Saturday, February 28, 2009
Chai inapunguza mshituko wa Moyo!
Utafiti mpya uliofanyika nchini Marekani unaonyesha kuwa kunywa chai vikombe vitatu kwa siku au zaidi kunapunguza msituko wa moyo kwa asilimia 21.
Haya shime tunywe chai wadau!
Mchanganyiko wa dawa za zamani huweza kutibu Kifua Kikuu
Watafiti wa masuala ya tiba wamesema kuwa, dawa mbili ambazo huko nyuma zilikuwa zinatumiwa kutibu magonjwa mengine, sasa zinaweza kusaidia kutibu ugonjwa wa kifua kikuu, ambao unawaumiza kichwa madakatari kwa kutokukubali dawa.
Wamesema katika uchunguzi wa maabara kuwa, mchanganyiko wa dawa aina ya 'Clavulanate" na 'Maropenem' umeonyesha kuwa na athari nzuri dhidi ya aina 13 za vijidudu vya TB ambavyo vimekuwa vikishindwa kuathiriwa (drug resistance) kwa kiasi kikubwa na dawa zinazotumiwa kutibu ugonjwa huo. Hata hivyo wataalamu ingawa wamesisitiza kuwa, kupatikana tiba mpya ya ugonjwa kifua kikuu ni jambo la dharura, wametoa tahadhari kuhusiana na utumiaji wa dawa hizo wakisema kuwa bado utafiti wa kina unafanyika.
Takwimu zinaonyesha kuwa theluthi moja ya watu duniani kote wameambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu (TB) lakini ni asilimia 10 tu ya wale walioambukizwa wanaonyesha dalili za ugonjwa huo.
Kumekuwa na wasiwasi mkubwa juu ya kuenea kwa aina ya kifua kikuu ijulikanayo kama XDC-TB ambayo haisikii dawa. Aina hiyo imekuwa haisikii dawa za kifua kikuu zinazotumika kama chaguo la kwanza la tiba hiyo ( first choice drug) kwa kiasi kikubwa na hata zile za chaguo la pili katika kutibu ugonjwa huo.
Uchunguzi zaidi kuhusiana na dawa hizo umepangwa kufanywa baadaye mwaka huu.
*Ugonjwa wa Kifua Kikuu unasababishwa na bacteria wajulikanao kama Mycobacterium Tuberclosis.
Kumbuka kuwa: Ugonjwa wa kifua kikuu unaambukiza, kama ugonjwa wa mafua, vijidudu vya kifua kikuu huenea katika hewa pale mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo anapokoa, kutema mate au hata kuzungumza. Mtu mzima huweza kuambukiza ugonjwa wa kifua kikuu kwa kuvuta hewa nyenye vijidudu vya ugonjwa huo (sputum). Pia kuna aina ya ugonjwa wa TB ambao huambukizwa kwa kunywa maziwa yasiyochemshwa. Aina hiyo inajulikana kama Mycobecterium Bovis TB. Kuchemsha maziwa au kunywa maziwa yalishemshwa viwandani na kuuawa bacteria (pasteurized) kunaepusha kupata ugonjwa huo.
::::::::::::::::::::::Afya yako ni tunu, basi daima tutunze afya zetu :::::::::::::::::
Friday, February 27, 2009
Wanaume wanashauriwa kumeza vidonge vya kuzuia kensa ya korodani( prostate cancer)
Kwa mara ya kwanza madaktari wameshauri wanaume kutumia baadhi ya dawa kwa lengo la kujikinga na ugonjwa wa kensa ya korodani.
Lakini wanume hao ni wale tu ambao wako katika hatari ya kukabiliwa na ugonjwa huo. Yaani wako at risk. Hawa ni wale ambao ndugu zao wa karibu kama baba, babu au hata kaka na baba mdogo wamepatwa na ugonjwa huo wa kensa ya korodani.
Ugonjwa wa kensa ya korodani ni ugonjwa unaosababisha buje au tumor inayokua polepole katika korodani zao (tests), buje ambalo huweza kujulikana tu kwa kufanya kipimo cha biopsy baada ya mgonjwa kupimwa na damu yake kutiliwa wasiwasi katika kipimo cha PSA.
Maelekezo mapya yaliyotolewa na Jumuiya ya magonjwa ya Saratani na Matatizo yanayoambatana na mfumo wa mkojo ya Marekani ni kuwa, kila mwanamme aliye hatarini ni bora atumie dawa aina ya FINESTERIDE (PROSCAR) bila kujali kuwa dawa hiyo inaweza kuwa na madhara kidogo(side effects).
kwani dawa hiyo inazuia kupatwa na kensa ya korodani kwa asilimia 25.
Dawa ya Finesteride hivi sasa inatumika kutibu baadhi ya magonjwa mbaliambali yanayoambatana na matatizo ya mkojo.
Wanasayansi wanaamini kuwa, dawa hiyo inamkinga mtu na maradhi ya kensa ya korodani kwa kupunguza ukubwa wa korodani na kupunguza kiwango cha homoni ya testosterone.
Haya shime kwa wanaume wote wanaokabiliwa na ugonjwa wa kensa ya korodan, kumbuka kuwa kukinga siku zote ni bora kuliko kutibu.
Tutazungumzia kensa ya korodani katika siku za mbele. Kama kawaida nawahusia kuzijali afya zenu!
Thursday, February 26, 2009
Attention! Virusi vya HIV vinajibadilisha kwa haraka sana ili kukabiliana na mfumo wa ulinzi wa mwili wa binadamu!
Nimekutana na makala hii ya kusikitisha na kukatisha tamaa kuhusiana na jitihada za kuutafutia chanjo na tiba ugonjwa sugu wa Ukimwi.
Timu ya wanasayansi wa dunia wametangaza jana kwamba, virusi vya ugonjwa hatari wa ukimwi, vinajibadilisha (Mutation) na kuepuka mfumo wa ulinzi wa mwili wa binadamu, suala ambalo limeongeza changamoto katika kutengenezwa chanjo ya ugonjwa wa ukimwi.(vaccine)
Wanasayansi hao wamesema katika utafiti wao huo uliochapishwa katika jarida la Nature, kujibadilisha huko na kuwa katika umbo jingine au mutation, kunavifanya virusi hivyo kuweza kuwa na mabadiliko ya kijenetiki ya haraka, ambayo yanaviwezesha kujihifadhi vyema zaidi dhidi ya chochote kila kinachovishambulia na kutaka kuviangamiza virusi hivyo, suala ambalo huviwezesha virusi vya HIV kuuharibu zaidi mfumo huo. Profesa Philip Goulder mtafiti wa chuo kikuu cha Oxford anasema kuwa, ingawa ni muda mfupi tangu virusi vya HIV viwepo katika jamii ya mwanadamu, lakini vimeweza kuwapa wanasayansi kazi ya ziada na kuzishinda jitihada zao za kuudhibiti mfumo wa ulinzi wa mwili wa mwanadamu dhidi ya virusi hivyo. Ameongeza kuwa, kasi ya kujibadilisha huko kwa virusi vya HIV ni ya juu zaidi kuweza kushuhudia katika kipindi cha miongo kadhaa (decades).
Timu hiyo ya mtafiti Goulder imefanyia utafiti kodi za jeni (genetic codes) na aina za virusi vya watu 2,800 walioathiriwa na ugonjwa wa Ukimwi kutoka Afrika Kaskazini, Visiwa vya Carribbean, Ulaya, nchi za chini ya jangwa la Sahara , Australia pamoja na Japan. Wataalamu hao walitilia mkazo zaidi jeni muhimu inayojulikana kama HLA au Human Leukocyte Antigen.
Hata hivyo wanasayansi hao wamesema kwamba, hali hiyo haiathiri athari inayopatikana kwa mgonjwa pindi anapotumia dawa za kupambana na virusi vya Ukimwi. Hii inaonyesha jinsi gani dawa zinazotumiwa na wagonjwa wa ukimwi zilivyo na umuhimu!.
*Tusisahau kuwa ugonjwa wa Ukimwi tayari umeshaua watu milioni 25 na inakadiriwa kuwa watu wengine milioni 33 tayari wameambukizwa ugonjwa huo duniani kote.
*Tukumbuke kuwa, virusi vya HIV haviwauwi watu wanaoathirika kwa kiasi sawa. Kwa wastani bila kutumia dawa za ukimwi, mgonjwa huweza kuishi mpaka miaka 10 tangu alipoathiriwa mpaka ugonjwa wa ukimwi utakapojitokeza. Lakini kuna baadhi ya watu baada ya kuingia mwilini mwao virusi vya HIV mpaka kuja kuonekana dalili zake, ikawachukua mwaka mmoja tu, huku wengine ikawachukua mpaka miaka 20. Hiyo yote inategemea mfumo wa ulinzi wa miili yao.
Wadau! Ugonjwa wa Ukimwi bado hauna kinga wala dawa, ni jukumu letu kujiepusha na njia zinazopelekea kupata ugonjwa huu. Sisi wenyewe na jamii nzima.
Wednesday, February 25, 2009
Onyo kwa wanawake wanywaji!
Wanawake wanaopendelea kunywa mvinyo kila usiku wameonywa kwamba, wako katika hatari kubwa ya kukabiliwa na kensa!
Watafiti wa Kensa wa Uingereza wametangaza kwamba, kunywa gilasi moja tu ya ulevi kwa siku kunasababisha kensa 7,000 za ziada, nyingi zikiwa ni za matiti, hasa kwa wanawake wa nchi hiyo.
Hatari ya kupata ugonjwa huo inaongezeka kila unywaji unavyoongezeka, na hakuna tofauti iwapo pombe hiyo ni spirits, mvinyo au bia ya Safar Lager!. Hayo ni kwa mujibu wa watafiti hao. Takwimu zimeonyesha kuwa, kunywa pombe chupa moja kwa siku kunaongeza uwezekano wa kupata aina zote za kensa kwa asilimia 6 kwa wanawake ambao wana umri wa mpaka miaka 75.
Haya chime kina mama wanyaji, msijisahau na mjali afya zenu!
Link..
http://news.bbc.co.uk/2/hi/health/7906355.stm
Tuesday, February 24, 2009
Dawa ya malaria yenye ladha ya cherry!
Dawa mpya ya malaria imetengenezwa na kuanza kuuzwa madukani yenye ladha ya cherry, lengo lake likiwa ni kuwafanya watoto wakubali kunywa dawa hiyo kwa urahisi. Tunajua dawa nyingi za vidonge za malaria ni chungu, suala ambalo linaleta kizuizi katika kutibiwa vizuri watoto wanaopatwa na malaria.
Watoto wengi hukataa kula dawa hizo hata baada ya kuongezwa sukari. Lakini dawa tamu inayopendwa na watoto ya malaria iitwayo Coartem inaonekana kuwa suluhisho la tatizo hilo.
Dawa hiyo huweza kuyeyuka katika maji na maziwa ya mama, lakini hunukia kama juice ya matunda ya cherry!.
Inatarajiwa kuwa dawa hiyo itaanza kutumika katika nchi za Kiafrika hivi karibuni.
Kumbuka kuwa:
Ugonjwa wa Malaria ni ugonjwa unaoua zaidi duniani, ambapo watu milioni 1 kufariki dunia kila mwaka kutokakana na ugonjwa huo. Wahanga wakubwa wa ugonjwa wa malaria ni watoto.
Mpende mwanao kwa kumkinga na malaria!
Monday, February 23, 2009
Kunywa maji, ni muhimu kwa mwili wako!
Je unajua asilimia 75 ya mwili wako ni maji? Na kama unajua, je unajua pia robo tatu ya uso wa dunia ni maji? Sawa pengine ukawa hilo unajua, lakini je, unajua pia maji ni kimiminiko muhimu katika kusafirisha chembechembe muhimu mwilini mwako? Vilevile ujajua kuwa kuna lita 42 za maji mwilini mwako na iwapo utapoteza lita 2.7 tu ya maji hayo basi uko hatarini kupungukiwa na maji mwilini?
Halikadhalika je, unajua kuwa, ukosefu au upungufu wa maji mwilini huweza kukusababishia matatizo kibao, kama vile kuchoka, kuwa na wasiwasi na hasira, kusikia kizunguzungu, udhaifu, maumivu ya kichwana mengineyo mengi?
Hii inaonyesha umuhimu wa maji mwilini mwako na kwa viumbe hao wote wanaotuzunguka.
Basi kunywa maji, ila usisahau kunywa maji safi na salama!
Saturday, February 21, 2009
Kuvuta sigara katika umri mdogo kunasababisha ugonjwa wa MS
Watu ambao wanaanza kuvuta sigara wakiwa katika umri wa kabla ya miaka 17, wako katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa Multiple Sclerosis au MS. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika mkutano wa 61 wa kila mwaka wa Taasisi ya magonjwa ya mishipa ya fahamu ya Marekani, zaidi ya asilimia 32 ya wagonjwa wa MS walikuwa ni wale walioanza kuvuta sigara katika umri mdogo. Utafiti huo umeonyesha kuwa, wanaovuta sigara katika umri mdogo wana uwezekano wa kupata ugonjwa wa MS mara 2.7 zaidi ya wengine. Utafiti huo lakini haukuonyesha kuwepo hatari hiyo kwa wale wanaoanza kuvuta sigara wakiwa na umri mkubwa. Ugonjwa wa multiple sclerosisi ni ugonjwa wa mfumo wa kinga ya mwili ambao hutokea pale mfumo huo unaposhambulia mfumo wa kati wa fahamu ( central nervous susytem), hali ambayo hupelekea seli za fahamu kushindwa kuwasiliana. Ugonjwa huo mara nyingi huanza kwa kupoteza hisia mbalimbali mwilini kama kuona, kuhisi, kushindwa kutembea, kupumua na mwishowe kupooza mwili mzima.
Shime tuungane kupinga vijana kuanza kuanza kuvuta sigara katika umri mdogo!
Monday, February 16, 2009
Matibabu ya Ukimwi kwa kutumia jeni yaleta matumaini
Matokeo ya jaribio la kutumia jeni (gene) kutibu ugonjwa wa Ukimwi limeleta matumani kuhusiana na tiba ya ugonjwa huo hatari. Baada ya jaribio hilo kufanywa kwa wagonjwa 74, imeonekana kuwa tiba hiyo ni salama na inaweza kupunguza madhara ya virusi vya HIV katika mfumo wa ulinzi wa mwanadamu yani Immune system. Wataalamu wanasema kuwa, kwa kutumiwa njia hiyo tiba moja tu ya jeni itakuwa inatosha badala ya mgonjwa wa ukimwi kutumia vidonge vinavyopunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi ambavyo inambidi muathiriwa avitumie umri wake wote. Jaribio hilo la kitiba pia limeonyesha kuwa, wagonjwa waliotumia tiba hiyo ya jeni miili yao ilikuwa na seli za CD nyingi zaidi. Hata hivyo tiba hiyo bado inachunguzwa ili kuhakikisha kuwa ni salama kutumiwa.
Tumuombe mola awezeshe tiba hiyo iwe salama na itumike ili kuwapunguzia maumivuu na mahangaiko wagonjwa wa ukimwi!
Link…. http://news.bbc.co.uk/2/hi/health/7883023.stm
Saturday, February 14, 2009
Kufanya mazoezi huzuia kupata kensa ya tumbo
Inaaminika kuwa kufanya mazoezi kunaweza kupunguza uwezekano wa kupata kensa ya tumbo (Bowel cancer). Wataalamu wa Marekani baada ya kufanya uchunguzi wamegundua kuwa, mazoezi ya aina mbalimbali kama vile kukimbia na kwenda gym kunaweza kupunguza uwezekano wa kupata kensa ya tumbo kwa asilimia 25.
Wanasema kuwa, kuwa na kiasi cha kawaida cha uzito ni moja ya njia za kupunguza uwezekano wa kupata kensa ya matumbo na kensa nyinginezo, suala ambalo linaweza kupunguza uwezekano wa kutokea kesi karibu 13,000 za ugonjwa huo duniani kila mwaka.
Tukumbuke kuwa, kensa inayoathiri utumbo mkubwa ni moja ya kensa hutokea zaidi katika kensa za tumbo.
Haya shime kufanya mazoezi ili tuzilinde afya zetu!
Thursday, February 12, 2009
Nadharia ya kuzaa watoto nane kwa mpigo (Octuplets
Mwanamke mmoja wa kimarekani amejifungua watoto nane huko California, ikiwa ni baada ya muongo mmoja tangu mwanamke mmoja wa Nigeria kujifungua kwa mara ya kwanza watoto nane hai duniani. Wataalamu wanasema suala la kuzaa watoto nane kwa mpigo linatokea kwa nadra sana na ni matukio kadhaa tu kama hayo yaliyoweza kutokea dunia, ambapo mpaka sasa hakuna watoto mapacha nane waliowahi kuishi baada ya kuzaliwa. Lakini watoto mapacha nane waliozaliwa huko California na mwanamke aitwaye Nadya Suleman wako hai na wanaendelea kuishi bila matatizo yoyote muhimu ya kiafya.
Lakini suala kubwa la kujiuliza hapa ni kuwa, suala hilo huweza kutokea vipi?
Mimba za mapacha za aina hiyo hutokea kwa nadra sana kwa njia ya utungwaji wa mimba wa kawaida. Mimba za mapacha wengi mara nyingi hutokea iwapo zimetumiwa dawa za kuyapa nguvu mayai ya mwanamke kwa lengo la kuzaliwa mayai mengi ili mwaname aweze kushika mimba kwa urahisi. Wanawake wanaobeba mimba kwa njia hiyo, huangaliwa kwa karibu na madaktari wao ili kuhakikisha kuwa mayai mengi hayazaliwi na kukua, na kama yakizaliwa basi hushauriwa kutobeba mamba kwa kujizuia kujamiana au kutumia njia za kuzuia mamba. Suala hilo huzuiliwa kwani mimba pacha za watoto wengi huhatarisha maisha ya mama na vichanga. Hii inamaanisha, kila kiwango kidogo cha watoto kinapokua katika mfuko wa uzazi wa mwanamke mjamzito ndio fursa nzuri inavyopatikana ya kukua vizuri watoto tumboni mwa mama. Kwa upande mwingine mama mjamzito kila anavyozidi kuwa na watoto wengi tumboni ndio matatizo kama vile kupata shinikizo la damu, kifafa cha mimba na sukari wakati wa ujauzito ndivyo yanavyoongezeka.
Hata hivyo watoto mapacha nane wa California wamezaliwa vizuri tu, ingawa wamezaliwa kabla ya umri wao kutimia, yaani wakiwa (premature) lakini wamezaliwa na uzito ambao si mdogo sana. Tusisahau kuwa mama huyo alikuwa akiangaliwa vyema na madaktari kabla ya kujifungua, na alijifungua kwa operesheni iliyofanywa na timu ya makumi ya madaktari wakihakikisha kuwa, vichanga hivyo vinazaliwa salama salimin.
Link….http://news.bbc.co.uk/2/hi/health/7853257.stm
Wednesday, February 11, 2009
Kula mayai kwa kiasi unachotaka hakuna madhara?
Uchunguzi umethibitisha kwamba kula mayai kwa kiasi cha kawaida kuna athari ndogo katika kuongeza kiasi cha kolestiroli mwilini. Timu ya wataalamu wa Surrey waliofanya uchunguzi huo wanasema kwamba uchunguzi wao umeonyesha kuwa watu wanaweza kula mayai kwa kiasi wanachotaka bila kuathiri afya zao. Wataalamu hao ambao wameangalia chunguzi kibao kuhusiana na lishe inayotokana na mayai wamesema kuwa, suala kuwa kula zaidi ya mayai matatu kwa wiki kunaleta madhara, limezoeleka lakini suala hilo si sahihi na ni kwa mujibu wa taarifa zilizopitwa na wakati. Ukweli ni kuwa kiasi cha kolestiroli (mafuta) kinachopatikana katika mayai kwa kawaida hakichangii kwa kiasi kikubwa katika kiasi cha kolestiroli ya damu yako.
Haya jamani shime kula mayai katika milo yetu ya kawaida na shime tupinge dhana potofu kuwa mama mjamzito haruhusiwi kula mayai, kwani mama mjamzito anatakiwa kula vyakula vyote katika lishe bora na ilojitosheleza.
Link…. http://news.bbc.co.uk/2/hi/health/7882850.stm
Haya jamani shime kula mayai katika milo yetu ya kawaida na shime tupinge dhana potofu kuwa mama mjamzito haruhusiwi kula mayai, kwani mama mjamzito anatakiwa kula vyakula vyote katika lishe bora na ilojitosheleza.
Link…. http://news.bbc.co.uk/2/hi/health/7882850.stm
Subscribe to:
Posts (Atom)