Thursday, February 26, 2009

Attention! Virusi vya HIV vinajibadilisha kwa haraka sana ili kukabiliana na mfumo wa ulinzi wa mwili wa binadamu!


Nimekutana na makala hii ya kusikitisha na kukatisha tamaa kuhusiana na jitihada za kuutafutia chanjo na tiba ugonjwa sugu wa Ukimwi.
Timu ya wanasayansi wa dunia wametangaza jana kwamba, virusi vya ugonjwa hatari wa ukimwi, vinajibadilisha (Mutation) na kuepuka mfumo wa ulinzi wa mwili wa binadamu, suala ambalo limeongeza changamoto katika kutengenezwa chanjo ya ugonjwa wa ukimwi.(vaccine)
Wanasayansi hao wamesema katika utafiti wao huo uliochapishwa katika jarida la Nature, kujibadilisha huko na kuwa katika umbo jingine au mutation, kunavifanya virusi hivyo kuweza kuwa na mabadiliko ya kijenetiki ya haraka, ambayo yanaviwezesha kujihifadhi vyema zaidi dhidi ya chochote kila kinachovishambulia na kutaka kuviangamiza virusi hivyo, suala ambalo huviwezesha virusi vya HIV kuuharibu zaidi mfumo huo. Profesa Philip Goulder mtafiti wa chuo kikuu cha Oxford anasema kuwa, ingawa ni muda mfupi tangu virusi vya HIV viwepo katika jamii ya mwanadamu, lakini vimeweza kuwapa wanasayansi kazi ya ziada na kuzishinda jitihada zao za kuudhibiti mfumo wa ulinzi wa mwili wa mwanadamu dhidi ya virusi hivyo. Ameongeza kuwa, kasi ya kujibadilisha huko kwa virusi vya HIV ni ya juu zaidi kuweza kushuhudia katika kipindi cha miongo kadhaa (decades).
Timu hiyo ya mtafiti Goulder imefanyia utafiti kodi za jeni (genetic codes) na aina za virusi vya watu 2,800 walioathiriwa na ugonjwa wa Ukimwi kutoka Afrika Kaskazini, Visiwa vya Carribbean, Ulaya, nchi za chini ya jangwa la Sahara , Australia pamoja na Japan. Wataalamu hao walitilia mkazo zaidi jeni muhimu inayojulikana kama HLA au Human Leukocyte Antigen.
Hata hivyo wanasayansi hao wamesema kwamba, hali hiyo haiathiri athari inayopatikana kwa mgonjwa pindi anapotumia dawa za kupambana na virusi vya Ukimwi. Hii inaonyesha jinsi gani dawa zinazotumiwa na wagonjwa wa ukimwi zilivyo na umuhimu!.
*Tusisahau kuwa ugonjwa wa Ukimwi tayari umeshaua watu milioni 25 na inakadiriwa kuwa watu wengine milioni 33 tayari wameambukizwa ugonjwa huo duniani kote.
*Tukumbuke kuwa, virusi vya HIV haviwauwi watu wanaoathirika kwa kiasi sawa. Kwa wastani bila kutumia dawa za ukimwi, mgonjwa huweza kuishi mpaka miaka 10 tangu alipoathiriwa mpaka ugonjwa wa ukimwi utakapojitokeza. Lakini kuna baadhi ya watu baada ya kuingia mwilini mwao virusi vya HIV mpaka kuja kuonekana dalili zake, ikawachukua mwaka mmoja tu, huku wengine ikawachukua mpaka miaka 20. Hiyo yote inategemea mfumo wa ulinzi wa miili yao.
Wadau! Ugonjwa wa Ukimwi bado hauna kinga wala dawa, ni jukumu letu kujiepusha na njia zinazopelekea kupata ugonjwa huu. Sisi wenyewe na jamii nzima.

No comments: