Saturday, February 28, 2009

Mchanganyiko wa dawa za zamani huweza kutibu Kifua Kikuu



Watafiti wa masuala ya tiba wamesema kuwa, dawa mbili ambazo huko nyuma zilikuwa zinatumiwa kutibu magonjwa mengine, sasa zinaweza kusaidia kutibu ugonjwa wa kifua kikuu, ambao unawaumiza kichwa madakatari kwa kutokukubali dawa.
Wamesema katika uchunguzi wa maabara kuwa, mchanganyiko wa dawa aina ya 'Clavulanate" na 'Maropenem' umeonyesha kuwa na athari nzuri dhidi ya aina 13 za vijidudu vya TB ambavyo vimekuwa vikishindwa kuathiriwa (drug resistance) kwa kiasi kikubwa na dawa zinazotumiwa kutibu ugonjwa huo. Hata hivyo wataalamu ingawa wamesisitiza kuwa, kupatikana tiba mpya ya ugonjwa kifua kikuu ni jambo la dharura, wametoa tahadhari kuhusiana na utumiaji wa dawa hizo wakisema kuwa bado utafiti wa kina unafanyika.
Takwimu zinaonyesha kuwa theluthi moja ya watu duniani kote wameambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu (TB) lakini ni asilimia 10 tu ya wale walioambukizwa wanaonyesha dalili za ugonjwa huo.
Kumekuwa na wasiwasi mkubwa juu ya kuenea kwa aina ya kifua kikuu ijulikanayo kama XDC-TB ambayo haisikii dawa. Aina hiyo imekuwa haisikii dawa za kifua kikuu zinazotumika kama chaguo la kwanza la tiba hiyo ( first choice drug) kwa kiasi kikubwa na hata zile za chaguo la pili katika kutibu ugonjwa huo.
Uchunguzi zaidi kuhusiana na dawa hizo umepangwa kufanywa baadaye mwaka huu.
*Ugonjwa wa Kifua Kikuu unasababishwa na bacteria wajulikanao kama Mycobacterium Tuberclosis.
Kumbuka kuwa: Ugonjwa wa kifua kikuu unaambukiza, kama ugonjwa wa mafua, vijidudu vya kifua kikuu huenea katika hewa pale mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo anapokoa, kutema mate au hata kuzungumza. Mtu mzima huweza kuambukiza ugonjwa wa kifua kikuu kwa kuvuta hewa nyenye vijidudu vya ugonjwa huo (sputum). Pia kuna aina ya ugonjwa wa TB ambao huambukizwa kwa kunywa maziwa yasiyochemshwa. Aina hiyo inajulikana kama Mycobecterium Bovis TB. Kuchemsha maziwa au kunywa maziwa yalishemshwa viwandani na kuuawa bacteria (pasteurized) kunaepusha kupata ugonjwa huo.
::::::::::::::::::::::Afya yako ni tunu, basi daima tutunze afya zetu :::::::::::::::::

No comments: