Monday, February 8, 2010

Maradhi anayopata mama mjamzito humpelekea mwanae kupata pumu


Utafiti mpya umegundua kuwa, baadhi ya magonjwa anayopata mama wakati wa ujauzito huongeza uwezekano wa mwanae kupatwa na ugonjwa wa pumu. Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Maendeleo ya Tiba za Watoto na Vijana, watoto ambao wanazaliwa na kina mama waliopatwa na maambukizo ya vijidudu katika mfuko wa uzazi au maji yanayomzunguka mtoto tumboni yanayojulikana kama (chorioamnionitis) huwa wana uwezekano mkubwa wa kupatwa na pumu wafikapo umri wa miaka 8. Suala hilo hilo pia huwatokea watoto waliozaliwa kabla muda wao wa kuzaliwa haujatimia au prematures. Maambukizo hayo yanasababishwa na bakteria mbalimbali wanaopatikana katika sehemu za uke kama vile E. Coli na bakteria kundi B, Streptococci. Magonjwa hao husababisha zaidi ya nusu ya watoto wazaliwe kabla muda wao haujatimia, huku watoto hao wakiwa mapafu yao hayajaimarika vya kutosha na hivyo kukabiliwa na hatari ya kupata magonjwa mbalimbali sugu ya kifua kama vile pumu. Wanasayansi kwa kutegemea utafiti huo wameweza kusema kuwa, maambukizo ya magonjwa yanayotokana na bakteria ndio sababu kuu inayopelekea watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda wao kutimia, wapatwe na pumu.
Hivyo wameshauri kuwa, wakinamama wanatakiwa kufahamu umuhimu wa kuhudhuria kiliniki na katika vituo vya afya wakati wa ujauzito na kufuata maelekezo wanayopewa wakati wakiwa na mimba ili kuepusha matatizo kama hayo yasitokee.

No comments: