Thursday, February 4, 2010

Bi. Michele Obama akosolewa kwa kuzungumzia lishe ya mabinti zake hadharani


Ikiwa ni wiki mbili tangu ilipotangazwa kuwa unene kwa watoto umeongezeka mara tatu nchini Marekani katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, na Mke wa Rais wa Marekani akatangaza nia yake ya kupambana na suala hilo, Bi. Michele Obama amekabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya kujadili hadharani masuala ya lishe ya mabinti zake. Hii ni baada ya daktari wa familia hiyo anayeshughulikia masuala ya watoto kumtaarifu kwamba, wanawe Sasha na Malia wanaanza kuwa wanene. Hata hivyo Bi. Michelle amepuuza suala hilo na kusema kwamba, anafikiri watoto wake wako sawa tu. Wengi waliomkosoa Michelle wamesema kuwa, anahatarisha mustakbali au future ya wanawe kwa kuanza kuwazungumzia hadharani kuhusiana na milo yao. Ingawa ni kweli kuwa nchini Marekani Waamerika weusi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kuongezeka uzito na kuwa na unene wa kupindukia ambapo wataalamu wanasema theluthi moja ya Waamerika weusi ni wanene, lakini bado matamshi ya Mrs. Obama ya kujadili lishe ya wanawe hadharani, yameonekana kuwa pengine yanaweza kuwasababisha wanawe kupata matatizo ya kula ukubwani. Wengi wanasema kwamba mke huyo wa Rais wa Marekani angeweza kutoa mifano mingine tu mingi lakini bila kuwaashiria moja kwa moja watoto wake, hasa ikizingatiwa kuwa, mabinti wake hao bado ni wadogo. Wakosoaji hao wamemtaka Bi. Michelle ajiepusha kukariri suala hilo na afuate mfano wa familia nyinginezo za Marais wa Marekani waliowahi kuishi White House.

No comments: