Sunday, February 28, 2010

Tikitimaji chungu zinasaidia kuzuia kensa ya matiti


Utafiti mpya umegundua kuwa mada zinayotokana na tikitimaji ambazo ni mboga mboga zinazopatikana sana India, China na Amerika ya Kusini zinaweza kusaidia kuwaepusha wanawake na kensa ya matiti. Kwa mujibu wa uchunguzi huo uliochapishwa kenye jarida la Utafiti wa Kensa, majimaji (extract) yanayotolewa katika tikitimaji chungu yanayojulikana kama 'karela' kwa kihindi yanaweza kupunguza kasi ya kukua kwa seli za kensa ya matiti au hata kuua kabisa seli hizo. Ratna Ray aliyeongoza uchunguzi huo anasema kwamba, tikitimaji chungu zina uwezo wa kuzuia kensa na kuchelewesha kutokea ugonjwa huo wa saratani ya matiti, lakini bado haijathibitika iwapo mboga mboga hizo zinaweza kutibu ugonjwa huo.
Wanasayansi wanasema kuwa uchunguzi zaidi unapaswa kufanywa ili kuhakikisha uwezo na usalama wa tikitimaji chungu kuhusiana na suala hilo. Ratna Ray aidha anasema kuwa, kutumia lishe asilia ni suala linalopewa umuhimu mkubwa hivi sasa na sayansi katika kuzuia ugonjwa wa saratani ambao umekuwa ukiongezeka siku baada ya siku. Mtaalamu huyo vilevile amesema, katika siku za usoni watafanya uchunguzi utakaowahusisha watu wengi zaidi walio na hatari ya kupata kensa ili kuona iwapo tikitimaji chungu zitawazuia wasipate ugonjwa huo au la.
Kwa muda mrefu tikitimaji chungu ambazo zina Vitamin C na mada ya flavonoid zimekuwa zikijulikana kwa kuwa na uwezo wa kuzuia kisukari na kupunguza kiwango cha sukari katika damu.

Kujipumzisha mchana huimarisha akili!


Uchunguzi mpya umeonyesha kuwa kulala kidogo wakati wa mchana huhuisha ubongo na kuimarisha uwezo wa kufahamu mambo mapya. Profesa Matthew P. Walker wa Kitengo cha Saikolojia na Sayansi ya ubongo cha Chuo Kikuu cha Calfornia aliyeongoza uchunguzi huo anasema kwamba, unahitaji kulala kabla ya kujifunza, ili kuutayarisha ubongo wako ili uwe kama sponchi kavu linalosubiri kunyonya taarifa mpya. Akielezea umuhimu wa kujipumzisha mchana hasa kwa wale wanaosoma na kujifunza Profesa Walker anasema kwamba, usingizi sio tu huondoa uchovu na kufuta makosa yanayotokana na kuwa macho muda mrefu, bali pia humrejesha mtu pale alipokuwepo kabla ya kulala. Wataalamu wanasema kuwa, kila mtu anapoongeza masaa ya kukaa macho ndivyo hivyo hivyo uwezo wa ubongo wake wa kuelewa mambo unavyopungua. Professa Walker akitoa mfano ili kufahamisha zaidi umuhimu wa kupumzisha ubongo ili kuongeza uwezo wa kujifunza, anaufananisha ubongo na sanduku la barua pepe na kusema kwamba iwapo sanduku hilo litajaa basi hutoweza kupata barua pepe mpya hadi pale utakapoondoa barua pepe zisizotakiwa au kuzipelekea katika folder jipya, na kulala nako huusaidia ubongo hivyo hivyo.
Uchunguzi huo unaunga mkono utafiti wa huko nyuma unaosema kwamba, kukaa macho muda mrefu usiku hupunguza uwezo wa mtu wa kuelewa mambo mapya kwa karibu asilimia 40, kwani baadhi ya sehemu za ubongo hufunga baada ya kukosa usingizi kwa muda mrefu.

Saturday, February 27, 2010

Nchini Tanzania ....Wanawake mijini walemewa vitambi


UWEZEKANO wa wanawake wa mijini kupata vitambi ni mkubwa mara mbili ya asilimia 32 kwa miaka kumi ijayo tofauti na wa vijijini kwa asilimia 12 katika miaka hiyo, imeelezwa.

Hata hivyo hali ya mama na mtoto kwa sasa ni bora, licha ya kujitokeza tatizo la vitambi na karibu matatizo yote yanayohusu ustawi wa mama ni makubwa zaidi kwa wanaoishi vijijini kuliko wa mjini.

Hayo yalielezwa na Mratibu wa Elimu ya Awali kutoka Idara ya Elimu ya Msingi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Clarence Mwinuka, Jumatano iliyopita wakati akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi minane.

Mratibu huyo alikuwa ni miongoni mwa wawezeshaji wa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, ambayo yalihusu hali halisi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Tanzania.

Alisema moja ya sababu kubwa za wanawake wa mjini kuota vitambi ni matumizi ya vyakula vya aina mbalimbali bila kuzingatia mazoezi ya mwili, tofati na wa vijijini ambao wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za uzalishaji mali.

Alisema utafiti uliofanyika miaka ya karibuni na Idara hiyo kushirikiana na baadhi ya taasisi na makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya watoto, ambapo wanawake wa mijini wanapaswa kufanya mazoezi ya viungo, ili waondokane na vitambi.

Hata hivyo, alisema utendaji mbovu, malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wadogo, ni kutokuwa na bajeti mahususi kwa ajili ya watoto, kukosekana mpango wa utekelezaji na mwongozo wa viwango vya huduma bora.

Kwa mujibu wa Mratibu huyo, watoto nchini wako katika hatari ya unyanyasaji, ukatili na uonevu, kutokana na kukosekana sheria ya kulinda mtoto inayotekelezeka na kuwa wanawake wamekuwa na sauti ndogo katika uamuzi wa mambo yanayowahusu.

Mratibu huyo alisema umuhimu wa lishe kama msingi wa makuzi bora bado haujatambuliwa ipasavyo nchini, ambapo matatizo yanayotokana na lishe duni kwa watoto wenye umri wa miaka chini ya mitano, ni udumavu kwa asilimia 37.7 na uzito mdogo asilimia 21.8 na ukondefu asilimia tatu.

Friday, February 26, 2010

Ajifungua watoto wawili baada ya kutolewa ovari na kurejeshewa tena!


Mwanammke mmoja wa Denmark amejifungua watoto wawili salama, baada ya kutolewa ovari za uzazi alipokuwa akiugua kensa, ovari hizo kuhifadhiwa katika barafu na baada ya mwaka mmoja zikarejeshwa tena mwilini mwake. Hadi sasa kuna watoto 8 tu ulimwenguni waliozaliwa baada ya mama zao kurejeshewa ovari, na Stinne Holm Bergholdt ni mwanamke wa kwanza duniani aliyeweza kujifungua mtoto wa pili baada ya ovazi zake kuondolewa na kurejeshwa tena. Bi. Bergholdt aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa kensa ya mifupa alipokuwa na miaka 27 na kutokana na hofu ya kutozaa kutokana na athari za tiba ya mionzi na dawa za kensa, aliwataka madaktari wake waondoe ovari zake na kumrejeshea baadaye akipona. Baada ya kupona na mwaka mmoja baadaye alirejeshewa ovari zake na kujifungua mtoto wa kwanza kwa njia ya kupandikizwa mayai katika maabara au Vitro Fertilizertion na kujifungua salama mtoto wa kike aitwaye Aviaja ambaye hivi sasa ana umri wa miaka mitatu. Furaha ya kumzaa mtoto huyo ilimfanya mwamake huyo wa Kidenmark afikirie kuzaa mtoto mwingine. Walipokwenda hospitali ikaonekana kuwa tayari ni mjamzito. Baada ya miezi 9 alijifungua mtoto wa pili wa kike aliyemuita Lucca. Kizazi cha mwanamke huyo kinaendelea vyema na hivi sasa anazuia uzazi ili ajiepushe kushika mimba nyingine.
Taarifa hiyo imeleta matumaini zaidi kwa madakatari na wagonjwa hasa wenye kensa waliokuwa na hofu ya kushindwa kupata watoto hasa baada ya kupata matibabu ya saratani.
Mmh.. suala hili linanifanya nikubaliane zaidi na usemi huu kuwa, Kwa kumtegea Mungu na kwa kupitia sayansi kila kitu kinawezekana!

