Saturday, November 28, 2009

Jinsi ya kuhakikisha tunapata lishe bora na salama hata wakati wa Eid


Eid ni wakati ambapo familia zinakusanyika pamoja kula na kupeana zawadi na kusherehekea sikukuu hiyo adhimu. Kwa kawaida chakula kina nafasi muhimu wakati wa sherehe hizo. Sikukuu ya idil Adh-ha husherehekewa kwa mnasaba wa kumalizika kipindi cha Hijja ambapo Waislamu huenda kuzuru nyuma ya Mwenyezi Mungu katika mji mtukufu wa Makka. Katika sherehe hiyo kwa kawaida wanyama huchinjwa na kutolewa sadaka, ambapo nyama hugawanywa kwa ndugu na marafiki pamoja na masikini. Kwa kawaida chakula kinachopikwa katika siku ya iddi kinatofautiana kutoka nchi hadi nchi na jamii moja na nyingine. Lakini suala la muhimu ni kujitahidi kupata lishe iliyo salama na bora wakati wa kusherehekea sikukua ya Eid. Vyakula vinavyopikwa siku ya idi vinaweza kuwa salama lakini kwa kuwa ni wakati wa sherehe, ni rahisi kusahau kula vyakula ambavyo huweza kuhatarisha afya zetu. Ingawa ni siku ya sikukuu lakini Kona ya Afya inakutaka uwe mwangalifu kuhusiana na kile unachokula na kuipikia familia yako, huku ukijitahidi kupata chakula bora na salama. Hivyo ifuatayo ni njia ya kuifanya lishe yako ya Eid iwe salama:
• Jiepushe kula vyakula vyenye chumvi nyingi na mafuta mengi, na ni bora utumie viungo ambavyo pia vina faida tele mwilini.
• Ni bora utumie mafuta ya mimea (vegetable oli) badala ya kutumia siagi au mafuta ya mgando wakati wa kutayarisha msosi wa iddi. Epuka kutumia mafuta mengi kuliko kawaida, kwani mafuta mengi sio utamu wa chakula, bali ni hatari kwa afya yako.
• Wakati unaponunua nyama au vitoweo vinginevyo, hakikisha unanunua nyama salama, ambayo haijakaa sana na isiyokuwa na mafuta mengi. Iwapo ina mafuta jitahidi uondoe sehemu zenye mafuta kabla ya kupika.
• Hakikisha unaitayarishia na kuipikia familia yako na wageni mbalimbali mlo kamili wakati wa sikukuu. Sio wali na nyama pekee, pilau na ndizi tu, bali jitahidi kuwepo na mboga mboga na matunda pia. Halikadhalika jiepushe kupika kwa wingi vitu vyenye sukari nyingi.
• Ili kuhakikisha vitamini na madini zinabakia katika chakula unachopika, mboga mboga zisipikwe kwa muda mrefu na vilevile ili kuepuka minyoo na magonjwa mengineyo, hakikisha mboga na matunda vinaoshwa vyema.
• Wakati wa kupika chai ya maziwa wa vitindamilo vinginevyo (desserts) hakikisha unatumia maziwa yasiyo kuwa na mafuta mengi au low fat milk.
• Ili kuepuka kupika vyakula vya kukaanga na vyenye mafuta mengi, unaweza ukaoka vyakula hivyo badala ya kuvikaanga na ukapata ladha nyingine na kuwa bora zaidi kwa afya yako nay a familia yako kwa ujumla.
• Kunawa mikono na kuhakikisha usafi unazingatiwa, ni miongoni mwa mambo muhimu wakati w akutayarisha na kupika vyakula kwa ajili ya sikukuu.
Naam kina mama na kina dada, eid ni wakati wako mwingine ambao mbali ya kuonyesha ufundi wako wa kupika vyakula vitamu na vya kila aina kwa ajili ya wale uwapendao na wageni mbalimbali, hakikisha pia unazingatia afya ya walaji na kutunza afya kwa ujumla.
Eid Njema!

No comments: