Wednesday, April 21, 2010

Wanamichezo hawapati ugonjwa wa moyo


Utafiti mpya umeonyosha kuwa, kufanya mazoezi kwa muda mrefu hakuhusiana na kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo. Huko nyuma kulikuwa na tafiti zilizoonyesha wasiwasi wa afya ya mishipa ya moyo kwa baadhi ya wanamichezo wa Olimpiki. Tafiti hizo zilisema kwamba, kupanuka kwa mioyo ya wanamichezo kunakoitwa kitaalamu “athlete’s heart” huufanya moyo kuwa dhaifu sana na kushindwa kuvumilia mazoezi mazito.
Lakini kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa kwenye Jarida la Marekani la Kitengo cha Magonjwa ya Moyo, mazoezi mazito hayana hatari kwa afya ya moyo.
Kiwango cha damu inayosukumwa katika miili ya wanamichezo hakibadiliki wakati wa mazoezi. Mbali na kupanuka kidogo baadhi ya sehemu za moyo, misuli ya moyo hubakia sawa wakati wa mazoezi. Wanasayansi wamehitimisha kwamba, mioyo ya wanamichezo ina afya nzuri na inaweza kuvumilia kirahisi mazoezi ya kiwango cha juu. Pia wamesema kwamba, baadhi ya dawa kama vile erythropoietin (EPO) zinazotumiwa na wanamichezo hao ili kuzipa nguvu chembe chembe nyekundu za damu, kunaufanya utendaji kazi wa moyo udhoofu, suala ambalo limekuwa likiwatokea wanamichezo hao na wala sio mazoezi mazito ya mwili wanayoyafanywa.

Sunday, April 18, 2010

Unataka kuacha sigara ?..... fuata njia zifuatazo!


 Je, unataka kuacha kuvuta sigara? Sawa, nakubaliana na wewe lakini unajua kwa nini unataka kuacha tabia hiyo ambayo umeizoea kwa muda mrefu?. Kwa sababu haitoshi tu utake kuacha kuvuta sigara bila kuwa na sababu muhimu inayokusukuma uache suala hilo. Kwa hivyo kwanza anza kujiuliza kwa nini unataka kuacha sigara. Kujua sababu kutakusaidia katika kutekeleza lengo lako vyema. Je, unaacha sigara kwa kuwa unataka kuilinda familia yako isipate madhara ya sigara unazovuta? Je, unataka kuacha sigara kwa kuwa umeogopa kupata kensa ya kifua? Au je, ungependa kuonekana kijana zaidi? Tafuta sababu muhimu ambayo itaizidi hamu yako ya kuvuta sigara.


 Jua kuwa ni jambo gumu kuacha tabia uliyoizoea kwa muda mrefu mara moja. Haitowezekana utupe kipande chako cha sigara yako mara moja na kutangaza kuwa umeacha kuvuta. Suala hilo ni gumu kwani asilimia 95 ya watu wanaojaribu kuacha sigara kwa mtindo huo hushindwa, inabidi upate ushauri na tiba mbadala ili kukusaidia kuacha kuvuta sigara, hii ni kwa sababu sigara inaleta uraibu wa nicotine, na ubongo unaizoea mada hiyo hivyo kuacha kuvuta husababisha uhisi dalili za kukosekana nicotine katika ubongo.
 Jaribu kutumia vitu vingine badala ya nicotine. Hii ni kwa sababu unapoacha sigara na kukatisha nicotine mwilini hukufanya usijisikie kama umechanganyikiwa, uhisi msongamano wa mawazo na kutotulia. Suala hilo linaweza kusaidiwa kwa kupata tiba mbadala ya kusaidi kuondo hisia hizo. Wataalamu wanashauri kutumia ubani wa nicotine (nicotine gum), pipi za nicotine na baadhi ya plasta za kubandika mwilini zenye kusaidia kuacha sigara bila kuhisi madhara ya kukosa nicotine. Kutumia vitu hivyo wakati ukiwa bado unafuta sigara hakushauriwi.



 Ikiwa hutaki kutumia vitu vingine vyenye nicotine wakati umeacha sigara, mwombe daktari wako akuandikie vidogo ambavyo vinavyoondoa athari za mwili kuzoea nicotine wakati unapoacha sigara.
 Usijiamulie peke yako na kwa siri, bali itangazie familia yako, waambie marafiki zako na wafanyakazi wenzako kwamba umeacha sigara! Kukupa moyo kwao kutakufanya uweze kufanikisha lengo lako hilo kwa urahisi zaidi. Pengine unaweza kujiunga na vikundi vya wanaoacha kuvuta sigara au kwenda kwa mshauri ili akusaidie suala hilo.




 Jizuie usipatwe na msongamano wa fikra na mawazo mengi. Hii ni kwa sababu moja ya sababu inayowafanya watu wavute sigara ni kwa kuwa nicotine huwafanya wajihisi hisia nzuri mwilini na mwili kulegea. Utakapoacha sigara itakubidi utafute njia za kukabiliana na stress. Ni bora ukipata masaji ya mwili kila mara, usikilize mziki mwororo, huku ukijizuia na yake yatakayo kufanya upate mawazo na msongamano wa fikra na ikiwezekana fanya yoga na mazoezi ya kulegeza mwili.
 Jiepushe na pombe na vitu vinginevyo vinavyoweza kukushawishi uvute sigara tena. Pombe ni miongoni mwa vishawishi vikubwa vya kukufanya uvute sigara. Hivyo kama wewe ni mnywaji ni bora inabidi uache kunywa hasa wakati huu unaotaka kuacha sigara. Kama kahawa pia inakufanya usijikie kuvuta, iacha na unywe chai badala yake. Na kama huwa unavuta baada ya mlo, basi tafuta kitu kingine cha kufanya kama vile kupiga mswaki au kutafuna ubani baada ya kula.


 Baada ya kuvuta sigara yako ya mwisho, tupa vidude vyote vya kuhifadhia majivu ya sigara na viberiti. Fua nguzo zako zote zinazonuka sigara na safisha kapeti lako na nyuma yako kwa ujumla. Tumia marashi ya kuondoa harufu ili kuondoa harufu ulioizoea ya sigara nyumbani kwao. Hii ni kwa ajili ya kukusaidia usihisi harufu yoyote itakayokukumbusha kuvuta sigara.
 Jaribu tena na tena! Usitosheke kwa kuacha kuvuta mara moja na kushindwa. Wavutaji wengi huacha sigara mara kadhaa kabla ya kufanikiwa. Fikiria kila mara azma yako ya kuacha kuvuta sigara na jipe moyo na mwishowe utafanikiwa.


]
 Kuushughulisha mwili na mazoezi kunaweza kukusaidia kupunguza hamu ya sigara na dalili zinazofuata baada ya kuacha kuvuta. Utakaposhawishika na kutaka kunyoosha mkono wako ili uchukue sigara, vaa viatu vyako na uende ukatembee kidogo, kacheze mpira au fanya mazoezi yoyote kama vile kukimbia na mengineyo.
 Usijaribu kujinyima chakula wakati unapoacha sigara. Badala yake kula wa wingi matunda, mbogamboga na maziwa. Uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Duke umeonyesha kwamba, vyakula hivyo vinakufanya uhisi ladha ya sigara ni mbaya.




 Jiwekee zawadi nono na jipongeze. Kuacha sigara mbali na kukufaidisha kiafya hukusaidia pia kujiwekea fedha zako ambazo ungezipoteza bure kwa kununua sigara. Jipongeze kwa kutumia sehemu ya fedha hizo kujinunulia zawadi.
 Acha sigara kwa afya yako! Tambua kuwa kuacha sigara kutakupatia faida kemkem kiafya kama vile kupunguza shinikizo la damu, kupunguza mapigo ya moyo. Siku moja tu baada ya kuacha sigara, kiwango cha Carbon monoxide cha damu yako kitarejea katika hali ya kawaida. Baada ya miezi mitatu hadi minne, hatari ya shinikizo la moyo hupungua na mapafu yako huanza kufanya kazi kama kawaida. Miongoni mwa faida za kuacha sigara ni hupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo, mshituko wa moyo, kensa ya mapafu pamoja na saratani nyinginezo.

Friday, April 16, 2010

Aspirin hutibu migreni


Wakati mauamivu makali ya kichwa au migraie yamekuwa yakitibiwa kwa dawa kali za maumivu, uchunguzi mpya umegundua kuwa dozi moja tu ya aspirini inaweza kuwaopunguzia maumivu walio na ugonjwa huo. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Cochrane Library, kunywa dozi moja ya aspirini ya kati ya miligramu 900 hadi 1000 kunaweza kupunguza mauvimu makali ya migraine kwa masaa mawili. Hata hivyo utafiti huo umesema dawa hizo zinaweza kuwafaa baadhi ya watu na zisiwafae wengine na kwamba hiyo ni kutokana na tofauti ya genetiki. Kunywa dozi kubwa ya asprini kumeripotiwa kuwa na athari ya kupunguza kichefuchefu, kutapika na hata hali ya kutoweza kuvumilia mwanga na sauti (photophobia na phonophobia) hali ambazo hujitokeza kwa wale wanaopatwa na migraine.
Lakini wataalamu wamewashauri wale wanaosumbuliwa na maumivu ya kichwa ya migraine wajiepushe kutumia vidonge hivyo kwa muda mrefu kwani aspirini zinaweza kuleta athari mbaya kama vile matatizo ya tumbo.

Vifo vya kinamama vimepungua duniani

Takwimu za mwisho zinaonyesha kwamba idadi ya vifo vya kimamama vimepungua duniani kutoka nusu milioni mwaka 1980 hadi chini ya vifo 350,000 mwaka 2008. Vifo vya kinamama vinavyotokana na ujauzito au Maternal ni vifo vya kina mama vinavyotokea wakati wa ujauzito au katika siku 42 mwishoni mwa ujauzito. Vifo hivi hutokana na sababu yoyote unayohusiana na ujauzito au masuala mengine yanayoambatana na hali hiyo.


Idadi hiyo ya vifo imekuwa ikitumika kutambua na kuonyesha kiwango cha hali ya huduma za afya katika maeneo mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa uchunguzi ulioshapishwa na jarida la The Lacent, idadi ya kinamama wanaofariki dunia kutokana na matatizo ya ujauzito imepungua kwa zaidi ya asilimia 35, katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Hii ni katika hali ambayo nchi kama vile China, Misri, Ecuador na Bolivia zimefanikiwa kufikia malengo ya kimataifa ya kupunguza idadi ya wanawake wanaofariki dunia kutokana na matatizo ya ujazito, huku nchi za Marekani na Norway zikiripotiwa kushuhudia ongezeko la vifo hivyo. Wengi wanasema kwamba, sababu kuu iliyopelekea ongezeko la vifo hivyo katika nchi hizo mbili ambazo ni tajiri na zenye huduma bora ya tiba ni kuongezeka magonjwa miongoni mwa kinamama wajawazito pamoja na kinamama kubeba mimba katika umri mkubwa.

Vilevile imeripotiwa kwamba kwenye nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika katika kila wanawake watano wajawazito mmoja kati yao ana virusi vya HIV. Ugonjwa ambao umesababisha vifo vya watu 61,400 katika mwaka 2008. Asimilia 80 ya vifo vya kina mama wajawazito hutokea katika nchi 21 duniani ambapo India, Pakistan, Nigeria, Afghanistan, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinachangia zaidi ya nusu ya idadi yote hiyo ya vifo vilivyoripotiwa.

Wednesday, April 7, 2010

Cheka unenepe na uishi maisha marefu


Utafiti mpya umeonyesha kwamba, kuna uhusiano kati ya kucheka na kuishi maisha marefu.
Utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la Saikolojia la Sayansi umeonyesha kwamba, watu wenye tabasamu pana linalojulikana kama "Dunchenne smile, huishi maisha marefu. Ernest L. Abel aliyeongoza utafiti huo amesema kwamba, watu ambao wanaonyesha hisia zao na kuziakisi kwa tabasamu pana, kimsingi huwa ni watu wenye furaha zaidi ya wale wenye kutabasamu kidogo. Hivyo watu hao hufaidika na suala hilo na kwa kawaida huishi maisha marefu.
Wataalamu wanasema kwamba watu wenye kutabasamu sana kwa kawaida huwa wana furaha, wana shaksia madhubuti, ndoa zao hudumu zaidi, wana ufahamu mzuri zaidi wa mambo na huashiriana vyema na watu wengine.

Monday, April 5, 2010

Yawezekana kuokoa maisha ya wenye HIV kwa kutumia dawa zisizo ghali

Wachunguzi wa masuala ya tiba wamesema kwamba, bado hakuna jitihada zinazofanywa za kuokoa maisha ya maelfu ya watu wanaoishi na virusi vya HIV kwa kutumia dawa rahisi na zisizo ghali. Wamesisitiza kwamba kuwapa dawa za anti-biotics kama vile co-trimoxazole wale ambao tayari wamegunduliwa kuwa na virusi vya Ukimwi kunaweza kupunguza idadi ya vifo vya wagonjwa hao mwanzoni tu wanapopata ugonjwa huo.

Uchunguzi huo uliochapishwa katika Jarida la Tiba la Lancet umegundua kuwa, kuwapa waathirika wa Ukimwi anti-biotics kunapunguza nusu ya vifo vya wagonjwa hao. Shirika la Afya Duniani WHO) tayari limeamuru kutolewa matibabu hayo lakini wataalamu na madakatari wanasema kuwa watu wengi bado hawapewi dawa hizo. Jitihada nyingi zimekuwa zikifanywa tu kuhakikisha kwamba wale walioathirika na Ukimwi wanapatiwa dawa za kuongeza maisha za antiretroviral ambazo zina athari kubwa katika kuwaongeza maisha. Hata hivyo, wagonjwa wengi wa Ukimwi katika wiki za mwanzo baada ya kugundulika kuwa wana ugonjwa huo, wanakabiliwa na hatari kubwa ya kushambuliwa na magonjwa mbalimbali kutokana na kudhoofu mfumo wao wa kinga wa mwili. Hivyo wataalamu wanasema kwamba, kuongezwa dawa kama vile co-trimoxazole ambazo ni anti-biotic zisizo ghali na ambazo hupatikana kwa urahisi, katika matibabu yao ya muda mrefu kunaweza kuwanusu na kifo.


Takwimu zimeonyesha kuwa, zaidi ya robo ya waathiriwa wa Ukimwi waliopewa dawa za kuongeza maisha za antiretroviral katika nchi za chini ya Jangwa la Sahara walifariki dunia katika mwaka wa kwanza wa matibabu. Lakini uchunguzi uliofanywa na Lancent umeonyesha kwamba, kati ya Waganda 3,179 wenye virusi vya Ukimwi, waliopewa dawa hizo pamoja na kuongezewa anti-biotic katika mpango wao wa matibabu, dawa hizo ziliwapunguzia vifo kwa asilimia 59 katika wiki 12 za kwanza, na kwa asilimia 44 kati ya wiki 12 na 72 za matibabu.
Hata hivyo imeonekana kwamba dawa hizo za anti-biotics hazipatikani katika maeneo mengi ya nchi za Uganda na Zimbabwe ambako kuna wathirika wengi wa Ukimwi.
Pia imeonekana kuwa kutumiwa dwa hizo za nyongeza kuna faida nyingine ya ziada ambayo ni kuepusha maambukizo ya ugonjwa wa Malaria kwa asilimia 15.

Sunday, April 4, 2010

Dawa ya kensa ya tezi kibofu (prostate cancer) yaonyesha matumaini zaidi

Dawa ya kensa ambayo tayari inatumiwa na wagonjwa wenye uvimbe wa tezi za kibofu imeonekana kuwa ina uwezo wa kuzuia ugonjwa huo usiendelee zaidi. Katika uchunguzi wa kimataifa imeonekana kuwa, wanaume waliopewa dawa hiyo ijulikanayo kama Dutasteride katika jaribio la kitiba, wameripotiwa kupungukiwa na hatari ya kupata ugonjwa wa kensa ya tezi kibofu (prostate cancer) kwa asilimia 23. Wanaume wote hao walikuwa wana uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huo maishani.

Wataalamu wamepokea kwa furaha matokeo hayo lakini wamesema kwamba bado utafiti wa muda mrefu unatakiwa kufanywa kuhusiana na dawa hiyo.
Huko nyuma pia wataalamu waligundua pia dawa nyingine kama hiyo iitwayo Finasteride inapunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kensa ya tezi kibofu lakini baadaye wakaona kuwa inaongeza uwezekano wa kutokea matezi makubwa ya kensa hiyo. Hivyo wamesisiza kwamba inahitajia muda mrefu ili kujua iwapo dawa hiyo haina madhara kabisa.
Inafaa kujua kuwa ugonjwa wa kensa ya tezi kibofu au prostate cancer huwapata wanaume hasa wanapofikia umri wa miaka 50 na wengine katika miaka ya 70. Nchini Marekani pekee mwaka 2005 inakadiriwa kwamba watu 230,000 walipatwa na ugonjwa huo na kusababisha vifo vya watu 30,000. Wanaume wenye matatizo ya shinikizo la damu wanaelekea kupatwa zaidi na kensa ya prostati.

Dalili za ugonjwa wa kenda ya korodani ni:
Kushindwa kukojoa.
Kuona ugumu wakati wa kukojoa.
Kushindwa kuzuia mkojo hasa usiku.
Mkojo kutoka kwa shinda, kuhisi maumivu wakati wa kukojoa.
Kuona damu imechanganyika na mkono na kuhisi maumivu upande wa chini wa kiuno na upande wa juu wa mapaja.
Lakini dalili zote hizo zinaweza kusababishwa na uvimbe wa tezi kibofu ambao hausababishwi na saratani.
Wanaume walio na dalili hizo wanatajwa kumuona daktari na kupata ushauri zaidi.

Saturday, April 3, 2010

Coca Cola huwafanya wanaume tasa!



Kinywaji cha coca cola kimeendelea kuwa maarufu duniani lakini utafiti mpya umeonyesha kuwepo uhusiano wa kunywa sana kinywaji hicho na matatizo ya uzazi kwa wanaume.
Kwa mjimu wa utafiti huo uliochapichwa kwenye Jarida la Epidemiology la Marekani, wanaume wanaokunywa zaidi ya lita moja ya coca cola kwa siku wanakabiliwa na hatari ya kuwa tasa. Wanaume waliotumia kinywaji hicho walikuwa na upungufu wa aslimia 30 ya mbegu za uzazi zilizohesabiwa, ikilinganishwa na wale ambao hawakutumia. Wanaume hao walionekana kuwa na matatizo ya uzazi zaidi kuliko wasiokunywa coca cola.

Friday, April 2, 2010

Chokoleti nyeusi zina faida kwa moyo

Japokuwa kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu taarifa kuhusu faida za kiafya za chokoleti, lakini utafiti mpya umedhihirishwa kwamba kula chokoleti nyeusi kuna faida kwa moyo. Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Moyo la Ulaya umeonyesha kwamba, kula kila siku gramu 7.5 za chokoleti, kiasi ambacho ni kidogo kuliko kipande mraba kidogo cha chokolati kunapunguza shinikizo la damu suala ambalo huondoa hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo kwa asilimia 39. Kula chokoleti kidogo huweza kumzuia mtu asipate ugonjwa wa moyo lakini iwapo tu italiwa badala ya vyakula vingine viliwavyo katikati ya mlo au asusa (snacks) vyenye kalori nyingi bila kuongeza uzito wa mwili.

Flavanols inayopatikana katika kakao huimarisha uwezo wa kiabiolojia wa seli wa kutengenezwa nitric oxide kuzunguka kuta za damu, suala ambalo hufanya mishipa laini ya damu ipumzike na kupanuka na hivyo kusaidia sana afya ya moyo. Kwa kuwa katika chokoleti nyeusi kuna kakao nyingi, aina hiyo ya chokolati ina taathira kubwa katika kupunguza mfumuko wa mawazo na wasiwasi pamoja (stress) na kusaidia mzunguko wa damu na kiwango cha chinikizo la damu. Lakini inaaminiwa kuwa chokoleti nyeupe hazina kabisa flavanol hivyo hazina faida hiyo.
Wataalamu wamesisitiza kwamba, watu wale chokolate nyeusi kila siku lakini kwa tahadhari kubwa kwani kiasi kidogo tu cha chokolati kina kiasi kikubwa cha kalori na mafuta ambavyo ni hatari kwa afya.

Thursday, April 1, 2010

Mammography inaweza kuokoa maisha ya wanawake wengi

Japokuwa kumekuwepo na mjadala mkubwa kuhusiana na uwezo wa kutambua ugonjwa wa kipimo kinachotumiwa kugundua kensa ya matiti, lakini utafiti mpya umethibitsiha kwamba, kipimo hicho kina faida kubwa.

Uchunguzi huo umeonyesha kuwa, kipimo cha mammography
faida zake ni kubwa zaidi kuliko hasara zake, na kutumiwa kwakwe kunaokoa zaidi maisha ya wanawake yanayoweza kupotea kutokana na kensa ya matiti. Mammography ina uwezo wa kuonyesha uvimbe (tumors), japokuwa kipimo hicho kinaweza kuonyesha uvimbe ambao hauna madhara, na kuwafanya baadhi ya wanawake kupata wasiwasi na kufanyiwa operesheni bure. Uchunguzi wa huko nyuma ulishauri kuwa, umri wa kufanyiwa kipimo cha mammography ili kujua kama mtu ana saratani ya matiti au la usogezwe kutoka miaka 40 hadi 50 ili kupunguza uwezekano wa wanawake kufanyiwa kipimo hicho mara nyingi maishani, Vilevile imesisitiza kwamba, kwa kila maisha ya mwanamke mmoja yanayonusuriwa kwa kufanywa mammography, kuna wanawake wengine 6 ambao wanafanyiwa kipimo hicho bila ya kuwa na ulazima.
Kwa hivyo wataalamu wamewashauri wanawake wasizembee na kuwahimiza wafanyiwe kipimo hicho, kwani faida yake ni kubwa zaidi kuliko hasara yake.
Nchini Uingereza pekee, zaidi ya wanawake 45,000 hugunduliwa kuwa wana kensa ya matiti kila mwaka, na zaidi ya wanawake 12,000 hufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

Saa moja ya mazoezi muhimu ili kupunguza uzito

Huku watu wakishauriwa kufanya mazoezi nusu saa kwa siku zisizopungua tano katika wiki ili kulinda afya zao, uchunguzi mpya umesema kuwa kwa wale wanaotaka kuzuia uzito usiongezeke inawabidi wafanye mazoezi zaidi ya muda huo. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, lisaa moja la kufanya mazoezi ya wastani linatakiwa kwa ajili ya kupunguza unene kwa wanawake.

Kila ambavyo mwanamke mwenye unene wa kawaida anavyofanya mazoezi ndivyo uzito wake utakavyopungua. Uchunguzi huo umesema kuwa kushughulisha mwili kuna umuhimu mkubwa katika kupunguza unene.
Hata hivyo wataalamu wamesisitiza kwamba kufanya mazoezi kunapaswa kuambatana na kula chakula bora ili kujenga afya vyema. Pia watu wazima wameshauri kula matunda na mboga mboga, kupunguza kula vyakula vyenye mafuta mengi na kufanya mazoezi ili kulinda afya zao na kuweza kuisha maisha marefu.