Saturday, February 6, 2010
Aatikwa figo ya dada yake ingawa figo hiyo haiendani nawe
Utaalamu mpya umemumezesha mwanamke mmoja Muingereza kuwekewa pigo ya dada yake ingawa figo hiyo haiendani nae. Maxine Bath alikuwa na matatizo ya figo ambapo alikuwa akisaidiwa na mashine kuzungushiwa damu mwilini au dialysis. Mwanamke huyo hakuweza kupata mtu wa kumpatia figo inayoendana naye kutoka katika familia yake. Lakini madaktari wa hospitali ya Conventry nchini Uingereza wametumia utaalamu mpya unaojulikana kama 'cryofiltration' ili kuondoa seli za kulinda mwili ambazo zinasababisha figo hiyo ishindwe kuungana na mwili, iwapo itaunganishwa mwilini kwa mgonjwa hali ya kuwa haiendani na seli za mwili wake. Madaktari hao baada ya kufanikisha operesheni hiyo ya kuatika figo wanasema kwamba, utaalamu huo mpya unaweza kuwasaidia watu wengi zaidi wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali na wanahitajia kupandwa viungo mwilini au transplant. Watu 927 hufanyiwa operesheni za kuatika figo kila mwaka nchini Uingereza, hata hivyo maelfu ya wagonjwa wengine huwa wanaendelea kusubiri ili waweze kupata watu wanaoendana nao walioko tayari kuwapatia figo, huku ikiwa vigumu kuwapata watu hao. Viungo pale vinapopandwa au kuatikwa katika miili ya wengine hukataa kushikamana na miili hiyo (organ rejection) suala ambalo hutokea pale mwili unapotambua kuwa kiungo kilichoungwa si chake, na kuruhusu mfumo wa kulinda mwili ukikatae kiungo hicho. Tatizo hilo linaweza kuondolewa iwapo kiungo kinachotaka kupandwa kinatoka kwa ndugu wa familia moja na mgonjwa, na iwapo mgonjwa atatumia dawa za kuudhoofisha mfumo wa kulinda mwili kwa maisha yake yote.
Lakini haikuwa hivyo kwa Bi. Maxine, ambaye ana umri wa miaka 41 na aliyepata matatizo ya figo tangu akiwa na miaka 15. Ingawa mwanamke huyo hakuweza kupata mtu wa familia moja wa kumpa figo inayoendana na seli za mwili wake, lakini kwa kuondolewa seli hizo aliweza kuunganishiwa figo ya dada yake bila tatizo lolote.
Wataalamu wanasema kwamba teknolojia hiyo mpya inaweza kutumika kusaidia watu wengi zaidi wenye tatizo hilo, na hii ni mara ya kwanza duniani imetumiwa ili kumsaidia mgonjwa aunganishwe kiungo kisichoendana naye.
Operesheni hiyo ilifanywa mwezi Novemba mwaka 2009 na imesaidia kuokoa maisha ya Maxine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment