalimbali ikiwemo msongamano wa mawazo au depression, anasema mtaalamu huyo. Inashauriwa kuwa tusilale masaa machache wala mengi bali tulala kwa masaa ya wastani ambayo ni masaa 8.

Monday, May 3, 2010

Madaktari waboronga katika upasuaji Afrika Kusini na kuhatarisha maisha


Gazeti moja nchini Afrika Kusini limefanya uchunguzi na kuripoti kuwa, madakitari wa upasuaji nchini humo wanafanya kazi isiyo ya kuridhisha na yenye kuhatarisha maisha ya wagonjwa wanaokwenda kupasuliwa. Gazeti la Sunday Independent limesema kuwa, uchunguzi wao umedhihirisha kuweko malalamiko ya waliopasuliwa, wengine wakilazimika kurudi kufanyiwa upasuaji mwingine, wanapogundua vifaa fulani vimeachwa mwilini mwao. Gazeti hilo limemnukuu msemaji wa Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Fidel Hadebe akisema, amepokea ripoti kwa mhasiriwa mmoja aliyedai kuwa, mikasi ilibakia tumboni mwake alipofanyiwa upasuaji. Aidha uchunguzi wa gazeti hilo umeonyesha kuwa, sababu ya kushuhudiwa hali kama hizo uhaba wa matabibu nchini humo, jambo linalopelekea madaktari wachache walioko, kuboronga katika kazi zao katika juhudi zao za kuhakikishwa wanawafanyia upasuaji wagonjwa wengi.

Sunday, May 2, 2010

Kula aina mbalimbali za matunda kuna faida zaidi kiafya



Uchunguzi mpya umeonyesha kwamba watu wanaweza kukabiliana kirahisi na magonjwa mbalimbali kwa kula matunda ya aina mbalimbali na mboga mboga badala ya kuongeza idadi ya matunda na mboga mboga hizo. Kwa mujibu wa uchunguzi huo uliotolewa katika Kongamano la Majaribio ya Kibiolojia huko Anahein California, baadhi ya matunda na mboga mboga yana faida kubwa ya lishe kuliko mengineyo. Uchunguzi huo umeeleza kwamba,ingawa karoti inaaminiwa kuwa ni chanzo kikubwa cha beta-carotene lakini kula viazi vitamu badala ya karoti kunaweza kuupatia mwili beta-carotene mara dufu kuliko karoti. Papai nalo lina beta-cryptoxanthin mara 15 zaidi ya machungwa. Halikadhalika mboga aina ya Kale huupatia mwili mada ya lutein/zeaxanthin mara tatu zaidi ya spinachi. Pia imeelezwa kuwa stroberi na rasberi zina ellagic asid mara tatu zaidi huku kikombe kimoja cha maji yanayotokana na mmea uotao majini wa watercress ikiwa na mada ya isothiocyanate sawa na inayopatikana katika vijiko vine vya chai vya haradali au mustard. Bi. Keith Rabdolph aliyeongeza uchunguzi huo anashauri kwamba, watu wajitahidi kujua umuhimu wa vyakula wanavyokula na kujua pia ubora na faida za matunda na mboga mboga wanazokula kwa afya ya miili yao.