Wednesday, February 3, 2010

Nchi za Afrika zakubaliana kutokomeza malaria


NCHI za Afrika zimekubaliana kuwa lengo kuu la serikali zao katika mapambano dhidi ya malaria, ni kuutokomeza ugonjwa huo.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania alisema hayo juzi mwishoni mwa kikao cha viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) walio katika mapambano dhidi ya malaria Afrika (ALMA).

Alisema Afrika inahitaji vyandarua 200 ingawa hadi sasa kuna ahadi ya vyandarua 50 tu, lakini hata hivyo aliitaka ALMA kuendelea na jitihada za kupata vyandarua vyote vitakavyokidhi mahitaji.

Rais Kikwete aliitisha kikao hicho kwa kushirikiana na AU ambapo mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ray Chambers, aliwataka viongozi hao kuweka nia ya dhati ya kisiasa katika jitihada hizi ili kufanikisha azma yao.

Kikao hicho ni cha pili cha kikazi baada ya kilichofanyika New York, Marekani chini ya Rais Kikwete, kama mwanzilishi wa jitihada hizo ambazo zilianza wakati akiwa Mwenyekiti wa AU.

Kikao hiki kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa AU, Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi, Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia, Hifikepunye Pohamba wa Namibia, Mwai Kibaki wa Kenya na Armando Guebuza wa Msumbiji. Wengine ni Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Rupia Banda wa Zambia na Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Nchi zingine zilizohudhria ni Burundi, Gabon, Misri na Somalia. Katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ALMA, Joy Phumaphi, alieleza mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo matumizi ya vyandarua yameongezeka kwani hadi mwaka juzi nchi 13 kati ya 35 zenye kiwango kikubwa cha malaria, asilimia 50 ya watu wao wanatumia vyandarua hivyo, ikilinganishwa na mwaka 2005 na pia matumizi ya dawa mseto yamepunguza maambukizi na vifo.

Phumaphi alisema mwamko huo wa matumizi bora ya vyandarua, umepunguza vifo na maambukizi pia kwa mama na mtoto ambao ndiyo waathirika wakubwa.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto nyingi ambazo zinahatarisha jitihada na kutokomeza malaria ikiwamo fedha kunakotokana na kutotimizwa kwa ahadi na wafadhili.

Rais Kikwete alimtaka kila mshiriki kupitia wizara zao za Afya kutuma maombi kwenda mfuko wa malaria duniani (Global Fund) ambayo yatahusisha si upatikanaji tu wa vyandarua, bali uwezeshwaji wa watumishi wa afya, vitendea kazi na vitu vyote muhimu vinavyohitajika katika jitihada hizi za kutokomeza malaria.

No comments: