Sunday, March 29, 2009

Kutahiri kunazuia magonjwa ya zinaa


Wataalamu wa Marekani hatimaye wamesisitiza kuwa, kutahiri ni njia yenye kuzuia kwa kiasi kikubwa maambukizo ya magonjwa ya zinaa. Wamesema hayo baada ya kufanywa uchunguzi uliogundua nafasi muhimu ya kutahiri katika kupunguza maambukizo ya ugonjwa wa malengelenge wa zinaa na virusi vya HPV unaosababisha kensa ya kizazi au Human Papillomavirus. Pia kutahiri kunapunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kupatwa na ugonjwa wa ukimwi.
Uchunguzi kama huo pia ulifanywa nchini Uganda na kuwashirikisha wanaume 3,500 ambao walichunguzwa mahusiano yao ya kijinsia kwa kipindi cha miaka miwili. Matokeo yake yalionyesha kuwa, kutahiri kunapunguza maaambukizi ya Ukimwi, suala ambalo lilipelekea jamii ya Uganda kufanya kampeni za kutahiri nchini.
Wataalamu wa chuo kikuu cha Johns Hopkns wamegundua kwamba, kutahiri huweza kupunguza uwezekano wa kuambukizwa ugonjwa wa zinaa wa Herpes kwa asilimia 25, na kupunguza maambukizo ya virusi vya Papiloma kwa theluthi moja!
Human Papilomavirus au HVP husababisha kensa ya kizazi kwa wanawake, na mapele katika sehemu za siri au genital warts kwa wanaume na wanawake pia.
….haya shime tushajiishe kutahiri, kwa wale ambao hawatilii umuhimu suala hilo katika jamii yetu.
Tukumbuke kuwa, watu wasio na maradhi, huijenga jamii salama, basi tusisahau kulinda afya zetu!

Thursday, March 26, 2009

Kiungulia au Heartburn


Kiungulia au Heartburn kwa kimombo, ni miongoni mwa mabadiliko ya ujauzito yanayowatokea baadhi ya akina mama. Tatizo hilo huwapata baadhi ya wakinamama wakati wa ujauzito, kama mabadiliko ya kimwili ya kawaida.
Ni wazi kuwa wanawake wengi hulalamikia kiungulia wakati wa ujauzito. Kiungulia hicho kinachompata mama akiwa na mimba ni wazi kuwa, ni mojawapo ya athari za kawaida kabisa zinazosababishwa na mimba. Kwa kawaida kiungulia hicho humpata mama mjamzito baada ya kula chakula. Mama anapopatwa na kiungulia, kuhisi kuchomeka au moto katika koo au kifuani mwake. Kiungulia kinaweza kutokea wakati wowote, lakini hudhihirika zaidi katika miezi mitatu ya mwisho hadi minne ya ujauzito. Kuna baadhi ya akinamama pia ambao hupatwa na kiungulia na huhisi kama vile wana uvimbe kwenye koo au kifuani. Kivyovyote vile, kiungulia kinakera na tatizo ambalo linaweza kupunguzwa na kumpatia mama nafuu.
Sababu kadhaa au masuala tofauti yametajwa kuwa yanasababisha kiungulia kwa mama mjamzito. Mojawapo ya sababu za kimsingi zinazomsababishia mama mjamzito kiungulia hicho ni mabadiliko ya homoni. Homoni hizo khususan progesterone, hulegeza valve yaani vali za tumbo au vilango tumbo ambavyo kwa kawaida huzuia asidi ya tumboni kurudi kwenye umio au esophagus. Kwa hiyo, mamamjamzito hupatwa na kiungulia yaani huhisi kuchomeka kooni au kifuani, iwapo vali hizo zitashindwa kuizuia asidi hiyo. Njia rahisi ya kupunguza tatizo hilo, ni kwa mama kugawa mlo wake wa siku nzima katika sehemu sita. Yaani badala ya kula mara tatu kwa siku kama ilivyozoeleka, mama mjamzito agawe mlo wake wa siku katika awamu sita. Kwa njia hiyo mamamjamzito atatakiwa kula mlo wake mara sita kwa siku kidogo kidogo bila ya kupoteza virutibisho muhimu. Uyabisi wa tumbo na kiungulia pia ni mambo yanayotokea mara kwa mara wakati mimba inapokuwa na miezi sita na kuendelea. Masuala haya hutokea pale mfuko wa uzazi wa mama unaokuwa unapozidisha presha kwenye matumbo pamoja na tumbo.
Kwa kuzingatia kuwa mama mjamzito hawezi kurekebisha kiwango chake cha homoni au kuuzuia mfuko wake wa uzazi kukua, kuna njia nyepesi kabisa ambazo mama anaweza kuzifuata na kumsaidia kupunguza kero ya kiungulia na kwa wengine kukizuia kabisa. Hatua hizo ni kama zifuatazo: Kwanza mama mjamazito anashauriwa kula milo midogo midogo kadhaa kwa siku nzima, ikiwa na maana kuwa, anaweza kula mara sita badala ya mara tatu. Anapaswa kujiepusha na vyakula vyenye viungo vingi au vyenye mafuta mengi. Anashauriwa mara zote kula chakula kwa uchache saa moja labla ya kuingia kitandani wakati wa usiku. Mama mjamzito hapaswi kulala muda mfupi baada ya kula chakula, kwani kitendo hicho kinaweza kuchangia kiungulia. Hatua nyingine za kufuata ni kama vile mama mjamzito anapaswa kunywa maziwa mengi au mtindi kama ana uwezo huo iwapo kiungulia kinamsumbua mara kwa mara, ajiepushe na unywaji maji mengi wakati wa kula chakula, ambao unaweza kujaza tumbo lake na kumsababishia kiungulia. Mama mjamzito ajiepushe na unywaji wa vinywaji vyenye caffeine na avae nguo pana zisizobana kifuani. Mbali na njia hizo, mama mjamzito anashauriwa kulalia upande wake wa kulia kwa kutumia mito kadhaa huku shingo ikiwa imeinuka, inasaidia pia iwapo hatua zote hizo hazitamfaa mamamjamzito katika kukabiliana na kiungulia alichonacho, anashauriwa kumona daktari kwa ushauri zaidi. Dawa za antiacid zinazopunguza asidi kame vile zile zenye mchangiko wa aluminium, magnesium na calcium zinashauriwa kutumiwa kwa kufuata maagizo ya daktari. Mama anaweza kutumia dawa hizo zikiwa katika muundo wa vidonge au majimaji.
Na sasa tuangalie dondoo moja muhimu ifuatayo.
*** Mama mjamzito anayetaka kusafiri kwenda sehemu moja au nyingine anapaswa kufanya mambo yafuatayo: Kwanza kabisa anatakiwa kuchukua tahadhari zote. Tahadhari hizo ni kama vile kujikinga na ugonjwa wa malaria ambao huzidisha idadi ya vifo vya akinamama wajawazito. Mama mjamzito anashauriwa kutosafiri kwenye maeneo yenye malaria. Aidha mama anatakiwa kuwa makini na kula vyakula vyenye sumu wakati akisafiri. Kujiepusha huko ni kwa kuzingatia usafi wake wa vyakula wakati akiwa safarini, awe makini wakati wa ulaji vyakula. Kwa wale wanaosafiri nje ya nchi, baadhi ya mashirika ya ndege, mabasi nk. Hayaruhusu kusafiri mama mjamzito akiwa na mamba ya zaidi ya wiki 35, kwa hiyo wanapswa kumuona dakatri na kupata ushauri kabla ya kuanza safari. Mama hao pia wanashauriwa kutojishughulisha na kazi zinazoweza kumdhuru yeye pamoja na mtoto aliyetumboni kama vile kufanya kazi nzito, kubeba mizigo nk. Akiwa safarini, mama mjamzito anatakiwa kuripoti mara moja dalili au alama hatari kama vile kuvuja damu, kutokwa na tishu au mabonge ya damu, maumivu ya tumboni, kuvunjika kwa chupa, maumivu ya kichwa na kujisikia kizunguzungu ili kupatiwa huduma mara moja.
Natumaini mmefaidika na makala hii, basi msisahau kuzitunza Afya zenu.
Makala hii imetayarishwa na rafiki yangu wa karibu, Asma.
Ahsante sana shosti!

Linebeke la makala za tiba


Wadau wangu wa Kona ya Afya, natumaini mu wazima na mnaendelea kuzitunza afya zenu. Kama ni hivyo basi, kwa leo ninawaletea makala muhimu hasa kwa kina mama wajawazito. Niliahidi huko nyuma kuwa tutakuwa tukichambua baadhi ya magonjwa na masuala mbalimbali kwa undani na libeneke hilo ndio leo nalianza kwa kuzungumzia suala la Kiungulia. Stay with me!
Shally's med corner

Wednesday, March 25, 2009

Je wajua? Moyo ndio kituo cha fahamu na wala sio ubongo!


Je wajua kwamba, moyo ulioko katika kifua cha mwanadamu kupiga mara 100,000 kwa siku, husukuma galoni mbili za damu kwa dakika, galoni 100 kwa saa, kwa masaa 24 kwa siku, miezi na miaka yote manadamu anayoishi duniani.
Mfumo wa mishipa ya damu ambayo
husafirisha damu katika mwili wa binadamu ina urefu wa maili 60,000. Ukubwa huo ni mara mbili zaidi ya mzunguko wa dunia!.
Suala la kustaajabisha zaidi na unalopaswa kujua kuhusiana na kiungo hiki muhimu katika mwili wa binaadamu ni kwamba moyo huanza kupiga katika mwili wa mtoto mchanga pale anapoaumbwa tumboni, hata kabla ya ubongo haujaumbwa. Moyo huanza kupiga kabla hata ya mfumo wa fahamu wa kati kuumbwa!.
Kuna nadharia maarufu kwamba mfumo wa kati wa fahamu hudhibiti na kusimamia vitendo vyote vya mwandamu kuanzia kwenye ubongo lakini utafiti unaonyesha kwamba mfumo wa fahamu hauanizishi mapigo ya moyo.
Kiuhakika mapigo ya moyo huanza yenyewe, na kuna wanaosema kuwa bado haijafahamika mapigo ya moyo huanzishwa na nini. Wataalamu wanasema kuwa moyo ni kituo cha ufahamu (consciousness) na wala sio ubongo kama wengi tunavyodhani.
Daima ilinde afya yako!

Wednesday, March 18, 2009

Chuchu bandia kumfanya mtoto asipende kunyonyesha


Utafiti mpya uliofanya huko Uholanzi unaonyesha kuwa, watoto wachanga wanaopewa chuchu bandia katika wiki za kwanza za maisha yao huwa hawapendi kuendelea kunyonya.
Kinamama wengi hupatwa na matatizo ya kuwanyonyesha watoto wao katika wiki ya kwanza baada ya kujifungua, sababu kubwa ikiwasababishwa na njia isiyokuwa sahihi ya kunyonyesha au kushindwa kuwapakata watoto wao wakati wa kunyonyesha kutokana na sababu mbalimbali. Suala hili huwapelekea kuwapa watoto wao chuchu bandia au pacifier.
Kutumia chuchu bandia huathiri mafanikio ya suala zima la kunyonyesha.
Wanasayansi wanawashauri wakinamama waliojifungua kuwanyonyesha watoto wao na kuepuka kuwapa chuchu bandia katika wiki za kwanza baada ya kuzaliwa.
Tusisahau kuwa maziwa ya mama yana umuhimu mkubwa katika ukuaji wa mtoto na kumuepusha na magonjwa mbalimbali katika kipindi cha utoto.

Tuesday, March 17, 2009

Wasiokula nyama hawapatwi sana na saratani



Uchunguzi uliofanyika nchini Uingereza umeonyesha kuwa chakula kisichukuwa na nyama (vegetarian diet) kinaweza kusaidia kuukinga mwili na ugonjwa wa saratani. Uchunguzi huo uliowapima wanaume na wanawake 52,7000 umeonyesha kwamba, wale amabo walikuwa hawali nyama hawakupatwa na magonjwa ya saratani sana ikilinganishwa na waliokuwa wakila nyama. Kumeonekana kuwa magonjwa ya saratani hutokea kwa kiwango kidogo pia kwa wale wanaokula samaki kwa wingi ikilinganishwa na wanaokula nyama.
Hata hivyo katika uchunguzi huo aina moja ya saratani ijulikanayo kama colorectal cancer imeonekana kutokea kwa wingi kwa watu wasiokula nyama(vegeterians) kuliko kwa watu wengine. Suala hilo limeshangaza, kwani linapingana na utafiti wa huko nyumba ulioihusisha aina hiyo ya kensa na matumizi ya nyama nyekundu (red meat).
Madaktari wanashauri kuwa ni bora mtu ale matunda na mbogamboga kwa wingi kila siku ili kupunguza uwezekano wa kupatwa na saratani na magonjwa mengineyo.

Monday, March 16, 2009

Ukubwa wa shingo, (neck thickness) unaashiria hatari ya ugonjwa wa moyo


Kupima ukubwa wa shingo bila kuzingatia ukubwa wa kiuno, kunaweza kuonyesha hatari anayokabiliwa nayo mtu ya kupata ugonjwa wa moyo. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na America Heart Association, ukubwa wa shingo unaweza kuonyesha kiwango cha mafuta kinchozunguka figo na moyo na hivyo kukadiria hatari inayomkabili mtu ya kupatwa na ugonjwa wa moyo.
Watu wenye shingo nene wanaweza kukabiliwa na magonjwa yanayohusiana na moyo, hata kama wana viuno vyembamba.
Utafiti mwingine umeonyesha kuwa, watu wa aina hii kwa kawaida huwa wana kiasi cha chini cha kolestroli nzuri yani HDL na kiasi kikubwa cha kolestroli mbaya yani LDL.
Hata hivyo ukubwa wa shingo (neck size) haujaripotiwa kuathiri kiwango cha LDL.
Wanasayansi wanasema kuwa, shingo nene inaashiria kuwa kiwango cha mafuta mwlini kiko juu, mafuta ambayo yanahusiana moja kwa moja na uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo. Lakini wamesema kuwa, kufanya mazoezi ni njia bora kabisa ya kupunguza mafuta mwilini.