Thursday, November 19, 2009

Mapacha wa Baghaladesh waliokuwa wameungana waachanishwa


Timu ya madaktari 16 wa Australia wamefanikiwa kuwatenganishwa watoto mapacha wa Bangladesh waliokuwa wameungana kwa miaka mitatu, katika operesheni iliyochukua masaa 27. Trishna na Krishna ni watoto mayatima wa Bangladesh waliokuwa wameungana katika sehemu za juu za kichwa na kuwa na mishipa ya damu ya pamoja. Madakatari wataalamu wa masuala ya ubongo wa Australiwa katika oparesheni hiyo waliugawa ubongo wa watoto hao kwa tahadhari kubwa na kuwaachanisha. Watoto hao wadogo wa kike walikuwa mahututi walipowasili nchini Australia miaka miwili iliyopita, ambapo tayari walikuwa wameshafanyiwa operesheni kadhaa za utangulizi. Madakatari huko nyuma walisema kuwa kwa kufanyiwa operesheni huo kulikuwa na uwezekano wa asilimia 25 kwamba mmoja kati ya mapacha hao angekufa na asilimia 50 watoto wote hao wawili wanngepatwa na matatizo ya kuharibika ubongo. Lakini Mkuu wa kitengo cha Upasuaji wa hospitali ilipofanywa oparesheni hiyo Dakta Leo Donnan amesema kuwa, watoto hao wanaendelea vyema baada ya kufanyiwa operesheni hiyo, lakini bado wako katika chumba cha uangalizi maalum wakisubiri operesheni nyingine ya kuzishona tena ngozi zao, mifupa na kuongezewa baadhi ya viungo bandia. Oparesheni za kuwatenganisha mapacha walioshikana ni kazi nzito ambayo kwa kawaida huwa hazifanywi katika hospitali mbalimbali duniani. Operesheni hizo zinapofanywa mara nyingi hupelekea vifo vya mapacha hao. Mapacha wanaoungana au Conjoined Twins hutokea kwa uchache katika mimba, mara moja katika kila kesi 200, na huwa katika mapacha wanaoshabihiana au identical twins. Mara nyingi hata kama mimba kama hizo zitatungwa lakini kwa asilimia 40 au 60 watoto hao hufia tumboni, au watoto wanaozaliwa kufariki dunia siku chache baada ya kuzaliwa. Mimba za mapacha wanaoungana kwa asilimia 70 huwa ni za watoto wa kike, sababu ambayo haijulikana.

No comments: