Thursday, November 12, 2009

Ongezeko la vifo vya UKIMWI nchini Afrika Kusini


Waziri wa Afrika wa Afrika Kusini amesema kwamba kiwango cha watu wanaofariki duniani nchini humo kimeongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kutokana na kuenea ugonjwa wa Ukimwi. Aaron Motsoaledi ameilaumu serikali iliyopita ya nchi hiyo wa Rais Thabo Mbeki akisema kwamba ilisababisha kupanda sana kiwango cha vifo nchini humo katika kipindi cha baina ya mwaka 1997 hadi 2008. Amesema karibu watu laki tatu walifariki dunia nchini Afrika Kusini mwaka 1997 ambapo mwaka 2007 idadi hiyo ilipanda na kufikia karibu watu laki 7 na 56 elfu. Waziri huyo wa afya wa Afrika Kusini ameongeza kuwa, kutokana na kuongezeka idadi ya vifo nchini humo, serikali ya hivi sasa imeamua kufanya marekebisho ya kimsingi katika siasa zake ili kupambana na ongezeko la ugonjwa hatari wa Ukimwi nchini humo. Idadi kubwa ya wahanga wa Ukimwi nchini Afrika Kusini ni vijana. Waziri wa Afya wa nchi hiyo anasema kwamba karibu asilimia 75 ya vifo vya watoto wadogo nchini humo vilitokea mwaka 2007 kutokana na ugonjwa wa Ukimwi. Hatua ya Waziri Aaron Motzoaledi ya kulaumu ongezeko la wahanga wa Ukimwi katika kipindi cha Urais wa Thabo Mbeki, kwa mara nyingine kunaonyesha hitilafu za wazi zilizopo baina ya Rais huyo wa zamani na Rais Jacob Zuma wa hivi sasa wa Afrika Kusini kuhusiana na namna ya kupambana na Ukimwi nchini humo. Itakumbukwa kwamba katika kipindi cha Urais wake, Thabo Mbeki alitilia shaka hata uhakika uliothibitishwa kielimu kwamba Ukimwi unasababishwa na virusi vya HIV. Hata Manto Msimang Waziri wa Afya wa serikali ya Thabo Mbeki aliwataka watu wenye virusi vya HIV nchini humo watumie mboga mboga badala ya dawa za kupambana na virusi hivyo. Alitoa mwito huo katika hali maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini walikuwa wakiendelea kufa kwa Ukimwi kutokana na ukosefu wa madawa. Hivi sasa na licha ya kuwa Afrika Kusini ina mradi mkubwa zaidi wa kupambana na Ukimwi duniani lakini bado inatathminiwa kwamba karibu watu milioni moja wanahitajia kutibiwa ugonjwa huo nchini humo.

No comments: