Monday, November 2, 2009

Ijue Homa ya Mafua ya Nguruwe (Swine Flu) ….sehemu ya kwanza


Homa ya mafua ya nguruwe inayojulikana kiingereza kama “Swine flue” ni ugonjwa unatokana na moja ya aina mbalimbali za virusi vya mafua ya influenza ya nguruwe au SIV. SIV au Swine Influenza Virus ni aina yoyote ya mafua ya influenza yanayotokana na virusi vinavyotokana na nguruwe. Virusi hivyo vinaweza kwa H1N1, H1N2, H3N1, H3N2 NA H2N3. Ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe ni ugonjwa wa kawaida kwa nguruwe duniani kote. Maambukizo ya ugonjwa ya virusi hivyo kutoka kwa nguruwe kwenda kwa binaadamu hayatokeo kila mara. Lakini iwapo maambukizo ya binaadamu yatatokea husababisha homa ya mafua ya nguruwe kwa binaadamu pia. Watu ambao wako karibu na nguruwe wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa homa ya mafua ya nguruwe, kama vile wafugaji nguruwe na wanaojishughulisha na wanyama hao.
Wataalamu wanasema kwamba mfumuko wa homa ya mafua ya nguruwe mwaka huu wa 2009, ambapo ilianzia nchini Mexico, umesababishwa zaidi na virusi vya H1N1, kwani ndio aina ya virusi ambavyo humpata zaidi mwanadamu. Ugonjwa huo kwa hivi sasa umeenea sana katika nchi nyingi duniani na Shirika la Afya Duniani WHO limeutangaza kuwa janga la kimataifa. Watu wengi wameambukizwa homa ya mafua ya nguruwe katika nchi nyingi duniani huku, ikikadiriwa kuwa karibu watu 700 hufariki dunia kila wiki kutokana na homa ya mafua ya nguruwe duniani kote. Kwa kuzingatia hayo Kona ya Afya imeona kuna ulazima wa kuzijua dalili za ugonjwa huo na kuelezea namna ya kujiepusha au kukabiliana na ugonjwa huo. Kumbuka kuwa hivi sasa ambapo nchi nyingi zinaingia katika majira ya badiri ambapo mfumuko wa magonjwa ya kifua na mafua huongezeka, hatari ya kupatwa na ugonjwa huo ni kubwa zaidi. Si lazima uwe karibu na nguruwe au unafuga na kula nguruwe ndio ufikiri unaweza kupatwa na ugonjwa huo, ukweli ni kuwa maambukizo ya homa ya mafua ya nguruwe kwa sasa ni kati ya mtu na mtu, au kwa Kiswahili kingine toka binadamu kwenda kwa binaadamu mwingine, hiyo inamanisha kuwa, sote tuko hatarini.
Dalili za homa ya mafua ya nguruwe
Kwa kawaida dalili za ugonjwa huu huwa sawa na ugonjwa wa kawaida wa mafua. Lakini pia kuwa baadhi ya watu huonyesha dalili mbaya zaidi au zinazotofautiana na mafua ya kawaida.
Iwapo mgonjwa atakuwa na homa kali zaidi ya sentigredi 30 au 100/F pamoja na moja ya dalili zifutazo, anaweza akawa amepatwa na homa ya mafua ya nguruwe na ni boda umuone daktari.
1. Maumivu ya mwili.
2. Kuumwa kichwa.
3. Mafua.
4. Mauvimu ya koo.
5. Kushindwa kupumua na kikohozi.
6. Kukosa hamu ya kula.
7. Mwili kuchoka sana kinyume cha kawaida.
8. Kuharisha na kutapika.
Ingawa ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe unaweza kuwapata watu wote lakini watu wafuatao wanakabiliwa na hatari zaidi ya kupatwa na ugonjwa huo:
 Kina mama waja wazito.
 Watu wenye magonjwa ya muda mrefu ambayo yamepelekea miili yao kuwa dhaifu kama vile kensa, magonjwa ya muda mrefu ya kifua, HIV n.k.
 Watoto wadogo walio chini ya miaka mitano.
 Wazee walio na umri wa zaidi ya miaka 65 na zaidi.
 Wagonjwa wenye matitizo ya asthma.
 Wagonjwa wanotumia dawa za kudhoofisha mfumo wa kulinda mwili au (immunosuppression).
…. Naam, usikose kujua namna ya kujikinga na kupatwa na ugonjwa huu hatari katika sehemu ya pili

No comments: