Sunday, February 14, 2010

Valentine special! ….Jikinge na umkinge umpendae na magonjwa ya zinaa



Leo ni siku ya wapendanao duniani. Katika siku ya leo mijini na mitaani kumejawa na shamshamra na harakati za watu wanaojali wawapendao ambao kwa namna mbalimbali huonekana wakiziweka wazi hisia zao ili kuwadhihirishia wapenzi wao pendo lao. Sio ajabu kukutana na wanaume waliobeba maua yanayoning'inia kadi zenye ujumbe moto moto wa siku hii ya wapendanao, huku wakinamama wakiandaa milo mitamu ili kuikoga moyo ya waume vipenzi wao pale watakaporejea majumbani. Wavulama na wasichana nao hupigana vikumbo katika maduka ya kadi na zawadi wakiwanunulia wapenzi na laazizi wao zawadi mbalimbali na vijana wanaoinukia wakionyesha kutokujali kwa kupigana mabusu barabarani, bila kuwasahau wale wanaojaza fedha simu zao angalau waweze kutuma sms au kuwasabahi kwa simu wapenzi wao ili wajue kuwa hawajawasahau katika siku hii. Yote haya ni katika kuonyesha hisia muhimu ya mapenzi kwa wawapendao katika siku hii maarufu iliyopewa jina la Valentine. Jambo muhimu ambalo lingependa wapendanao wajiulize katika siku hii yao muhimu ni je, kwa kiasi unachomjali na kumpenda mpenzi wako, mke au mume wako na ukawa uko tayari kumdhihirishia penzi lako siku hii kwa zawadi, maua, kadi au hata ujumbe wa sms, je ni kwa kiasi gani pia unamjali mpenzi wako huyo katika kumkinga na magonjwa?. Je, kama penzi lako ni la dhati kwa mpenzi wako je unamjali na kumlinda?. Je unajali kumkinga na magonjwa mbalimbali ya kiafya na ya kimapenzi? … Sitaki kuwachafulia uwanja hasa katika siku hii ambayo wengi hawataki kusikia lolote isipokuwa masuala ya mapenzi lakini nafikiri kama unamjali mpenzi wako kikweli basi pengine katika siku hii unapodhihirisha mapenzi yake kwake pia utachukua japo dakika chache kufikiria ni kwa kiasi gani unamlinda na magonjwa mbalimbali ambayo maambukizo yake hutokea wakati wa kufanya mapenzi. STD au Sexually Transmitted Infection kwa Kiswahili magonjwa ya zinaa ni maambukizo ambayo hutokea wakati wa kujamiiana. Miongoni mwa magonjwa hayo ni gonjwa hatari la Ukimwi, kaswende, kisosonono, Clamydia, Trichomonia, Hepetitis B, Herpes au ugonjwa wa malengelenge neva ngozini na kadhalika. Kona ya Afya inachotaka kusema katika siku ya wapendanao ni kwamba, moja ya misingi muhimu ya kukuepusha wewe na mpenzi wako na magonjwa ya zinaa ni kuwa muaminifu kwa mpenzi wako, mke au mume wako. Kuhakikisha umpendae unamlinda kwa kufuata maelekezo ya kujikinga na maradhi hayo yanayoambukizwa wakati wa kufanya mapenzi kama vile kutumia mipira, kupata kinga na matibabu yanayotakiwa. La muhimu zaidi ni kumjulisha umpendaye pindi unapoyakwaa maradhi hayo ili naye akapime na apatiwe tiba, kwa sababu mengi ya maradhi hayo ya zinaa tiba yake hukamilika pale wawili wanaoshiriki mapenzi wanapotibiwa pamoja. Kujidanganya kujitibu mwenyewe na kuficha ugonjwa kwa mpenzi wako, zaidi ya kukufanya usipone kikamilifu magonjwa hayo, pia huleta hatari kubwa ya kueneza magonjwa hayo katika jamii. Kwa hivyo njia ya kwanza ni kuyajua magonjwa ya S.T.D na kuzijua dalili zake na kuwa wazi kuhusiana na magonjwa hayo pale yanapotupata.
Kona ya Afya inasema… kama kweli unampenda basi mlinde!
Nawatakia wadau wote Valentine Njema!

No comments: