Saturday, October 10, 2009

Kujitayarisha kabla ya Ujauzito


Kina mama na wanawake wanashauriwa kufanya matayarisho kabla ya kushika mimba. Imeonekana kuwa kufanya matayarisho kabla ya mimba haijatunga kuna faida kubwa kwa mama mwenyewe na mtoto anayezaliwa. Kuutayarisha mwili wa mama kabla hajabeba mimba, huifadhi afya ya mama wakati wa ujauzito hata baada ya kujifungua uwe na faya bora zaidi. Miongoni mwa matayarisho anayotakiwa kufanya mwanamke kabla ya kushika ujauzito ni pamoja na kupima magonjwa mbalimbali kama vile kisukari, presha na ugonjwa wa moyo ili kuona kama ana magonjwa hayo au la. Vilevile mama anashauriwa kujitahidi kuwa na uzito unaotakiwa kwa kuzingatia kimo chake. Yaani asiwe mnene au mwembamba sana kabla ya kubeba mimba bali awe na uzito wa wastani.
Suala hilo linaweza kutekelezwa kwa mwanamke anayetaka kubeba mimba kuhudhuria hospitalini au kuonana daktari mtaalamu wa masuala ya uzazi au mkunga. Daktari wa kawaida pia anaweza kutoa ushauri kuhusiana na suala hilo.
Mimba nyingi hutungwa bila kupangwa, suala ambalo mara nyingi hupelekea mama na hata mtoto aliye tumboni akabiliwe na hatari mbalimbali hasa wakati wa wiki 8 ya mwanzo ya ujauzito. Kwani wakati huo kina mama wajawazito huwa hawafahamu kuwa wana mimba, na wakati wanapotambua na kwenda hospitalini au kumuona daktari au mkunga, muda mwingi unakuwa umeshapita. Mwanamke anapokwenda hospitalini au kumuona daktari kwa matayarisho kabla ya kubeba mimba, huchunguzwa mambo mablimbali. Baadhi ya mambo hayo ni.
 Uzito aliokuwa nao, kama ni mnene sana hushauriwa kupunguza unene wake kwa kufanya mazoezi na kula vyakula vinavyotakiwa na kama ni mwembamba sana pia hushauriwa kuongeza uzito ili kufikia kiwango kinachotakiwa.
 Hupimwa magonjwa mbalimbali kama vile kisukari na kuangaliwa iwapo ana kisukari aina ya kwanza au ya pili.
 Hupimwa kama ana shinikizo la damu au la.
 Hushauriwa kutumia vidonge vya Vitamini E na C, kula vyakula vyenye Calcium, ufumwele, Magnesium na chuma (Iron).
 Hushauriwa kuanza kutumia vidonge vya Folic Acid na kula vyakula vinavyoweza kuupatia mwili wake mada hiyo. Imeonekana kuwa, Foic Acid humzuia mtoto aliyeko tumboni asipatwe na matatizo ya ubongo na mfumo wa fahamu. Mama mjamzito anashauriwa kuanza kutumia vidonge vyenye faida kubwa vya Folic Acid miezi mitatu kabla ya kutunga mimba.
 Kujiepusha au kupunguza kula vyakula vyenye Kafeini kama vile chai, kahawa, hot chocolate na vinywaji vyenye kafeini kama Coca Cola.
 Kujiepusha au kuacha uvutaji sigara.
 Kupima baadhi ya magonjwa ya kurithi na magonjwa mengineyo kama vile Talasemia, HIV na kadhalika.
 Kufanya mazoezi ili kuutayarisha mwili na kubeba ujauzito. Imeonekana kuwa kufanya mazoezi kabla ya kubeba mimba kuna faida nyingi kwa mama na mtoto anayezaliwa.

No comments: