Thursday, March 26, 2009

Kiungulia au Heartburn


Kiungulia au Heartburn kwa kimombo, ni miongoni mwa mabadiliko ya ujauzito yanayowatokea baadhi ya akina mama. Tatizo hilo huwapata baadhi ya wakinamama wakati wa ujauzito, kama mabadiliko ya kimwili ya kawaida.
Ni wazi kuwa wanawake wengi hulalamikia kiungulia wakati wa ujauzito. Kiungulia hicho kinachompata mama akiwa na mimba ni wazi kuwa, ni mojawapo ya athari za kawaida kabisa zinazosababishwa na mimba. Kwa kawaida kiungulia hicho humpata mama mjamzito baada ya kula chakula. Mama anapopatwa na kiungulia, kuhisi kuchomeka au moto katika koo au kifuani mwake. Kiungulia kinaweza kutokea wakati wowote, lakini hudhihirika zaidi katika miezi mitatu ya mwisho hadi minne ya ujauzito. Kuna baadhi ya akinamama pia ambao hupatwa na kiungulia na huhisi kama vile wana uvimbe kwenye koo au kifuani. Kivyovyote vile, kiungulia kinakera na tatizo ambalo linaweza kupunguzwa na kumpatia mama nafuu.
Sababu kadhaa au masuala tofauti yametajwa kuwa yanasababisha kiungulia kwa mama mjamzito. Mojawapo ya sababu za kimsingi zinazomsababishia mama mjamzito kiungulia hicho ni mabadiliko ya homoni. Homoni hizo khususan progesterone, hulegeza valve yaani vali za tumbo au vilango tumbo ambavyo kwa kawaida huzuia asidi ya tumboni kurudi kwenye umio au esophagus. Kwa hiyo, mamamjamzito hupatwa na kiungulia yaani huhisi kuchomeka kooni au kifuani, iwapo vali hizo zitashindwa kuizuia asidi hiyo. Njia rahisi ya kupunguza tatizo hilo, ni kwa mama kugawa mlo wake wa siku nzima katika sehemu sita. Yaani badala ya kula mara tatu kwa siku kama ilivyozoeleka, mama mjamzito agawe mlo wake wa siku katika awamu sita. Kwa njia hiyo mamamjamzito atatakiwa kula mlo wake mara sita kwa siku kidogo kidogo bila ya kupoteza virutibisho muhimu. Uyabisi wa tumbo na kiungulia pia ni mambo yanayotokea mara kwa mara wakati mimba inapokuwa na miezi sita na kuendelea. Masuala haya hutokea pale mfuko wa uzazi wa mama unaokuwa unapozidisha presha kwenye matumbo pamoja na tumbo.
Kwa kuzingatia kuwa mama mjamzito hawezi kurekebisha kiwango chake cha homoni au kuuzuia mfuko wake wa uzazi kukua, kuna njia nyepesi kabisa ambazo mama anaweza kuzifuata na kumsaidia kupunguza kero ya kiungulia na kwa wengine kukizuia kabisa. Hatua hizo ni kama zifuatazo: Kwanza mama mjamazito anashauriwa kula milo midogo midogo kadhaa kwa siku nzima, ikiwa na maana kuwa, anaweza kula mara sita badala ya mara tatu. Anapaswa kujiepusha na vyakula vyenye viungo vingi au vyenye mafuta mengi. Anashauriwa mara zote kula chakula kwa uchache saa moja labla ya kuingia kitandani wakati wa usiku. Mama mjamzito hapaswi kulala muda mfupi baada ya kula chakula, kwani kitendo hicho kinaweza kuchangia kiungulia. Hatua nyingine za kufuata ni kama vile mama mjamzito anapaswa kunywa maziwa mengi au mtindi kama ana uwezo huo iwapo kiungulia kinamsumbua mara kwa mara, ajiepushe na unywaji maji mengi wakati wa kula chakula, ambao unaweza kujaza tumbo lake na kumsababishia kiungulia. Mama mjamzito ajiepushe na unywaji wa vinywaji vyenye caffeine na avae nguo pana zisizobana kifuani. Mbali na njia hizo, mama mjamzito anashauriwa kulalia upande wake wa kulia kwa kutumia mito kadhaa huku shingo ikiwa imeinuka, inasaidia pia iwapo hatua zote hizo hazitamfaa mamamjamzito katika kukabiliana na kiungulia alichonacho, anashauriwa kumona daktari kwa ushauri zaidi. Dawa za antiacid zinazopunguza asidi kame vile zile zenye mchangiko wa aluminium, magnesium na calcium zinashauriwa kutumiwa kwa kufuata maagizo ya daktari. Mama anaweza kutumia dawa hizo zikiwa katika muundo wa vidonge au majimaji.
Na sasa tuangalie dondoo moja muhimu ifuatayo.
*** Mama mjamzito anayetaka kusafiri kwenda sehemu moja au nyingine anapaswa kufanya mambo yafuatayo: Kwanza kabisa anatakiwa kuchukua tahadhari zote. Tahadhari hizo ni kama vile kujikinga na ugonjwa wa malaria ambao huzidisha idadi ya vifo vya akinamama wajawazito. Mama mjamzito anashauriwa kutosafiri kwenye maeneo yenye malaria. Aidha mama anatakiwa kuwa makini na kula vyakula vyenye sumu wakati akisafiri. Kujiepusha huko ni kwa kuzingatia usafi wake wa vyakula wakati akiwa safarini, awe makini wakati wa ulaji vyakula. Kwa wale wanaosafiri nje ya nchi, baadhi ya mashirika ya ndege, mabasi nk. Hayaruhusu kusafiri mama mjamzito akiwa na mamba ya zaidi ya wiki 35, kwa hiyo wanapswa kumuona dakatri na kupata ushauri kabla ya kuanza safari. Mama hao pia wanashauriwa kutojishughulisha na kazi zinazoweza kumdhuru yeye pamoja na mtoto aliyetumboni kama vile kufanya kazi nzito, kubeba mizigo nk. Akiwa safarini, mama mjamzito anatakiwa kuripoti mara moja dalili au alama hatari kama vile kuvuja damu, kutokwa na tishu au mabonge ya damu, maumivu ya tumboni, kuvunjika kwa chupa, maumivu ya kichwa na kujisikia kizunguzungu ili kupatiwa huduma mara moja.
Natumaini mmefaidika na makala hii, basi msisahau kuzitunza Afya zenu.
Makala hii imetayarishwa na rafiki yangu wa karibu, Asma.
Ahsante sana shosti!

2 comments:

Anonymous said...

Kweli nimefaidika na baadhi ya maelezo.
cherry

Shally's Med Corner said...

Ahsante sherry, na hilo ndio lengo letu, karibu!