Sunday, February 28, 2010

Kujipumzisha mchana huimarisha akili!


Uchunguzi mpya umeonyesha kuwa kulala kidogo wakati wa mchana huhuisha ubongo na kuimarisha uwezo wa kufahamu mambo mapya. Profesa Matthew P. Walker wa Kitengo cha Saikolojia na Sayansi ya ubongo cha Chuo Kikuu cha Calfornia aliyeongoza uchunguzi huo anasema kwamba, unahitaji kulala kabla ya kujifunza, ili kuutayarisha ubongo wako ili uwe kama sponchi kavu linalosubiri kunyonya taarifa mpya. Akielezea umuhimu wa kujipumzisha mchana hasa kwa wale wanaosoma na kujifunza Profesa Walker anasema kwamba, usingizi sio tu huondoa uchovu na kufuta makosa yanayotokana na kuwa macho muda mrefu, bali pia humrejesha mtu pale alipokuwepo kabla ya kulala. Wataalamu wanasema kuwa, kila mtu anapoongeza masaa ya kukaa macho ndivyo hivyo hivyo uwezo wa ubongo wake wa kuelewa mambo unavyopungua. Professa Walker akitoa mfano ili kufahamisha zaidi umuhimu wa kupumzisha ubongo ili kuongeza uwezo wa kujifunza, anaufananisha ubongo na sanduku la barua pepe na kusema kwamba iwapo sanduku hilo litajaa basi hutoweza kupata barua pepe mpya hadi pale utakapoondoa barua pepe zisizotakiwa au kuzipelekea katika folder jipya, na kulala nako huusaidia ubongo hivyo hivyo.
Uchunguzi huo unaunga mkono utafiti wa huko nyuma unaosema kwamba, kukaa macho muda mrefu usiku hupunguza uwezo wa mtu wa kuelewa mambo mapya kwa karibu asilimia 40, kwani baadhi ya sehemu za ubongo hufunga baada ya kukosa usingizi kwa muda mrefu.

No comments: