Wednesday, September 30, 2009

Watoto wa wakinamama wanaofanya kazi hawana afya bora!


Uchunguzi umegundua kuwa watoto ambao mama zao wanafanya kazi, maisha yao ya kiafya ni ya chini ikilinganisha na wale ambao mama zao wako majumbani. Uchunguzi huo uliofanywa na Taasisi ya Afya ya Watoto ya Uingereza umewachunguza zaidi ya watoto 12,500 wenye umri wa miaka mitano na kugundua kuwa watoto ambao mama zao ni wafanya kazi wana harakati kidogo na mara nyingi hula vyakula visivyo salama. Wataalmu hao wamesema kuwa watoto wenye miaka mitano ambao mama zao wanafanya kazi za kudumu au part time, hunywa sana vinywaji venye sukari, katika kipindi cha kati ya milo ya kawaida. Pia hutumia komputa na kuangalia televisheni kwa masaa yasiopungua mawili kwa siku wakilinganishwa na watoto ambao mama zao wako majumbani ambao hutumia chini ya saa moja katika shughuli hizo.
Wataalamu hao lakini wamejitetea kuwa, uchunguzi wao huo haumaanishi kuwa wakinamama wasiende makazini, lakini kunatakiwa kuwepo na sera na mikakati ya kuwasaidi kina mama.

Monday, September 28, 2009

USAFI WA MWILI WA WATOTO NA UMUHIMU WAKE


Makala hii inahusu usafi wa mwili na umuhimu wake kwa watoto. Natumai kuwa mtanufaika nayo.
Wazazi na walezi wanaweza kuwa na nafasi kuu na muhimu katika makuzi na usafi wa mtoto, masuala ambayo atakuwa nayo katika maisha yake ya kila siku. Kitendo cha kumfunza mtoto kuhusu usafi wa mwili ni njia bora kabisa ya kumuepusha na maambukizo na maradhi mbalimbali. Ni jukumu la mzazi au mlezi kumfunza mtoto misingi sahihi ya usafi wa mwili wakati mtoto akiwa na umri mdogo kabisa, jambo ambalo litamsaidia mtoto huyo na familia yake katika maisha yao ya baadaye. Misingi ya usafi inapaswa kufundishwa na kuwa sehemu moja ya maisha ya kila siku ya mtu, na pia kuwa njia bora ya wazazi kuwafunza watoto wao kuhusu usafi wa miili yao, kwanza kabisa kwa wazazi hao kuwa mfano mbele ya watoto. Maambukizo ya magonjwa hupungua miongoni mwa watoto wakiwa mashuleani, kwenye maeneo wanayochezea na kadhalika, iwapo watakuwa wamefunzwa namna ya kujilinda na maradhi kwa kuweka miili yao safi na kwa kufuata kikamilifu kanuni za afya kila siku. Mambo ya kuzingatia katika usafi wa mwili wa mtoto yako mengi, lakini hapa nitaorodhesha kwa kifupi haya yafuatayo: Usafi wa Kinywa. Meno na kinywa vyote vinapaswa kuwa visafi wakati wote ili kuzuia magonjwa ya meno na fizi. Aidha usafi wa meno kwa mtoto ni muhimu ili kuzuia kuoza na kuvunjika kwa meno akiwa na umri mdogo. Upigaji mswaki wa mara ka mara, yaani kabla ya kifungua kinywa na baada ya chakula na kabla ya kulala usiku unashauriwa kwa watoto. Upigaji mswaki baada ya kula vyakula vyenye sukari pia ni muhimu kwa watoto, ili kuzuia meno kuoza na harufu mbaya. Pili, uoshaji mikono ni jambo linalopasa kuzingatiwa sana kwa watoto, baada ya kutoka msalani, kabla ya kula au kushika takataka au vitu vingine vichafu, kushika wanyama n.k. Kitendo cha kuosha mikono sio tu ni muhimu kwa watoto, bali hata kwa watu wazima. Uoshaji mikono ni muhimu kwa ajili ya kuzuia kupatwa na magonjwa mbalimbali, ambayo huweza kupatikana iwapo kanuni sahihi za usafi wa choo hazizingatiwi. Wakati mtoto anapofikia umri wa kwenda shuleni au kwenye shule ya chekechea, anatarajiwa kuwa na uwezo wa kutumia choo na kusafisha mikono yake mwenyewe baada ya kutoka msalani bila ya kusimamiwa na mtu.
Maambukizo ya fungus za miguuni na kichwani pia yanaweza kuzuilika iwapo uoshaji mikono sahihi utafuata. Watoto wanapaswa kuosha vizuri mikono yao, yani kati ya vidole na chini ya kucha, na ikiwezekana tumia brashi kusafisha mikono ya watoto. Ukaushaji vizuri wa mikono na vidole vile vile ni muhimu ili kuzuia maambukizo ya fungus. Watoto nao wanapaswa kuelewa umuhimu wa jambo hilo.
Usafi wa mwili unajumuisha pia usafi wa kucha. Wazazi wanapasa kuwakataza watoto tabia ya kutafuna kucha, kwani kucha za watoto mara nyingi huwa chafu na rahisi kubeba vijidudu maradhi. Kitendo cha kukata kucha za mtoto kitasaidi kupunguza kiwango cha vimelea vya maradhi vilivyoko chini ya kucha.
Tukiangalia usafi wa nywele tunaona kuwa, nywele za mtoto zinatakiwa kuwa fupi kama ni za kuchana na kama ni ndefu zinapaswa kusukwa mara kwa mara na kusafishwa vizuri kwa kutumia maji na sabuni au shampoo. Hii itasaidia kupunguza ringworm au chawa wa kichwani iwapo nywele zitakuwa chafu na kutooshwa vizuri. Watoto pia wanapaswa kushajiishwa kusafisha mikono yao kabla ya chakula, hii ni kwa sababu kitendo hicho kitasaidia kuzuia maambukizo ya magonjwa yanayoweza kuathiri mfumo wa chakula, wa kupumua na viungo vingine vya mwili. Nguo za mtoto pia ni lazima ziwe safi wakati wote , bila ya kusahau soksi, viatu na mahali anapolala. Mto anatakiwa kuvaa soksi kavu zisizo na unyevunyevu, ili kuzuia kuzaliana kwa fungus za miguuni. Avae viatu visivyobana, kama ni msimu wa joto mpatie viatu vilivyo wazi vyenye kupitisha hewa, mbadilishie mashuka yake anayolalia mara yakichafuka na kukifanya chumba au mahali anapolalia kuwa mahali safi na salama kwa afya yake. Mtengee mtoto taulo lake pekee yake, ili kuzuia maambukizo mbalimbali kama vile ya ngozi na kadhalika. Kwa kufanya hivyo ni matumaini yetu kuwa tutawaepusha watoto wetu na milipuko mbalimbali ya magonjwa.

Sunday, September 27, 2009

Kusikiliza MP3 kwa sauti kubwa huenda kukakuletea matatizo ya kusikia!


Utafiti unaonyesha kuwa kusikiliza MP3 kwa sauti kubwa kwa saa moja kwa siku, kunaweza kuleta madhara makubwa katika kusikiliza kwa mtu. Kwa mujibu wa utafiti huo, kusikiliza mziki kwa sauti kubwa yawezekana kukapelekea mtu kusikia sauti za ajabu ajabu masikioni.
Uchunguzi uliofanywa na taasisi moja ya wasiosikia umeonyesha kwamba, watu wenye umri wa miaka 16 mpaka 34, husikiliza muziki kwa sauti kubwa bila kujali madhara yake . Wataalamu wanasemakwamba, kusikia sauti kama ya mruzi masikioni, au sauti nyinginezo ni kwa sababu ya kusikiliza mziki kwa sauti kubwa, ambako husababishwa na kuharibika seli za masikio kutokana na sauti kubwa ya mziki na kwa muda mrefu.
Uchunguzi uliofanywa barani Ulaya umeonyesha kwamba, kati ya watu 10 wanaotumia mp3, mmoja kati yao anakabiliwa na matatizo ya kusikia.
Hivo basi wataalamu wanatushauri kutosikiliza mziki kwa sauti kubwa, hasa wakati wa kufanya mazoezi kwa kutumia vifaa vya mazoezi au wakati wa kukimbia, kwani watu wengi kufikiria kuwa kila wanapongeza sauti ya mziki wakati wa mazoezi ndivyo wanavyoweza kuwa na mbio zaidi, suala ambalo si kweli.

Saturday, September 26, 2009

Kuna tofauti kati ya lishe ya mwanaume na mwanamke?


Wanaume kwa kuwa na kiasi kikubwa cha misuli, miili yao inahitajia na kutumia vyakula zaidi, au kwa maneno mengine kitendo cha Metabolism katika miili yao chenye maana ya kusaga chakula na kuzalisha nishati, hufanyika zaidi katika miili ya wanaume ikilinganishwa na wanawake. Suala hilo hupelekea wanaume wahitajie nishati (energy), vitamini na madini zaidi kuliko wanawake. Mifupa yao mipana, misuli iliyojengeka, pamoja na mfumo mzimo mzima wa mwili wa mwanaume ni mkubwa zaidi ikilinganishwa na wanawake, na ili kuhifadhi misuli yao wanajitajia kiwango kikubwa zaidi cha protini. Hivyo, wanaume wanahitaji kiasi kikubwa zaidi cha chakula kwa ujumla, ikilinganishwa na wanawake. Wanaume wanahitajia kilokalori 600 zaidi za chakula, kuliko wanavyohitajia wanawake. Hata hivyo kiwango kichotakiwa cha sukari (carbohydrates) na ufumwele (fibires) kwa wanaume ni sawa sawa na kwa wanawake. Hii ni katika hali ambayo wanawake wanahitajia mafuta au fatty acids zaidi kwa asilimia 60 kuliko wanaume.

Uchauri wa kiafya na lishe kwa wanaume:
1. Wanashauriwa kula matunda na mboga mboga kwani vyakula hivyo huilinda miili yao.
2. Wanashauriwa kujiepusha na vyakula vyenye mafuta ya mgando (unsaturated fatty acids) na pia wale nyama nyekundu (red meat) kwa uchache.
3. Wajiepushe kuwa na wasiwasi na mawazo (stress).
4. Wajiepushe na kuvuta sigara na hata kuwwepo katika sehemu zenye moshi wa sigara.
5. Wajitahidi kuwa na uzito unaotakiwa, sio mdogo wala mkubwa sana, kwani uzito mkubwa husababisha mafuta kukusanyika katika mzunguko wa kiuno na tumbo, suala ambalo huongeza hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo.
6. Wasizembee kujishughulisha na michezo na kutunza afya zao.
7. Na mwisho wajiahidi kufanyiwa uchunguzi wa kitiba (check up) kila baada ya muda fulani. Kwani magonja kama kensa ya korodani yanapogunduliwa mapema hutibika kwa urahisi zaidi kuliko yanapocheleweshwa.
…… Haya tena Blog ya Kona ya Afya inawahimiza kinababa wazijali afya zao, kwani kwa kuwa baba ni kichwa cha familia, basi afya na uzima wa kinababa ni muhimu kwa familia na jamii nzima!

Tuesday, September 22, 2009

Watoto wenye harakati nyingi hulala kwa urahisi zaidi


Uchunguzi mpya umethibitisha imani ya muda mrefu kuwa pale mtoto anapokuwa na harakati nyingi wakati wa mchana, humsaidia kulala kwa urahisi na mapema zaidi.
Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa katika makala ya Achieves of Diseases in Childhood, mtoto ambaye hutulia tu na hana harakati yoyote, hupata usingizi kwa taabu na huchukua muda mrefu hadi pale anapolala. Kila saa moja inayotumiwa kwa harakati kama vile kukumbia, inapunguza muda unaotakiwa kwa dakika 6 wa kupata usingizi mtoto. Kila mtoto anapokuwa na harakati ndivyo muda mchache zaidi unavyotakiwa kumafanya alale. Pia imeripotiwa kuwa, watoto wanaopata usingizi kwa haraka, vilevile hulala kwa muda mrefu.
Kulala kwa muda mfupi kwa watoto halikadhalika kumehusishwa na mtoto kuwa mnene sana au obesity. Wataalamu wanasema kuwa, kuwa na harakati mtoto sio tu kwamba ni muhimu sana kwa afya yake, moyo na humfanya awe na uzito unatakiwa bali pia husaidia mtoto aweze kulala vizuri.
Haya akina mama na walezi wote kwa ujumla, msihofu pale mtoto anapokuwa na harakati nyingi na pale wanapocheza sana wakati wa mchana, kwani hilo humsadia kupata usingizi kwa urahisi na kulala vizuri wakati wa usiku. Tusisahau kuwa kipimo cha afya njema ya mtoto ni harakati anazofanya na wala sio kukaa tu kwa utulivu na bila kufanyaa harakati yoyote.
Nakutakieni malezi mema akina baba na akina mama!

Saturday, September 19, 2009

Karoti


Karoti ina umuhimu mkubwa kwa lishe ya mwanadamu. Ikiwa katika umbo la mboga mboga aina ya mzizi, (root vegetable) ina rangi ya machungwa yenye kijani kigogo, inayosababishwa na mada ya Beta carotene, yenye umuhimu katika kutengeneza Vitamin A. Karoti kwanza ina kiasi kukubwa cha ufumwele au fibres, kwa kiasi ambacho katika kila gramu 100 ya karoti, zinapatikana gramu 2 za ufumwele, gramu 240 za Potassium na mikrogiramu 5,330 za Beta-Carotene. Kiasi hicho cha Beta karotini huweza kuufaidisha ubongo kwa zaidi ya kiasi kinachotakiwa. Mada hiyo ya Beta karotine hubadilishwa na mwili na kuwa Vitamin A ambayo ni muhimu sana katika kuimarisha mfumo wa ulinzi wa mwili na ufanyaji kazi mzuri wa ngozi, mapafu na utumbo. Pia husaidia katika ukuaji bora wa seli mwilini. Hivyo watu wenye kusumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu (High Blood Pressure) au wale wanaotaka kupungua uzito na hawataki miili yao ipate nguvu sana kupitia chakula, wanashauriwa kula vyakula vyenye mboga mboga ( vegetables) ikiwemo karoti. Karoti inapunguza kiwango cha mafuta mwilini (cholesterol) na ina Iron, Magnesium, Manganese, Phophorus, na hata Sulphur. Kuna yenyewe ina asilimaia 87 ya maji, vitamin B6, Thiamine, Folic acid na hata Calcium. Ingawa Beta carotene inapatikana katika mboga na matunda mengine lakini hakuna tunda lenye kiasi kikubwa cha mada hiyo zaidi ya karoti. Nukta muhimu ya kuzingatiwa hapa ni kuwa, karoti iliyopikwa inaupa mwili kiasi kingi zaidi cha Beta carotene kuliko karoti mbichi au ambayo haijapikwa.
Jamani shime tule tusisahau karoti katika vyakula vyetu!

Saturday, September 12, 2009

Je unajua?....Tikiti hupunguza shinikizo la damu!


Kula matunda yenye madini ya potassium na mboga boga kama vile tikiti maji, au matunda mengine yanayopatikana katika msimu wa joto, kunaweza kusaidia kupunguza shinikizo la damu.
Haya shime wadau msisahau kula matunda na mboga mboga ili kuboresha afya zetu

Friday, September 11, 2009

Kuishi maisha mazuri kunapunguza hatari ya kupata saratani ya matiti


Utafiti mpya umeonyesha kuwa, kuishi maisha mazuri na kunyonyesha mtoto kunaweza kuazuia kesi 70, 000 za kensa ya matiti kila mwaka.
Ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Marekani ya Wataalamu wa Uchunguzi wa Saratani Duniani imeonyesha kuwa, ingawa ni kweli jeni zina uhusiano katika kusababisha kensa ya matiti, lakini mabadiliko kuhusiana na jinsi mtu anavyoishi, pia huweza kuzuaia mtu kupatwa na ugonjwa huo hatari kwa kiasi kikubwa.
Bi. Susan Higginbotham mmoja wa wataalamu hao anasema kuwa, inakadiriwa asilimia 40 ya kesi za ugonjwa wa kensa ya matiti au kesi 70, 000 za ugonjwa huo zinaweza kuzuiwa, nchini Marekani, kwa kufanyika tu mabadiliko ya jinsi watu wanavyoishi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kula vyakula visivyokuwa na mafuta mengi, kuwa na uzito unaotakiwa kiafya, kuishi maisha yaliyojaa harakati pamoja na kupunguza matumizi ya pombe, bila kusahau kunyonyesha, huweza kusaidia sana katika kutopata ugonjwa wa saratani ya matiti.
Wanasayansi wamehitimisha kwa kusema kuwa, namna mtu anavyoishi ndio suala muhimu sana linaloainisha iwapo mtu anaweza kupata ugonjwa huo au la.
Kwa hivyo, tumeshauriwa kufanya mazoezi kila siku kwa muda usiopungua nusu saa, huku wakinamama wakihusiwa kupunguza kunywa pombe.

Wednesday, September 9, 2009

Wataalamu wanasema kulala kitanda kimoja na mpenzio si kuzuri kwa afya yako!


Wapenzi wanashauriwa kufikiria kulala vitanda tofauti, kwani kufanya hivyo ni vizuri kwa afya na uhusiano wao. Mtaalamu wa masuala ya usingizi Dakta Neil Stanley amesema katika Warsha ya Sayansi ya Uingereza jinsi kulala kitanda kimoja wapenzi kunavyoweza kusababisha mapishano juu ya kukoroma na hata kugombaniana shuka usiku uliopita. Utafiti umeonyesha kwamba, kwa wastani wapenzi wanakabiliwa kwa asilimia 50 na matatizo ya usingizi pale wanapolala kitanda kimoja. Mtaalamu huyo ambaye analala mbali na mkewe, amesema kuwa kihistoria hatukutakiwa kulala kitanda kimoja. Ameelezea kuwa, desturi ya kisasa ya vitanda vya harusi ilianza tu wakati wa mapinduzi ya viwanda, ambapo watu walianza kuhamia kwenye miji na vitongoji vyenye misongamano ya watu na hapo ndipo walipojikuta wanakabiliwa na uhaba wa nafasi. Anaendelea kueleza kuwa, kabla ya kipindi cha Vitoria haikuwa imezoeleka kwa waliooana kulala pamoja. Na wakati wa Urumi ya zamani, vitanda vya harusi vilikuwa ni sehemu ya kukutana kimwili lakini si kwa ajili ya kulala. Kwa hivyo Dkt Stanley amesema kuwa, watu hivi sasa wanatakiwa kufikiria kufanya hivyo.
Naye Dkt Robert Meodows ambaye ni mtaalamu wa elimu ya Sosholojia katika chuo kikuu cha Surrey anasema, watu wanafikiri wanalala vizuri zaidi wakati wakilala na wenzi wao, lakini ushahidi unaonyesha kinyume chake. Uchunguzi uliofanywa kwa kuwashirikisha wapenzi 40 umeonyesha kuwa, wakati wenzi wakilala kitanda kimoja, na iwapo mmojawapo anahangaika hangaika wakati wa usingizi, kuna uwezekano kwa silimia 50, mwenzi wake akasumbuka kutokana na hali hiyo. Uchunguzi huo umegundua kuwa, hata hivyo wapo wenzi wanaolala vitanda tofauti lakini wachache, huku wale walio kwenye umri wa miaka 40 au 50 kwa asilimia 8 hulala vyumba tofauti.

Monday, September 7, 2009

Chanjo mpya ya kensa ya mlango wa uzazi (Cervical Cancer) yagunduliwa


Wanasayansi hivi karibuni wametengeneza chanyo mpya ambayo inazuia virusi vinavyosababisha saratani ya mlango wa uzazi au cervical cancer. Kwa mujibu wa shirika la Chakula na Madawa la Marekani FDA, chanjo hiyo iliyotengenezwa na shirika la GlaxoSmithKline inaweza kuzuia aina mbalimbali za virusi kwa karibu asilimia 93, vinavyoweza kusababisha kensa ya mlango wa uzazi. Matumizi ya chanjo hiyo mpya hayana athari zozote mbaya muhimu kwa mtumiaji, isipokuwa maumivu kidogo na uvimbe sehemu inapochomwa dawa. FDA imesema kuwa chanyo hiyo inaweza kutumiwa kwa wanawake wenye umri wa miaka 10 hadi 25.
Ugonjwa wa kensa ya mlango wa uzazi unasababishwa na virusi vya Papilomma (HPV) ambapo aina 15 za vijidudu hivyo huweza kusababisha ugonjwa huo. Kensa ya mlango wa uzazi ni kensa ya tano miongoni mwa saratani zinazosababisha vifo vya wanawake ulimwenguni, ambapo wanawake karibu 473,000 hupatwa ugonjwa huo kila mwaka. Inasemekena kuwa karibu asilimia 85 ya vifo vya wanawake katika nchi zinazoendelea vinasababishwa na kensa ya mlango wa uzazi. Nchini Marekani pekee wanawake 11,999 hupata ugonjwa huo na serikali kutumia karibu dola bilioni 2 kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa huo kwa mwaka.

http://www.presstv.ir/detail.aspx?id=105373§ionid=3510210

Saturday, September 5, 2009

Wataalamu wavumbua kingamwili za kuzuia waathirika wa HIV kuelekea katika hali ya Ukimwi


Wataalamu wa Marekani wamefanikiwa kuvumbua kingamwili mbili au antibodies ambazo zinaweza kuzuaia virusi vya HIV visikugawanyika na kuongezeka mwilini, hali itakayopelekea muathiriwa kutoelekea katika hali mbaya zaidi ya ugonjwa huo ya Ukimwi. Uvumbuzi huo ambao ni matokeo ya uchunguzi uliofanyika kwa karibu miongo miwili kuhusiana na virusi vya Ukimwi, unaonekana kuwa ni hatua mihimu inayoweza kupelekea kutengenezwa kinga ya ugonjwa huo. Wataalam hao wamesema kuwa kingamwili hizo zinaweza kutumika kutibu watu walioathirika na ugonjwa wa virusi vya HIV ambao tayari wako katika hali ya Ukimwi.
Uchunguzi huo umefanywa na taasisi ya uchuguzi ya Scripps ya Los Angeles Marekani kwa kutumia sampuli zaidi ya 1,800 za damu za waathiriwa wa Ukiwmi kutoka Thailand, Australia na barani Afrika.