Monday, September 28, 2009

USAFI WA MWILI WA WATOTO NA UMUHIMU WAKE


Makala hii inahusu usafi wa mwili na umuhimu wake kwa watoto. Natumai kuwa mtanufaika nayo.
Wazazi na walezi wanaweza kuwa na nafasi kuu na muhimu katika makuzi na usafi wa mtoto, masuala ambayo atakuwa nayo katika maisha yake ya kila siku. Kitendo cha kumfunza mtoto kuhusu usafi wa mwili ni njia bora kabisa ya kumuepusha na maambukizo na maradhi mbalimbali. Ni jukumu la mzazi au mlezi kumfunza mtoto misingi sahihi ya usafi wa mwili wakati mtoto akiwa na umri mdogo kabisa, jambo ambalo litamsaidia mtoto huyo na familia yake katika maisha yao ya baadaye. Misingi ya usafi inapaswa kufundishwa na kuwa sehemu moja ya maisha ya kila siku ya mtu, na pia kuwa njia bora ya wazazi kuwafunza watoto wao kuhusu usafi wa miili yao, kwanza kabisa kwa wazazi hao kuwa mfano mbele ya watoto. Maambukizo ya magonjwa hupungua miongoni mwa watoto wakiwa mashuleani, kwenye maeneo wanayochezea na kadhalika, iwapo watakuwa wamefunzwa namna ya kujilinda na maradhi kwa kuweka miili yao safi na kwa kufuata kikamilifu kanuni za afya kila siku. Mambo ya kuzingatia katika usafi wa mwili wa mtoto yako mengi, lakini hapa nitaorodhesha kwa kifupi haya yafuatayo: Usafi wa Kinywa. Meno na kinywa vyote vinapaswa kuwa visafi wakati wote ili kuzuia magonjwa ya meno na fizi. Aidha usafi wa meno kwa mtoto ni muhimu ili kuzuia kuoza na kuvunjika kwa meno akiwa na umri mdogo. Upigaji mswaki wa mara ka mara, yaani kabla ya kifungua kinywa na baada ya chakula na kabla ya kulala usiku unashauriwa kwa watoto. Upigaji mswaki baada ya kula vyakula vyenye sukari pia ni muhimu kwa watoto, ili kuzuia meno kuoza na harufu mbaya. Pili, uoshaji mikono ni jambo linalopasa kuzingatiwa sana kwa watoto, baada ya kutoka msalani, kabla ya kula au kushika takataka au vitu vingine vichafu, kushika wanyama n.k. Kitendo cha kuosha mikono sio tu ni muhimu kwa watoto, bali hata kwa watu wazima. Uoshaji mikono ni muhimu kwa ajili ya kuzuia kupatwa na magonjwa mbalimbali, ambayo huweza kupatikana iwapo kanuni sahihi za usafi wa choo hazizingatiwi. Wakati mtoto anapofikia umri wa kwenda shuleni au kwenye shule ya chekechea, anatarajiwa kuwa na uwezo wa kutumia choo na kusafisha mikono yake mwenyewe baada ya kutoka msalani bila ya kusimamiwa na mtu.
Maambukizo ya fungus za miguuni na kichwani pia yanaweza kuzuilika iwapo uoshaji mikono sahihi utafuata. Watoto wanapaswa kuosha vizuri mikono yao, yani kati ya vidole na chini ya kucha, na ikiwezekana tumia brashi kusafisha mikono ya watoto. Ukaushaji vizuri wa mikono na vidole vile vile ni muhimu ili kuzuia maambukizo ya fungus. Watoto nao wanapaswa kuelewa umuhimu wa jambo hilo.
Usafi wa mwili unajumuisha pia usafi wa kucha. Wazazi wanapasa kuwakataza watoto tabia ya kutafuna kucha, kwani kucha za watoto mara nyingi huwa chafu na rahisi kubeba vijidudu maradhi. Kitendo cha kukata kucha za mtoto kitasaidi kupunguza kiwango cha vimelea vya maradhi vilivyoko chini ya kucha.
Tukiangalia usafi wa nywele tunaona kuwa, nywele za mtoto zinatakiwa kuwa fupi kama ni za kuchana na kama ni ndefu zinapaswa kusukwa mara kwa mara na kusafishwa vizuri kwa kutumia maji na sabuni au shampoo. Hii itasaidia kupunguza ringworm au chawa wa kichwani iwapo nywele zitakuwa chafu na kutooshwa vizuri. Watoto pia wanapaswa kushajiishwa kusafisha mikono yao kabla ya chakula, hii ni kwa sababu kitendo hicho kitasaidia kuzuia maambukizo ya magonjwa yanayoweza kuathiri mfumo wa chakula, wa kupumua na viungo vingine vya mwili. Nguo za mtoto pia ni lazima ziwe safi wakati wote , bila ya kusahau soksi, viatu na mahali anapolala. Mto anatakiwa kuvaa soksi kavu zisizo na unyevunyevu, ili kuzuia kuzaliana kwa fungus za miguuni. Avae viatu visivyobana, kama ni msimu wa joto mpatie viatu vilivyo wazi vyenye kupitisha hewa, mbadilishie mashuka yake anayolalia mara yakichafuka na kukifanya chumba au mahali anapolalia kuwa mahali safi na salama kwa afya yake. Mtengee mtoto taulo lake pekee yake, ili kuzuia maambukizo mbalimbali kama vile ya ngozi na kadhalika. Kwa kufanya hivyo ni matumaini yetu kuwa tutawaepusha watoto wetu na milipuko mbalimbali ya magonjwa.

No comments: