Tuesday, March 30, 2010

Ni wakati gani mazoezi hayaruhusiwi kwenye ujauzito?


Kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa na Chuo Kikuu Cha Marekani cha Masuala ya Uzazi na Magonjwa ya Wanawake, mama mjamzito haruhusiwi kufanya mazoezi iwapo atakuwa na matataizo yafuatayo:
• Ugonjwa wa moyo.
• Ugonjwa wa mapafu.
• Kizazi kisichojitocheleza au kitaalamu cervical insufficiency/cerclage.
• Mimba ya mapacha, mapacha wawili, watatu na kuendelea na iwapo ana hatari ya kujifungua mapema kabla ya muda kutimia.
• Kutokwa na damu kunakoendelea katika miezi mitatu ya pili na ya tatu ya mimba.





• Mfuko wa uzazi ulioko upande wa chini wa kizazi au placenta previa. Hasa baada ya wiki 26 ya mimba.
• Uwezekano wa kujifungua mapema kabla muda haujatimia.
• Iwapo chupa imevunjika.
• Kifafa cha mimba (preeclamsia)
• Shinikizo sugu la damu.
• Ukosefu mkubwa wa damu.
• Kutokwa na majimaji ukeni.
• Ongezeko la mapigo ya moyo, hata wakati wa mapumziko.
Mama mjamzito pia anatakiwa kuzingatia dalili zifuatazo wakati anapofanya mazoezi, na anashauriwa kuacha haraka kufanya mazoezi anapohisi kuwa na dalili hizo:
• Kutoka damu ukeni.
• Kuhisi kizunguzungu au kuzimia, au kukosa nguvu.
• Kukosa pumzi au pumzi kumbana.
• Maumivu ya kichwa.
• Maumivu ya kifua.
• Misuli kukosa nguvu.
• Miguu kuuma na kuvimba.
• Maimivu ya mgongo na kiuno.
• Kujisikia uchungu au dalili za kujifungua kabla ya muda.
• Kupungua harakati ya mtoto ( kupungua hali ya kupiga mtoto tumboni)

Monday, March 29, 2010

Umuhimu wa Mazoezi wakati wa Ujauzito


Kufanya mazoezi wakati wa ujauzito kuna umuhimu mkubwa kwa afya ya mama mjamzito mwenyewe na mtoto wake ambaye bado hajazaliwa. Wanawake wengi wanatambua umuhimu wa kula lishe bora, kuhudhuria kliniki, kuacha kuvuta sigara na kunywa pombe wakati wakiwa na mimba. Lakini si wanawake wengi wanaoelewa umuhimu wa kutumia muda wao kufanya mazoezi wakati wa ujauzito. Mazoezi yana umuhimu mkubwa kiafya wakati wa ujauzito kama ilivyo kabla ya ujauzito. Kufanya mazoezi wakati unapobeba mimba kunaleta faida kubwa wakati wa kujifungua. Wakati wa ujauzito ni muhimu kudhibiti ongezeko la uzito wa mama. Kwa kujishughulisha mama mjamzito na kuwa na harakati humsaidia awe na afya bora na kumsaidia aweze kupitisha kipindi cha uchungu na kujifungua kwa urahisi zaidi. Zaidi ya kumsaidia mama asiongeze uzito mkubwa wakati wa mimba, kufanya mazoezi humsaidia mama pia kurejea katika uzito wake wa kawaida kwa urahisi baada ya kujifungua kwa kawaida au kwa uparesheni. Kwa ujumla mama mjamzito kama ambayo anavyoshauri kula chakula bora na kuwa na afya nzuri wakati wa ujauzito, hivyo hivyo hushauriwa pia kuzingatia suala zima la kufanya mazoezi na kuchunga mwili wake usiongeze uzito mkubwa. Pia kufanya mazoezi huufanya mwili utoe mada ya endorphins, ambayo husaidia kumfanya mama asipate matatizo ya kifikra na msongamano wa mawazo (emotional stress na depression).
Zifuatazo ni faida anazozipata mama mjamzito iwapo atafanya mazoezi
1. Mazoezi hupunguza maumivu ya kichwa, kukosa choo na kuvimba mwili.
2. Mazoezi huongeza nguvu na kuupa mwili stamina.
3. Mazoezi hukufanya ujisikie vizuri na kukufanya uwe katika hali ya furaha.
4. Mazoezi hupunguza maumivu ya mgongo na huimarisha mifupa ya mgongo, makalio na mapaja na kuifanya iwe na uwezo wa kuvumulia vyema uzito wa mimba.
5. Mazoezi husaidia huongeza mtiririko wa damu na hewa katika ngozi na kuifanya ngozi yako ionekane nzuri.
6. Mazoezi hutayarisha mwili wako uwe tayari kwa ajili ya kuhisi uchungu kwa muda mfupi na kujifungua kwa urahisi.
7. Mazoezi hufanya mwili wako urudi upesi katika muonekano wake wa kawaida baada ya kujifungua.
8. Mazoezi humsaidia mama mjamzito apate usingizi kwa wepesi na kulala vyema.
Hata hivyo mama majamzito anashauriwa kabla ya kuanza kufanya mazoezi apate ushauri wa daktari na kuhakikisha kuwa hana matatizo ambayo kwa kufanya mazoezi pengine yakahatarisha mimba yake. Kwa wale waliokuwa wakifanya mazoezi kabla ya kubeba mimba wanashauriwa kuendelea na mazoezi yao lakini kwa kuwa waangalifu na kwa kiwango kidogo. Lakini kwa wale ambao walikuwa hawafanyi mazoezi hawaruhusiwi kufanya aina zote za mazoezi wakati wa ujauzito. Mazoezi kama vile kuogelea (kwa wale anaojua kuogelea), kutembea na yoga ni miongoni mwa mazoezi yanayoshauriwa wakati wa ujauzito. La muhimu ni mama mjamzito kutokaa tu na kujiepusha na uvivu na pengine kwa kufanya shughuli zake tu za kawaida ambazo mama huwa anazifanya nyumbani kila siku ikawa inatosha kuwa mazoezi yake na akaongeza kwa kutembea kidogo ( walking) kila jioni. Kutembea ni mazoezi salama na rahisi kwa kila mama mjamzito na yanayojulikana na kila mtu na kuweza kufanywa mahala popote. Ni bora kama unaweza fanya mazoezi na mwenza wako, rafiki au hata ndugu na jamaa yako ili uweze kufurahia zaidi mazoezi hayo. La muhimu ni kufuata maelekezo ya daktari kwani si kila mama mjamzito anaruhusiwa kufanya mazoezi wakati wa ujauzito kutokana na sababu tofauti. Baadhi ya mazoezi ambayo yana madhara kwa afya ya mama mjamzito na kwa mtoto hayaruhusiwi kabisa kufanywa wakati wa ujauzito. Mazoezi hayo ni kama vile mazoezi ya aerobic, ski, kupanda mawe, kupanda farasi na mengineyo kama hayo. Iwapo unaishi katika miji iliyoendelea basi unaweza kupata kwa urahisi vituo maalum kwa ajili ya kufanyia mazoezi mama wajawazito, na katika vituo hivyo kwa kawaida wakina mama wajawazito hukusanyika na kufanya mazoezi kwa pamoja. Lakini kama uko katika miji ambayo vituo hivyo hakuna usife moyo, na jitahidi kufanya mazoezi hayo peke yako huku ukishirikiana na familia yako.
Makala hii inaendelea...

Sunday, March 28, 2010

Vidonge vya uzazi havileti saratani - Mtaalam


MTAALAMU wa masuala ya uzazi wa mpango, wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Calista Simbakalia, amesema vidonge vya uzazi wa mpango havileti saratani ya uzazi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Simbakalia alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa mada katika semina ya kutambulisha uzinduzi wa mpango mkakati wa uzazi wa mpango utakaofanyika Machi 30, chini ya wizara hiyo kitengo cha Uzazi wa Mpango na Mtoto.
Alisema si kweli kuwa vidonge vya uzazi wa mpango husababisha ugonjwa wa saratani ya uzazi bali vidonge hivyo hutumika pia kwa matibabu ya ugonjwa huo.
“Kumekuwa na kundi kubwa la watu ambao wamekuwa wakiamini matumizi ya dawa hizo huleta saratani ya uzazi wakati ukweli ni kwamba zimekuwa zikisaidia kutibu ugonjwa huo.”
Simbakalia alisema kuwa mwanamke asiyetumia njia za uzazi wa mpango hubeba mimba kila wakati jambo linalomfanya muda mwingi autumie katika kulea watoto badala ya kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Alibainisha kuwa ubebaji mimba wa mara kwa mara humfanya mwanamke kuwa tegemezi sambamba na kuifanya familia husika kutopiga hatua za maendeleo.
“Mama atakapotumia uzazi wa mpango unamsaidia kutopata mimba ambayo hakuipanga; hivyo atatumia muda wake mwingi kufanya shughuli za kumuongezea kipato,” alisema.
Naye mratibu wa taifa wa shughuli za uzazi wa mpango nchini, Maurice Hiza, alisema uzazi wa mpango unasaidia kupunguza vifo kwa kina mama wajawazito sambamba na kuboresha afya ya mama na mtoto wake.
Alibainisha kuwa uzazi wa mpango pia huisaidia serikali kuboresha huduma za jamii kama elimu, miundombinu, huduma za afya ambazo zimekuwa zikilegalega kutokana na uwiano mdogo kati ya idadi ya watu na uwezo wa serikali.
Alisema wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamepanga kuwaelimisha wanaume ambao inadaiwa ndiyo kikwazo kikubwa cha kuwakubalia wake zao au wao wenyewe kutumia njia zinazotakiwa za uzazi wa mpango.
Aliongeza kuwa iwapo elimu ya uzazi wa mpango itayafikia makundi ya vijana wanaochipukia na wanaume wakaelewa dira ya taifa ya mpango mkakati wa kupunguza vifo vya kina mama hadi kufikia mwaka 2010 -2015 itafanikiwa kirahisi.

Monday, March 15, 2010

Kensa zinazoshambulia kizazi … sehemu ya kwanza


Kuna kensa mbalimali tofauti zinazoweza kushambulia sehemu mbalimbali za kizazi na mfuko wa uzazi. Lakini kensa ambayo inajulikana sana pengine kutokana na kuwepo vipimo vya kujua kama kensa hiyo ipo au la ni kensa ya mlango wa uzazi (cervical cencer) ambayo hushambulia mdomo au shingo ya kizazi. Kensa hiyo huweza kugunduliwa mapema na kwa urahisi baada ya wanawake kufanyiwa kipimo cha kupima kensa hiyo na pale inapoonekana kuna mabadiliko yasiyo ya kawaida katika seli za kizazi ambazo mwanzoni huwa bado hasijageuka kuwa kensa kamili. Mabadiliko ya mwanzo ya seli hizo kuelekea kwenye saratani huwa ni rahisi kutubiwa, suala ambalo limepelekea idadi ya wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa huo ipungue katika miaka ya hivi karibuni. Kensa nyingine inayowatokea sana wanawake ni kensa ya kizazi (uterine cancer) au kensa inayoshambulia mji wa mimba. Kensa hiyo hushambulia kuta za kizazi. Kensa ya kizazi kwa hakika ni kensa inayoshambulia mwili wa kizazi ambao umejengwa kwa tishu mbalimbai kutoka katika mlango wa uzazi hadi ndani ya kizazi chenyewe. Kensa ya kizazi mara nyingi huwapata wanawake wenye umri mkubwa ambao hedhi yao imeshakatika, na mara nyingi hushauriwa waondolewa kizazi. Wataalamu wanasema kwamba, suala muhimu linaloweza kufanikisha matibabu ya kensa ya mlango wa uzazi na ya kizazi ni kugunduliwa mapema magonjwa hayo. Kensa nyingine ambayo haishuhudiwi sana ni kensa inayoshambulia kizazi iitwayo Uterine Sarcoma, ambayo hushambulia misuli ya kizazi. Kensa hiyo hufananishwa zaidi na saratani nyinginezo zinazoshambulia misuli kuliko saratani za kizazi.
Si vibaya kujua yafuatayo kuhusiana na ugonjwa wa kensa:
Kensa ya matiti ndio kensa inayotokea zaidi duniani huku kensa ya korodani ikiwa inatokea kwa chache zaidi.
Hii ni katika hali ambayo kensa inayoongoza kwa kusababisha vifo vingi zaidi vya wanawake ni kesna ya kensa matiti huku kensa ya mapafu ikishika namba ya kwanza kwa kupelekea wanaume kufa kwa wingi.
Kati ya watu watatu mmoja anatabiriwa kupata kensa nchini Uingereza kwenye miaka ijayo.
Kensa ya matiti inaongezeka huku kensa ya mapafu ikitarajiwa kupungua kutokana na kupungua wafutaji sigara.
Usikose kufuatilia zaidi makala zijazo zinatakazojadili kensa mbalimbali.
Daima na tutunze afya zetu!

Saturday, March 13, 2010

Kula Pistachio ujikinge na kensa!


Pistachio zina uwezo wa kupambana na seli zinazosababisha kensa na zinaweza kuzuia seli zisiharibiwe na radikali huru na kusababisha saratani. Hayo yameelezwa na watafiti wa Ujerumani ambao wameshauri kwamba, kula pistachio kila siku kunaweza kupunguza hatari ya kupata kensa kwa kuongeza uzalishaji wa mada iitwayo gamma-tocopherol mwilini.
Suala hilo limeongezewa mashiko na uchunguzi mwingine wa Marekani ambao umesema kwamba, pistachio zina kiwango kikubwa cha gamma-tocopherol mada ambayo inatokana na Vitamin E inayoulinda mwili usipate satarani.
Pistachio ambazo zamani zilikuwa zikiliwa tu na familia tajiri hivi sasa baada ya watu kujua umuhimu wake wa kiafya zinaliwa na watu wote na wataalamu wa afya wameshauri watu wazitumie kwa wingi hasa kama (snack) asusa au kumbwe kwa Kiswahili sanifu.
 Zaidi ya faida hiyo iliyotajwa hapo juu, nyungu hizo zenye mvuto wa kipekee na ladha tamu zina madini ya Copper, Phosporus, Pottassium, Megnesium, na vitamin B6.
 Pistachio pia zimejaa ufumwele (fiber) na kama unatafuta snack yenye ufumwele wa kutosha uwapo kazini au safarini basi usisahau kubeba paketi ya pistachio.
 Kama hutaki kula vitu vyenye protini inayotokana na nyama, basi pistachio ndio jawabu lako kwani zitakupatia protini ya kutosha inayotokana na mimea.
 Pistachio pia zina mada ya caratenoids lutein na zeaxanthi ambazo husaidia kupunguza hatari ya kupata upofu wa uzeeni.
 Pistachio pia zina sterols inayotokana na mimea ambayo inaaminiwa kuwa hupunguza ufyonzaji wa cholestrol inayotakana na chakula. Hivi sasa sterols inayotokana na mimea huongezwa katika vyakula kutokana na faida yake hiyo.
Ili kukuwezesha mdau kula pistachio na kufaidika na lishe hiyo, kona ya afya inashauri uzitengeneza na kuzila kwa mitindo ifuatayo:
 Weka pistachio zilizopondwa au kukatwa katwa katika mtindi au cream cheese.
 Weka pistachio katika skonsi, vileja na hata keki.
 Jitahidi mara nne kwa wiki uwe umekula njugu 30 au gramu 18 za pistachio.
 Pistachio zisizokuwa na chumvi zinaweza kuliwa pamoja na vyakula kwa wale wasiokula nyama.
" Daima Tutunze Afya Zetu"

Mwanga wa jua unasaidia kuimarisha kinga ya mwili


Huku kwa muda mrefu ikiwa inaaminiwa kwamba Vitamini D inayotokana na mwanga wa jua inaimarisha mifupa, uchunguzi mpya umeonyesha kwamba mwanga wa jua pia una umuhimu mkubwa katika kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili na uwezo wake wa kukabiliana na magonjwa.
Uchunguzi huo umeeleza kwamba, seli zinazoshambulia maradhi za mfumo wa kinga ya mwili ambazo hujulikana pia kama 'T Seli" zinategemea sana Vitamin D ili kuzifanya zitekeleze kazi yake.
Carsten Geisler aliongoza uchuguzi huo amesema kuwa, wakati T seli zinapokutana na kidudu toka nje ya mwili, hufungua antena yake inayoitwa 'D receptor' ambayo inaitumia kwa ajili ya kusaka vitamin D. Wakati kunapokuwa hakuna vitamin hiyo inayotokana na jua suala ambalo hutokea kwa watu zaidi ya nusu duniani, seli hizo hushindwa kufanya kazi na kushindwa kufahamu tishio linalosababishwa na vijidudu vinavyosababisha maradhi.
Wataalamu wana matumaini kwamba uchunguzi huo mpya utawezesha kuandaliwa mazingira ya kuwekwa mikakati mipya kwa ajili ya kupambana na magonjwa katika siku zijazo.

Wednesday, March 10, 2010

Ujue ugonjwa wa kichocho na namna ya kujikinga na ugonjwa huo


Kichocho ni ugonjwa unaosababishwa na minyoo ambayo humpata mtu anapotumia maji yaliyo na vijidudu hivyo vya maradhi khususan katika nchi za kitropiki (yaani zenye hali ya joto jingi). Bilharzia ni jina la kimelea cha ugonjwa huu. Aina za minyoo au Chistosomes inayosababisha ugonjwa wa kichocho kikuu kinachomuathiri binadamu ni hii ifuatayo: Mosi, Chistosoma mansoni ambayo imeenea katika nchi 53 na kwenye maeneo kadhaa ya Afrika, Caribbean, mashariki mwa Mediteranean na Amerika ya Kusini. Aina ya Pili, ni Chistosoma japonicum/ Chistosoma mekongi, inayoathiri utumbo. Tatu Chostosoma intercalatum- inayojulikana kama bilharizia ya mkojo. Na nne ni ile ya Chistosoma haematobium , ambayo inaziathiri nchi nyingi za Afrika .Ugonjwa wa kichocho unahesabiwa kuwa ugonjwa wa pili unaonea kwa wingi zaidi katika nchi zenye joto jingi.
Viini vya ugonjwa wa kichocho vilivyokomaa huishi katika mishipa kwenye kibofu cha mkojo na utumbo. Kimelea cha kike hutaga mayai mengi ambayo hutoka kwa mtu aliyeathiriwa na kwenda kwenye maji wakati wa kukojoa au haja kubwa. Mayai yanapokuta maji huanguliwa na kutoa viluwiluwi, ambao hupenya na kuingia ndani ya konokono wa majini. Aidha viluwiluwi hawa hukuwa ndani ya konokono hao, kuongezeka na hatimaye kutoka. Itafahamika kuwa viluwiluwi hawa wana uwezo wa kupenya ndani ya ngozi ya mwanadamu na wakisha penya huingia hadi katika mishipa ya ini, ambako hukua na kukomaa. Baada ya hapo huingia katika mishipa ya kibofu cha mkojo na utumbo mpana. Vimelea hivi hutaga mayai kwa wastani wa miaka 3 na nusu, ns vinaweza kuongezeka zaidi. Mayai yanayotagwa katika kuta za utumbo mpana na kibofu husababisha madhara makubwa. Iwapo ugonjwa wa kichocho hautatibiwa ipasavyo, unaweza kusababisha matatizo ya ini, utumbo mpana na ugonjwa wa figo. Aidha maambukizo yake yanaweza kuenea katika uti wa mgongo na hata wakati mwingine kuathiri ubongo. Karibu watu milioni 600 duniani wako katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa kichocho.
Hebu sasa tuangalie ugonjwa wa kichocho unasababishwa na nini?
Masuala au matatizo yafuatayo yanapelekea watu kupatwa au kuambukizwa ugonjwa wa kichocho:
Umaskini uliokithiri, ufahamu mdogo kuhusu ugonjwa huo, ukosefu au uchache wa suhula za afya kwa jamii, usafi duni wa mazingira tunayoishi n.k.. Ugonjwa huo pia huweza kuenezwa kutoka kwa watu wanaohama kutoka katika nchi nyingine ambazo ugonjwa huo umeenea.
Katika siku za awali wakati vimelea vya kichocho vinapoingia katika mwili wa mwanadamu, kijipele au swimmer's itch hujitokeza. Aidha baada ya kupita mwezi mmoja au miwili, mtu aliyekwishaambukizwa huanza kujisikia hali ya kuchoka, homa, homa ya baridi, huwa na kikohozi kikavu, maumivu ya misuli, maumivu ya tumbo, kuhara, na hukojoa mkojo ulio na damu. Kipindi hiki huenda sambamba na ukuaji wa minyoo katika mwili wa mwanadamu na hujulikana kama homa ya Katayama. Kuweko damu katika mkojo ni dalili tosha ya kuonyesha kwamba mtu huyo amepatwa na kichocho cha mkojo au kitaalamu hujulikana kama urinary bilharzias. Na iwapo mgojwa hatatibiwa, anaweza kupata madhara mengine makubwa katika ini na bandama.
Kichocho huaathiri zaidi makundi yafuatayo:
Watu wazima wanaojishughulisha na kilimo na wale walio katika sekta ya uvuvi.
Kichocho kinachoathiri kibofu cha mkono huwaathiri watoto milioni 66 katika zaidi ya nchi 54 duniani.
Kidha katika ameneo mengi watoto waliona umri wa kati ya miaka 10 na 14 wanaambukizwa ugonjwa wa kichocho. Kimsingi maradhi haya huathiri ukuaji wa watoto na mahudhurio yao shuleni.
Mtu anatakiwa kumuona daktari iwapo atakuwa amesafiri katika eneo ambalo lina maambukizo ya kichocho, iwapo ngozi yake itagusana na maji yenye vimelea vya ugonjwa huo na iwapo atakojoa mkono ulio na damu.
Ugonjwa wa kichocho unaweza kuzuiwa kwa urahisi iwapo kanuni za kiafya zitazingatiwa. Hata hivyo hadi sasa hakuna chanjo iliyopatikana ya kudhibiti ugonjwa huo. Si maji yote ni salama kwenye maeneo yaliyo na ugonjwa huu. Sehemu hatari zaidi za ugonjwa huo ni maeneo kama vile kingo za maziwa, mito na mabwawa ambapo maji yametuama na kuna uoto wa mimea. Sehemu salama ni kama vile katika fukwe za bahari na zile zenye mawimbi ambazo si rahisi kukuta konokono wa majini. Mabwawa ya kuogelea ni salama iwapo yatanyunyiziwa dawa ya klorini.
Ili kuweza kukabiliana na kuzuia maambukizo ya ugonjwa wa kichocho, masuala yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:
 Miongoni mwao ni kuacha kuoga kwenye maji yaliyotuama kama vile ya kingo za mabwawa, mito n.k.
 Hakikisha kuwa maji ya kunywa ni salama kwa kuyachemsha na kuyachuja ili kuuwa vijidudu maradhi.
 Unaweza pia kuchemsha maji ya kuoga angalau kwa nyuzi joto 65 kwa muda wa dakika tano.
 Maji yaliyohifadhiwa kwenye tanki kwa muda usiopungua masaa 48 ni lazima yawe salama kwa ajili ya kuogea.
 Kama unalima, unashauriwa kuvaa mabuti marefu ya mpira.
Ni vyema tujue kuwa, mtu anapaswa kumuona daktari baada ya kuwa na dalili za ugonjwa na yeye ndiye atakayemuainishia dawa za kutumia. Ni matarajio yetu kuwa iwapo tutafuata kanuni na misingi yote hiyo ya kiafya hapo juu, basi tutafanikiwa kushinda vita dhidi ya maradhi ya kichocho.
Daima tutunze afya zetu!

Monday, March 8, 2010

Ulimwengu waadhimisha siku ya wanawake huku wanawake wakikabiliwa na matatizo mengi


Leo ni tarehe 8 Machi ambayo ni siku ya Kimataifa ya Wanawake. Kwanza nashukua fursa hii kuwapongeza wanawake wote ulimwenguni katika siku yenu hii. Ulimwengu unaadhimisha siku ya wanawake katika hali ambayo ingawa karne nyingi zimepita na ustaarabu unaonekana karibu katika mataifa yote duniani lakini mwanamke katika kila jamii bado anazungukwa na matatizo mengi. Ingawa maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kitiba yanaendele kushuhudiwa duniani kote lakini mwanamke bado ni mhanga wa mauaji ya holela, vita, uchumi mbovu, siasa za kibabe, ukosefu wa usawa, huduma bora katika jamii na unyanyaswaji wa kijinsia. Hilo limewekwa wazi na ripoti imetolewa leo na Helen Clark Mkuu wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) katika mji mkuu wa India, New Delhi kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mwanamke. Bi. Clark amesema kuwa eneo la Kusini mwa Asia ndilo hasa linaloshuhudiwa kuwa na vitendo vinavyodhihirisha pengo kubwa la kijinsia hata zaidi ya nchi za Afrika zilizo chini ya jangwa la Sahara. Aidha amesema kuwa usawa wa kijinsia unasaidia sana katika maendeleo ya mwanadamu na kwamba kutoshirikishwa kwa wingi wanawake katika nguvu kazi kunaleta athari mbaya katika ukuaji wa maendeleo. Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa pia huku ikiashiria nchi za Pakistan, Baghladesh, China, India, Korea Kusini na Nepal imeeleza kwamba, bara la Asia lina idadi kubwa zaidi ya watoto wa kiume wanaozaliwa ikilinganishwa na wanawake duniani, huku utoaji mimba kwa ajili ya kuchagua jinsia ya mtoto na mauaji ya watoto wachanga yakisababisha kuwepo na upungufu wa wanawake karibu milioni 96 katika nchi hizo.
Zaidi ya hayo siku chache zilizopita Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Ukimwi (UNAIDS) ulitangaza kuwa Ukimwi ndio ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake walio katika umri wa kuzaa katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kukomesha machafuko na unyanyasaji wa kijinsia unaofanyika dhidi ya wanawake ndio njia muhimu ya kukabiliana na ugonjwa huo. UNAIDS imesema kuwa, karibu asilimia 70 ya wanawake katika maeneo mbalimbali duniani hasa katika nchi za Kusini mwa Afrika wameripotiwa kufanya ngono zembe au mapenzi yasiyokuwa salama.
Dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya Mwanamke huku wanawake wakishuhudia ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia katika sehemu nyingi duniani. Wanawake wanabakwa kwa makundi katika maeneo yenye vita barani Afrika Afrika kama Ivory Coast, Congo DRC, Guinea Conakry na kwengineko, huku upande wa kisiasa wakiwakilishwa na kiwango kidogo katika serikali na sehemu muhimu za utoaji maamuzi za jamii. Ingawa demokrasia inaonekana kuimarisha na usawa ukipigiwa nara kila mahala, lakini viongozi na marais wanawake duniani bado hata hawafiki idadi ya vidole vya mikono duniani kote. Nafasi ya mama imezidi kushuka huku katika nchi nyingi nafasi ya mwanamke katika jamii bado ni ndogo na isiyoridhisha.
Upande wa tiba na afya, wanawake wanakufa kwa makumi kila uchao kutokana na maradhi yanayoweza kutibika, ukosefu wa huduma muhimu wakati wa ujauzito na kujifungua, lishe dhaifu na umasikini huku wakiwa ndio wenye nafasi kubwa ya ulezi wa jamii.
Mila na desturi zilizopitwa na wakati za baadhi ya jamii kama ukeketaji, kuridhi wajane, kuoa wake kadhaa bila kuwa na uwezo wa kuwangalia, uchawi na kadhalika vkiendelea kumfanya mwanamke kuwa muhanga na kupata magonjwa mbalimbali yanayotibika na yasiyotibika. Utoaji mimba usio salama na kukosa gharama za matibabu nayo ni baadhi ya matatizo mengine yanayogharimu maisha ya wanawake kila siku duniani kote.
Hivyo huku tukiadhimisha au kusherehekea siku ya Kimataifa ya Wanawake inapasa pia tukae chini na kuangalia ni vipi tunaweza kutatua matatizo ya wanawake duniani kote na hasa katika nchi zinazoendelea za Bara la Afrika.
Kona ya Afya kwa mara nyingine inawahusia wanawake wote ulimwenguni wazijali na kuzitunza afya zao.

Sunday, March 7, 2010

Kiungulia cha ujauzito na namna ya kukiepuka


Kiungulia cha ujauzito au HeartBurn kwa kimombo ni miongoni mwa matatizo yanayowapata wanawake wengi wanapobeba mimba. Kiungulia ni hali inayopelekea mtu ajihisi kuungua au kuwaka moto sehemu ya katikati mwa kifua. Tatizo hilo huwapata wajawazito mara nyingi katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito, lakini pia wapo wakina mama wajawazito wanaopatwa na kiungulia miezi ya mwanzoni ya mimba. Ili kuelewa namna ya kuzuia kiungulia kisitokee ni bora kwanza tufahamu kiungulia kinasababishwa na nini wakati wa mimba. Kiungulia hutokea wakati kiwambo au valvu kilichopo kati ya tumbo na umio (esophagus) kinapolegea na kushinda kuzuia asidi ya tumbo isipenye na kurejea katika umio. Mimba huongeza kiungulia kwa sababu homoni ya progesterone hulegeza kiwambo hicho. Hivyo asidi inayozalishwa tumboni hasa baada ya kula hurejea katika umio na kuleta kiungulia. Kiungulia hutokea katika miezi mitatu ya mwisho ya mimba kutokana na fuko la uzazi kuwa kubwa na kubana utumbo mdogo na tumbo. Mbano huo wa tumbo hupelekea vilivyoko tumboni kusukumbwa upande wa umio au esophagus.
Kwa kawaida kutokula vyakula vyenye kusababisha asidi na gesi tumboni, hupunguza kiungulia. Vyakula hivyo ni kama vinywaji vyenye gesi ya carboni, vyakula vyenye kiasi kikubwa cha asidi kama vile jamii ya maharagwe kama maharagwe, kunde, mbaazi n.k, nyanya, vyakula vyenye viungo, matunda kama machungwa na juisi ya machungwa, chocolates, vyakula vyenye mafuta mengi, grape fruit na hata kitunguu swaumu. Lakini pia inategemea mtu na mtu inabidi ujichunguze na kuona ni vyakula gani ukila unapata kiungulia na gesi.
Zifuatazo ni njia za kujiepusha na kiungulia:

1. Kutumia baadhi ya dawa salama zinazozuia kiungulia na gesi wakati wa ujauzito. Kwa nchi zetu za Afrika Mashariki sote tunaifahamu dawa iitwayo Magnesium ambayo husaidia kuondoa tatizo hilo. Kama upo nchi nyinginezo pia natumaiani unaweza kupata dawa hiyo kwa msaada wa daktari wako. (Muhimu ni kupata ushauri wa daktari utumie dawa gani ya kuondoa heartburn au kiungulia ambayo ni salama wakati wa ujauzito).
2. Hakikisha unakula kiasi kidogo cha chakula na usile ukashiba sana. Kwa kuwa mama mjamzito huwa anasikia njaa mara kwa mara na anahitajia kula vyema ili aujenge vizuri mwili wake na watoto, basi ni bora chakula chake ukigawe katika sehemu kadhaa ndogo, na ale mara kadhaa, badala ya kula sana wakati mmoja. Suala hilo litafanya tumbo lake lisijae na kusaidia kuzuia asidi isipande juu ya tumbo na kusababisha kiungulia na gesi.
3. Jitahidi usinywe maji mengi sana baada ya chakula au wakati wa kula, kwani husaidia kuzalisha asidi tumboni kwa haraka na kuleta kiungulia.
4. Unaweza kula ubani au chewing gum baada ya kula, kwani ubani kutengeneza mate na mate hupunguza asidi.
5. Jitahidi usilale tu mara baada ya kula, subiri kama nusu saa hivi ipite ndio ulale. Unapolala usilaze kichwa moja kwa moja bila mto, bali tumia mito kuegemeza kichwa ili kuzuia asidi isirejee juu ya tumbo na kusababisha kiungulia.
Unapohisi kiungulia kunywa glasi ya maziwa au kula mtindi.
Na kama hali hiyo haijatoweka kunywa maji ya moto glasi moja yaliyowekwa kijiko kimoja cha asali.

Wednesday, March 3, 2010

Mama wajawazito wenye kuongezeka uzito sana wana hatari ya kupata kisukari cha mimba


Kina mama wenye mimba ambao huongezeka uzito kwa kasi katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito wanakabiliwa na hatari ya kupata kisukari cha mimba (gestational diabetes). Kifafa cha mimba ni hali ambayo wanawake ambao huko nyuma hawakuwa na ugonjwa wa kisukari huonekana kuwa na ongezeko la sukari katika damu kwa mara ya kwanza wakati wa ujauzito. Kwa mujibu wa uchunguzi mpya, mama wajawazito ambao wataongeza uzito wa gramu 403.70 kwa wiki wako katika hatari ya kupata kisukari cha ujauzito zaidi ikilinanishwa na wale watakaoongeza uzito wa chini ya gramu 272.15 kwa wiki. Bi. Monique Hedderson aliyeongoza uchunguzi huo amesema kuwa, ongezeko kubwa la mafuta ya mama mwanzoni mwa mimba kunaweza kukaathiri kwa kiasi kikubwa tishu za mwili na kuzifanya zisikubali insulin, jambo ambalo taratibu husababisha kisukari cha ujauzito. Kwa ajili hiyo wataalamu wameshauri kwamba, wakina mama wenye mimba hasa wale wanene na wenye uzito mkubwa wanapaswa wajiepushe na kuongezeka uzito mwanzoni mwa mimba ili wasipwatwe na kisukari cha mimba.
Sio vibaya kutambua kwamba, asilimia 4 ya kina mama ambao watapata kisukari wakati wa ujauzito wanakabiliwa na hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari baadaye maishani mwao, hiyo ikiwa ni pamoja na watoto wao. Kisukari cha ujauzito kina dalili kadhaa lakini kwa kawaida huainishwa kwa vipimo (screening) vinavyochukuliwa wakati wa ujauzito.

Monday, March 1, 2010

Kikombe kimoja cha kahawa kwa siku chapunguza hatari ya ugonjwa wa moyo


Mbali na faida kemkem tunazozijua zinazopatikana kwenye kahawa, utafiti mpya umesema kwamba kunywa kikombe kimoja tu cha kahawa kwa siku kunapunguza hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo. Utafiti huo uliotolewa katika Kongamano la Jumuiya ya Mshituko wa Moyo la Kimataifa nchini Marekani, umeeleza kwamba kunywa kikombe kimoja cha kahawa ya kawaida na isiyokuwa na kafeini kila siku huzuia kupatwa na mshituko wa moyo kwa asilimia 30. Hata hivyo wataalamu wameonya kuwa kutumia sana kinywaji hicho matokeo yake huweza kuwa kinyume.
Tafiti za huko nyuma pia zilionyesha kuwa, kunywa kila siku kahawa kunaweza kumzuia mtu asipate kisukari aina ya pili na ugonjwa wa akili.
Mpenzi mdau baada ya kufahamu hayo, nimeonea nichukue fursa hii kuelezea baadhi ya faida za kahawa. Mbali ya kawaha kuwa kinywaji murua ambacho kinaweza kukufanya uchangamke asubuhi baada ya kuamka, au kwa wale kina yakhe wanaopenda kuburudika kwa kunywa kahawa kwa kashata vijiweni au kando ya barabara huku wakipiga gumzo, kinywaji hicho kina faida kemkem kiafya
1. Wataalamu wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Harvard cha Marekani wamegundua kuwa kunywa kahawa kunazuia kupatwa na ugonjwa wa kibofu nyongo (gall bladder) au kuzuia mawe katika nyongo (gall stones).
2. Kahawa inazuia kupatwa na ugonjwa wa Alzheimer au kusahau hasa uzeeni.
3. Kahawa ina anti-oxidants ambazo hupambana na seli ambaya zinazosabisha saratani.
4. Kahawa hulichangamsha tumbo na kulifanya lifanye kazi vyema na kuzuia matatizo ya kukosa choo. (Bowel stimulant and a laxative).
5. Kahawa huongeza uwezo wa ufahamu wa akili.
6. Kahawa huuzuia ugonjwa wa figo.
7. Na kahawa pia huzuia ugonjwa wa uvimbe wa viungo hasa vikononi na miguuni au gout.
Lakini wataalamu wanatutahadharisha kwamba ingawa kunywa kahawa kuna faida nyingi kama tulivyoona hapo juu lakini haifai kunywa kahawa kwa wingi kila siku. Kwani kila kitu kinachotumiwa sana badala ya kuwa na faida kinaweza kutuletea madhara.
Si vibaya kujua kwamba mmema wa kahawa ambayo ni maarufu uliwenguni kote uligunduliwa mara ya kwanza katika nchi za Yemen, Saudi Arabia na kaskazini mashariki mwa Ethiopia na kwa mara ya kwanza zao hilo lilikuwa likilimwa na kutumiwa sana katika nchi za Kiarabu.