Wednesday, February 17, 2010

Dawa za Herpes zinaweza kuwasaidia wagonjwa wa UKIMWI


Utafiti mpya umeonyesha kwamba, dawa zinazotumiwa kutibu ugonjwa wa Herpes au ugonjwa wa malengelenge neva ngozini kwa Kiswahili, zinaweza kuwasaidia pia waathirika wa HIV ili wasianze kutumia dawa ya ARV mapema. Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Lanset, dawa hizo zinazoitwa Acyclovir husaidia kupunguza uwezekano wa Ukimwi kushika kasi kwa asilimia 16 kwa mgonjwa. Hata hivyo kutumiwa Acyclovir hakupunguzi maambukizo ya HIV kwa watu wengine, na wataalamu wamesisitiza kwamba dawa za kurefusha maisha ya waathiriwa wa Ukimwi au antiretroviral drugs zina athari zaidi kuliko dawa hiyo ya acyclovir katika kuudhibiti Ukimwi. Madakatari wanasema kwamba, dawa hiyo ambayo haigharimu fedha nyingi inafaa kuokoa maisha ya waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, na kuongeza muda kabla ya kuanza kutumia dawa nyinginezo ambazo ni ghali.
…Tukishirikiana pamoja tutaushinda Ukimwi!

Monday, February 15, 2010

Wanawake wenye umri zaidi ya miaka 35 wasisahau kuzuia mimba, umri sio tija!


Wataalamu wamewapa tahadhari wanawake wenye umri mkubwa kwamba wasijisahau kutumia dawa za kuzuia uzazi, wakiamini kimakosa kwamba hawawezi kupata mimba kwa kuwa wamepitisha umri wa kubeba mimba. Wataalamu wanasema kuwa, ingawa kiwango cha ubebaji mimba hupungua kadri umri wa mwanamke unavyopita miaka 30 lakini haimaanishi kwamba wanawake hao hawawezi kubeba mimba wakiwa katika miaka ya 40 au 50. Imeonekana kuwa watu wengi wakipitisha miaka 35 hujisahau na kudhani kwamba hawawezi kupata mimba tena na hivyo huacha kutumia njia za kuzuia mimba suala ambalo limesababisha kiwango cha utoaji mimba katika nchi za Maghribi kama vile Uingereza kwa wanawake wenye umri wa miaka 40 hadi 44 kiwe sawa na cha wasiachana walio chini ya miaka 16. Kuna sababu nyingi zinazowapelekea baadhi ya wanawake waamue kutoa mimba, mojawapo ni kuhofia hatari ya kuzaa watoto wenye matatizo (abnormalities) tatizo ambalo hutokea sana kwa wanawake wanaobeba mimba katika umri mkubwa. Lakini wataalamu wanasema kwamba sababu nyingineyo ni wanawake waliobeba mimba bila kujua kwa kuwa walidhani hawatapata mimba kwa kuwa wana umri mkubwa. Kwa ajili hiyo madakatari wanawashauri wanawake wote waliofikisha miaka 35 na kuendelea wachukue tahadhari kuhusiana na mimba zisizopangwa na waendelee kutumia njia mbalimbali za kuzuia uzazi hadi pale wanapofikia kukoma hedhi au menopause, iwapo hawataki kupata watoto.
Kwa kawaida kitaalamu umri mzuri wa kubeba mimba ni kati ya miaka 20 hadi 35. Kubeba mimba kabla ya miaka 20 huweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto kutokana na sababu mbalimbali za kiafya, kisaikolojia na kiuchumi na kubebea mimba baada ya miaka 35 nako kuna uwezekano mkubwa wa kuhatarisha maisha ya mama na mtoto. Mimba zinazobebwa baada ya miaka 35 hambatana na matatizo mbalimbali kama vile shinikizo la damu, kifafa cha ujauzito, kisukari cha ujauzito na kadhalika huku mtoto anayezaliwa akiwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na matatizo ya kuzaliwa (abnormalities). Wataalamu wanashauri kuwa iwapo utapata mimba baada ya miaka 35 ni vyema ufanyiwe baadhi ya vipimo wakati mimba bado ni ndogo ili kujua iwapo mtoto aliye tumboni ana matatizo au la.

Sunday, February 14, 2010

Valentine special! ….Jikinge na umkinge umpendae na magonjwa ya zinaa



Leo ni siku ya wapendanao duniani. Katika siku ya leo mijini na mitaani kumejawa na shamshamra na harakati za watu wanaojali wawapendao ambao kwa namna mbalimbali huonekana wakiziweka wazi hisia zao ili kuwadhihirishia wapenzi wao pendo lao. Sio ajabu kukutana na wanaume waliobeba maua yanayoning'inia kadi zenye ujumbe moto moto wa siku hii ya wapendanao, huku wakinamama wakiandaa milo mitamu ili kuikoga moyo ya waume vipenzi wao pale watakaporejea majumbani. Wavulama na wasichana nao hupigana vikumbo katika maduka ya kadi na zawadi wakiwanunulia wapenzi na laazizi wao zawadi mbalimbali na vijana wanaoinukia wakionyesha kutokujali kwa kupigana mabusu barabarani, bila kuwasahau wale wanaojaza fedha simu zao angalau waweze kutuma sms au kuwasabahi kwa simu wapenzi wao ili wajue kuwa hawajawasahau katika siku hii. Yote haya ni katika kuonyesha hisia muhimu ya mapenzi kwa wawapendao katika siku hii maarufu iliyopewa jina la Valentine. Jambo muhimu ambalo lingependa wapendanao wajiulize katika siku hii yao muhimu ni je, kwa kiasi unachomjali na kumpenda mpenzi wako, mke au mume wako na ukawa uko tayari kumdhihirishia penzi lako siku hii kwa zawadi, maua, kadi au hata ujumbe wa sms, je ni kwa kiasi gani pia unamjali mpenzi wako huyo katika kumkinga na magonjwa?. Je, kama penzi lako ni la dhati kwa mpenzi wako je unamjali na kumlinda?. Je unajali kumkinga na magonjwa mbalimbali ya kiafya na ya kimapenzi? … Sitaki kuwachafulia uwanja hasa katika siku hii ambayo wengi hawataki kusikia lolote isipokuwa masuala ya mapenzi lakini nafikiri kama unamjali mpenzi wako kikweli basi pengine katika siku hii unapodhihirisha mapenzi yake kwake pia utachukua japo dakika chache kufikiria ni kwa kiasi gani unamlinda na magonjwa mbalimbali ambayo maambukizo yake hutokea wakati wa kufanya mapenzi. STD au Sexually Transmitted Infection kwa Kiswahili magonjwa ya zinaa ni maambukizo ambayo hutokea wakati wa kujamiiana. Miongoni mwa magonjwa hayo ni gonjwa hatari la Ukimwi, kaswende, kisosonono, Clamydia, Trichomonia, Hepetitis B, Herpes au ugonjwa wa malengelenge neva ngozini na kadhalika. Kona ya Afya inachotaka kusema katika siku ya wapendanao ni kwamba, moja ya misingi muhimu ya kukuepusha wewe na mpenzi wako na magonjwa ya zinaa ni kuwa muaminifu kwa mpenzi wako, mke au mume wako. Kuhakikisha umpendae unamlinda kwa kufuata maelekezo ya kujikinga na maradhi hayo yanayoambukizwa wakati wa kufanya mapenzi kama vile kutumia mipira, kupata kinga na matibabu yanayotakiwa. La muhimu zaidi ni kumjulisha umpendaye pindi unapoyakwaa maradhi hayo ili naye akapime na apatiwe tiba, kwa sababu mengi ya maradhi hayo ya zinaa tiba yake hukamilika pale wawili wanaoshiriki mapenzi wanapotibiwa pamoja. Kujidanganya kujitibu mwenyewe na kuficha ugonjwa kwa mpenzi wako, zaidi ya kukufanya usipone kikamilifu magonjwa hayo, pia huleta hatari kubwa ya kueneza magonjwa hayo katika jamii. Kwa hivyo njia ya kwanza ni kuyajua magonjwa ya S.T.D na kuzijua dalili zake na kuwa wazi kuhusiana na magonjwa hayo pale yanapotupata.
Kona ya Afya inasema… kama kweli unampenda basi mlinde!
Nawatakia wadau wote Valentine Njema!

Saturday, February 13, 2010

Unene unasababisha watoto wa kiume wachelewe kubaleghe


Uchunguzi mpya umeonyesha kuwa watoto wa kiume walio wanene huchelewa kubaleghe kuliko wenzao walio na uzito wa kawaida. Hii ni tofauti na watoto wa kike ambapo unene huwasababishia hufikia baleghe mapema. Huko nyuma pia wataalamu walisema kwamba, kuna uhusiano kati ya BMI na kubaleghe mapema watoto wa kike na kuongeza kwamba, suala hilo kusababishwa na kuongezeka kwa homoni inayojulikana kama Leptin kwa watu wanene. Uchunguzi mpya umesema homoni hiyo hiyo husababisha watoto wa kiume walio wanene wachelewe kubaleghe. Kuna uwezekano kuwa homoni hiyo inageuza homoni za kiume na kuwa za kike katika tishu za mafuta na kusababisha watoto wa kiume wachelewe kukubaleghe.
Kwa upande mwingine utafiti mpya umesema kwamba, unene huanza kabla ya mtoto kufikia miaka miwili. Utafiti huo uliofanywa na wataalamu wa Marekani umesema kwamba, unene ambao huweza mtu kuwa nao katika umri wake wote huanza wakati anapokuwa na miaka miwili. Uchunguzi huo uliowafanywa kwa kuwahusisha watoto wanene 100 na vijana umegundua kwamba, nusu ya watoto hao walikuwa wanene walipokuwa na miezi 24 na kwa asilimia 90 walikuwa ni wenye uzito mkubwa walipokuwa na miaka mitano.
Si vibaya kujua kuwa nchini Uingereza asilimia 27 ya watoto wa nchi hiyo ni wanene. Ingawa sababu hasa inayopelekea watoto wawe wanene mapema katika umri wao haijajulikana lakini wataalamu wanasema kwamba lishe mbovu, kuanza kupewa watoto vyakula vigumu mapema pamoja na kutofanya mazoezi mapema na kujibweteka ni mausala yanayochangia watoto kuwa wawe na unene wa kupindukia tangua wakiwa wadogo.

Monday, February 8, 2010

Maradhi anayopata mama mjamzito humpelekea mwanae kupata pumu


Utafiti mpya umegundua kuwa, baadhi ya magonjwa anayopata mama wakati wa ujauzito huongeza uwezekano wa mwanae kupatwa na ugonjwa wa pumu. Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Maendeleo ya Tiba za Watoto na Vijana, watoto ambao wanazaliwa na kina mama waliopatwa na maambukizo ya vijidudu katika mfuko wa uzazi au maji yanayomzunguka mtoto tumboni yanayojulikana kama (chorioamnionitis) huwa wana uwezekano mkubwa wa kupatwa na pumu wafikapo umri wa miaka 8. Suala hilo hilo pia huwatokea watoto waliozaliwa kabla muda wao wa kuzaliwa haujatimia au prematures. Maambukizo hayo yanasababishwa na bakteria mbalimbali wanaopatikana katika sehemu za uke kama vile E. Coli na bakteria kundi B, Streptococci. Magonjwa hao husababisha zaidi ya nusu ya watoto wazaliwe kabla muda wao haujatimia, huku watoto hao wakiwa mapafu yao hayajaimarika vya kutosha na hivyo kukabiliwa na hatari ya kupata magonjwa mbalimbali sugu ya kifua kama vile pumu. Wanasayansi kwa kutegemea utafiti huo wameweza kusema kuwa, maambukizo ya magonjwa yanayotokana na bakteria ndio sababu kuu inayopelekea watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda wao kutimia, wapatwe na pumu.
Hivyo wameshauri kuwa, wakinamama wanatakiwa kufahamu umuhimu wa kuhudhuria kiliniki na katika vituo vya afya wakati wa ujauzito na kufuata maelekezo wanayopewa wakati wakiwa na mimba ili kuepusha matatizo kama hayo yasitokee.

Saturday, February 6, 2010

Aatikwa figo ya dada yake ingawa figo hiyo haiendani nawe


Utaalamu mpya umemumezesha mwanamke mmoja Muingereza kuwekewa pigo ya dada yake ingawa figo hiyo haiendani nae. Maxine Bath alikuwa na matatizo ya figo ambapo alikuwa akisaidiwa na mashine kuzungushiwa damu mwilini au dialysis. Mwanamke huyo hakuweza kupata mtu wa kumpatia figo inayoendana naye kutoka katika familia yake. Lakini madaktari wa hospitali ya Conventry nchini Uingereza wametumia utaalamu mpya unaojulikana kama 'cryofiltration' ili kuondoa seli za kulinda mwili ambazo zinasababisha figo hiyo ishindwe kuungana na mwili, iwapo itaunganishwa mwilini kwa mgonjwa hali ya kuwa haiendani na seli za mwili wake. Madaktari hao baada ya kufanikisha operesheni hiyo ya kuatika figo wanasema kwamba, utaalamu huo mpya unaweza kuwasaidia watu wengi zaidi wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali na wanahitajia kupandwa viungo mwilini au transplant. Watu 927 hufanyiwa operesheni za kuatika figo kila mwaka nchini Uingereza, hata hivyo maelfu ya wagonjwa wengine huwa wanaendelea kusubiri ili waweze kupata watu wanaoendana nao walioko tayari kuwapatia figo, huku ikiwa vigumu kuwapata watu hao. Viungo pale vinapopandwa au kuatikwa katika miili ya wengine hukataa kushikamana na miili hiyo (organ rejection) suala ambalo hutokea pale mwili unapotambua kuwa kiungo kilichoungwa si chake, na kuruhusu mfumo wa kulinda mwili ukikatae kiungo hicho. Tatizo hilo linaweza kuondolewa iwapo kiungo kinachotaka kupandwa kinatoka kwa ndugu wa familia moja na mgonjwa, na iwapo mgonjwa atatumia dawa za kuudhoofisha mfumo wa kulinda mwili kwa maisha yake yote.
Lakini haikuwa hivyo kwa Bi. Maxine, ambaye ana umri wa miaka 41 na aliyepata matatizo ya figo tangu akiwa na miaka 15. Ingawa mwanamke huyo hakuweza kupata mtu wa familia moja wa kumpa figo inayoendana na seli za mwili wake, lakini kwa kuondolewa seli hizo aliweza kuunganishiwa figo ya dada yake bila tatizo lolote.
Wataalamu wanasema kwamba teknolojia hiyo mpya inaweza kutumika kusaidia watu wengi zaidi wenye tatizo hilo, na hii ni mara ya kwanza duniani imetumiwa ili kumsaidia mgonjwa aunganishwe kiungo kisichoendana naye.
Operesheni hiyo ilifanywa mwezi Novemba mwaka 2009 na imesaidia kuokoa maisha ya Maxine.

Siri ya kasi ya mbegu za kiume yagunduliwa!


Wataalamu wanasema wamegundua kwamba mbegu za kiume huanza kwenda kwa kasi wakati zinapofika karibu na yai la mwanamke, suala ambalo huenda siku zijazo likasaidia katika kupatikana dawa ya kuzuia mimba ya wanaume. Vitundu vidogo vilivyoko juu ya mbegu hizo za kiume huziwezesha kubadilisha PH yake ya ndani, ambayo hufanya mkia wa mbegu hizo uanze harakati. Wataalamu hao wa Chuo Kikuu cha California huko San Francisco wanasema kuwa, ugunduzi huo unaweza pia kusaidia kuelezea kwa nini marijuana huwafanya wanaume wawe tasa na kwamba suala hilo litaleta mabadiliko makubwa katika kufahau suala zima la uwezo wa kuzaa wa mwanaume.
Kwa kawaida mbegu za wanaume hazianzi kwenda mbio baada tu ya kumwagwa, na ili kuweza kulifikia yai la mwanamke huhitajia kujiepusha na kasi hadi pale zinapokaribia yai. Wanasayansi kwa muda mrefu wamekuwa wakifahamu kwamba mwendo wa mbegu za kiume umekuwa ukisimamiwa na PH ya ndani, na kuwa kwake katika hali ya asidi au alikali lakini walikuwa hawafahamu ni jambo gani hasa linalowezesha kubadilika PH hiyo. Wataalamu wamesema, sasa wamejua kuwa ili kuongeza PH ili iwe ya alkali, mbegu huhitajia protoni zinaoitwa Jettison, na kwamba wamegundua vijitundu vidogo vilivyoko juu ya mbegu hizo ndio huruhusu mabadiliko hayo. Daktari Yuriy Kirichok aliyeongoza utafiti huo anasema, iwapo utafungua vijitundu hivyo, protoni inatoka nje, na wao wamefahamu molekuli ambazo huruhusu protoni hizo zitoke nje. Anaendelea kueleza kwamba, vijitundu hivyo vilivyopewa jina la Hv1 proton Channels, hufunguka pale inapofikia wakati muafaka wa kufunguka na hutegemea kitu kingine kinachoitwa, anandamine. Anandamide ziko katika mirija ya uzazi ya mwanamke katika eneo ambalo ni karibu na yai.
Katika marijuana kuna mada inaitwa cannabidoid ambayo inaaminika kuwa inapunguza uwezo wa anandamide, suala ambalo sasa limeweza kuelezea ni kwa nini marijuana kusababisha ugumba kwa wanaume. Dk, Kirichok anasema kwamba, marijuana pia huzipa kasi mbegu za kiume mapema, na huzifanya ziungue baada ya masa kadhaa. Watafiti hao wanatupa moyo kwamba, kwa kufahamu vyema masuala hayo, sasa ni wazi kuwa wanaweza kutafuta dawa ya kuzuia mimba kwa wanaume. Kwani kwa kuziziba molekuli hizo, pengine wakafanikiwa kuzuia na kutoruhusu mbegu isikutane na yai, na njia hiyo ikatumika kama dawa ya kuzuia mimba kwa wanaume.

Thursday, February 4, 2010

Samahani kwa maatizo ya kufundi!



Wapenzi wadau wa Kona ya Afya,
Shally's Med Corner inachukua fursa hii kuwaomba radhi kutokana na matatizo ya kiufundi ambayo yamesababisha blogi ya Kona ya Afya ivurugike kimuundo. Ingawa suala hilo halijaathiri uwekaji wa makala katika blogi hii, lakini nawaomba muwe na subira na uvumilivu hadi pale matatizo hayo yatakaporekebishwa. Kona ya Afya inawaahidi kwamba hivi karibuni mambo yatanyooshwa na muonekano wa blog utarudi katika hali yake ya kawaida.
Daima tulinde afya zetu!
Shally

Bi. Michele Obama akosolewa kwa kuzungumzia lishe ya mabinti zake hadharani


Ikiwa ni wiki mbili tangu ilipotangazwa kuwa unene kwa watoto umeongezeka mara tatu nchini Marekani katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, na Mke wa Rais wa Marekani akatangaza nia yake ya kupambana na suala hilo, Bi. Michele Obama amekabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya kujadili hadharani masuala ya lishe ya mabinti zake. Hii ni baada ya daktari wa familia hiyo anayeshughulikia masuala ya watoto kumtaarifu kwamba, wanawe Sasha na Malia wanaanza kuwa wanene. Hata hivyo Bi. Michelle amepuuza suala hilo na kusema kwamba, anafikiri watoto wake wako sawa tu. Wengi waliomkosoa Michelle wamesema kuwa, anahatarisha mustakbali au future ya wanawe kwa kuanza kuwazungumzia hadharani kuhusiana na milo yao. Ingawa ni kweli kuwa nchini Marekani Waamerika weusi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kuongezeka uzito na kuwa na unene wa kupindukia ambapo wataalamu wanasema theluthi moja ya Waamerika weusi ni wanene, lakini bado matamshi ya Mrs. Obama ya kujadili lishe ya wanawe hadharani, yameonekana kuwa pengine yanaweza kuwasababisha wanawe kupata matatizo ya kula ukubwani. Wengi wanasema kwamba mke huyo wa Rais wa Marekani angeweza kutoa mifano mingine tu mingi lakini bila kuwaashiria moja kwa moja watoto wake, hasa ikizingatiwa kuwa, mabinti wake hao bado ni wadogo. Wakosoaji hao wamemtaka Bi. Michelle ajiepusha kukariri suala hilo na afuate mfano wa familia nyinginezo za Marais wa Marekani waliowahi kuishi White House.

Wednesday, February 3, 2010

Nchi za Afrika zakubaliana kutokomeza malaria


NCHI za Afrika zimekubaliana kuwa lengo kuu la serikali zao katika mapambano dhidi ya malaria, ni kuutokomeza ugonjwa huo.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania alisema hayo juzi mwishoni mwa kikao cha viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) walio katika mapambano dhidi ya malaria Afrika (ALMA).

Alisema Afrika inahitaji vyandarua 200 ingawa hadi sasa kuna ahadi ya vyandarua 50 tu, lakini hata hivyo aliitaka ALMA kuendelea na jitihada za kupata vyandarua vyote vitakavyokidhi mahitaji.

Rais Kikwete aliitisha kikao hicho kwa kushirikiana na AU ambapo mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ray Chambers, aliwataka viongozi hao kuweka nia ya dhati ya kisiasa katika jitihada hizi ili kufanikisha azma yao.

Kikao hicho ni cha pili cha kikazi baada ya kilichofanyika New York, Marekani chini ya Rais Kikwete, kama mwanzilishi wa jitihada hizo ambazo zilianza wakati akiwa Mwenyekiti wa AU.

Kikao hiki kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa AU, Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi, Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia, Hifikepunye Pohamba wa Namibia, Mwai Kibaki wa Kenya na Armando Guebuza wa Msumbiji. Wengine ni Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Rupia Banda wa Zambia na Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Nchi zingine zilizohudhria ni Burundi, Gabon, Misri na Somalia. Katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ALMA, Joy Phumaphi, alieleza mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo matumizi ya vyandarua yameongezeka kwani hadi mwaka juzi nchi 13 kati ya 35 zenye kiwango kikubwa cha malaria, asilimia 50 ya watu wao wanatumia vyandarua hivyo, ikilinganishwa na mwaka 2005 na pia matumizi ya dawa mseto yamepunguza maambukizi na vifo.

Phumaphi alisema mwamko huo wa matumizi bora ya vyandarua, umepunguza vifo na maambukizi pia kwa mama na mtoto ambao ndiyo waathirika wakubwa.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto nyingi ambazo zinahatarisha jitihada na kutokomeza malaria ikiwamo fedha kunakotokana na kutotimizwa kwa ahadi na wafadhili.

Rais Kikwete alimtaka kila mshiriki kupitia wizara zao za Afya kutuma maombi kwenda mfuko wa malaria duniani (Global Fund) ambayo yatahusisha si upatikanaji tu wa vyandarua, bali uwezeshwaji wa watumishi wa afya, vitendea kazi na vitu vyote muhimu vinavyohitajika katika jitihada hizi za kutokomeza malaria.

Monday, February 1, 2010

Utoaji mimba usio salama unauwa akina mama elfu sabini kila mwaka


Utoaji mimba usio salama husababisha akima mama elfu sabini kupoteza maisha yao kila mwaka duniani kote. Taasisi mashuhuri ya Guttmacher imeripoti kuwa, japokuwa utumiami wa njia za uzazi wa mpango hupunguza kiwango cha kuharibika kwa mimba, lakini ulimwengu unashuhudia wakinamama wapatao elfu sabini wakifariki dunia kila mwaka kutokana na utoaji mimba usio salama. Imeongeza kuwa, utoaji mimba usio salama unaendelea kuwa tatizo miongoni mwa walimwengu. Imesema kuwa, zaidi ya nusu ya vifo hivyo vya akinamama hutokea katika nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara.