Sunday, November 8, 2009

Unene wa kupindukia, ndio chanzo cha kesi 100,000 za kensa nchini Marekani



Unene wa kupindukia au Obesity unaaminiwa kuwa ndio sababu ya kutokea zaidi ya kesi 100,000 za kensa kila mwaka nchini Marekani, huku unene pia ukiwa unamletea mtu hatari ya kupatwa na magonjwa mengi kama vile kisukari na hata homa ya mafua ya nguruwe. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Kitengo cha Utafiti wa Kensa cha Marekani, unene unasababisha aina mbalimbali za kensa, zikiwepo kesi 33,000 za kensa ya matiti, unene ambao unaweza kutokana na lishe isiyofaa, kukosekana harakati pamoja na kuwa na mafuta mengi mwilini.
Taarifa hiyo pia imesema kwamba, tatizo la kuwa na unene wa kupindukia lina athari kubwa tatu katika aina saba za saratani. Imeonekana ushahidi wa kuwepo uhusiano kati ya unene au obesity na kensa za mfumo za koo, kongosho, figo, matiti na utumbo.
Wataalamu wanasema kuwa, mafuta mengi mwilini huongeza kiwango cha homoni aina ya steroids na homoni nyinginezo ambazo zinahusiana na kutokea kensa. Seli za mafuta ni maarufu kwa kutengeneza ostrogen, ambayo imeonekana kuwa inashajiisha ukuaji wa seli katika kensa ya matiti. Halikadhalika mafuta mengi mwilini hupunguza uwezo wa kinga ya mwili na kuongeza mada za oxidative ambazo hupelekea kuharibika DNA na mwishowe kusababisha saratani.
Inakadiriwa kuwa asilimia 49 ya kesi za saratani ya kizazi ambayo ni aina maarufu zaidi ya kensa za mfumo wa uzazi, na asilimia 35 ya kesi za saratani ya koo nchini Marekani zinahusiana na unene wa kupindukia.
Inafaa kuashiria hapa pia kuwa, asilimia 34 ya Wamarekani wenye umri wa miaka 20 na kuendelea wana unene wa kupindukia au Obesity.

No comments: