Friday, April 16, 2010

Aspirin hutibu migreni


Wakati mauamivu makali ya kichwa au migraie yamekuwa yakitibiwa kwa dawa kali za maumivu, uchunguzi mpya umegundua kuwa dozi moja tu ya aspirini inaweza kuwaopunguzia maumivu walio na ugonjwa huo. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Cochrane Library, kunywa dozi moja ya aspirini ya kati ya miligramu 900 hadi 1000 kunaweza kupunguza mauvimu makali ya migraine kwa masaa mawili. Hata hivyo utafiti huo umesema dawa hizo zinaweza kuwafaa baadhi ya watu na zisiwafae wengine na kwamba hiyo ni kutokana na tofauti ya genetiki. Kunywa dozi kubwa ya asprini kumeripotiwa kuwa na athari ya kupunguza kichefuchefu, kutapika na hata hali ya kutoweza kuvumilia mwanga na sauti (photophobia na phonophobia) hali ambazo hujitokeza kwa wale wanaopatwa na migraine.
Lakini wataalamu wamewashauri wale wanaosumbuliwa na maumivu ya kichwa ya migraine wajiepushe kutumia vidonge hivyo kwa muda mrefu kwani aspirini zinaweza kuleta athari mbaya kama vile matatizo ya tumbo.

Vifo vya kinamama vimepungua duniani

Takwimu za mwisho zinaonyesha kwamba idadi ya vifo vya kimamama vimepungua duniani kutoka nusu milioni mwaka 1980 hadi chini ya vifo 350,000 mwaka 2008. Vifo vya kinamama vinavyotokana na ujauzito au Maternal ni vifo vya kina mama vinavyotokea wakati wa ujauzito au katika siku 42 mwishoni mwa ujauzito. Vifo hivi hutokana na sababu yoyote unayohusiana na ujauzito au masuala mengine yanayoambatana na hali hiyo.


Idadi hiyo ya vifo imekuwa ikitumika kutambua na kuonyesha kiwango cha hali ya huduma za afya katika maeneo mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa uchunguzi ulioshapishwa na jarida la The Lacent, idadi ya kinamama wanaofariki dunia kutokana na matatizo ya ujauzito imepungua kwa zaidi ya asilimia 35, katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Hii ni katika hali ambayo nchi kama vile China, Misri, Ecuador na Bolivia zimefanikiwa kufikia malengo ya kimataifa ya kupunguza idadi ya wanawake wanaofariki dunia kutokana na matatizo ya ujazito, huku nchi za Marekani na Norway zikiripotiwa kushuhudia ongezeko la vifo hivyo. Wengi wanasema kwamba, sababu kuu iliyopelekea ongezeko la vifo hivyo katika nchi hizo mbili ambazo ni tajiri na zenye huduma bora ya tiba ni kuongezeka magonjwa miongoni mwa kinamama wajawazito pamoja na kinamama kubeba mimba katika umri mkubwa.

Vilevile imeripotiwa kwamba kwenye nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika katika kila wanawake watano wajawazito mmoja kati yao ana virusi vya HIV. Ugonjwa ambao umesababisha vifo vya watu 61,400 katika mwaka 2008. Asimilia 80 ya vifo vya kina mama wajawazito hutokea katika nchi 21 duniani ambapo India, Pakistan, Nigeria, Afghanistan, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinachangia zaidi ya nusu ya idadi yote hiyo ya vifo vilivyoripotiwa.

Wednesday, April 7, 2010

Cheka unenepe na uishi maisha marefu


Utafiti mpya umeonyesha kwamba, kuna uhusiano kati ya kucheka na kuishi maisha marefu.
Utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la Saikolojia la Sayansi umeonyesha kwamba, watu wenye tabasamu pana linalojulikana kama "Dunchenne smile, huishi maisha marefu. Ernest L. Abel aliyeongoza utafiti huo amesema kwamba, watu ambao wanaonyesha hisia zao na kuziakisi kwa tabasamu pana, kimsingi huwa ni watu wenye furaha zaidi ya wale wenye kutabasamu kidogo. Hivyo watu hao hufaidika na suala hilo na kwa kawaida huishi maisha marefu.
Wataalamu wanasema kwamba watu wenye kutabasamu sana kwa kawaida huwa wana furaha, wana shaksia madhubuti, ndoa zao hudumu zaidi, wana ufahamu mzuri zaidi wa mambo na huashiriana vyema na watu wengine.

Monday, April 5, 2010

Yawezekana kuokoa maisha ya wenye HIV kwa kutumia dawa zisizo ghali

Wachunguzi wa masuala ya tiba wamesema kwamba, bado hakuna jitihada zinazofanywa za kuokoa maisha ya maelfu ya watu wanaoishi na virusi vya HIV kwa kutumia dawa rahisi na zisizo ghali. Wamesisitiza kwamba kuwapa dawa za anti-biotics kama vile co-trimoxazole wale ambao tayari wamegunduliwa kuwa na virusi vya Ukimwi kunaweza kupunguza idadi ya vifo vya wagonjwa hao mwanzoni tu wanapopata ugonjwa huo.

Uchunguzi huo uliochapishwa katika Jarida la Tiba la Lancet umegundua kuwa, kuwapa waathirika wa Ukimwi anti-biotics kunapunguza nusu ya vifo vya wagonjwa hao. Shirika la Afya Duniani WHO) tayari limeamuru kutolewa matibabu hayo lakini wataalamu na madakatari wanasema kuwa watu wengi bado hawapewi dawa hizo. Jitihada nyingi zimekuwa zikifanywa tu kuhakikisha kwamba wale walioathirika na Ukimwi wanapatiwa dawa za kuongeza maisha za antiretroviral ambazo zina athari kubwa katika kuwaongeza maisha. Hata hivyo, wagonjwa wengi wa Ukimwi katika wiki za mwanzo baada ya kugundulika kuwa wana ugonjwa huo, wanakabiliwa na hatari kubwa ya kushambuliwa na magonjwa mbalimbali kutokana na kudhoofu mfumo wao wa kinga wa mwili. Hivyo wataalamu wanasema kwamba, kuongezwa dawa kama vile co-trimoxazole ambazo ni anti-biotic zisizo ghali na ambazo hupatikana kwa urahisi, katika matibabu yao ya muda mrefu kunaweza kuwanusu na kifo.


Takwimu zimeonyesha kuwa, zaidi ya robo ya waathiriwa wa Ukimwi waliopewa dawa za kuongeza maisha za antiretroviral katika nchi za chini ya Jangwa la Sahara walifariki dunia katika mwaka wa kwanza wa matibabu. Lakini uchunguzi uliofanywa na Lancent umeonyesha kwamba, kati ya Waganda 3,179 wenye virusi vya Ukimwi, waliopewa dawa hizo pamoja na kuongezewa anti-biotic katika mpango wao wa matibabu, dawa hizo ziliwapunguzia vifo kwa asilimia 59 katika wiki 12 za kwanza, na kwa asilimia 44 kati ya wiki 12 na 72 za matibabu.
Hata hivyo imeonekana kwamba dawa hizo za anti-biotics hazipatikani katika maeneo mengi ya nchi za Uganda na Zimbabwe ambako kuna wathirika wengi wa Ukimwi.
Pia imeonekana kuwa kutumiwa dwa hizo za nyongeza kuna faida nyingine ya ziada ambayo ni kuepusha maambukizo ya ugonjwa wa Malaria kwa asilimia 15.

Sunday, April 4, 2010

Dawa ya kensa ya tezi kibofu (prostate cancer) yaonyesha matumaini zaidi

Dawa ya kensa ambayo tayari inatumiwa na wagonjwa wenye uvimbe wa tezi za kibofu imeonekana kuwa ina uwezo wa kuzuia ugonjwa huo usiendelee zaidi. Katika uchunguzi wa kimataifa imeonekana kuwa, wanaume waliopewa dawa hiyo ijulikanayo kama Dutasteride katika jaribio la kitiba, wameripotiwa kupungukiwa na hatari ya kupata ugonjwa wa kensa ya tezi kibofu (prostate cancer) kwa asilimia 23. Wanaume wote hao walikuwa wana uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huo maishani.

