Monday, November 30, 2009

Binadamu anaweza kusikia kwa kupitia ngozi!


Huku masikio yakiwa hayachukuliwa tena kuwa ni njia pekee ya kusikia mwanadamu, uchunguzi mpya umeonyesha kuwa ngozi pia inaweza kusaidia katika kuleta kusikia. Chunguzi za huko nyuma zilionyesha kuwa, ishara za macho kama vile mzungumzaji kutikisa kichwa zinaweza kuwa kuathiri namna mtua navyosiakia kitu. Na pia inajulikana kuwa zaidi ya masikio suala zima la kusikia sauti hufanywa pia kwa kupitia mifupa ya kichwa. Uchunguzi mpya hata hivyo umehitimisha kwamba kuna masuala mengineyo zaidi ya ishara za kusikia na macho ambazo zinaathiri suala zima la kusikia. Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la Nature, binadamu wanaweza kutafisiri sio tu ishara zilizotolewa kwa macho, bali pia huweza kutafisri taarifa wanazohisi kupitia ngozi zao wakati wanaposikia jambo. Wanasayansi wana matumaini kwamba ugunduzi wao huo utafungua njia ya kuimarishwa vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya watu wasiosikia vyema.

Saturday, November 28, 2009

Jinsi ya kuhakikisha tunapata lishe bora na salama hata wakati wa Eid


Eid ni wakati ambapo familia zinakusanyika pamoja kula na kupeana zawadi na kusherehekea sikukuu hiyo adhimu. Kwa kawaida chakula kina nafasi muhimu wakati wa sherehe hizo. Sikukuu ya idil Adh-ha husherehekewa kwa mnasaba wa kumalizika kipindi cha Hijja ambapo Waislamu huenda kuzuru nyuma ya Mwenyezi Mungu katika mji mtukufu wa Makka. Katika sherehe hiyo kwa kawaida wanyama huchinjwa na kutolewa sadaka, ambapo nyama hugawanywa kwa ndugu na marafiki pamoja na masikini. Kwa kawaida chakula kinachopikwa katika siku ya iddi kinatofautiana kutoka nchi hadi nchi na jamii moja na nyingine. Lakini suala la muhimu ni kujitahidi kupata lishe iliyo salama na bora wakati wa kusherehekea sikukua ya Eid. Vyakula vinavyopikwa siku ya idi vinaweza kuwa salama lakini kwa kuwa ni wakati wa sherehe, ni rahisi kusahau kula vyakula ambavyo huweza kuhatarisha afya zetu. Ingawa ni siku ya sikukuu lakini Kona ya Afya inakutaka uwe mwangalifu kuhusiana na kile unachokula na kuipikia familia yako, huku ukijitahidi kupata chakula bora na salama. Hivyo ifuatayo ni njia ya kuifanya lishe yako ya Eid iwe salama:
• Jiepushe kula vyakula vyenye chumvi nyingi na mafuta mengi, na ni bora utumie viungo ambavyo pia vina faida tele mwilini.
• Ni bora utumie mafuta ya mimea (vegetable oli) badala ya kutumia siagi au mafuta ya mgando wakati wa kutayarisha msosi wa iddi. Epuka kutumia mafuta mengi kuliko kawaida, kwani mafuta mengi sio utamu wa chakula, bali ni hatari kwa afya yako.
• Wakati unaponunua nyama au vitoweo vinginevyo, hakikisha unanunua nyama salama, ambayo haijakaa sana na isiyokuwa na mafuta mengi. Iwapo ina mafuta jitahidi uondoe sehemu zenye mafuta kabla ya kupika.
• Hakikisha unaitayarishia na kuipikia familia yako na wageni mbalimbali mlo kamili wakati wa sikukuu. Sio wali na nyama pekee, pilau na ndizi tu, bali jitahidi kuwepo na mboga mboga na matunda pia. Halikadhalika jiepushe kupika kwa wingi vitu vyenye sukari nyingi.
• Ili kuhakikisha vitamini na madini zinabakia katika chakula unachopika, mboga mboga zisipikwe kwa muda mrefu na vilevile ili kuepuka minyoo na magonjwa mengineyo, hakikisha mboga na matunda vinaoshwa vyema.
• Wakati wa kupika chai ya maziwa wa vitindamilo vinginevyo (desserts) hakikisha unatumia maziwa yasiyo kuwa na mafuta mengi au low fat milk.
• Ili kuepuka kupika vyakula vya kukaanga na vyenye mafuta mengi, unaweza ukaoka vyakula hivyo badala ya kuvikaanga na ukapata ladha nyingine na kuwa bora zaidi kwa afya yako nay a familia yako kwa ujumla.
• Kunawa mikono na kuhakikisha usafi unazingatiwa, ni miongoni mwa mambo muhimu wakati w akutayarisha na kupika vyakula kwa ajili ya sikukuu.
Naam kina mama na kina dada, eid ni wakati wako mwingine ambao mbali ya kuonyesha ufundi wako wa kupika vyakula vitamu na vya kila aina kwa ajili ya wale uwapendao na wageni mbalimbali, hakikisha pia unazingatia afya ya walaji na kutunza afya kwa ujumla.
Eid Njema!

Eid Mobarak!


Nawatakia Eid njema wadau.
Msisahau kuzitunza vyema afya zenu.

Watu milioni 25 wamefariku dunia duniani kote kutokana na UKIMWI


Taarifa ya pamoja ya Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na shirika la UNAIDS imesema kwamba, idadi ya watu waliofariki dunia duniani kote kutokana na ugonjwa wa Ukimwi imefikia milioni 25. Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa hivi karibuni, inakadiriwa kwamba watu wengine milioni 33.4 wanaishi na virusi vya HIV duniani. Ripoti hiyo aidha imesema kwamba, karibu watu milioni 60 wakiwemo watu 25 milioni waliofariki dunia, wameambukizwa virusi vya HIV tangu ugonjwa huo ulipoanza. Ingawa idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa wa HIV imeongeza, lakini takwimu za watu wanaofariki kutokana na ugonjwa huo, zimepungua ikilinganishwa na huko nyuma.
Matumizi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi au anti-retroviral drugs, yanaaminika kuwa yamepunguza kwa asilimia 10 vifo vinavyotokana na magonjwa yanayoambatana na ugonjwa wa Ukimwi katika miaka mitano iliyopita.
Ripoti hiyo pia imesema kwamba, bara la Afrika bado ni sehemu yenye maambikizo makubwa zaidi ya virusi vya Ukimwi ikilinganishwa na sehemu nyinginezo duniani na kwamba ugonjwa huo unasababisha nusu ya wakinamama wanojifungua kufariki dunia katika bara hilo.

Monday, November 23, 2009

Sababu kuu zinazomfanya mtu aweze kupata mshituko wa moyo!..sehemu ya 2


Kwanza tutazungumzi baadhi ya sababu zisizoweza kuzilika zinazosababisha mshituko wa moyo. Nazo ni kama ifuatavyo:-
Kuongezeka umri: Asilimi 83 ya watu wanaokufa na magonjwa ya moyo ni wale waliofikia umri wa miaka 65 na kuendelea. Umri unapokuwa mkubwa, wanawake ambao kwa kawaida hawapatwi sana na ugonjwa moyo, nao pia huanza kukabiliwa na hatari ya magonjwa hayo ukiwemo mshituko wa moyo.
Jinsia ya kiume: Wanaume wanakabiliwa na hatari zaidi ya kupatwa mashituko wa moyo kuliko wanawake, ambapo hupata ugonjwa huo katika umri mdogo. Wanawake baada ya kukatika hedhi au menopause, nao pia huanza kukabiliwa na hatari hiyo lakini si kwa kiasi kikubwa kama wanaume.
Urithi: Watoto ambao wazazi wao wana na magonjwa ya moyo au walipatwa na mshituko wa moyo nao pia wanakabiliwa na hatari ya kupaatwa na magonjwa hayo. Waamerika Weusi wanapatwa na shinikizo la damu zaidi wakilinganishwa na watu wenye asili ya Caucasian au wazungu. Magonjwa ya moyo pia hutokea sana kwa watu wenye asili ya Mexico, India, Hawaii na Asia. Watu ambao familia zao zina historia ya magonjwa ya moyo wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo mara mbili zaidi kuliko wengine, kwani mtu hawezi kuchagua umri wake, jinsia na asili yake.
Zifuatazo sasa ni baadhi ya sababu zinazoweza kuepukika zinazosababishwa mshituko wa moyo:-
 Kuvuta sigara: wavuta sigara wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo mara 2 hadi 4 zaidi ya watu wasiovuta sigara. Uvutaji sigara ni sababu kubwa inayojitegemea inayoweza kusababisha mshituko wa moyo kwa wagonjwa wenye maradhi ya moyo. Kuvuta sigara hadhani au mbele ya wengine kunawafanya watu hao nao wakabiliwe na hatari hiyo magonjwa ya moyo.
 Kiwango kikubwa cha mafuta katika damu au High Blood Cholesterol: Kila kiwango cha mafuta kinapoongezeka katika damu ndio uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya moyo nao unavyoongezeka. Iwapo mtu atakuwa na sababu nyinginezo kama ufutaji sigra, shinikizo la damu na kadhalika, basi mtu huyo ana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata shinikizo la moyo. Kiwango cha mafuta katika damu pia kinathiriwa na umri, jinsi, urithi na lishe.
 Shinikizo la damu: Shinikizo la damu huongeza ufanyajikazi wa moyo, suala linalopelekea mishipa ya moyo iwe minene na migumu. Pia huongeza hatari ya kupata mshituko wa moyo, mshituko wa ubongo, figo kutofanya kazi na moyo kushindwa kufanya kazi. Shinikizo la damu linapokuwa pamoja na unene wa kupindukia, uvutaji sigara, kiwango cha juu cha mafuta kwenye damu au kisukari, humfanya mtu apatwe kwa urahisi na mshituko wa moyo.
 Kutoushughulisha mwili: Kuishi maisha yasiyokuwa ya kushughulika kifizikia ni miongoni mwa sababu za kupatwa na ugonjwa wa moyo. Shughuli za kawaida husaidia kuzuia magonjwa ya moyo na kuongezeka kiwango cha mafuta katika damu. Unapoushughulisha mwili wako zaidi ndivyo unavyojisaidia zaidi kiafya. Kushughulisha mwili husaidia kudhibiti kisukari, unene wa kupindukia, kiasi kikubwa cha mafuta katika damu na hata kupunguza shinikizo la damu.
 Unene wa kupindukia au Obesity: Watu wenye unene wa kupindukia wana mafuta mengi mwilini na iwapo mafuta yamejikusanya katika nyonga na kiuno wanaweza kukabiliwa na hatari ya kupata mshituko wa moyo. Unene mkubwa huufanya moyo ufanye kazi zaidi. Pia huongeza shinikizo la damu na kiwango cha mafuta katika damu. Halikadhalika unene humsababisha mtu apatwe na kisukari.
Sababu nyinginezo ni pamoja na
 Mtu kuwa na mawazo na fikra kila mara, kwani wataalamu wanasema kuwa kuna uhusiano kati ya kuwa na mawazo na fikra na magonjwa ya moyo. Kwani mtu mwenye mawazo mengi kwa kawaida huwa na ghadhabu, huenda akavuta sigara na mengineyo ambayo huweza kupelekea ugonjwa wa hatari.
 Kunywa sana pombe: Kunywa sana pombe husababisha shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na kupelekea mshituko wa moyo. Pia huongeza kiasi cha mafuta katika damu, kensa na magonjwa mengineyo na hata husababisha moyo kupiga hovyo. Vilevile huchangia katika kusababisha unene wa kupindukia, ulevi wa kupindukia, kujiua na ajali.

Saturday, November 21, 2009

Kitunguu swaumu kinazuia influenza!



Kitunguu swaumu tangu kale kimekuwa kikijulikana kama 'dawa ya kushangaza' na kutumiwa na watu wengi katika kutibu mafua na influenza. Miongoni mwa faida za kitunguu swaumu ni kuzuia kupatwa na magonjwa mbalimbali na maambukizo ya virusi. Hivyo kitunguu swaumu hujulikana kama antibiotiki ya asilia. Uchunguzi umeonyesha kwamba kula kitunguu swaumu kunapunguza kushadidi ugonjwa wa influenza na hata kuzuia kupatwa na ugonjwa huo. Vilevile kula kila mara kitunguu swaumu, huzuia kupatwa na magonjwa ya moyo, kwani kitunguu swaumu huzuia damu isigande kwenye mishipa ya damu.
Halikadhalika kitunguu swaumu ambacho pia ni kiungo muhimu cha chakula kina potassium, na hivyo watu wenye ugonjwa wa shinikizo la damu wanashauriwa kula vyakula vilivyopikwa kwa kitunguu swaumu.
Si vibaya kujua kuwa katika uchunguzi uliochapishwa mwaka 2001, imeelezwa kwamba, kitunguu swaumu kina athari kubwa na nzuri pale kinapochanganywa na baadhi ya dawa nyinginezo katika kutibu Ukimwi au HIV.
Haya shime jamani… kuanzia leo vyakula visikose kuungwa na kitunguu thomu, iwapo unaogopa kupatwa na influenza kama mimi!

UNICEF yasema, Afghanistan ndiyo sehemu mbaya zaidi ya kuzaliwa mtoto duniani


Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema kuwa nchi ya Afghanistan iliyoharibiwa kwa vita ni sehemu mbaya zaidi duniani ya kuzaliwa mtoto. Shirika hilo limetangaza kwamba, Afghanistan ina idadi kubwa zaidi ya vifo vya watoto duniani ambapo vifo 257 vya watoto hutokea kati ya kila watoto 1,000 wanaozaliwa.
Daniel Toole Mkurugenzi wa Unicef wa kusini mwa Asia amesema kwamba, ripoti yake ya mwaka kuhusiana na watoto duniani imegundua kwamba, Afghanistan ni sehemu hatari kwa wasichana na kwamba kukosekana usalama kumepunguza idadi ya watoto wanaohudhuria shuleni hasa wa kike. Aidha mkurugenzi huyo wa Unicef amelaumu mashambulio ya mara kwa mara ya shule za wasichana ambayo yamesababisha elimu ya wanawake kuporomoka kabisa nchini Afghanistan.