Monday, February 8, 2010

Maradhi anayopata mama mjamzito humpelekea mwanae kupata pumu


Utafiti mpya umegundua kuwa, baadhi ya magonjwa anayopata mama wakati wa ujauzito huongeza uwezekano wa mwanae kupatwa na ugonjwa wa pumu. Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Maendeleo ya Tiba za Watoto na Vijana, watoto ambao wanazaliwa na kina mama waliopatwa na maambukizo ya vijidudu katika mfuko wa uzazi au maji yanayomzunguka mtoto tumboni yanayojulikana kama (chorioamnionitis) huwa wana uwezekano mkubwa wa kupatwa na pumu wafikapo umri wa miaka 8. Suala hilo hilo pia huwatokea watoto waliozaliwa kabla muda wao wa kuzaliwa haujatimia au prematures. Maambukizo hayo yanasababishwa na bakteria mbalimbali wanaopatikana katika sehemu za uke kama vile E. Coli na bakteria kundi B, Streptococci. Magonjwa hao husababisha zaidi ya nusu ya watoto wazaliwe kabla muda wao haujatimia, huku watoto hao wakiwa mapafu yao hayajaimarika vya kutosha na hivyo kukabiliwa na hatari ya kupata magonjwa mbalimbali sugu ya kifua kama vile pumu. Wanasayansi kwa kutegemea utafiti huo wameweza kusema kuwa, maambukizo ya magonjwa yanayotokana na bakteria ndio sababu kuu inayopelekea watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda wao kutimia, wapatwe na pumu.
Hivyo wameshauri kuwa, wakinamama wanatakiwa kufahamu umuhimu wa kuhudhuria kiliniki na katika vituo vya afya wakati wa ujauzito na kufuata maelekezo wanayopewa wakati wakiwa na mimba ili kuepusha matatizo kama hayo yasitokee.

Saturday, February 6, 2010

Aatikwa figo ya dada yake ingawa figo hiyo haiendani nawe


Utaalamu mpya umemumezesha mwanamke mmoja Muingereza kuwekewa pigo ya dada yake ingawa figo hiyo haiendani nae. Maxine Bath alikuwa na matatizo ya figo ambapo alikuwa akisaidiwa na mashine kuzungushiwa damu mwilini au dialysis. Mwanamke huyo hakuweza kupata mtu wa kumpatia figo inayoendana naye kutoka katika familia yake. Lakini madaktari wa hospitali ya Conventry nchini Uingereza wametumia utaalamu mpya unaojulikana kama 'cryofiltration' ili kuondoa seli za kulinda mwili ambazo zinasababisha figo hiyo ishindwe kuungana na mwili, iwapo itaunganishwa mwilini kwa mgonjwa hali ya kuwa haiendani na seli za mwili wake. Madaktari hao baada ya kufanikisha operesheni hiyo ya kuatika figo wanasema kwamba, utaalamu huo mpya unaweza kuwasaidia watu wengi zaidi wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali na wanahitajia kupandwa viungo mwilini au transplant. Watu 927 hufanyiwa operesheni za kuatika figo kila mwaka nchini Uingereza, hata hivyo maelfu ya wagonjwa wengine huwa wanaendelea kusubiri ili waweze kupata watu wanaoendana nao walioko tayari kuwapatia figo, huku ikiwa vigumu kuwapata watu hao. Viungo pale vinapopandwa au kuatikwa katika miili ya wengine hukataa kushikamana na miili hiyo (organ rejection) suala ambalo hutokea pale mwili unapotambua kuwa kiungo kilichoungwa si chake, na kuruhusu mfumo wa kulinda mwili ukikatae kiungo hicho. Tatizo hilo linaweza kuondolewa iwapo kiungo kinachotaka kupandwa kinatoka kwa ndugu wa familia moja na mgonjwa, na iwapo mgonjwa atatumia dawa za kuudhoofisha mfumo wa kulinda mwili kwa maisha yake yote.
Lakini haikuwa hivyo kwa Bi. Maxine, ambaye ana umri wa miaka 41 na aliyepata matatizo ya figo tangu akiwa na miaka 15. Ingawa mwanamke huyo hakuweza kupata mtu wa familia moja wa kumpa figo inayoendana na seli za mwili wake, lakini kwa kuondolewa seli hizo aliweza kuunganishiwa figo ya dada yake bila tatizo lolote.
Wataalamu wanasema kwamba teknolojia hiyo mpya inaweza kutumika kusaidia watu wengi zaidi wenye tatizo hilo, na hii ni mara ya kwanza duniani imetumiwa ili kumsaidia mgonjwa aunganishwe kiungo kisichoendana naye.
Operesheni hiyo ilifanywa mwezi Novemba mwaka 2009 na imesaidia kuokoa maisha ya Maxine.

Siri ya kasi ya mbegu za kiume yagunduliwa!


Wataalamu wanasema wamegundua kwamba mbegu za kiume huanza kwenda kwa kasi wakati zinapofika karibu na yai la mwanamke, suala ambalo huenda siku zijazo likasaidia katika kupatikana dawa ya kuzuia mimba ya wanaume. Vitundu vidogo vilivyoko juu ya mbegu hizo za kiume huziwezesha kubadilisha PH yake ya ndani, ambayo hufanya mkia wa mbegu hizo uanze harakati. Wataalamu hao wa Chuo Kikuu cha California huko San Francisco wanasema kuwa, ugunduzi huo unaweza pia kusaidia kuelezea kwa nini marijuana huwafanya wanaume wawe tasa na kwamba suala hilo litaleta mabadiliko makubwa katika kufahau suala zima la uwezo wa kuzaa wa mwanaume.
Kwa kawaida mbegu za wanaume hazianzi kwenda mbio baada tu ya kumwagwa, na ili kuweza kulifikia yai la mwanamke huhitajia kujiepusha na kasi hadi pale zinapokaribia yai. Wanasayansi kwa muda mrefu wamekuwa wakifahamu kwamba mwendo wa mbegu za kiume umekuwa ukisimamiwa na PH ya ndani, na kuwa kwake katika hali ya asidi au alikali lakini walikuwa hawafahamu ni jambo gani hasa linalowezesha kubadilika PH hiyo. Wataalamu wamesema, sasa wamejua kuwa ili kuongeza PH ili iwe ya alkali, mbegu huhitajia protoni zinaoitwa Jettison, na kwamba wamegundua vijitundu vidogo vilivyoko juu ya mbegu hizo ndio huruhusu mabadiliko hayo. Daktari Yuriy Kirichok aliyeongoza utafiti huo anasema, iwapo utafungua vijitundu hivyo, protoni inatoka nje, na wao wamefahamu molekuli ambazo huruhusu protoni hizo zitoke nje. Anaendelea kueleza kwamba, vijitundu hivyo vilivyopewa jina la Hv1 proton Channels, hufunguka pale inapofikia wakati muafaka wa kufunguka na hutegemea kitu kingine kinachoitwa, anandamine. Anandamide ziko katika mirija ya uzazi ya mwanamke katika eneo ambalo ni karibu na yai.
Katika marijuana kuna mada inaitwa cannabidoid ambayo inaaminika kuwa inapunguza uwezo wa anandamide, suala ambalo sasa limeweza kuelezea ni kwa nini marijuana kusababisha ugumba kwa wanaume. Dk, Kirichok anasema kwamba, marijuana pia huzipa kasi mbegu za kiume mapema, na huzifanya ziungue baada ya masa kadhaa. Watafiti hao wanatupa moyo kwamba, kwa kufahamu vyema masuala hayo, sasa ni wazi kuwa wanaweza kutafuta dawa ya kuzuia mimba kwa wanaume. Kwani kwa kuziziba molekuli hizo, pengine wakafanikiwa kuzuia na kutoruhusu mbegu isikutane na yai, na njia hiyo ikatumika kama dawa ya kuzuia mimba kwa wanaume.

Thursday, February 4, 2010

Samahani kwa maatizo ya kufundi!



Wapenzi wadau wa Kona ya Afya,
Shally's Med Corner inachukua fursa hii kuwaomba radhi kutokana na matatizo ya kiufundi ambayo yamesababisha blogi ya Kona ya Afya ivurugike kimuundo. Ingawa suala hilo halijaathiri uwekaji wa makala katika blogi hii, lakini nawaomba muwe na subira na uvumilivu hadi pale matatizo hayo yatakaporekebishwa. Kona ya Afya inawaahidi kwamba hivi karibuni mambo yatanyooshwa na muonekano wa blog utarudi katika hali yake ya kawaida.
Daima tulinde afya zetu!
Shally

Bi. Michele Obama akosolewa kwa kuzungumzia lishe ya mabinti zake hadharani


Ikiwa ni wiki mbili tangu ilipotangazwa kuwa unene kwa watoto umeongezeka mara tatu nchini Marekani katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, na Mke wa Rais wa Marekani akatangaza nia yake ya kupambana na suala hilo, Bi. Michele Obama amekabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya kujadili hadharani masuala ya lishe ya mabinti zake. Hii ni baada ya daktari wa familia hiyo anayeshughulikia masuala ya watoto kumtaarifu kwamba, wanawe Sasha na Malia wanaanza kuwa wanene. Hata hivyo Bi. Michelle amepuuza suala hilo na kusema kwamba, anafikiri watoto wake wako sawa tu. Wengi waliomkosoa Michelle wamesema kuwa, anahatarisha mustakbali au future ya wanawe kwa kuanza kuwazungumzia hadharani kuhusiana na milo yao. Ingawa ni kweli kuwa nchini Marekani Waamerika weusi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kuongezeka uzito na kuwa na unene wa kupindukia ambapo wataalamu wanasema theluthi moja ya Waamerika weusi ni wanene, lakini bado matamshi ya Mrs. Obama ya kujadili lishe ya wanawe hadharani, yameonekana kuwa pengine yanaweza kuwasababisha wanawe kupata matatizo ya kula ukubwani. Wengi wanasema kwamba mke huyo wa Rais wa Marekani angeweza kutoa mifano mingine tu mingi lakini bila kuwaashiria moja kwa moja watoto wake, hasa ikizingatiwa kuwa, mabinti wake hao bado ni wadogo. Wakosoaji hao wamemtaka Bi. Michelle ajiepusha kukariri suala hilo na afuate mfano wa familia nyinginezo za Marais wa Marekani waliowahi kuishi White House.

Wednesday, February 3, 2010

Nchi za Afrika zakubaliana kutokomeza malaria


NCHI za Afrika zimekubaliana kuwa lengo kuu la serikali zao katika mapambano dhidi ya malaria, ni kuutokomeza ugonjwa huo.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania alisema hayo juzi mwishoni mwa kikao cha viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) walio katika mapambano dhidi ya malaria Afrika (ALMA).

Alisema Afrika inahitaji vyandarua 200 ingawa hadi sasa kuna ahadi ya vyandarua 50 tu, lakini hata hivyo aliitaka ALMA kuendelea na jitihada za kupata vyandarua vyote vitakavyokidhi mahitaji.

Rais Kikwete aliitisha kikao hicho kwa kushirikiana na AU ambapo mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ray Chambers, aliwataka viongozi hao kuweka nia ya dhati ya kisiasa katika jitihada hizi ili kufanikisha azma yao.

Kikao hicho ni cha pili cha kikazi baada ya kilichofanyika New York, Marekani chini ya Rais Kikwete, kama mwanzilishi wa jitihada hizo ambazo zilianza wakati akiwa Mwenyekiti wa AU.

Kikao hiki kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa AU, Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi, Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia, Hifikepunye Pohamba wa Namibia, Mwai Kibaki wa Kenya na Armando Guebuza wa Msumbiji. Wengine ni Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Rupia Banda wa Zambia na Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Nchi zingine zilizohudhria ni Burundi, Gabon, Misri na Somalia. Katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ALMA, Joy Phumaphi, alieleza mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo matumizi ya vyandarua yameongezeka kwani hadi mwaka juzi nchi 13 kati ya 35 zenye kiwango kikubwa cha malaria, asilimia 50 ya watu wao wanatumia vyandarua hivyo, ikilinganishwa na mwaka 2005 na pia matumizi ya dawa mseto yamepunguza maambukizi na vifo.

Phumaphi alisema mwamko huo wa matumizi bora ya vyandarua, umepunguza vifo na maambukizi pia kwa mama na mtoto ambao ndiyo waathirika wakubwa.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto nyingi ambazo zinahatarisha jitihada na kutokomeza malaria ikiwamo fedha kunakotokana na kutotimizwa kwa ahadi na wafadhili.

Rais Kikwete alimtaka kila mshiriki kupitia wizara zao za Afya kutuma maombi kwenda mfuko wa malaria duniani (Global Fund) ambayo yatahusisha si upatikanaji tu wa vyandarua, bali uwezeshwaji wa watumishi wa afya, vitendea kazi na vitu vyote muhimu vinavyohitajika katika jitihada hizi za kutokomeza malaria.

Monday, February 1, 2010

Utoaji mimba usio salama unauwa akina mama elfu sabini kila mwaka


Utoaji mimba usio salama husababisha akima mama elfu sabini kupoteza maisha yao kila mwaka duniani kote. Taasisi mashuhuri ya Guttmacher imeripoti kuwa, japokuwa utumiami wa njia za uzazi wa mpango hupunguza kiwango cha kuharibika kwa mimba, lakini ulimwengu unashuhudia wakinamama wapatao elfu sabini wakifariki dunia kila mwaka kutokana na utoaji mimba usio salama. Imeongeza kuwa, utoaji mimba usio salama unaendelea kuwa tatizo miongoni mwa walimwengu. Imesema kuwa, zaidi ya nusu ya vifo hivyo vya akinamama hutokea katika nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara.