Saturday, January 30, 2010

Chanjo inaweza kuwaokoa waathirika wa HIV wasife na TB


Wataalamu wamesema kuwa, wamepata chanjo inayoweza kuwasaidia wagonjwa wa TB ambao wameathirika na HIV. Chanjo hiyo inafanya kazi kwa kuupa nguvu mfumo wa kulinda mwili kwa wagonjwa ambao tayari waliwahi kupata chanjo ya BCG walipokuwa wadogo. Utafiti huo uliochapisha katika Jarida la AIDS umebainisha kuwa, wagonjwa wengi wenye Kifua Kikuu ambao walipewa chanjo hiyo walionekana kupata nafuu. Wataalamu hao kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Dartmouth cha Marekani wamejaribu chanjo hiyo kwa waathirika wa Ukimwi elfu mbili nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka 7 na kuthibitisha kwamba, ugonjwa wa TB uliweza kupunguzwa kwa asilimia 39 kwa wale waliopatiwa chanjo hiyo. Wataalamu hao wanasema kuwa, chanjo hiyo inaweza kuwa chaguo lisilogharimu fedha nyingi hasa kwa nchi zinazojitahidi kutafuta fedha kwa ajili ya kununua madawa ya kupambana na HIV. Chanjo hiyo inasemekana kuwa na uwezo zaidi wa kumlinda mgonjwa asipate kifua kikuu, pia inaweza kumlinda mgonjwa kwa miaka kadhaa. Profesa Ford von Reyn aliongoza utafiti huo, amesema hiyo ni hatua kubwa na kushauri kuwa, pale watu wanapogunduliwa wameathirika na HIV wanaweza kupewa chanjo hiyo, kabla hata ya kuanza kutumia vidonge vya kuongeza maisha ya antriretroviral. Reyn aidha amesema kwamba hii ni mara ya kwanza wamefanikiwa kupata chanjo ambayo ina athari kubwa katika kuzuia magonjwa yanayosababishwa na vijidudu vinavyowashambulua wagonjwa pale wanapokuwa na UKIMWI.
Ni muhimu kujua kuwa, Kifua Kikuu ni tatizo kubwa kwa watu wanaoishi na virusi vya HIV barani Afrika. Ugonjwa wa Tb unaongoza katika kuwasababishia vifo waathiriwa wa Ukimwi. Shirika la Afya Duniani linakadiria watu milioni 10 wana ugonjwa wa Kifua Kikuu pamoja na UKIMWI duniani, ambapo wengi wao wanaishi katika nchi za Afrika zilizoko chini ya Jangwa la Sahara. TB inaua kila mgonjwa mmoja kati ya watatu ambao wana UKIMWI.

Friday, January 29, 2010

Vidonge vya kuzuia mimba baada ya siku 5 vyaingia madukani


Vidonge vya kuzuia mimba kwa dharura (the morning after pills) zimeingia madukani, ambapo inaaminiwa dawa hizo zina uwezo wa kumzuia mwanamke asipate mimba hata baada ya kuzitumiwa ikiwa siku 5 tayari zimepita baada ya kujamiina. Uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa Uingereza umegundua kuwa, daw ahizo mpya zina uwezo zaidi wa kuzuia mimba kuliko zile za zamani ambazo zilikuwa zikizuia mimba hadi baada ya siku tatu tu toka wakati wa kufanya mapenzi. Kwa kawaida dawa za kuzuia mimba kwa dharura au emergency contraception zinatumia homoni ambazo aidha huzuua yai lizitoke katika ovari masaa kadhaa baada ya kujamiiana, au kuzuia yai lisijikite katika mfuko wa uzazi.
Si vibaya hapa nielezee vidonge vya kuzuia mimba kwa dharura ni dawa za aina gani?
The Morning after pills ni vidonge ambavyo huzuia mtu asipate mimba iwapo hakutumia njia yoyote ya kuzuia mimba kabla au wakati wa kufanya tendo la ndoa. Ingawa dawa hizo zinajulikana kwa vidonge vinazotumiwa asubuhi kama lilivyo jina lake lakini kihakika dawa hizo huwa na uwezo wa kumzuia mtu asipate ujauzito kwa muda wa masaa 72 au siku 3 kwa kawaida (Huku zile mpya nilizoungumzi hapo juu zikiweza na uwezo wa kuzuia mimba hadi siku 5). Lakini dawa hizo kila zinapotumiwa mapema zaidi baada ya tendo la ndoa, matokeo yake huwa bora zaidi. Vidonge hivyo hufanya kazi vizuri zaidi vinapotumiwa katika masaa 12 baada ya kufanya mapenzi bila kujikinga. Dawa hizo huwa zina homoni inayoitwa Lovenorgestrel ambayo ni moja ya vitu vilivyoko katika vidonge vya kawaida vya kuzuia mimba (contraceptive pills). Unaweza kuapata vidonge hivyo katika vituo vya afya au mahospitalini.
Uingereza na katika nchi nyingi za Ulaya vidonge hivyo huitwa 'emergency contraceptive pill' wakati Wamarekani na nchi nyinginezo huviita 'The Morning After Pill'.
Viodnge vya kuzuia mimba baada ya kujamiina kwa kawaida husaidia kwa asilimia 100 kutopata mimba, na kushindwa kwake ni kwa asilimia chache.
Vidonge hivyo vinatumika katika masuala mbalimbali kama vile:
1. Kuwazuia kupata mimba wanawake waliofanya mapenzi bila kujikinga kabla au bila kutumia kizuizi chochote wakati wa tendo la ndoa.
2. Kwa wale waliobakwa, na kuna hatari kwamba wanaweza wakapata mimba.
3. Kwa mke na mume au wale wapenzi ambao wakati wa kujamiiana condom ilipasuka.
4. Kwa wale waliofanya ngono zembe kwa kushawishiwa, wakiwa wamelewa au kutumia madawa ili kuwazuia wasibebe mimba.
Kumbuka kuwa, hakuna hatari yoyote kutumia dawa hizo. Lakini ni bora upate ushauri wa mtaalamu kabla ya kutumia. Ni asilimia chache sana ya wanawake ambao hupata matatizo madogo madogo baada ya kutumia dawa hizo kama yale wanayoyapata wakati wa kutumia vidonge vya kuzuia mimba vya kawaida. Matatizo hayo ni kama vile.
Maumivu ya kichwa kidogo.
Tumbo kuuma kidogo
Maziwa kuuma kidogo.
Kuona matone ya damu kidogo.
Kujisikia kizunguzingu kidogo.
Ni muhimu pia kujua kuwa, kuna wanawake ambao hawaruhusiwi kabisa kutumia dawa hizo na hao ni wale ambao wana matatizo ya figo au wale wenye matatizo yanayoitwa porphyria.
KUMBUKA KUWA KUZUIA MIMBA NI BORA KULIKO KUTOA!
Na daima tunza Afya yako!

Wednesday, January 27, 2010

Bill Gates aahidi ulimwengu kupata kinga ya Malaria miaka mitatu ijayo


Bill Gates mgunduzi wa Microsoft amesema kwamba kinga ya Malaria itakuwa tayari baada ya miaka mitatu ijayo. Gates anaongoza kampeni za kupambana na ugonjwa wa Malaria, ambao unasababisha vifo vya mamilioni ya watu duniani kila mwaka hasa watoto wadogo. Bili Gates anaamini kuwa kama ilivyokuwa kwa ugonjwa wa ndui, Malaria pia inaweza kutokomezwa. Hata hivyo mpaka hivi sasa hakujapatikana kinga yoyote ya ugonjwa huo, lakini Gates ana matumain kwamba kinga hiyo itagunduliwa hivi karibuni. Gates ambaye ameunda taasisi inayotumia mabilioni ya dola kupambana na ugonjwa wa Malaria, amesema kuwa hivi sasa kuna kinga ambayo inafanyiwa majaribio ya mwisho, na kinga ya muda inaweza kuanza kupatikana baadaya miaka mitatu, lakini kinga kamili ya ugonjwa huo itaweza kuchukua hadi miaka 10 kutengenezwa. Hata hivyo Gates ambaye anaaminika kuwa tajiri zaidi duniani, ametahadharisha kwamba, ana wasiwasi nchi zinazoendelea zitatumia fedha zao zote zinazotokana na misaada ya kigeni katika kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa, na kupuuza masuala ya afya. Gates amesema kwa mtazamo wake suala hilo ni makosa na kwamba viongozi wa nchi zinazoendelea wanapaswa pia kuboresha hali ya afya ya wananchi wao na kwa upande mwingine kujitahidi kudhibiti kukua kwa idadi ya watu, suala ambalo lina athari kubwa kwa mabadiliko ya hali ya hewa.
 Malaria ni moja ya magonjwa yanayosabaisha vifo vingi sana duniani hasa katika bara la Afrika.
 Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani, ugonjwa huo unasababishwa vifo vya watu kati ya milioni 1.5 hadi 2.7 kila mwaka duniani. Watoto walio chini ya miaka mitano ndio wanaoathirika sana na ugonjwa huo, huku zaidi ya watu milioni moja wakifariki kila mwaka barani Afrika kutokana na ugonjwa wa Malaria.
 Miongoni mwa vimelea vinavyosababishwa ugonjwa wa Malaria Plasmodium Falciparum ndio kijidudu inachosababisha malaria mbaya zaidi, na kila uchao kimeleo hicho huzidi kukwepa dawa za malaria na kujiimarisha.
 Si vibaya kutambua kwamba, Malaria inauwa watu 8,000 nchini Brazil kila mwaka, hii inamanaisha kwamba ugonjwa huo unaua watu wengi zaidi nchini humo ikilinganishwa na idadi ya watu wa nchi hiyo wanaokufa kutokana na UKIMWI pamoja kipindupindu.
 Gharama inayotumika kutibu ugonjwa wa Malaria barani Afrika kwa mwaka ni zaidi ya dola bilioni 3.

Monday, January 25, 2010

Kula Blueberry kunaongeza uwezo wa ubongo


Utafiti mpya umegundua kuwa, kunywa vikombe viwili na nusu vya juisi ya blueberry kwa siku ( mie naziita kunazi za bluu) kunaongeza uwezo wa ubongo wa kufahamu, na kuondoa matatizo ya usahaulifu yanayotokana na utu uzima. Wataalamu wanasema kuwa kunywa kila siku juisi hiyo kunamzuia mtu uwezekano wa kupatwa na ugonjwa wa kupoteza akili uzeeni au wendawazimu. Blueberry kwa kuwa na kiwango kikubwa cha phytochemical, tunda hilo lina limejaa anti oksidanti na lina uwezo wa kuzuia uvimbe. Vilevile kunazi za bluu kwa kuwa na mada iitwayo Anthocyanin, huweza kusaidia kuongeza kumbukumbu katika ubongo. Pia tunda hilo husaidia kupunguza kasi ya kitendo cha kupungua kumbukumbu katika ubongo kwa kuondoa gulukosi zinazopatikana kwenye ubongo. Uchunguzi huo umebaini kwamba, kula blueberry kupitia vidonge maalum vya kusaidia afya au supplements kunaweza kumpatia mtu faida kubwa katika ubongo. Hata hivyo wataalamu hao wameshauri kuwa ni bora tunda hilo liliwe katika hali ya kawaida.
Huko nyuma pia wataaamu walieleza kuwa, Blueberry husaidia kupunguza usongo wa mawazo pamoja na kiwango cha juu cha gulukosi katika damu.
Haya tena wadau…usichelewa kula tunda hili, najua katika nchi zetu za Afrika tunda hili halipatikana na ndio sababu hata jina lake katika kamusi yetu haliko, lakini usife moyo unaweza kupata tunda hilo madukani na katika supermarkets ambapo huhifadhiwa katika makopo au kama juisi. Kwa wale walioko ughaibuni basi hakuna tabu hiyo na usikose kula tunda hilo tamu wakati wa msimu wake na wakati miwngine wowote.
Daima tuzilinde afya zetu!

FDA yathibitisha na kuitangaza dawa ya kwanza ya kutibu ugonjwa wa MS


Shirika la Kusimamia Chakula na Madawa la Marekani la FDA limethibitisha na kuipitisha dawa ya kwanza iliyotengenezwa kwa ajili ya kutibu tatizo la kutembea kwa wagonjwa wa MS (Multiple Sclerosis). Multiple Sclerosis ni ugonjwa wenye kuudhoofisha mwili kwa kiasi kikumbwa ambapo mfumo wa kulinda mwili hushambulia mfuko unaohifadhi mfumo wa kati wa neva au central nervous system, na kusababisha mwili kufa ganzi na kupooza. Wagonjwa wa MS huwa wanapoteza uwezo wa kutembea na hata kuhitajia msaada wa kibaiskeli ili waweze kutembea. Kwa bahati mbaya hakuna tiba ya ugonjwa huo, ambao unawapata karibu watu milioni 2.5 duniani kote hasa watu wazima. Kwa mujibu wa FDA, wagonjwa wa MS waliopewa dawa hiyo inayojulikana kama Ampyra yenye jina la kitaalamu la Dalfampridine, wameweza kutembea vizuri. Wagonjwa hao wameweza kutembea masafa marefu, kusimama kwa muda mrefu na hata kupanda ngazi kwa urahisi. Watengenezaji wa dawa hiyo wana matumaini kuwa dawa hiyo itaanza kuingia madukani hivi karibuni.

Saturday, January 23, 2010

Mungu Ni Mkubwa


Ingawa sio kawaida yangu kuposti picha au kuzungumzi masuala ambayo si masuala ya Afya, lakini picha hii imenivuta na nikashindwa kuikalia kimya... Kweli Mungu Mkubwa

Friday, January 22, 2010

Je, Madawa ya Kudhibiti Virusi vya Ukimwi Yanasaidia Vipi Kuzuia Ukimwi?


Leo nitazungumzia kuhusu dawa za kurefusha maisha ya waathirika wa ukimwi yaani ARV.
Madawa haya huitwa Antiretroviral therapy (ARVs) kwa lugha ya Kiingereza. Dawa hizi hupigana dhidi ya virusi vinavyosababisha ukimwi. Madawa haya huwasaidia wale walio na virusi hivi kukaa katika afya nzuri. Aina nyingine ya madawa haya ni Protease Inhibitors. Aina hii huzingira virusi na kuzizuia kuzaana. Aina mbili hizi za madawa zikitumiwa pamoja, hupunguza idadi ya virusi hivyo na mwishowe hupunguza idadi ya vifo. Takwimu zinaonyesha kuwa watu wengi waliotumia mchanganyiko huo wamepata nafuu. Mfano watu wengine walikuwa wameshindwa kufanya kazi, lakini wameweza kurudi makazini baada ya kutumia madawa hayo.
Matibabu kwa Kutumia Aina Moja ya Dawa (Monotherapy)
Matibabu mengine ya haya ya kutumia dawa aina moja tu. Matumizi haya hupunguza hatari ya kuambukiza virusi hivyo. Kwa mfano kutoka kwa mama hadi kwa mtoto wake mchanga. Tiba ya aina hii haitumiwi sana kwa sababu, mwili hujenga kinga dhidi ya aina moja ya dawa baada ya muda fulani.
Matibabu kwa Kutumia Mchanganyiko wa Madawa (Combination Therapy)
Matumizi ya aina mbili au zaidi wa dawa hizo hutumika kuwasaidia watu wenye ukimwi. Hii ni kwa sababu aina mbali mbali za madawa hupigana na virusi kwa njia tofauti, na kwa hivyo huwa na mafanikio zaidi zinapotumiwa kwa pamoja. Kuna mchanganyiko wa aina tofauti, lakini madawa mengine hayawezi kutumiwa kwa pamoja kwani, yanafanya kazi kinyume cha madawa mengine. Madawa ya aina hiyo yanaweza kutumiwa na watoto kwa kiasi fulani. Lakini ni vyema tukumbushe hapa kuwa watu wengi wanaendelea kuambukizwa virusi ivya ukimwi barani Afrika hasa katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara. Na Imeelezwa kuwa nusu ya maambukizo hayo huwakumba watu wasio na uwezo wa kununua madawa hayo pamoja na kushindwa kuyatumia inavyopasa.
Je utumiaji wa dawa hizo unaweza kuwa njia ya kuzuia ukimwi?
Matumizi ya madawa haya yanaweza kuwa njiai ya kuzuia kuenea kwa ukimwi kwa njia mbili. Mosi kwa kuwatibu watu walioingia kwenye hatari ya kupata ukimwi au kuwapa nafuu watu walio na virusi ili kuzuia maambukizo zaidi kwa wapenzi wao.
Matibabu ya Kuzuia Uambukizo Mara Mtu Anapoingia Katika Hatari (Yaani Post-Exposure Prophylaxis) PEP
Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kuwa, utumiaji wa dawa za AZT mara tu baada ya kudungwa sindano iliyo na damu yenye virusi vya ukimwi, umepunguza maambukizo kwa asilimia 79. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, hatari ya wauguzi au matabibu kupata ukimwi baada ya kudungwa na sindano iliyo na damu yenye virusi hivyo ni karibu asilimia 0.32. Hatari ya kupata ugonjwa kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya kwa sindano au kwa kufanya mapenzi, ni kubwa mno pia. Inakadiriwa kwa wale wote wanaofanya mapenzi kwa kutumia sehemu ya haja kubwa wana hatari ya kuambukizwa virusi vya ukimwi kutoka kwa mpenzi aliye na vyo kwa asilimia 0.5 hadi 3 na wale wanaotumia njia ya kawaida kwa asilimia 0.1. Aidha hatari ya kupata ugonjwa wa ukimwi kwa kutumia pamoja sindano ya madawa ya kulevya ni asilimia 0.4 hadi 3.
Nukta ya Kuzingatia:
Matumizi ya madawa haya ya kuongeza muda wa kuishi kwa waathirika wa ukimwi yanahitaji mgonjwa kula chakula bora kila mara, chakula ambacho kinaambatana na madawa haya. Mgonjwa pia anapaswa kunywa maji mengi na kuhakikisha kwamba anahifadhi dawa hizi katika mazingira mazuri. Kwa hiyo dawa hizi hutumiwa na wale walioambukizwa virusi vya HIV baada ya kupima na kushauriwa kiutaalamu hospitalilini au kwenye kituo cha afya na huanza kutumia madawa hayo kulingana na namna alivyoathirika. Mgonjwa anaweza k kutumia madawa haya kwa uarahisi, lakini bado kuna gumu kwa wagonjwa wengi wanaoishi katika hali duni ya maisha. Hofu ya kudhulumiwa, kushukiwa na kubaguliwa yote hayo huwafanywa wagonjwa wengi barani Afrika wakatae dawa hizo za ARV,s.

Thursday, January 21, 2010

Siri ya kuishi maisha marefu


Kundi moja la wataalamu wa moyo limeelezea masuala muhimu ambayo yanamsaidia mtu kuishi maisha marefu kama ifuatayo:-
1. Jiweke mbali na sigara.
2. Epuka unene.
3. Fanya mazoezi.
4. Kula lishe bora.
5. Hakikisha unacheki na kupima kiwango cha kolestero mwilini, shinikizo la damu na sukari na kuhakikisha viko katika kiwango kinachotakiwa.
Uchunguzi huo umeonyesha kwamba watu wengi umri wa kuanzia miaka 50 ambao wanaishi kwa kufuata masharti hayo huwa na uwezo wa kuishi miaka 40 zaidi bila kupata shinikizo la damu na ugonjwa wa moyo, ambayo ni magonjwa makuu mawili yanayoua watu zaidi duniani. Wataalamu wamesema kwamba, kila mtu anayetaka kuishia maisha marefu anatakiwa kufuata ushauri ufuatao:
• Jiepushe kuvuta sigara au acha kuvuta sigara kabisa.
• Hakikisha BMI yako haizidi 25.
• Kila wiki pata dakika zisizopungua 150 za kufanya mazoezi ya kawaida.
• Jitahidi kufuata maelekezo ya kula lishe bora ambayo ni: vikombe 4 na nusu vya matunda na mboga mboga kwa siku, samaki mara mbili au tatu kwa wiki. Usinywe sana vinywaji vyenye sukari, kula vyakula vyenye ufumwele kila siku na chumvi isizidi miligram 1,500 kwa siku.
• Kiwango cha kolestero au mafuta katika damu yako kisizidi 200.
• Shinikizo lako la damu lisiwe zaidi ya 120 chini ya 80.
• Sukari katika damu iwe chini ya 100.

Wednesday, January 20, 2010

Jinsia ya mtoto kupimwa kwa kupitian damu


Uchunguzi mpya umeonyesha kwamba, wazazi wataweza katika siku zijazo kujua jinsia ya watoto wao ambao bado hawajazaliwa wakati wa ujauzito kwa kupimwa damu. Kwa kawaida kipimo cha Utrasound huweza kuonyesha jinsia ya kijusi ( fetus) wakati wa miezi mitatu ya pili ya ujauzito. Hivyo, pale inapotakiwa kujua jinsia ya mtoto atakayezaliwa katika wakati wa mwanzo wa ujauzito kutokana na sababu za kitiba, huwa inabidi zitumike njia nyinginezo ambazo ni ngumu zaidi kama vile kupimwa homoni na mada ziliozoko katika maji yanayomzunguka mtoto tumboni au amniocentesis, njia mbayo baadhi ya wakati huweza kuifanya mimba itoke.
Lakini kumepatikana matumaini mapya ya kujua kwa urahisi na mapema jinsia ya mtoto aliyeko tumboni, baada ya uchunguzi uliochapishwa katika jarida la Magonjwa ya Wanawake na Uzazi kueleza kuwa, kipimo hicho cha damu ya mama mjamzito, kinachoweza kufanywa mapema katika wiki ya 7 ya ujauzito, kinaweza kuonyesha kwa uhakika jinsia ya mtoto kijusi. Katika majaribio mbalimbali kipimo hicho kimeonyesha kuwa sahihi kwa asilimia 100, kwa kutumia jeni mbili zinazopatikana katika kromozomu ya jinsia ya Y.
Wataalamu wanaamini kwamna kipimo hicho kitaanza kutumika hivi karibuni na kuchukua nafasi ya njia nyinginezo ngumu na zenye hatari, ili kujua jinsia ya mtoto aliyeko tumboni mapema wakati wa ujauzito, na kusaidia kuamua iwapo mimba itolewe au istolewa pale inapogunduliwa kuwepo kwa baadhi ya magonjwa ya kurithi yanayoambatana na jinsia.

Monday, January 18, 2010

Kwikwi husababishwa na nini?


Baada ya kusoma makala inayohusu kijana mmoja aliyesumbuliwa na kwikwi kwa zaidi ya miaka miwili na nusu, na baadaye kutibiwa tatizo hilo kwa kufanyiwa upasuaji wa ubongo na kutolewa tezi, nimeamua leo nizungumzie kwikwi.
Kwiki ni kitendo kisichozuilika ambacho hutokana na kusinyaa kwa kuta za kiwambo cha moyo au diaphragm. Kwa kawaida kwikwi ni kitendo kinachojirudia rudia mara nyingi. Sauti ya 'hic' inayotokea wakati unapokuwa na kwikwi husababishwa na kidaka tonge (epiglottis) ambacho hufunga haraka wakati hewa inapoingia kwenye koo. Kupiga kwikwi kwa kawaida hakuna maumivu lakini mara nyingine husumbua hasa inapoendelea kwa muda mrefu. Kwikwi ya kawaida huweza kutulizwa kwa kunywa maji, lakini wakati mwingine kufanya hivyo hakusaidii.
Zifutazo ni sababu zinazoweza kukuletea kwikwi
1. Kula kwa haraka.
2. Kula chakula cha moto na kunywa maji baridi baada yake.
3. Kulia au kukasirika.
4. Kula chakula chenye viungo vingi au pilipili.
5. Kula chakula cha moto sana.
6. Kunywa pombe au soda kwa wingi.
7. Kukohoa sana.
8. Kucheka kupita kiasi.
9. Kufurahi sana, kusisimka au kupatwa na msituko.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, vitu ambavyo vinakiletea karaha kiwambo cha moyo au diaphragm husababisha kwikwi. Kuna sababu nyingi ambazo husababisha jambo hilo na hizo tulizotaja hapo juu ni miongoni mwazo,ambapo matokeo yake ni humfanya mtu apige kwikwi. Kwikwi kwa kawaida huisha baada ya dakika chache au hata sekunde. Lakini iwapo kwikwi itaendelea kwa masaa au kwa siku, huweza kuwa ni tatizo muhimu la kitiba na pengine hali kama hiyo inaweza ikawa inasababiswa na ugonjwa.
Kuna baadhi ya watu hupata kwikwi sana wakati wa ujauzito, baada ya kufanyiwa operesheni na hata watoto wachanga pia hupatwa na kwikwi mara kwa mara. Wajawazito hupata kwikwi sana mwishoni mwa miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito na mwanzoni mwa miezi mitatu ya pili. Kwikwi hutokea wakati wa ujauzito ni kwa sababu wakati huo uwezo wa kuvuta hewa ndani ya mapafu na kutoa nje huongezeka kwa asilimia 30 hadi 40 ikilinganishwa na hali ya kawaida. Hakuna sababu inayojulikana inayosababisha kwikwi kwa watoto wachanga, na wazazi wanashauriwa wasitiwe hofu na suala hilo. Hii ni katika hali ambayo kwikwi baada ya upasuaji husababishwa na nusu kaputi au anesthesia.

Liche ya Mediterani huzuia hatari ya kupatwa na kensa ya tumbo


Uchunguzi mpya umebaini kuwa, lishe ya Mediterani inaweza kusadia kupunguza uwezekano wa kupatwa na kensa ya tumbo. Lishe hiyo pia ina faida mbalimali kwa afya. Lishe ya Mediterani pia inapunguza hatari ya kupatwa na magonjwa kadhaa kama vile kisukari, magonjwa ya kuzaliwa, magonjwa ya mishipa ya damu, Alzheimer, msongamano wa mawazo na fikra,(depression) uvimbe na vifo vya watoto wachanga. Lishe ya Mediterani ni lishe yenye matunda, mboga mboga, ufumwele samaki, nafaka, mafuta ya zaituni huku nyama nyekundu na vyakula vinavyotokana na maziwa vikiwa kwa uchache.
Inaaminiwa kwamba, lishe nya namna hiyo inamlinda mtu asipatwe na kensa ya tumbo, huku ikisisitizwa kwamba lishe za aina nyinginezo huongeza hatari ya ugonjwa huo. Saratani ya utumbo ni saratani ya pili inayowapata watu kwa wingi ulimwenguni, na wataalamu wanasema kuwa kula lishe ya Mediterani hupunguza uwezekano wa kupatwa na kensa hiyo kwa asilimia 33.
Wataalamu wanawahusia watu kula vyakula ambavyo ni bora kwa afya zao na kuvijua vyakula ambavyo vinawalinda watu wasipatwe na magonjwa mbalimbali kama huo wa saratani ya tumbo.

Saturday, January 16, 2010

Je… Waijua homa?.... sehemu ya kwanza


Homa hutokea pale joto la mwili linapopanda. Kitaalamu joto la mwili hupanda pale linapozidi nyuzi joto 37 au Farenheit 98.6 kwa kipimo kinachokuliwa mdomoni au nyuzi joto 37.2 au Farenheit 99 kwa kipimo kinachochukuliwa katika makalio (rectal temperature). Hata hivyo kipimo cha wastani na joto la mwili huweza kupanda au kupungua kwa nyuzi joto 0.6 au Farenheit 1 kutoka Farenheit 98.5. Joto la miwli huweza kuongezeka kwa nyuzi joto 0.6 au Farenheit 1 wakati wa mchana. Kwa hivyo homa haichukuliwi kuwa ni hatari hadi pale joto la mwili llinapozidi nyuzi joto 38 au Farenheit 100.4. Homa inasaidia mwili kujilinda na bakteria na virusi ambavyo haviwezi kuishi katika joto kali. Kwa sababu hiyo, joto la chini kwa kawaida halitibiwi, hadi pale linapoambatana na dalili mbalimbali nyinginezo. Homa ni dalili mojawapo ya ugonjwa, na mara nyingi haizingatiwi hadi pale inapoandamana na dalili nyinginezo kama kukohoa, kuvimba koo, maumivu na kadhalika. Homa ya kufikia nyuzi joto 40 au Farenheit 104 inahitajia matibabu ya haraka, kwani isipotibiwa huweza kusababisha matatizo ya ubongo yanayopelekea kutapatapa usingizini kama vile kuota njozi au mawenge, pamoja na degedege hasa kwa watoto.
Themometa za dijitali zinaweza kutumika kupima joto kwa njia ya mdomoni, kwapani au katika makalio. Wataalamu wanashari ni bora isitumiwe themometa ya glasi yenye mekyuri, na ni bora wazazi wasiwe na themometa za aina hizo majumbani ili kuzuia hatari ya mada hiyo hatari yenye sumu.
Ni muhimu kutambua kuwa kipimo cha joto kinachochukuliwa kwapani si sahihi sana kikilinganishwa na kile cha mdomoni na makalioni (rectal) na kwa kawaida huwa pungufu kwa nyuzi joto moja kuliko kile kinachochukuliwa mdomoni.
….makala hii inaendelea.

Thursday, January 14, 2010

Umbo la kibantu hoyee… makalio makubwa na mahips bora kwa afya


Haya tena ukishangaa ya Musa utaona ya Firauni!...uchunguzi uliofanywa nchini Uingereza umeendelea kulipandisha chati umbo la kibantu, kwa kusema kwamba, kuwa na unene zaidi eneo la mapajani, katika makalio na katika mahips ni vizuri kiafya, na humzuia mtu asipate matatizo ya kiafya.
Wataalamu wanasema kuwa, mafuta yanayopatikana katika mahips, huondoa fati asidi mbaya kiafya ambazo huwa na mada za kuzuia uvimbe ambazo huifanya mishipa ya damu isizibe. Timu hiyo ya wachunguzi imesema kuwa, makaliao makubwa ni bora kuliko mafuta ya zaida yanayojilundika katika mzunguko wa kiuno, ambayo hayasaidii chochote. Wachunguzi hao wamesema katika Jarida la Kimataifa la Obesiti kwamba, sayansi inapaswa kuangalia jinsi ya kuongeza mafuta katika eneo la mahips na pengine katika siku zijazo madaktari watatakiwa kuangalia njia za kuyahamisha mafuta mwilini na kuyapalekea katika sehemu za mahips ili kulinda afya za watu kutokana na magonjwa ya mishipa ya moyo na magonjwa mengineyo kama kisukari. Watafiti hao wameeleza kuwa, kuwa na mafuta kidogo katika hips kunaweza kupelekea matatizo makubwa ya umetaboli.
Wataalamu hao wameendelea kusema kwamba, ushahidi unaonyesha kwamba, mafuta yanayozunguka mapaja na sehemu za nyuma ni vigumu kuyeyuka kuliko yale yaliyo katika kiuno. Ingawa suala hilo linaonekama kana kama ni kinyume, lakini ni kweli kwamba kutoyeyuka huko kuna faida kwani, wakati mafuta yanapoyeyuka kwa urahisi hutoa mada inayoitwa cytokines ambayo huleta uvimbe katika mwili. Mada za cytokines zinahusiana moja kwa moja na magonjwa ya moyo na kisukari. Kuyeyuka taratibu kwa mafuta katika mapaja pia husababisha homoni ya adiponectin izalishwe kwa wingi na husaidia kudhibiti sukari katika damu na jinsi mafuta yanavyochomeka. Kuwa na mafuta mengi katika mzunguko wa tumbo na kuwa na umbo mviringo kama 'tufaha' kunaongeza hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo na sukari. Dakta Konstantinos Manolopoulos aliyeongoza utafiti huo kutoka chuo kikuu cha Oxford amesema kuwa, la muhimu ni umbo na wapi mafuta yanakusanyika, na kwamba unene wa mahips na mapaja ni mzuri kuliko unene wa tumbo.
Ameongeza kuwa, katika ulimwengu wa kawaida pia watu huonekana vyema wanapokuwa wanene mapajani, iwapo tu tumbo linakuwa dogo. Daktari huyo ameeleza kuwa, uchunguzi huo umewasaidia kufahamu vyema mafuta katika mwili ili kutafuta mikakati mipya ya kupunguza magonjwa ya moyo na mishipa ya damu. Iwapo mtu ana uzito mkubwa au ni mnene, au pale anapohisi kuwa mzunguko wa kiuno chake umeongezeka, ni muhimu kuanza kufanya mabadiliko ya jinsi anavyoishi kwa kula lishe bora na kufanya mazoezi ili kupunguza uwezekano wa kuapata matatizo ya moyo.

Wednesday, January 13, 2010

Chai ya kijani yaendelea kupigiwa debe kiafya



Huku chunguzi kemkem zikiendelea kuonyesha faida ya kunywa chai ya kijani au kwa kimombo green tea, wataalamu wa ugonjwa wa kensa wa Chuo Kikuu cha Taiwan wametangaza kwamba, kunywa chai ya kijani kunazuia kensa ya kifua. Utafiti huo unaofanywa kwa kuwashirikisha watu zaidi ya 500 unaongezea nguvu ushahidi unaosema kuwa, chai hiyo ina uwezo wa kuzuia kensa. Katika utafiti huo, watu wanaovuta sigara na wale wasiovuta ambao walikunjwa kikombe kisichopungua kimoja cha chai kijani kwa siku, walipunguza uwezekano wa mapafu yao kupatwa na kensa. Hata hivyo wataalamu hao wamesema kwamba, utafiti huo mpya haumaanishi kwamba sigara sio hatari kwa afya.
Chai ya kijani hutengenezwa kutoakana na majani makavu ya mmea wenye asili ya bara Asia unaoitwa Camellia sinesis, na hunywewa sana katika bara la Asia. Imeripotiwa kuwa kuna idadi ndogo ya wagonjwa wa saratani barani Asia ikilinganishwa na sehemu nyinginezo duniani, suala ambalo linafungamanishwa na unywaji wa chai ya kijani.