Wataalamu wamepokea kwa furaha matokeo hayo lakini wamesema kwamba bado utafiti wa muda mrefu unatakiwa kufanywa kuhusiana na dawa hiyo.
Huko nyuma pia wataalamu waligundua pia dawa nyingine kama hiyo iitwayo Finasteride inapunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kensa ya tezi kibofu lakini baadaye wakaona kuwa inaongeza uwezekano wa kutokea matezi makubwa ya kensa hiyo. Hivyo wamesisiza kwamba inahitajia muda mrefu ili kujua iwapo dawa hiyo haina madhara kabisa.
Inafaa kujua kuwa ugonjwa wa kensa ya tezi kibofu au prostate cancer huwapata wanaume hasa wanapofikia umri wa miaka 50 na wengine katika miaka ya 70. Nchini Marekani pekee mwaka 2005 inakadiriwa kwamba watu 230,000 walipatwa na ugonjwa huo na kusababisha vifo vya watu 30,000. Wanaume wenye matatizo ya shinikizo la damu wanaelekea kupatwa zaidi na kensa ya prostati.

Dalili za ugonjwa wa kenda ya korodani ni:
Kushindwa kukojoa.
Kuona ugumu wakati wa kukojoa.
Kushindwa kuzuia mkojo hasa usiku.
Mkojo kutoka kwa shinda, kuhisi maumivu wakati wa kukojoa.
Kuona damu imechanganyika na mkono na kuhisi maumivu upande wa chini wa kiuno na upande wa juu wa mapaja.
Lakini dalili zote hizo zinaweza kusababishwa na uvimbe wa tezi kibofu ambao hausababishwi na saratani.
Wanaume walio na dalili hizo wanatajwa kumuona daktari na kupata ushauri zaidi.

Saturday, April 3, 2010

Coca Cola huwafanya wanaume tasa!



Kinywaji cha coca cola kimeendelea kuwa maarufu duniani lakini utafiti mpya umeonyesha kuwepo uhusiano wa kunywa sana kinywaji hicho na matatizo ya uzazi kwa wanaume.
Kwa mjimu wa utafiti huo uliochapichwa kwenye Jarida la Epidemiology la Marekani, wanaume wanaokunywa zaidi ya lita moja ya coca cola kwa siku wanakabiliwa na hatari ya kuwa tasa. Wanaume waliotumia kinywaji hicho walikuwa na upungufu wa aslimia 30 ya mbegu za uzazi zilizohesabiwa, ikilinganishwa na wale ambao hawakutumia. Wanaume hao walionekana kuwa na matatizo ya uzazi zaidi kuliko wasiokunywa coca cola.

Friday, April 2, 2010

Chokoleti nyeusi zina faida kwa moyo

Japokuwa kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu taarifa kuhusu faida za kiafya za chokoleti, lakini utafiti mpya umedhihirishwa kwamba kula chokoleti nyeusi kuna faida kwa moyo. Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Moyo la Ulaya umeonyesha kwamba, kula kila siku gramu 7.5 za chokoleti, kiasi ambacho ni kidogo kuliko kipande mraba kidogo cha chokolati kunapunguza shinikizo la damu suala ambalo huondoa hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo kwa asilimia 39. Kula chokoleti kidogo huweza kumzuia mtu asipate ugonjwa wa moyo lakini iwapo tu italiwa badala ya vyakula vingine viliwavyo katikati ya mlo au asusa (snacks) vyenye kalori nyingi bila kuongeza uzito wa mwili.

Flavanols inayopatikana katika kakao huimarisha uwezo wa kiabiolojia wa seli wa kutengenezwa nitric oxide kuzunguka kuta za damu, suala ambalo hufanya mishipa laini ya damu ipumzike na kupanuka na hivyo kusaidia sana afya ya moyo. Kwa kuwa katika chokoleti nyeusi kuna kakao nyingi, aina hiyo ya chokolati ina taathira kubwa katika kupunguza mfumuko wa mawazo na wasiwasi pamoja (stress) na kusaidia mzunguko wa damu na kiwango cha chinikizo la damu. Lakini inaaminiwa kuwa chokoleti nyeupe hazina kabisa flavanol hivyo hazina faida hiyo.
Wataalamu wamesisitiza kwamba, watu wale chokolate nyeusi kila siku lakini kwa tahadhari kubwa kwani kiasi kidogo tu cha chokolati kina kiasi kikubwa cha kalori na mafuta ambavyo ni hatari kwa afya.