Monday, March 8, 2010
Ulimwengu waadhimisha siku ya wanawake huku wanawake wakikabiliwa na matatizo mengi
Leo ni tarehe 8 Machi ambayo ni siku ya Kimataifa ya Wanawake. Kwanza nashukua fursa hii kuwapongeza wanawake wote ulimwenguni katika siku yenu hii. Ulimwengu unaadhimisha siku ya wanawake katika hali ambayo ingawa karne nyingi zimepita na ustaarabu unaonekana karibu katika mataifa yote duniani lakini mwanamke katika kila jamii bado anazungukwa na matatizo mengi. Ingawa maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kitiba yanaendele kushuhudiwa duniani kote lakini mwanamke bado ni mhanga wa mauaji ya holela, vita, uchumi mbovu, siasa za kibabe, ukosefu wa usawa, huduma bora katika jamii na unyanyaswaji wa kijinsia. Hilo limewekwa wazi na ripoti imetolewa leo na Helen Clark Mkuu wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) katika mji mkuu wa India, New Delhi kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mwanamke. Bi. Clark amesema kuwa eneo la Kusini mwa Asia ndilo hasa linaloshuhudiwa kuwa na vitendo vinavyodhihirisha pengo kubwa la kijinsia hata zaidi ya nchi za Afrika zilizo chini ya jangwa la Sahara. Aidha amesema kuwa usawa wa kijinsia unasaidia sana katika maendeleo ya mwanadamu na kwamba kutoshirikishwa kwa wingi wanawake katika nguvu kazi kunaleta athari mbaya katika ukuaji wa maendeleo. Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa pia huku ikiashiria nchi za Pakistan, Baghladesh, China, India, Korea Kusini na Nepal imeeleza kwamba, bara la Asia lina idadi kubwa zaidi ya watoto wa kiume wanaozaliwa ikilinganishwa na wanawake duniani, huku utoaji mimba kwa ajili ya kuchagua jinsia ya mtoto na mauaji ya watoto wachanga yakisababisha kuwepo na upungufu wa wanawake karibu milioni 96 katika nchi hizo.
Zaidi ya hayo siku chache zilizopita Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Ukimwi (UNAIDS) ulitangaza kuwa Ukimwi ndio ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake walio katika umri wa kuzaa katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kukomesha machafuko na unyanyasaji wa kijinsia unaofanyika dhidi ya wanawake ndio njia muhimu ya kukabiliana na ugonjwa huo. UNAIDS imesema kuwa, karibu asilimia 70 ya wanawake katika maeneo mbalimbali duniani hasa katika nchi za Kusini mwa Afrika wameripotiwa kufanya ngono zembe au mapenzi yasiyokuwa salama.
Dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya Mwanamke huku wanawake wakishuhudia ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia katika sehemu nyingi duniani. Wanawake wanabakwa kwa makundi katika maeneo yenye vita barani Afrika Afrika kama Ivory Coast, Congo DRC, Guinea Conakry na kwengineko, huku upande wa kisiasa wakiwakilishwa na kiwango kidogo katika serikali na sehemu muhimu za utoaji maamuzi za jamii. Ingawa demokrasia inaonekana kuimarisha na usawa ukipigiwa nara kila mahala, lakini viongozi na marais wanawake duniani bado hata hawafiki idadi ya vidole vya mikono duniani kote. Nafasi ya mama imezidi kushuka huku katika nchi nyingi nafasi ya mwanamke katika jamii bado ni ndogo na isiyoridhisha.
Upande wa tiba na afya, wanawake wanakufa kwa makumi kila uchao kutokana na maradhi yanayoweza kutibika, ukosefu wa huduma muhimu wakati wa ujauzito na kujifungua, lishe dhaifu na umasikini huku wakiwa ndio wenye nafasi kubwa ya ulezi wa jamii.
Mila na desturi zilizopitwa na wakati za baadhi ya jamii kama ukeketaji, kuridhi wajane, kuoa wake kadhaa bila kuwa na uwezo wa kuwangalia, uchawi na kadhalika vkiendelea kumfanya mwanamke kuwa muhanga na kupata magonjwa mbalimbali yanayotibika na yasiyotibika. Utoaji mimba usio salama na kukosa gharama za matibabu nayo ni baadhi ya matatizo mengine yanayogharimu maisha ya wanawake kila siku duniani kote.
Hivyo huku tukiadhimisha au kusherehekea siku ya Kimataifa ya Wanawake inapasa pia tukae chini na kuangalia ni vipi tunaweza kutatua matatizo ya wanawake duniani kote na hasa katika nchi zinazoendelea za Bara la Afrika.
Kona ya Afya kwa mara nyingine inawahusia wanawake wote ulimwenguni wazijali na kuzitunza afya zao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment