Monday, October 19, 2009

Je wajua vyakula unavyokula kila kimoja kina umuhimu gain? Part1



Pengine methali hii kuwa "tunakula ili tuishi" si ngeni masikioni mwa wengi. Chakula kimekuwa na nafasi hai katika maisha yetu ya kila siku, kiasi kwamba tumelizoea jambo hilo na kuona kuwa ni mfululizo tu wa kila siku, bila kujali tunachokula au kutaka kujua vyakula tunavyokula vina umuhimu gani kwa afya zetu. Kwa kutambua umuhimu wa vyakula mbalimbali kwa miili yetu na afya zetu, kutasaidia tuweze kuchagua tule vyakula gani, na sufuria na sahani zetu kila siku zijae vyakula vya aina gani zinapokuwa mezani. Ama pale tunapoelekea sokoni, tuchague na kununua nini ili kuyajaza makapu yetu kabla ya kuelekea nyumbani kutayarisha chakula.
Katika sehemu hii ya kwanza tutaelezea baadhi ya faida zinazotokana na ndizi kwa ajili ya Afya zetu.
Ndizi:
Ndizi ni chakula kinachujulikana kama tiba asilia kwa matatizo mengi ya kiafya. Ukifananisha ndizi na tufaha (apple), ndizi zina protini mara nne zaidi, sukari mara mbili, potassium mara tatu vitamini A na chuma mara tano zaidi. Vile vile vitamini na madini nyinginezo hupatikana pia katika tunda hilo. Ndizi zina sukari asilia ya sucrose, fructose na glucose iliyochanganyika na ufumwele (fibre). Kwa kula ndizi unaupatia mwili nishati na nguvu ya haraka. Pia uchunguzi umeonyesha kuwa, kula ndizi mbili huweza kuupatia mwili nguvu za kutosha kwa ajili ya kujitayarisha kufanya mazoezi kwa dakika 90! Pengine ndio sababu, ndizi zikawa ni tunda la kwanza linalotumiwa zaidi kwa ajili ya wanamichezo hasa wanaokimbia mbio ndefu. Nishati sio kitu pekee chenye faida kinachoweza kupatikana kwenye ndizi kwa ajili ya miili yetu, bali pia huweza kusaidia miili kuzuia magonjwa na matatizo kadhaa.
Ndizi kwa kuwa na kiasi kikubwa cha chuma, husaidia kushajiisha uzalishwaji wa hemoglobin katika damu. na hivyo kusaidi kuondoa upungufu wa damu wa Anemia.
Ndizi kwa kuwa na kiwango cha juu sana cha potassium na kiasi kidogo cha chumvi, hulifanya tunda hilo lifae katika kupambana na shinikizo la damu (blood pressure).
Ndizi huweza kusaidia mwili katika kuimarisha uwezo wake wa kufyonza calcium, na hivyo kuifanya mifupa kuwa imara.
Imeonekana kwamba ndizi husaidia ubongo na kuongeza uwezo wa kujifunza na kufahamu mambo. Hivyo wataalamu wanashauri kuwa tunaweza kuwapa ndizi watoto washule wakati wa mitihani katika kipindi cha mapumziko, wakati wa chakula cha mchana au staftahi (breakfast).
Kwa kuwa na kiasi kikubwa ha ufumwele, ndizi husaidia tumbo kufanya kazi vyema na kupambana na matatizo ya choo au constipation.]
Kwa wale wanaosumbuliwa na ulevi na pale wanapotaka kuondokana na hali ya hangover, basi suluhisho lao ni ndizi. Kwa kunywa mchanganyiko wa ndizi, maziwa na asali (banana milkshake) wanaweza kuondokana haraka na hali ya ulevi.
Pale unapong'atwa na mdudu, kabla ya kutumia krimu ya kuua sumu ya wadudu, jaribu kusugua sehemu ya ndani ya ganda la ndizi pale ulipong'atwa. Kufanya hivyo husaidia kupunguza maumivu, uvimbe na kuwasha.
Ndizi zina kiasi kikubwa cha vitamin B, hivyo husaidia mfumo wa fahamu.
Kwa wanawake na wasichama wanashauriwa kula ndizi kabla ya siku zao za mwezi, kwani husaidia kukabilina na PMS au kutojisikia vyema kabla ya hedhi.
Ndizi zinaweza kuwasaidia wale wanaotaka kuacha kuvuta sigara.
Na kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya MIND, watu wenye matatizo ya msononeko wa mawazo na fikra, (depression) hujisikia vyema pale wanapokula ndizi. Hii ni kwa sababu ndizi zina tryptophan, ambayo ni aina ya protini inayobadilishwa mwilini na kuwa serotonini, mada ambayo huufanya mwili ujisikie vyema na kwa ujumla humfanya mtu asikie furaha.
Basi kwa kujua baadhi tu ya faida za ndizi, mtakubaliana na mimi kuwa ni muhimu tule ndizi kwa ajili ya afya zetu.
Lakini kumbuka kuwa, haushauriwi kula ndizi iwapo una ugonjwa wa kisukari na haifai kuhifadhi ndizi katika jokovu au friji kwani kufanya hivyo hupelekea ndizi kupoteza uwezo wake huo wa kitiba.
Haya shime na tusikose ndizi katika vyakula vyetu.

No comments: