Sunday, April 18, 2010

Unataka kuacha sigara ?..... fuata njia zifuatazo!


 Je, unataka kuacha kuvuta sigara? Sawa, nakubaliana na wewe lakini unajua kwa nini unataka kuacha tabia hiyo ambayo umeizoea kwa muda mrefu?. Kwa sababu haitoshi tu utake kuacha kuvuta sigara bila kuwa na sababu muhimu inayokusukuma uache suala hilo. Kwa hivyo kwanza anza kujiuliza kwa nini unataka kuacha sigara. Kujua sababu kutakusaidia katika kutekeleza lengo lako vyema. Je, unaacha sigara kwa kuwa unataka kuilinda familia yako isipate madhara ya sigara unazovuta? Je, unataka kuacha sigara kwa kuwa umeogopa kupata kensa ya kifua? Au je, ungependa kuonekana kijana zaidi? Tafuta sababu muhimu ambayo itaizidi hamu yako ya kuvuta sigara.


 Jua kuwa ni jambo gumu kuacha tabia uliyoizoea kwa muda mrefu mara moja. Haitowezekana utupe kipande chako cha sigara yako mara moja na kutangaza kuwa umeacha kuvuta. Suala hilo ni gumu kwani asilimia 95 ya watu wanaojaribu kuacha sigara kwa mtindo huo hushindwa, inabidi upate ushauri na tiba mbadala ili kukusaidia kuacha kuvuta sigara, hii ni kwa sababu sigara inaleta uraibu wa nicotine, na ubongo unaizoea mada hiyo hivyo kuacha kuvuta husababisha uhisi dalili za kukosekana nicotine katika ubongo.
 Jaribu kutumia vitu vingine badala ya nicotine. Hii ni kwa sababu unapoacha sigara na kukatisha nicotine mwilini hukufanya usijisikie kama umechanganyikiwa, uhisi msongamano wa mawazo na kutotulia. Suala hilo linaweza kusaidiwa kwa kupata tiba mbadala ya kusaidi kuondo hisia hizo. Wataalamu wanashauri kutumia ubani wa nicotine (nicotine gum), pipi za nicotine na baadhi ya plasta za kubandika mwilini zenye kusaidia kuacha sigara bila kuhisi madhara ya kukosa nicotine. Kutumia vitu hivyo wakati ukiwa bado unafuta sigara hakushauriwi.



 Ikiwa hutaki kutumia vitu vingine vyenye nicotine wakati umeacha sigara, mwombe daktari wako akuandikie vidogo ambavyo vinavyoondoa athari za mwili kuzoea nicotine wakati unapoacha sigara.
 Usijiamulie peke yako na kwa siri, bali itangazie familia yako, waambie marafiki zako na wafanyakazi wenzako kwamba umeacha sigara! Kukupa moyo kwao kutakufanya uweze kufanikisha lengo lako hilo kwa urahisi zaidi. Pengine unaweza kujiunga na vikundi vya wanaoacha kuvuta sigara au kwenda kwa mshauri ili akusaidie suala hilo.




 Jizuie usipatwe na msongamano wa fikra na mawazo mengi. Hii ni kwa sababu moja ya sababu inayowafanya watu wavute sigara ni kwa kuwa nicotine huwafanya wajihisi hisia nzuri mwilini na mwili kulegea. Utakapoacha sigara itakubidi utafute njia za kukabiliana na stress. Ni bora ukipata masaji ya mwili kila mara, usikilize mziki mwororo, huku ukijizuia na yake yatakayo kufanya upate mawazo na msongamano wa fikra na ikiwezekana fanya yoga na mazoezi ya kulegeza mwili.
 Jiepushe na pombe na vitu vinginevyo vinavyoweza kukushawishi uvute sigara tena. Pombe ni miongoni mwa vishawishi vikubwa vya kukufanya uvute sigara. Hivyo kama wewe ni mnywaji ni bora inabidi uache kunywa hasa wakati huu unaotaka kuacha sigara. Kama kahawa pia inakufanya usijikie kuvuta, iacha na unywe chai badala yake. Na kama huwa unavuta baada ya mlo, basi tafuta kitu kingine cha kufanya kama vile kupiga mswaki au kutafuna ubani baada ya kula.


 Baada ya kuvuta sigara yako ya mwisho, tupa vidude vyote vya kuhifadhia majivu ya sigara na viberiti. Fua nguzo zako zote zinazonuka sigara na safisha kapeti lako na nyuma yako kwa ujumla. Tumia marashi ya kuondoa harufu ili kuondoa harufu ulioizoea ya sigara nyumbani kwao. Hii ni kwa ajili ya kukusaidia usihisi harufu yoyote itakayokukumbusha kuvuta sigara.
 Jaribu tena na tena! Usitosheke kwa kuacha kuvuta mara moja na kushindwa. Wavutaji wengi huacha sigara mara kadhaa kabla ya kufanikiwa. Fikiria kila mara azma yako ya kuacha kuvuta sigara na jipe moyo na mwishowe utafanikiwa.


]
 Kuushughulisha mwili na mazoezi kunaweza kukusaidia kupunguza hamu ya sigara na dalili zinazofuata baada ya kuacha kuvuta. Utakaposhawishika na kutaka kunyoosha mkono wako ili uchukue sigara, vaa viatu vyako na uende ukatembee kidogo, kacheze mpira au fanya mazoezi yoyote kama vile kukimbia na mengineyo.
 Usijaribu kujinyima chakula wakati unapoacha sigara. Badala yake kula wa wingi matunda, mbogamboga na maziwa. Uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Duke umeonyesha kwamba, vyakula hivyo vinakufanya uhisi ladha ya sigara ni mbaya.




 Jiwekee zawadi nono na jipongeze. Kuacha sigara mbali na kukufaidisha kiafya hukusaidia pia kujiwekea fedha zako ambazo ungezipoteza bure kwa kununua sigara. Jipongeze kwa kutumia sehemu ya fedha hizo kujinunulia zawadi.
 Acha sigara kwa afya yako! Tambua kuwa kuacha sigara kutakupatia faida kemkem kiafya kama vile kupunguza shinikizo la damu, kupunguza mapigo ya moyo. Siku moja tu baada ya kuacha sigara, kiwango cha Carbon monoxide cha damu yako kitarejea katika hali ya kawaida. Baada ya miezi mitatu hadi minne, hatari ya shinikizo la moyo hupungua na mapafu yako huanza kufanya kazi kama kawaida. Miongoni mwa faida za kuacha sigara ni hupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo, mshituko wa moyo, kensa ya mapafu pamoja na saratani nyinginezo.

No comments: