Sunday, January 16, 2011

Sigara huharibu DNA mwilini na kuongeza hatari ya kupata kensa!


Kemikali za sumu zilizoko katika tumbaku ya sigara huharibu DNA za mwili wa binadamu dakika chache tu baada ya mtu kuanza kuvuta sigara. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni, kemikali hizo zinazoitwa Polycylic Aromatic Hydrocarbons (PAHs) husababisha DNA ziharibike na kuongeza uwezekano wa mtu kupata kensa. Katika uchunguzi huo watalamu walichukua kemikali hizo katika miili ya wavuta sigara na kuzifanyia uchunguzi, ambapo waligundua kuwa, kemikali za PHA hubadilika haraka mwilini na kuwa sumu ambayo huharibu DNA baada ya kupita dakika 15 hadi 30 tangu kuingia tumbaku katika mwili wa binadamu. Sumu hiyo hubadilisha seli mwilini au kufanya mutation, kitendo ambacho huweza kusababisha kensa. Wataalamu hao wanasema, kitendo hicho hufanyika kwa haraka sana kama vile inavyoingizwa mada ya sumu kwenye damu kwa sindano. Habari hii ni tahadhari kwa watu wanaotaka kuanza kuvuta sigara, kwani takwimu zinatuonyesha kwamba, watu 3,000 hufariki dunia kila siku umwenguni kutokana na kensa ya mapafu, maradhi ambayo husababishwa kwa asilimia 90 na uvutaji sigara. Madhara ya kuvuta sigara kwa muda mrefu yanajulikana na wengi, ambayo ni pamoja na magonjwa ya moyo na kensa mbalimbali, lakini wataalamu wanatuasa ya kuwa, madhara ya sigara huanza pale tu mtu anapoanza kupiga pafu ya kwanza na kuingiza moshi wa sigara mwilini. Hivyo bado hujachelewa na unaweza kuacha sigara hii leo!

No comments: