Wednesday, December 30, 2009

WHO yasema, ni mapema mno kutangaza ushindi dhidi ya virusi vya H1N1


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO amesema kuwa ni mapema mno kuweza kutangaza ushindi dhidi ya virusi vya homa ya mafua ya nguruwe akiashiria uwezekano wa virusi hivyo kubadili sura yake na kuwa hatari kubwa zaidi kwa mwanadamu. Margaret Chan amesema kuwa virusi vya H1N1 bado vinaendelea kuzagaa na tayari vimewasibu mamilioni ya watu. Mkuu wa Shirika la Afya Duniani amesema habari njema ya kitiba kuhusu virusi hivyo ni kupungua kasi yake licha ya kwamba vimekwisha sababisha vifo vya watu 12 elfu wengi wao wakiwa wanawake waja wazito, watoto wadogo na watu wenye maradhi sugu. Chan amesema idadi hiyo rasmi ya watu waliofariki dunia kutokana na virusi vya mafua ya nguruwe haiakisi ukweli wa mambo na kwamba idadi kamili ya wahanga wa ugonjwa huo itajulikana baada ya kupita miaka miwili.

Sukari kupimwa kupitia lensi za macho



Wanasayansi wamegundua teknolojia mpya itakayowezesha kupimwa kiwango cha sukari katika damu bila ya kuhitajia mgonjwa kutolewa damu kila siku. Wataalamu hao wa Chuo Kikuu cha Ontario magharibi huko Hamilton, wamegundua teknolojia hiyo mpya ambapo sukari huweza kupimwa kwa kutumia lensi za macho za aina ya hudrogel zilizotengenezwa kwa vipendo vidogo vidogo vya nano. Wagonjwa wa kisukari watakaovaa lensi hizo wataweza kujua kuhusana na kiwango cha sukari mwilini mwao, kutokana na mabadiliko ya rangi ya lensi hizo za macho. Vipande vya nano vilivyotumika kutengeneza lensi hizo, hubadilika kwa kuzingatia molekuli za glukosi zilizoko kwenye machozi, suala ambalo husababisha mabadiliko ya kikemia na mabadiliko ya rangi. Wanasayansi wana matumaini kwamba, kwa kugunduliwa lensi hizo mpya na kuanza kutumika, katika siku zijazo kutakuwa hakuna tena haja ya wagonjwa wa kisukari kudungwa sindano na kuchukuliwa damu kila siku ili kujua kiwango cha sukari mwilini.

Saturday, December 26, 2009

Kujiingiza katika mapenzi kwenye umri mdogo husababisha kensa ya mlango wa kizazi


Huko nyuma iliaminiwa kuwa, virusi aina ya papiloma au (HPV) pamoja na vipimo duni ndio sababu kuu inayopelekea ugonjwa wa kensa ya mlango wa kizazi, lakini uchunguzi mpya umeonyesha kuwa kuna sababu nyinginezo muhimu zinzosababisha ugonjwa huo. Kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa katika jarida la Kensa la Uingereza, mahusiano ya kijinsia yanayofanywa katika umri mdogo huongeza uwezekano wa kupata kensa ya mlango wa kizazi mara dufu. Suala jingine lililohesabiwa kuchangia maambukizo hayo, ni muda mwanamke anapopata mtoto wake wa kwanza.
Katika uchunguzi huo, imeonekana kuwa wanawake wanaoishi maisha ya kimasikini, huanza kujiingiza katika masuala ya kimapenzi miaka minne mapema kuliko wengineo. Hivyo kuna uwezekano wa kupata maambukizo ya virusi vya HPV mapema zaidi, na hivyo kuvipa muda zaidi virusi hivyo kuzaliana kwa muda mrefu na baadaye kusababisha kensa ya kizazi. Wanasayansi waliofanya uchunguzi huo wamependekeza kwamba ni bora chanjo dhidi ya virusi vya HVP itolewe mapema, hasa kwa wasichana wanaoishi katika jamii masikini, ili kuwakinga na ugonjwa wa kensa ya mlango wa kizazi.
Inafaa kujua kuwa, kensa ya mlango wa kizazi au kwa kimombo cervical cancer, ni saratani inayoshambulie lango la uzazi, sehemu ya chini kabisa na nyembamba ya kizazi. Ugonjwa huo unaweza kugunduliwa kirahisi kwa kufanya kipimo cha Pap smear. Ni muhimu kufahamu kwamba ugonjwa wa kensa ya kizazi ni ugonjwa hatari lakini unaweza kuzuiwa na kutibiwa kwa urahisi. Naahidi kuelezea kwa undani juu ya ugonjwa huo hapo baadaye.

Friday, December 25, 2009

X-Mass Njema Wadau


Leo ni sikukuu ya Christmas, kwanza kabisa blogi ya Kona ya Afya inatoa mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa kuzaliwa masihi, Issa Bin Maryam, (Yesu Kristo) kwa wafuasi wote wa dini hiyo ya mwenyezi Mungu. Ni matumaini yetu kuwa katika wakati huu wa sikukuu ya X-mass wadau wote huku wakisherekea sikukuu na kuwa mapumzikoni, hawatazembea pia kuzitunza afya zao. Kwa ajili hiyo basi zifuatazo ni nukta kadhaa za kufuata ili kuepusha wasiwasi na mfadhaiko wa mawazo (stress) wakati huu wa mapunziko na sikukuu, na zinazosadia kuhakikisha kwamba tunabaki katika afya njema kimwili, kiakili na kihisia.
• Jitahidi kushikamana na ibada. Kushikamama na ibada za kiroho wakati huu wote wa sikukuu, na kuwa karibu na muumba ( kwa kutegemea imani na dini ya mtu) kwa kufanya ibada kama kusali, kwenda kanisani au msikitini husaidia kumfanya mtu ajisikie vizuri kiroho.
• Pata hewa nzuri. Kila unavyojitahidi kuwa nje ya nyumba na kufanya shughuli mbalimbali ndivyo mwili wako unavyopata nishati zaidi. Kuvuta hewa safi na salama kutaufanya ubongo wako upate oksijeni zaidi na kuupa mwili wako nishati. Hivyo wakati huu wa sikukuu jitahidi kufanya michezo kama vile kukimbia, kusketi, kupanda baiskeli, kutembea kando ya bahari au mto na kadhalika.
• Jishughulishe na masuala ya sikukuu kama vile kuwanunualia watu zawadi madukani, kuwatembela ndugu jamaa na marafiki na hata wagonjwa, kualika au kwenda katika mialiko mbalimbali na kadhalika. Vitendo hivyo ni bora kuliko kukaa tuu nyumbani na kula na kunywa peke yako huku akiangalia tv au filamu.
• Pata usingizi wa kutosha na pumzisha mwili wako. Unaweza ukalala kidogo mchana au kuamka kwa kushelewa kidogo wakati wa asubuhi.
• Tenda kile moyo wako inachopenda. Kuwa na afya njema wakati wa X-mass ni pamoja na kufanya kile kinachoburudisha moyo wako. Imba kama unapenda kuimba, cheza kama unapenda kucheza, andika, tembea, chora picha, pika nakadhalika, ilimradi utende chchote kili kinachofaurahisha moho wako.
• Kula na kunya kusizidi kiasi, na bila kusahau vyakula visivyo na mafuta mengi au sukari nyingi ambavyo ni salama kwa afya zetu. Wale wenye magonjwa mbalimbali sugu wasijisahau na kuvunja miiko ya vyakula wasivyotakiwa kula. Usisahau kuwa, sikukuu itapita lakini afya yako ni muhimu sana kwa maisha yako yote… Sikukuu njema wadau huku tukitunza afya zetu!

Wednesday, December 23, 2009

Jeli ya nyanya ni bora kuliko aspirini


Utafiti mpya uliofanywa kwa majaribio umegundua kuwa katika mbegu za nyanya kuna mada asilia, inayoweza kusadia mzungumzo wa kawaida wa damu na kuzuia damu isigande. Mada hiyo iliyoko kwenye mbegu za nyanya iligunduliwa mwaka 1999 na Profesa Adim Dutta-Roy. Jeli hiyo inayozunguka mbegu za nyanya, hunaweza kusaidia mzunguko wa damu.
Jeli hiyo isiyokuwa na rangi wala ladha, huzuia chembe za damu aina ya platelets zisishikane, suala ambalo hupunguza uwezekano wa damu kuganda, kama inavyofanya aspirini lakini bila kuwa na madhara.
Wachunguzi wa Uingereza wamesema kwamba, athari za geli hiyo huanza masaa matatu tangu inapoanza kutumiwa na kudumu kwa masaa 18, hivyo inahitaji kutumiwa kila siku.
Wataalamu hao wamependekeza kwamba, kuongeza jeli hiyo katika vyakula mbalimbali kunaweza kuepusha matumizi ya aspirini kwa ajili ya kuzuia hatari ya magonjwa ya mishipa ya moyo.

Mshituko wa moyo mara nyingi hutokea saa tatu asubuhi


Wataalamu wa magonjwa ya moyo wamesema kuwa hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo hutokea zaidi mapema asubuhi, hasa saa tatu asubuhi.
Utafiti huo uliotangazwa katika Kongress ya 4 magonjwa ya moyo ya Mashariki ya Kati imesema kuwa, watu wanaokabiliwa na hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo, hutokewa na ugonjwa huo mapema asubuhi kwa sababu ya mabadiliko ya homini ambayo huongeza hitajio la oksijeni la mishipa ya moyo katika wakati huo, na kusababisha mshituko wa moyo. Uchunguzi huo umeelezea pia kuwa, ripoti zinaonyesha ongezeko la matukio ya mshituko wa moyo katika siku za Jumatatu, suala ambalo huenda likawa linachangiwa na kiasi kikubwa na kula kupita kiasi siku za wikiendi. Wataalamu hao pia wamesema kuwa, mishipa ya juu ya mwili huwa inasinyaa msimu wa baridi, hali ambayo ni kinyume na utendaji wa mishipa ya moyo na husababisha kupungua kiwango cha oksijeni inayohitajiwa na misuli ya moyo. Wamesema hii ndio sababu, watu hupata mishtuko wa moyo kwa wingi wakati wa mapukutiko (fall) na baridi (winter).
Uchunguzi huo pia umeachiria kwamba, umri wa watu wanaopatwa ugonjwa huo imeshuka na hata kufikia chini ya miaka 55 katika baadhi ya nchi.

Monday, December 21, 2009

Ujuwe ugonjwa wa Kifua Kikuu au TB ....sehemu ya kwanza



Karibuni wapenzi wadau wa Kona ya Afya katika mfululizo mwingine wa
kujadili magonjwa mbalimbali. Leo tumepata fursa ya kuzungumzia ugonjwa wa kifua kikuu, ambacho maambukizo yake yanaongezeka kwa kasi kubwa ulimwenguni, khususan katika nchi zinazoendelea. Kwa kuzingatia kuwa ugonjwa wa kifua kikuu huathiri watu wa rika zote na hasa vijana kati ya miaka 15 hadi 45 ambayo ndiyo nguvu kazi katika nchi nyingi za dunia, kunapaswa kufanyika jitihada kubwa za kudhibiti maambukizo ya ugonjwa huo. Kifua Kikuu ambao kitaalamu hujulikana kama Tuberculosis ni ugonjwa wa kuambukiza ambao huenezwa kwa njia ya hewa. Kifua kikuu husababishwa na bacteria au kimelea aina ya Mycobacterium tuberculosis au (tubercle bacterium). Ugonjwa huu kwa kawaida huathiri mapafu, lakini pia huweza kushambulia viuongo vingine vya mwili kama vile tezi za limfu, ubongo na mifupa.
Tb inambukizwa kwa namna gani? :
Mtu mwenye kifua kikuu au Tb ambaye hajatibiwa, anapokohoa, kupiga chafya, kutema mate au makozi husambaza bacteria au vimelea hivyo vya ugonwja huo hewani. Kwa hivyo mtu mwingine akivuta hewa yenye vimelea hivyo anaweza kuambukizwa kifua kikuu. Kwa mfano takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa nchini Tanzania ugonjwa wa Kifua Kikuu umekuwa ukiongezeka kwa kasi kubwa ambapo watu elfu 65,000 hivi sasa wanaugua kifua kikuu nchini humo. Kati yao asilimia 50 pia wana ukimwi. Hapa linajitokeza swali kwamba dalili za Kifua Kikuu ni zipi?
Mtu ambaye amepatwa na ugonjwa wa Tb au Kifua Kikuu huwa na dalili au husumbuliwa na hali zifuatazo:
Kukohoa kwa muda usiopungua wiki mbili na mara nyingine kukohoa damu, homa za jioni za mara kwa mara, kutokwa na jasho usiku, kukosa hamu ya kula, kupungua uzito kwa kiasi kikubwa na kadhalika.
Kundi ambalo liko kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa Tb au kifua kikuu ni la wale wanaoishi kwa karibu na kwa muda mrefu na mtu yule aliyekwisha ambukizwa ugonjwa huo. Kwa hiyo hapa nitaorodhesha makundi ambayo yako kwenye hatari na ya uwezekano mkubwa wa kuambukizwa Tb iwapo watakuwa karibu na mgonjwa. Watu hawa ni rahisi kupatwa na kifua kikuu kwa sababu kinga zao za mwili huwa ni za kiwango chini: Watoto wadogo na wazee, wale wote wanaougua kisukari, watu wnaotumia dawa aina ya steroids au dawa nyinginezo zinazoathiri mfumo wa kinga ya mwili, waathirika wa ukimwi na HIV, wale wote wanaoishi maeneo yenye msongamano mkubwa watu yaliyoduni kiafya, wanaoishi kwenye sehemu zisizokuwa na hewa ya kutosha, watu wanaotumia dawa mbalimbali, au pombe na mwisho wale wenye lishe duni.
Usikuko muendelezo wa makala hii, na daima linda afya yako.