Monday, October 5, 2009
Hatimaye Wizara yaagiza vyumba vya 'leba' visafishwe
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, amewaagiza wakunga katika hospitali za Serikali wahakikishe kwamba vyumba kwa ajili ya akinamama kujifungua ni visafi kila siku.
Nyoni amesema, kama chumba kwa ajili ya kujifungua ni kisafi hakutakuwa na maambukizi yoyote kwa mama au mtoto anayezaliwa.
Amewataka wakunga hao wahakikishe kwamba, suala hilo linakuwa sehemu ya kazi yao kila siku. Amesema, hospitali nyingi za Serikali hasa wodi wanazotumia akinamama kujifungua ni chafu.
“Usafi ni tiba kwa asilimia 60 hivyo hakikisheni kwamba sehemu mnazofanyia kazi zinakuwa safi ili kuwapa imani akinamama wanaokuja kupata huduma yenu,” amesema Nyoni.
Nyoni amesema, tabia ya wakunga wengi kutojali maeneo wanayofanyia kazi inasababisha hali hiyo. Ameyasema hayo leo wakati anafungua mkutano ulioandaliwa na Chama cha Wakunga Tawi la Muhimbili, Dar es Salaam kujadili kuhusu matumizi ya njia bora za uzazi wa mpango.
Nyoni amesema,katika ziara zake za kutembelea hospitali mbalimbali za Serikali nchini, amekuta uchafu wa kutisha.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Serikali, uchafu huo unaweza kusababisha maambukizi mapya kwa akinamama hao. Aliwataka wakunga hao waache visingizio kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu.
Kwa mujibu wa Nyoni, Bohari Kuu ya Dawa (MSD), imenunua kila aina ya kifaa kinachohitajika katika hospitali za serikali.
“Jamani kwa hili naomba usafi kiwe kipau mbele chenu, nilienda pale Muhimbili hali niliyoikuta sikuifurahia; lakini wameniahidi kuwa nikirudi tena sitakuta ile hali ya uchafu,” amesema.
Nyoni pia aliwataka wakunga hao kuwa wawazi kwa wagonja wanaowahudumia ili kuweka ujirani kati yake na mgonjwa.
Amesema, kumekuwa na tabia ya wakunga kutokuwa wawazi kwa wagonjwa wao hivyo kumfanya mgonjwa kutokuwa na habari kamili kuhusu ugonjwa wake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment