Monday, November 30, 2009

Binadamu anaweza kusikia kwa kupitia ngozi!


Huku masikio yakiwa hayachukuliwa tena kuwa ni njia pekee ya kusikia mwanadamu, uchunguzi mpya umeonyesha kuwa ngozi pia inaweza kusaidia katika kuleta kusikia. Chunguzi za huko nyuma zilionyesha kuwa, ishara za macho kama vile mzungumzaji kutikisa kichwa zinaweza kuwa kuathiri namna mtua navyosiakia kitu. Na pia inajulikana kuwa zaidi ya masikio suala zima la kusikia sauti hufanywa pia kwa kupitia mifupa ya kichwa. Uchunguzi mpya hata hivyo umehitimisha kwamba kuna masuala mengineyo zaidi ya ishara za kusikia na macho ambazo zinaathiri suala zima la kusikia. Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la Nature, binadamu wanaweza kutafisiri sio tu ishara zilizotolewa kwa macho, bali pia huweza kutafisri taarifa wanazohisi kupitia ngozi zao wakati wanaposikia jambo. Wanasayansi wana matumaini kwamba ugunduzi wao huo utafungua njia ya kuimarishwa vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya watu wasiosikia vyema.

Saturday, November 28, 2009

Jinsi ya kuhakikisha tunapata lishe bora na salama hata wakati wa Eid


Eid ni wakati ambapo familia zinakusanyika pamoja kula na kupeana zawadi na kusherehekea sikukuu hiyo adhimu. Kwa kawaida chakula kina nafasi muhimu wakati wa sherehe hizo. Sikukuu ya idil Adh-ha husherehekewa kwa mnasaba wa kumalizika kipindi cha Hijja ambapo Waislamu huenda kuzuru nyuma ya Mwenyezi Mungu katika mji mtukufu wa Makka. Katika sherehe hiyo kwa kawaida wanyama huchinjwa na kutolewa sadaka, ambapo nyama hugawanywa kwa ndugu na marafiki pamoja na masikini. Kwa kawaida chakula kinachopikwa katika siku ya iddi kinatofautiana kutoka nchi hadi nchi na jamii moja na nyingine. Lakini suala la muhimu ni kujitahidi kupata lishe iliyo salama na bora wakati wa kusherehekea sikukua ya Eid. Vyakula vinavyopikwa siku ya idi vinaweza kuwa salama lakini kwa kuwa ni wakati wa sherehe, ni rahisi kusahau kula vyakula ambavyo huweza kuhatarisha afya zetu. Ingawa ni siku ya sikukuu lakini Kona ya Afya inakutaka uwe mwangalifu kuhusiana na kile unachokula na kuipikia familia yako, huku ukijitahidi kupata chakula bora na salama. Hivyo ifuatayo ni njia ya kuifanya lishe yako ya Eid iwe salama:
• Jiepushe kula vyakula vyenye chumvi nyingi na mafuta mengi, na ni bora utumie viungo ambavyo pia vina faida tele mwilini.
• Ni bora utumie mafuta ya mimea (vegetable oli) badala ya kutumia siagi au mafuta ya mgando wakati wa kutayarisha msosi wa iddi. Epuka kutumia mafuta mengi kuliko kawaida, kwani mafuta mengi sio utamu wa chakula, bali ni hatari kwa afya yako.
• Wakati unaponunua nyama au vitoweo vinginevyo, hakikisha unanunua nyama salama, ambayo haijakaa sana na isiyokuwa na mafuta mengi. Iwapo ina mafuta jitahidi uondoe sehemu zenye mafuta kabla ya kupika.
• Hakikisha unaitayarishia na kuipikia familia yako na wageni mbalimbali mlo kamili wakati wa sikukuu. Sio wali na nyama pekee, pilau na ndizi tu, bali jitahidi kuwepo na mboga mboga na matunda pia. Halikadhalika jiepushe kupika kwa wingi vitu vyenye sukari nyingi.
• Ili kuhakikisha vitamini na madini zinabakia katika chakula unachopika, mboga mboga zisipikwe kwa muda mrefu na vilevile ili kuepuka minyoo na magonjwa mengineyo, hakikisha mboga na matunda vinaoshwa vyema.
• Wakati wa kupika chai ya maziwa wa vitindamilo vinginevyo (desserts) hakikisha unatumia maziwa yasiyo kuwa na mafuta mengi au low fat milk.
• Ili kuepuka kupika vyakula vya kukaanga na vyenye mafuta mengi, unaweza ukaoka vyakula hivyo badala ya kuvikaanga na ukapata ladha nyingine na kuwa bora zaidi kwa afya yako nay a familia yako kwa ujumla.
• Kunawa mikono na kuhakikisha usafi unazingatiwa, ni miongoni mwa mambo muhimu wakati w akutayarisha na kupika vyakula kwa ajili ya sikukuu.
Naam kina mama na kina dada, eid ni wakati wako mwingine ambao mbali ya kuonyesha ufundi wako wa kupika vyakula vitamu na vya kila aina kwa ajili ya wale uwapendao na wageni mbalimbali, hakikisha pia unazingatia afya ya walaji na kutunza afya kwa ujumla.
Eid Njema!

Eid Mobarak!


Nawatakia Eid njema wadau.
Msisahau kuzitunza vyema afya zenu.

Watu milioni 25 wamefariku dunia duniani kote kutokana na UKIMWI


Taarifa ya pamoja ya Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na shirika la UNAIDS imesema kwamba, idadi ya watu waliofariki dunia duniani kote kutokana na ugonjwa wa Ukimwi imefikia milioni 25. Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa hivi karibuni, inakadiriwa kwamba watu wengine milioni 33.4 wanaishi na virusi vya HIV duniani. Ripoti hiyo aidha imesema kwamba, karibu watu milioni 60 wakiwemo watu 25 milioni waliofariki dunia, wameambukizwa virusi vya HIV tangu ugonjwa huo ulipoanza. Ingawa idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa wa HIV imeongeza, lakini takwimu za watu wanaofariki kutokana na ugonjwa huo, zimepungua ikilinganishwa na huko nyuma.
Matumizi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi au anti-retroviral drugs, yanaaminika kuwa yamepunguza kwa asilimia 10 vifo vinavyotokana na magonjwa yanayoambatana na ugonjwa wa Ukimwi katika miaka mitano iliyopita.
Ripoti hiyo pia imesema kwamba, bara la Afrika bado ni sehemu yenye maambikizo makubwa zaidi ya virusi vya Ukimwi ikilinganishwa na sehemu nyinginezo duniani na kwamba ugonjwa huo unasababisha nusu ya wakinamama wanojifungua kufariki dunia katika bara hilo.

Monday, November 23, 2009

Sababu kuu zinazomfanya mtu aweze kupata mshituko wa moyo!..sehemu ya 2


Kwanza tutazungumzi baadhi ya sababu zisizoweza kuzilika zinazosababisha mshituko wa moyo. Nazo ni kama ifuatavyo:-
Kuongezeka umri: Asilimi 83 ya watu wanaokufa na magonjwa ya moyo ni wale waliofikia umri wa miaka 65 na kuendelea. Umri unapokuwa mkubwa, wanawake ambao kwa kawaida hawapatwi sana na ugonjwa moyo, nao pia huanza kukabiliwa na hatari ya magonjwa hayo ukiwemo mshituko wa moyo.
Jinsia ya kiume: Wanaume wanakabiliwa na hatari zaidi ya kupatwa mashituko wa moyo kuliko wanawake, ambapo hupata ugonjwa huo katika umri mdogo. Wanawake baada ya kukatika hedhi au menopause, nao pia huanza kukabiliwa na hatari hiyo lakini si kwa kiasi kikubwa kama wanaume.
Urithi: Watoto ambao wazazi wao wana na magonjwa ya moyo au walipatwa na mshituko wa moyo nao pia wanakabiliwa na hatari ya kupaatwa na magonjwa hayo. Waamerika Weusi wanapatwa na shinikizo la damu zaidi wakilinganishwa na watu wenye asili ya Caucasian au wazungu. Magonjwa ya moyo pia hutokea sana kwa watu wenye asili ya Mexico, India, Hawaii na Asia. Watu ambao familia zao zina historia ya magonjwa ya moyo wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo mara mbili zaidi kuliko wengine, kwani mtu hawezi kuchagua umri wake, jinsia na asili yake.
Zifuatazo sasa ni baadhi ya sababu zinazoweza kuepukika zinazosababishwa mshituko wa moyo:-
 Kuvuta sigara: wavuta sigara wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo mara 2 hadi 4 zaidi ya watu wasiovuta sigara. Uvutaji sigara ni sababu kubwa inayojitegemea inayoweza kusababisha mshituko wa moyo kwa wagonjwa wenye maradhi ya moyo. Kuvuta sigara hadhani au mbele ya wengine kunawafanya watu hao nao wakabiliwe na hatari hiyo magonjwa ya moyo.
 Kiwango kikubwa cha mafuta katika damu au High Blood Cholesterol: Kila kiwango cha mafuta kinapoongezeka katika damu ndio uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya moyo nao unavyoongezeka. Iwapo mtu atakuwa na sababu nyinginezo kama ufutaji sigra, shinikizo la damu na kadhalika, basi mtu huyo ana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata shinikizo la moyo. Kiwango cha mafuta katika damu pia kinathiriwa na umri, jinsi, urithi na lishe.
 Shinikizo la damu: Shinikizo la damu huongeza ufanyajikazi wa moyo, suala linalopelekea mishipa ya moyo iwe minene na migumu. Pia huongeza hatari ya kupata mshituko wa moyo, mshituko wa ubongo, figo kutofanya kazi na moyo kushindwa kufanya kazi. Shinikizo la damu linapokuwa pamoja na unene wa kupindukia, uvutaji sigara, kiwango cha juu cha mafuta kwenye damu au kisukari, humfanya mtu apatwe kwa urahisi na mshituko wa moyo.
 Kutoushughulisha mwili: Kuishi maisha yasiyokuwa ya kushughulika kifizikia ni miongoni mwa sababu za kupatwa na ugonjwa wa moyo. Shughuli za kawaida husaidia kuzuia magonjwa ya moyo na kuongezeka kiwango cha mafuta katika damu. Unapoushughulisha mwili wako zaidi ndivyo unavyojisaidia zaidi kiafya. Kushughulisha mwili husaidia kudhibiti kisukari, unene wa kupindukia, kiasi kikubwa cha mafuta katika damu na hata kupunguza shinikizo la damu.
 Unene wa kupindukia au Obesity: Watu wenye unene wa kupindukia wana mafuta mengi mwilini na iwapo mafuta yamejikusanya katika nyonga na kiuno wanaweza kukabiliwa na hatari ya kupata mshituko wa moyo. Unene mkubwa huufanya moyo ufanye kazi zaidi. Pia huongeza shinikizo la damu na kiwango cha mafuta katika damu. Halikadhalika unene humsababisha mtu apatwe na kisukari.
Sababu nyinginezo ni pamoja na
 Mtu kuwa na mawazo na fikra kila mara, kwani wataalamu wanasema kuwa kuna uhusiano kati ya kuwa na mawazo na fikra na magonjwa ya moyo. Kwani mtu mwenye mawazo mengi kwa kawaida huwa na ghadhabu, huenda akavuta sigara na mengineyo ambayo huweza kupelekea ugonjwa wa hatari.
 Kunywa sana pombe: Kunywa sana pombe husababisha shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na kupelekea mshituko wa moyo. Pia huongeza kiasi cha mafuta katika damu, kensa na magonjwa mengineyo na hata husababisha moyo kupiga hovyo. Vilevile huchangia katika kusababisha unene wa kupindukia, ulevi wa kupindukia, kujiua na ajali.

Saturday, November 21, 2009

Kitunguu swaumu kinazuia influenza!



Kitunguu swaumu tangu kale kimekuwa kikijulikana kama 'dawa ya kushangaza' na kutumiwa na watu wengi katika kutibu mafua na influenza. Miongoni mwa faida za kitunguu swaumu ni kuzuia kupatwa na magonjwa mbalimbali na maambukizo ya virusi. Hivyo kitunguu swaumu hujulikana kama antibiotiki ya asilia. Uchunguzi umeonyesha kwamba kula kitunguu swaumu kunapunguza kushadidi ugonjwa wa influenza na hata kuzuia kupatwa na ugonjwa huo. Vilevile kula kila mara kitunguu swaumu, huzuia kupatwa na magonjwa ya moyo, kwani kitunguu swaumu huzuia damu isigande kwenye mishipa ya damu.
Halikadhalika kitunguu swaumu ambacho pia ni kiungo muhimu cha chakula kina potassium, na hivyo watu wenye ugonjwa wa shinikizo la damu wanashauriwa kula vyakula vilivyopikwa kwa kitunguu swaumu.
Si vibaya kujua kuwa katika uchunguzi uliochapishwa mwaka 2001, imeelezwa kwamba, kitunguu swaumu kina athari kubwa na nzuri pale kinapochanganywa na baadhi ya dawa nyinginezo katika kutibu Ukimwi au HIV.
Haya shime jamani… kuanzia leo vyakula visikose kuungwa na kitunguu thomu, iwapo unaogopa kupatwa na influenza kama mimi!

UNICEF yasema, Afghanistan ndiyo sehemu mbaya zaidi ya kuzaliwa mtoto duniani


Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema kuwa nchi ya Afghanistan iliyoharibiwa kwa vita ni sehemu mbaya zaidi duniani ya kuzaliwa mtoto. Shirika hilo limetangaza kwamba, Afghanistan ina idadi kubwa zaidi ya vifo vya watoto duniani ambapo vifo 257 vya watoto hutokea kati ya kila watoto 1,000 wanaozaliwa.
Daniel Toole Mkurugenzi wa Unicef wa kusini mwa Asia amesema kwamba, ripoti yake ya mwaka kuhusiana na watoto duniani imegundua kwamba, Afghanistan ni sehemu hatari kwa wasichana na kwamba kukosekana usalama kumepunguza idadi ya watoto wanaohudhuria shuleni hasa wa kike. Aidha mkurugenzi huyo wa Unicef amelaumu mashambulio ya mara kwa mara ya shule za wasichana ambayo yamesababisha elimu ya wanawake kuporomoka kabisa nchini Afghanistan.

Friday, November 20, 2009

Haya kinadada macho juu!…. Viagra ya wanawake yagunduliwa!


Wataalamu wamegundua bila kutarajia Viagra ya wanawake, wakati walipokuwa wakifanya uchunguzi wa dawa ya kuondoa mfadhaiko wa mawazo au antidepressant. Katika majaribio matatu tofauti, imeonekana kuwa dawa iitwayo flibanserin ina athari ya ajabu katika kuongeza nguvu za kufanya mapenzi kwa wanawake, bila dawa hiyo kuwa na athari yoyote katika kuondoa mfadhaiko wa fikra. Wanasayansi hao wa Chuo Kikuu cha Carolina Kaskazini nchini Marekani wamesema kuwa, katika chunguzi huo usiokuwa wa kutarajiwa, imeonekena kuwa dawa hiyo inaongeza nguvu za kujamiina kwa wanyama wa maabara na binaadamu pia. Wamesema kuwa, ni muhimu kupatikana dawa kama Viagra kwa wanawake, kwani itatumiaka kutibu kutokuwa na matamanio ya kufanya mapenzi au libido kitaalamu, ambayo ni moja ya matatizo sugu ya kijinsia waliyonayo wanawake.

Seli mama zinaweza kutengeneza ngozi mpya kwa walioungua moto


Wataalamu wa Ufaransa wamesema kuwa, wamegundua njia mpya ya kutumia seli mama za kiini tete cha mwanaadamu (human embryonic stem sells) kutengeneza ngozi mpya ambayo inaweza kutumika kwa watu waliongua na moto. Wamesema kuwa, katika uchunguzi wao seli mama imeweza kuota na kuwa ngozi kamili, wiki 12 baada ya kupandwa katika panya wa maabara. Wataalamu hao wameonyesha matumaini yao kwamba, ngozi hiyo inaweza kutatua tatizo la kuangaliwa vibaya na hata kukataliwa wagonjwa walioungua vibaya na moto katika jamii. Wataalamu wa seli mama wamesema kwamba, ugunduzi huo ni mafanikio muhimu.
Kwa zaidi ya miaka 20 sasa wagonjwa walioungua vibaya kwa moto wamekuwa wakitumia teknolojia inayokuza ngozi mpya katika maabara, lakini kwa kutumia seli za ngozi zao wenyewe. Lakini teknolojia hiyo inachukua wiki tatu, suala ambalo linamfanya mgonjwa aliyeungua akabiliwe na hatari ya kupoteza maji ya mwili na kupata maradhi mbalimbali au infection.

Thursday, November 19, 2009

Mapacha wa Baghaladesh waliokuwa wameungana waachanishwa


Timu ya madaktari 16 wa Australia wamefanikiwa kuwatenganishwa watoto mapacha wa Bangladesh waliokuwa wameungana kwa miaka mitatu, katika operesheni iliyochukua masaa 27. Trishna na Krishna ni watoto mayatima wa Bangladesh waliokuwa wameungana katika sehemu za juu za kichwa na kuwa na mishipa ya damu ya pamoja. Madakatari wataalamu wa masuala ya ubongo wa Australiwa katika oparesheni hiyo waliugawa ubongo wa watoto hao kwa tahadhari kubwa na kuwaachanisha. Watoto hao wadogo wa kike walikuwa mahututi walipowasili nchini Australia miaka miwili iliyopita, ambapo tayari walikuwa wameshafanyiwa operesheni kadhaa za utangulizi. Madakatari huko nyuma walisema kuwa kwa kufanyiwa operesheni huo kulikuwa na uwezekano wa asilimia 25 kwamba mmoja kati ya mapacha hao angekufa na asilimia 50 watoto wote hao wawili wanngepatwa na matatizo ya kuharibika ubongo. Lakini Mkuu wa kitengo cha Upasuaji wa hospitali ilipofanywa oparesheni hiyo Dakta Leo Donnan amesema kuwa, watoto hao wanaendelea vyema baada ya kufanyiwa operesheni hiyo, lakini bado wako katika chumba cha uangalizi maalum wakisubiri operesheni nyingine ya kuzishona tena ngozi zao, mifupa na kuongezewa baadhi ya viungo bandia. Oparesheni za kuwatenganisha mapacha walioshikana ni kazi nzito ambayo kwa kawaida huwa hazifanywi katika hospitali mbalimbali duniani. Operesheni hizo zinapofanywa mara nyingi hupelekea vifo vya mapacha hao. Mapacha wanaoungana au Conjoined Twins hutokea kwa uchache katika mimba, mara moja katika kila kesi 200, na huwa katika mapacha wanaoshabihiana au identical twins. Mara nyingi hata kama mimba kama hizo zitatungwa lakini kwa asilimia 40 au 60 watoto hao hufia tumboni, au watoto wanaozaliwa kufariki dunia siku chache baada ya kuzaliwa. Mimba za mapacha wanaoungana kwa asilimia 70 huwa ni za watoto wa kike, sababu ambayo haijulikana.

Monday, November 16, 2009

Kumbuka yafuatayo kabla ya kupaka rangi nywele zako


• Osha nywele zako vizuri kwa shampuu kabla ya kuweka rangi.
• Usiweke kondishena na usitumie shampuu zenye kondishena kwani kondishena itasababishwa rangi isiingie vyema katika nywele.
• Iwapo kichwa chako ni sensitive au nywele zako zimeharibika au kavu, subiri dakika 12 hadi 24 baada ya kuosha ndio upake dawa ya kubadilisha nywele rangi.
• Na wakati unapopaka dawa ya kutia rangi nywele fuata maelekezo vizuri kama yalivyoandikwa.
• Tumia glavu pamoja na taulo, rangi ya nywele inaweza kukuchafua kila mahali, hasa ikiwa katika suala hili wewe si mjuzi.
• Ili kuzuia rangi ya nywele kuingia katika ngozi yako, unaweza kupaka vaselini kuzunguka kichwa, lakini hakikisha haiingia katika nywele kwani inaweza kuingiliana na rangi na kufanya rangi isikole vyema.
• Iwapo rangi itaingia katika ngozi yako, usihofu itaondoka baada ya kuoga mara mbili au tatu. Na wakati unapaka rangi iwapo utaiona imeingia katika ngozi, hapo hapo chukua tishu au karatasi laini na ipake shampuu kidogo na uifute. Itatoka bila matatizo yoyote.
• Tumia kondishena baada ya kuzipaka rangi nywele zako. Ni bora utumie kondishena ambayo ni maalum kwa ajili ya nywele zilizotiwa rangi.

Kinadada wasihofu tena…. kwani rangi za nywele hazisababishi kensa!


Taasisi ya Ujerumani ya kuchunguza hatari za vitu imetangaza kwamba rangi za nywele hazisabishi kensa. Uchunguzi wa taasisi hizo umesema kuwa mada zinazosababishwa kensa hazijashuhudiwa katika rangi za nywele. Hata hivyo taasisi hizo imesema kuwa uchunguzi unatakiwa kufanywa zaidi ili kujua iwapo katika rangi hizo kunatiwa mada ambazo husababisha allergy kwa watumiaji.

Saturday, November 14, 2009

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Kisukari



Leo ni Jumamosi tarehe 14 Novemba ambayo ni siku ya kimataifa ya ugonjwa wa kisukari au diabete. Hii ni siku ambayo kampeni za tahadhari hufanywa dunia nzima kuhusiana na ugonjwa wa kisukari. Kwa ajili hiyo Shirika la Afya Dunia (WHO) pamoja na taasisi nyingine za Tiba na Afya duniani, zikishirikiana na madaktari, wataalamu na wadau wa Afya uliwemnguni kote, hutumia siku hii ili kuelimisha na kufunza zaidi jamii kuhusiana na ugonjwa wa kisukari. Taasisi ya Kisukari ya Kimataifa inakadiria kuwa watu milioni 344 duniani wako katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari aina ya pili, au Type 2 Diabates. Idadi hiyo ni sawa na idadi yote ya wananchi wa Marekani, iwapo utawahesabu wakaazi wa California mara mbili. Taasisi hiyo pia imetangaza kuwa, watu milioni 285 tayari wanasumbuliwa na ugonjwa huo duniani kote.
Kwa mnasaba huo basi Kona ya Afya inachukua fursa hiyo kuelezea ni nini ugonjwa wa kisukari?
Kisukari ni ugonjwa unaotokea pale mwili unaposhindwa kusaga vyema chakula ili kutoa nishati na kusaidia ukuaji wa mwili. Kila tunachokula husangwa na kubadilishwa kuwa glukosi. Glukosi ni aina ya sukari kwenye damu ambayo ndio chanzo cha nishati au kama mafuta kwa ajili miili yetu.
Baada ya chakula kuyeyushwa hushika njia kuelekea katika damu. Seli zetu za mwili hutumia glukosi kama chanzo cha nishati na kukua. Hata hivyo, glukosi haiwezi kuingia katika seli zetu za mwili bila kutumia wenzo unaoitwa insulini. Insulin huwezesha seli zetu za mwili kuchukua glukosi. Insulini ni homoni ambayo inatengenezwa na kongosho au pancreases.
Tukishwa kula chakula, kongosho zenyewe hutoa kiasi cha kutosha cha insulini kinachoweza kuhamisha glukosi iliyoko kwenye damu kwenda kwenye seli, na kwa njia hiyo kiwango cha sukari katika damu hupungua.
Mtu mwenye kisukari ana hali ambayo kiwango cha sukari katika damu yake kiko juu sana au hyperglycemia. Hii husababishwa na moja kai ya hali tatu zfuatazo. Moja ni kwa sababu mwili huwa hauwezi kutoa kiasi cha Insulini inayotakiwa . Mbili ni pale inapokuwa hakuna insulini inayotengenezwa mwilini, na tatu ni pale seli za mwili zinapokuwa hazishughuliswi ipaswavyo na insulini inayotengenezwa na kongosho.
Matokeo ya hali hizo hupelekea kujikusanya sukari kwa wingi katika damu. Sukari hiyo nyingi kwenye damu polepole hutoka nje ya mwili kama mkojo. Hivyo, ingawa damu ina kiasi kikubwa cha sukari, lakini seli za mwili haziwezi kuitumia sukari hiyo ili kukidhi mahitaji muhimu ya kuupatia mwili nishati na nishati na kwa ajili ya kukua.
Kuna aina tatu za Kisukari.
1. Kisukari aina ya kwanza au Diabates Type 1, aina hii hutokea pale mwili unaposhindwa kuzalisha insulini kabisa.
2. Kisukari aina ya pili au Diabates Type 2, aina hii hutokea pale mwili uanapozalisha insulini lakini insulini hiyo ikawa haiwezi kutumika ipaswavyo.
3. Kisukari cha Ujauzito au Gestational Diabates, kisukari cha aina hii hutokea wakati wa ujauzito.
Inafaa kufahamu kuwa kisukari aina ya kwanza na ya pili ni magonjwa sugu, ikimaanishwa kuwa ni ugonjwa unaoendelea na kwa kawaida mara nyingi hautibiki na kumalizika, bali mgonjwa hubakia nao umri wake wote. Lakini kisukari cha wakati wa ujauzito kwa kawaida hutokea tu wakati huo wa mamba, na baada ya mtoto kuzaliwa ugonjwa huo huisha.

Friday, November 13, 2009

Mshituko wa Moyo ( Heart Attack) au Myocardial Infarction….sehemu ya kwanza



Mshituko wa moyo unatokea wakati mzunguko wa damu katika misuli ya moyo unapozuiwa. Iwapo mzunguko huo wa damu hautoendelea haraka, kitendo hicho huifanya misuli ya moyo kuharibika kwa kukosa oksijeni na huaza kufa. Mshituko wa moyo kwa lugha ya tiba unajulikana kama 'Myocardial Infarction' inayomaanisha "Myo".. muscles au msuli, 'cardio'…. Heart au moyo, "infrct"….death of tissue from lack of oxygen au kufa tishu kwa kukosa oksijeni.
Kama vilivyo viungo vingine mwilini hasa misuli, moyo nao huhitajia damu. Bila damu seli za moyo hudhoofika suala ambalo hupelekea mtu kuhisi maumivu. Shinikizo la damu hutokea pale mshipa mmoja wa damu au zaidi inaposhindwa kusafirisha damu yenye oksijeni katika moyo, kutokana na kuziba mishipa hiyo. Mishipa ya damu inaweza kuziba kutokana na:
1. Kuta za mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo (coronary arteries) kuwa nene.
2. Chembechembe za mafuta kukusanyika katika mishipa ya damu.
3. Kudhoofika na kukonda mishipa ya damu.
4. Mishipa ya damu mara inaposinjaa na kushikana au spasm.
5. Kujitokeza donge la damu katika mishipa ya damu.

Lakini ni wakati gani mtu anakabiliwa na hatari ya kupata mshituko wa moyo?
• Kuongeza umri au umri mkubwa
• Unene wa kupindukia
• Kuvuta sigara
• Shinikizo la damu
• Maisha yasikuwa na harakati na kujishughulisha (sedentary lifestyle)
• Kiwango cha juu cha mafuta katika damu ( High Blood Cholesterol)
• Kisukari
• Kuwa na mawazo, wasiwasi na fikra nyingi.
• Baadhi ya magonjwa ya moyo.
• Kufanyiwa operesheni ya moyo.
• Kuwa na ndugu ambao wana matatizo ya moyo.
• Wanaume.
……msikose kuungana nami katika sehemu ya pili ambapo tutajadili kwa undani sababu hizo na mengineyo.

Thursday, November 12, 2009

Ongezeko la vifo vya UKIMWI nchini Afrika Kusini


Waziri wa Afrika wa Afrika Kusini amesema kwamba kiwango cha watu wanaofariki duniani nchini humo kimeongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kutokana na kuenea ugonjwa wa Ukimwi. Aaron Motsoaledi ameilaumu serikali iliyopita ya nchi hiyo wa Rais Thabo Mbeki akisema kwamba ilisababisha kupanda sana kiwango cha vifo nchini humo katika kipindi cha baina ya mwaka 1997 hadi 2008. Amesema karibu watu laki tatu walifariki dunia nchini Afrika Kusini mwaka 1997 ambapo mwaka 2007 idadi hiyo ilipanda na kufikia karibu watu laki 7 na 56 elfu. Waziri huyo wa afya wa Afrika Kusini ameongeza kuwa, kutokana na kuongezeka idadi ya vifo nchini humo, serikali ya hivi sasa imeamua kufanya marekebisho ya kimsingi katika siasa zake ili kupambana na ongezeko la ugonjwa hatari wa Ukimwi nchini humo. Idadi kubwa ya wahanga wa Ukimwi nchini Afrika Kusini ni vijana. Waziri wa Afya wa nchi hiyo anasema kwamba karibu asilimia 75 ya vifo vya watoto wadogo nchini humo vilitokea mwaka 2007 kutokana na ugonjwa wa Ukimwi. Hatua ya Waziri Aaron Motzoaledi ya kulaumu ongezeko la wahanga wa Ukimwi katika kipindi cha Urais wa Thabo Mbeki, kwa mara nyingine kunaonyesha hitilafu za wazi zilizopo baina ya Rais huyo wa zamani na Rais Jacob Zuma wa hivi sasa wa Afrika Kusini kuhusiana na namna ya kupambana na Ukimwi nchini humo. Itakumbukwa kwamba katika kipindi cha Urais wake, Thabo Mbeki alitilia shaka hata uhakika uliothibitishwa kielimu kwamba Ukimwi unasababishwa na virusi vya HIV. Hata Manto Msimang Waziri wa Afya wa serikali ya Thabo Mbeki aliwataka watu wenye virusi vya HIV nchini humo watumie mboga mboga badala ya dawa za kupambana na virusi hivyo. Alitoa mwito huo katika hali maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini walikuwa wakiendelea kufa kwa Ukimwi kutokana na ukosefu wa madawa. Hivi sasa na licha ya kuwa Afrika Kusini ina mradi mkubwa zaidi wa kupambana na Ukimwi duniani lakini bado inatathminiwa kwamba karibu watu milioni moja wanahitajia kutibiwa ugonjwa huo nchini humo.

Wednesday, November 11, 2009

Vyakula vinavyosaidia mwili kujilinda na maambukizo ya homa ya mafua ya nguruwe



Kula karoti, uyoga, komamanga na chai ya kijani ( green tea) kunasaidia kuulinda mwili katika kukabilina na kupatwa na ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe.
Kama mnavyojua kila siku zinavyokwenda, ndivyo idadi ya watu wanaopatwa na influenza aina ya H1N1 inavyoongezeka duniani kote, basi tunapaswa kujua namna ya kuilinda miili yate ili kuepuka kupatwa na ugonjwa huo. Wataalamu wameelezea vyakula kama vile karoti, uyoga, komamanga na chai ya kijani huufanywa mfumo wa kulinda mwili kuwa na uwezo wa kukabiliana na virusi hivyo hatari vinavyosababishwa hama ya mafua ya nguruwe.
 Karoti zinaonekana kufaa sana katika suala hilo kwani zina mada ya beta carotine husaidia mwili katika kukabiliana na ugonjwa huo. Imeonekana kuwa kila betacarotine inavyokuwa mwilini kw aingi ndivyo seli za kulind amiwli zinavyoongezeka.Basi tutumie karoti katika vyakula vyetu ikibidi kila siku. Tunaweza kutengeneza saladi, juice ya karoti au hata maji ya karoti na maziwa.
 Uyoga nao vile vile huimairisha kinga ya mwili na ni chakula kinachoupatia mwili protini pia. Tunaweza kupika uyoga kama mboga au kuutumia katika saladi, sosi au kuuchanganya katika vyakula vinginevyo kama vile pizza n.k.
 Komamanga ni tunda ambalo linasifika sana kwa kuwa na uwezo wa anti oxidanti ambapo anti oxidant huzuia radikali huru ambazo ni hatari sana kwa mwili wetu. Uwezo huo humepekea mwili kukabilina na magonjwa mbalimbali ukiwepo ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe. Kama huwezi kupata tunda la Komamanga sokoni, basi unaweza kutumia juisi ya kamamanga.
 Chai ya kijani (Green Tea) ina aina mojawapo ya anti oxidanti inayojulikana kama Catechin ambayo huweza kuongeza seli za kulinda miwli. Wataalamu wanasema kuwa Catechin huvipavya virusi vya homa ya mafua ya nguruwe visiweze kusambaa mwbilini.Tusisahau pia kuwa mojawapo ya faida za chai ya kijani ni kuwa husadia kuongeza umri wa mtu na kuimarisha mfumo wa kulinda mwili.

Monday, November 9, 2009

Kula nyanya kwa Afya yako!


Pengine wengi tunafikiri nyanya hazina umuhimu sana kwa mwili, lakini labda kwa kujua yanayopatikana ndani yake, tukabadilika mawazo yetu. Nyanya si kiungo cha chakula tu kinachotoa ladha nzuri kwenye mchuzi na kachumbari lakini pia zina faida kubwa kwa mwili.
Nyanya inaupatia mwili wetu faida zifuatazo.
• Vitamin C, A na K
• Pottasium
• Manganese
• Ufumwele
• Cromium
• Vitamini B1 na B6
• Chuma
• Kopa
• Vitamin B2 na B3
• Magnesium
• Folate, Phosphorous
• Protini ingawa kwa kiasi kidogo.
• Tryptohan, Folate na Molybdenum.

Kweli inabidi kwa kujua hivyo, tusiidharua nyanya tena!

Sunday, November 8, 2009

Unene wa kupindukia, ndio chanzo cha kesi 100,000 za kensa nchini Marekani



Unene wa kupindukia au Obesity unaaminiwa kuwa ndio sababu ya kutokea zaidi ya kesi 100,000 za kensa kila mwaka nchini Marekani, huku unene pia ukiwa unamletea mtu hatari ya kupatwa na magonjwa mengi kama vile kisukari na hata homa ya mafua ya nguruwe. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Kitengo cha Utafiti wa Kensa cha Marekani, unene unasababisha aina mbalimbali za kensa, zikiwepo kesi 33,000 za kensa ya matiti, unene ambao unaweza kutokana na lishe isiyofaa, kukosekana harakati pamoja na kuwa na mafuta mengi mwilini.
Taarifa hiyo pia imesema kwamba, tatizo la kuwa na unene wa kupindukia lina athari kubwa tatu katika aina saba za saratani. Imeonekana ushahidi wa kuwepo uhusiano kati ya unene au obesity na kensa za mfumo za koo, kongosho, figo, matiti na utumbo.
Wataalamu wanasema kuwa, mafuta mengi mwilini huongeza kiwango cha homoni aina ya steroids na homoni nyinginezo ambazo zinahusiana na kutokea kensa. Seli za mafuta ni maarufu kwa kutengeneza ostrogen, ambayo imeonekana kuwa inashajiisha ukuaji wa seli katika kensa ya matiti. Halikadhalika mafuta mengi mwilini hupunguza uwezo wa kinga ya mwili na kuongeza mada za oxidative ambazo hupelekea kuharibika DNA na mwishowe kusababisha saratani.
Inakadiriwa kuwa asilimia 49 ya kesi za saratani ya kizazi ambayo ni aina maarufu zaidi ya kensa za mfumo wa uzazi, na asilimia 35 ya kesi za saratani ya koo nchini Marekani zinahusiana na unene wa kupindukia.
Inafaa kuashiria hapa pia kuwa, asilimia 34 ya Wamarekani wenye umri wa miaka 20 na kuendelea wana unene wa kupindukia au Obesity.

Saturday, November 7, 2009

Soda za kupunguza uzito (Diet Soda) husababisha matatizo ya figo


Wakati soda za kupunguza uzito au diet soda zin pendwa na kutumiwa sana hasa na watu wanaohofia suala la uzito wa miili yao na kiasi cha kalori wanazokula, uchunguzi mpya umeonyesha kuwa oada hizo zinasababisha matatizo ya figo.
Wataalamu wa Marekani wametangaza kwamba, kunywa soda mbili au zaidi za diet kwa siku, kunazidisha mara mbili uwezekano wa kupata matatizo ya figo. Katika uchunguzi huu, asilimia 30 ya wanawake wanaokunywa soda hizo mbili au zaidi kwa siku, wameonekana kuwa wamepatwa na matatizo ya figo yanayojulikana kama GFR au Glomerular Filtration Rate ambapo ugonjwa huo huzifanya figo zipoteze uwezo wake wa kuchuja vyakula.
Wataalamu hao pia wameongeza kuwa, kula chumvi nyingi nako kunapelekea figo zishindwe kufanya vyema kazi zake.

Tibu chunusi kwa kutumia limau!


Limau kulina tindikali aina ya citric ambayo inasaidia kuponya chunusi. Vilevile tunda hilo lina Vitamin C ambayo ni muhimu katika kuifanya ngozi iwe na afya wakati alkali inayopatikana katika limau nayo husaidia kuua vijidudu vinavyosababisha chunusi.
Kunywa juisi ya limau kama chakula cha kwanza asubuhi kunaaminika kusadia kuboresha ngozi.
Jinsi ya kutengeneza nyumbani mchanganyiko wa limau kwa ajili ya kutibu chunusi:
• Kwa kutumia pamba paka maji ya limau katika sehemu yenye chunusi na wacha kwa usiku kucha.
• Safisha kwa maji safi asubuhi inayofuata.
• Ingawa unaweza ukahisi kuwashwa wakati unapopatumia mchanganyiko huo juu ya ngozi mara ya kwanza, lakini baadaye hali hiyo huzoeleka.
Au

1. Changanya maji ya limau ulioyakamu kutoka katika kipnde kimoja cha limao na changanya na maji ya waridi (rose water) au asali nyepesi kwa kiwango hicho hicho.
2. Paka mchanganyiko huo katika sehemu za ngozi zenye chunusi na subiri kwa muda usiopungua nusu saa mpaka saa lizima.
3. Baadye osha kwa maji.
Mchanganyiko huu unapaswa kupakwa mara mbili kwa siku, bora utumiea asubuhi na jioni.
Muhimu: kutumia mchanganyiko huu hakuna madhara na ni wa asilia, lakini iwapo chunusi zinazidi au kuna vidonda vinavyoambatana na chunusi ni bora upate uchauri wa daktari kwanza.

Friday, November 6, 2009

Namna ya Kujikinga na Homa ya Mafua ya Nguruwe….Sehemu ya Pili



1. Vaa mask za uso ili kujikinga kupata ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe, hasa unapokuwa katika maeneo ya mikusanyiko.
2. Ziba pua na mdomo pale unapokohoa au kupiga chafya, ni bora ukitumia soft tissue ( karatasi za kufutia uso). Tupa katarasi hiyo baada ya kutumia mara moja tu. Ni bora ujiepushe kutumia vitambaa kwani kitambaa hutumika mara kadhaa na huweza kusadia kubeba vijidudu.
3. Ni bora ujiepushe kwenda kwenye mikusanyiko isiyo ya dharura, kwani sehemu kama hizo huweza kuwa mazingira mazuri ya kuambukizana homa ya mafua ya nguruwe.
4. Dumisha usafi, osha mikono na uso vizuri kwa sabuni mara kwa mara. Suala hilo hupunguza maambukizo ya virusi vya mafua ya nguruwe. Ni bora iwapo utatumia sabuni za kuua vijududu kama vile dettol n.k.
5. Waangalie vyema watoto kwani wao vi rahisi kupata ugonjwa huo. Wafundishe kuosha mikono kila mara na kudumisha usafi na ni bora kama watapata kinga ya ugonjwa huo.
6. Jiepushe kula hovyo, hasa vyakula vya vinavyotayarishwa nje ya nyumba, kwani huenda vikawa si salama na vikakusababishia kuambukizwa virusi vya mafua ya nguruwe.
7. Kunywa maji yaliyochemshwa.
8. Jiepushe kuwashika au kuwa karibu na nguruwe, ni bora wanyama hao watengwe ili kuepusha maambukizo ya ugonjwa huo.
9. Iwapo utajisikia dalili za mafua au dalili nyinginezo za homa ya mafua ya nguruwe ni vyema umuone haraka daktari.

Thursday, November 5, 2009

Namna ya kupima kiwango cha mafuta mwilini kwa kutumia BMI


BMI au Body Mass Index nia njia inayotumiwa kupima uzito wa mwili ukilinganishwa na urefu. Ingawa kipimo hicho hakionyeshi kiwango cha mafuta mwilini moja kwa moja lakini kinaonyesha kiwango cha unene ambao hukadiria hatari ya kupatwa magonjwa mbalimbali. Kipimo cha BMI kinatumika kwa wanawake na wanaume walio na umri wa kuanzia miaka 20 na kuendelea.
Namna ya kuhesabu BMI:
Uzito kwa kiwango cha kilogramu, gawanja kwa meta mraba ya urefu.
Kiwango cha BMI sawa au chini ya 18.5 kinaonyesha kuwa uzito wa mtu ni mdogo chini ya kiwango kinachotakiwa kiafya.
Kiwango cha BMI kikiwa sawa na 18.5 hadi 24.9 kinaonyesha kwamba uzito wa mwili ni wa kawaida na unaotakiwa.
Kiwango cha BMI kinapokuwa kati ya 25.0 na 29.9 kinaonyesha kuwa mtu ana uzito mkubwa.
Lakini kiwango cha BMI kinapokuwa 30 na kuendelea inaonyeshea kuwa uzito wa mtu ni mkubwa mno au ana obesity.
Mbali na BMI vilevile mzunguko wa kiuno au (waist size) unaozidi nchi 40 kwa wanaume na wanawake nchi 35, unaonyesha kuwa mtu yuko katika hatari ya kupata matatizo ya kiafya kama vile kisukari, shinikizo la damu pamoja na magonjwa ya moyo.

Monday, November 2, 2009

Ijue Homa ya Mafua ya Nguruwe (Swine Flu) ….sehemu ya kwanza


Homa ya mafua ya nguruwe inayojulikana kiingereza kama “Swine flue” ni ugonjwa unatokana na moja ya aina mbalimbali za virusi vya mafua ya influenza ya nguruwe au SIV. SIV au Swine Influenza Virus ni aina yoyote ya mafua ya influenza yanayotokana na virusi vinavyotokana na nguruwe. Virusi hivyo vinaweza kwa H1N1, H1N2, H3N1, H3N2 NA H2N3. Ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe ni ugonjwa wa kawaida kwa nguruwe duniani kote. Maambukizo ya ugonjwa ya virusi hivyo kutoka kwa nguruwe kwenda kwa binaadamu hayatokeo kila mara. Lakini iwapo maambukizo ya binaadamu yatatokea husababisha homa ya mafua ya nguruwe kwa binaadamu pia. Watu ambao wako karibu na nguruwe wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa homa ya mafua ya nguruwe, kama vile wafugaji nguruwe na wanaojishughulisha na wanyama hao.
Wataalamu wanasema kwamba mfumuko wa homa ya mafua ya nguruwe mwaka huu wa 2009, ambapo ilianzia nchini Mexico, umesababishwa zaidi na virusi vya H1N1, kwani ndio aina ya virusi ambavyo humpata zaidi mwanadamu. Ugonjwa huo kwa hivi sasa umeenea sana katika nchi nyingi duniani na Shirika la Afya Duniani WHO limeutangaza kuwa janga la kimataifa. Watu wengi wameambukizwa homa ya mafua ya nguruwe katika nchi nyingi duniani huku, ikikadiriwa kuwa karibu watu 700 hufariki dunia kila wiki kutokana na homa ya mafua ya nguruwe duniani kote. Kwa kuzingatia hayo Kona ya Afya imeona kuna ulazima wa kuzijua dalili za ugonjwa huo na kuelezea namna ya kujiepusha au kukabiliana na ugonjwa huo. Kumbuka kuwa hivi sasa ambapo nchi nyingi zinaingia katika majira ya badiri ambapo mfumuko wa magonjwa ya kifua na mafua huongezeka, hatari ya kupatwa na ugonjwa huo ni kubwa zaidi. Si lazima uwe karibu na nguruwe au unafuga na kula nguruwe ndio ufikiri unaweza kupatwa na ugonjwa huo, ukweli ni kuwa maambukizo ya homa ya mafua ya nguruwe kwa sasa ni kati ya mtu na mtu, au kwa Kiswahili kingine toka binadamu kwenda kwa binaadamu mwingine, hiyo inamanisha kuwa, sote tuko hatarini.
Dalili za homa ya mafua ya nguruwe
Kwa kawaida dalili za ugonjwa huu huwa sawa na ugonjwa wa kawaida wa mafua. Lakini pia kuwa baadhi ya watu huonyesha dalili mbaya zaidi au zinazotofautiana na mafua ya kawaida.
Iwapo mgonjwa atakuwa na homa kali zaidi ya sentigredi 30 au 100/F pamoja na moja ya dalili zifutazo, anaweza akawa amepatwa na homa ya mafua ya nguruwe na ni boda umuone daktari.
1. Maumivu ya mwili.
2. Kuumwa kichwa.
3. Mafua.
4. Mauvimu ya koo.
5. Kushindwa kupumua na kikohozi.
6. Kukosa hamu ya kula.
7. Mwili kuchoka sana kinyume cha kawaida.
8. Kuharisha na kutapika.
Ingawa ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe unaweza kuwapata watu wote lakini watu wafuatao wanakabiliwa na hatari zaidi ya kupatwa na ugonjwa huo:
 Kina mama waja wazito.
 Watu wenye magonjwa ya muda mrefu ambayo yamepelekea miili yao kuwa dhaifu kama vile kensa, magonjwa ya muda mrefu ya kifua, HIV n.k.
 Watoto wadogo walio chini ya miaka mitano.
 Wazee walio na umri wa zaidi ya miaka 65 na zaidi.
 Wagonjwa wenye matitizo ya asthma.
 Wagonjwa wanotumia dawa za kudhoofisha mfumo wa kulinda mwili au (immunosuppression).
…. Naam, usikose kujua namna ya kujikinga na kupatwa na ugonjwa huu hatari katika sehemu ya pili

Kila dakika moja mwanamke anafariki dunia akijifungua


Imetangazwa kuwa idadi ya wanawake wanaofariki dunia wakati wa ujauzito na kujifungua imeongezeka katika nchi nyingi. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mfuko wa Idadi ya watu wa Umoja wa Mataifa (UNFPA), kila dakika moja mwanamke mmoj hufariki dunia wakati wa kujifungua.
Katika mkutano uliofanywa na Mawaziri wa Ulinzi kutoka nchi 150 duniani mjini Addis Ababa Ethiopia, kumeripotiwa kuwa uzazi unasababisha idadi kubwa zaidi ya wanawake wapoteze maisha ikilinganishwa na matukio mengineo kama vile vita. Kutokuwepo wakunga wenye ujuzi wa kutosha, na umbali mkubwa kati ya maeno ya vijijini hadi kwenye vituo vya afya ni miongoni mwa sababu zinazochangia matatizo makubwa na vifo vya wanawake wajawazito. Mawaziri hao wamekubalina kwamba, kuzaa kwa mpango ni moja ya njia za kukabilina na matatizo kama hayo na kwamba, inahitajika serikali ziwekeze zaidi katika elimu ya huduma ya afya.

Sunday, November 1, 2009

Idadi ya watu wanaokufa kutokana na homa ya mafua ya nguruwe duniani yaongezeka


Twakimu za hivi karibuni kabisa za Shirika la Afya Dunian WHO zinaonyesha kwamba, zaidi ya watu 700 wanakufa kila wiki kutokana na homa ya mafua ya nguruwe!
Zaidi ya vifo 5,700 viliripotiwa Oktoba 25 ikilinganishwa na vifo 5,000 vilivyotokea wiki moja kabla.
Watu wengi wamefariki zaidi katika maeneo ya Amerika ambapo zaidi ya vifo 4,175 vimeripotiwa. Baadhi ya nchi kama vile Ukraine vimefunga mashule na kupiga marufuku mikusanyiko ya hadhara kama njia ya kukabiliana na mfumuko wa ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe hasa katika msimu huu wa baridi. WHO imetangaza kwamba, nchi nyingi hazihesabu tena watu wanaopatwa na ugonjwa huo na kwa sababu hiyo basi inakadiriwa kwamba watu walioambukizwa virusi vya H1N1 ni wengi sana duniani.
Ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe ulianzia nchini Mexico April mwaka huu, na hivi sasa ugonjwa huo umeenea katika nchi nyingi duniani, suala lililopelekea ugonjwa huo kutangazwa kuwa janga la ulimwengu.
Kona ya Afya inawahusia wadau wa globu hii kuzingatia kuosha mikono vizuri kwa sabuni kila mara na kuvaa mask wanapokuwa kwenye mikusanyiko ili kujiepusha kupatwa na homa ya mafua ya nguruwe. Naahidi kuwa hivi karibuni niaelezea kwa kina kuhusiana na ugonjwa huo. Tuzilinde Afya zetu!

Maboga yanaweza kuzuia magonjwa yanayotokana na kuvu au Fungus


Kwa muda mrefu maboga yamekuwa yanajulikana kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kutumika kama dawa, vilevile chakula hicho kina protini yenye nguvu ambayo inaweza kupambana na magonjwa mbalimbali yanayotokana na kuvu au fungus.
Maboga yamekuwa yakitumika sana katika tiba za kiasili katika kutibu magonjwa tofauti kama vile kisukari, shinikizo la damu, kiasi kikubwa cha mafuta mwilini pamoja na saratani katika nchi kama vile China, Korea, India, Yugoslavia, Argentina, Mexico, Barazil na kwingineko.
Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Kilimo na Kemia ya Vyakula, imeonyeshwa kuwa protini inayotokana na boga iitwayo Pr-2, inapambana vilivyo na ugonjwa unaosababishwa kuvu au fungus wa sehemu za uke (Vaginal yeast infection). Vilevile michubuko inavyotokana na mkojo au nepi (diaper rashes) pamoja na matatizo mengine ya kiafya. Protini hiyo ya Pr-2 iliyoko kwenye maboga halikadhalika inazuia aina 10 za fungus au kuvu ikiwemo aina hatari ya fungus wajulikanao kama Candida Albicans. Fungus hao ni maarufu kwa kusababisha matatizo kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari na kupelekea kupata fungus midomoni, katika ngozi, chini ya kucha pamoja na katika mfumo mzima wa mwili.
Waaalamu wana matumaini kuwa, protini hiyo inayopatikana kwenye maboga inaweza kupelekea mafanikio ya kutengezezwa tiba asilia ya kupambana na magonjwa ya kuvu au fungus.
… Haya shime kama ulikuwa unadharau kula maboga, nafikiri inakubidi ufikirie tena!