Kuangalia televisheni muda mrefu kunapunguza umri


Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kwamba kuangalia televisheni kwa zaidi ya masaa mnne kwa siku kunapunguza umri. Wataalamu wa Australia wamegundua kwamba, watu ambao hukaa kwa muda mrefu wakitazama televisheni, wanakabliwa na hatari kubwa ya kupatwa na matatizo ya afya hasa magonjwa ya mishipa ya damu, suala ambalo huhatarisha maisha yao na kuwapunguzia umri. Wanasema kwamba, kukaa muda mrefu mbele ya TV kuna hatari kubwa kwa maisha ya mtu kutokana na kuwa shughuli za kawaida za mtu ambazo ni pamoja na kusimama na kutumia misuli ya mwili huwa hazifanywi na mtu hukaa tu chini. Wataalamu hao wameelezea kuwa, watu wengi kwa siku hujongea tu kutoka kiti kimoja hadi kingine, kutoka katika gari kuelekea ofisini na kutoka katika kiti cha ofisini hadi nyumbani katika kiti kingine mbele ya televisheni.
Uchunguzi huo umetahadharisha kwamba, hata watu wenye afya zao za kawaida wanaweza wakawa wanakabiliwa na hatari kubwa kutokana na kukaa kwa muda mrefu suala ambalo huathiri kiwango cha sukari na mafuta katika damu. Hatari ya kukaa kwa muda mrefu haiwezi kuondolewa kwa kuanza kufanya mazoezi, kwani uchunguzi huo umegundua kuwa, hata watu wanaofanya mazoezi, iwapo wanaangalia tv kwa muda mrefu, pia wana hatari ya kuwa na maisha mafupi.

Monday, January 11, 2010

Matatizo ya Homoni huwafanya wakinamama wasipende kunyonyesha


Wakinamama wasiopenda kuwanyesha watoto wao wamekuwa wakitupiwa lawama nyingi katika jamii, lakini uchunguzi mpya umeonyesha kwamba huenda hali hiyo ikawa inasababishwa na matatizo la homini mwilini. Kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa katika Jarida la Uzazi na Magonjwa ya Wanawake la Scandinavia, kiwango cha juu cha homini za testosterone za kiume wakati wa ujauzito, hupelekea wakinamama wasijisikie kunyonyesha baada ya kujifungua. Homoni za testosterone zina athari hasi katika ustawi wa tishu za matezi ya matiti ya kinamama, suala mbalo huathiri uwezo wa mama wa kumnyonyesha mwanaye.
Chunguzi nyingi zimeeleza kumnyonyesha mtoto kuna faida tele kwa afya ya mama na mtoto, huku watoto wanaonyonyeshwa na maziwa ya mama wakionekana kuwa na afya zaidi na kutopatwa na hatari ya kuwa na unene wa kupindukia, wakilinganishwa na wale wanaopewa maziwa ya kopo. Kunyonyesha pia humzuia mtoto asipatwe na magonjwa ya moyo, kisukari, magonjwa kadhaa ya kifua, masikio, shinikizo la damu, ugonjwa wa ngozi (eczema), upungufu wa damu na asthma, huku kukimzuia mama kupata kensa ya matiti.
Uchunguzi huo lakini umesema kuwa, kwa ujumla afya ya watoto wanaopewa maziwa ya kopo haina tofauti sana na ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama. Hivyo wakinamama wasioweza kunyonyesha kutokana na sababu mbalimbali wasijisikie vibaya kutokana na suala hilo, na bora tu kuhakikisha kuwa afya ya mtoto inalindwa vyema.

Operesheni ya kwanza duniani ya moyo kwa kutumia MRI yafanywa Uingereza


Mtoto wa kiume wa miaka 6 nchini Uingereza amekuwa mtu wa kwanza duniani, kufanyiwa operesheni ya kupanua chemba ya moyo kwa kutumia muongozo wa MRI badala ya kutumia taswira ya X-ray. Jack Walborn alizaliwa na tatizo la moyo linalojulikana kama Pulmonary Valve Stenosis, hali ambayo huzuia damu kuingia katika mapafu. Kwa kutumia MRI, kunamaanisha kwamb wagonjwa hawatakuwa tena na haja ya kupigwa miale ya X- ray, hasa watoto wadogo. MRI pia inaonyesha taswira nzuri zaidi na kutoa taarifa kuhusiana na tishu za mwili wakati huo huo wa upasuaji. Mtoto Jack alikuwa na tatizo ambalo, damu iliyotoka upande wa kulia wa moyo wake haikuweza kuzunguka. Madaktari wa upasuaji waliamua kuwa, mtoto huyo anahitajia operesheni inayoitwa "valvuloplastry" ili kupanua chemba ya moyo na kuongeza mzunguzuko wa damu. Suala hilo hufanyika kwa kuingizwa mrija au katheta (catheter) katika mshipa wa damu kwenye mkono na kuuisukuma tararibu mrija huo au kuuongoza hadi kwenye moyo. Katika ncha ya mrija huo hufungwa puto ambalo hujazwa hewa ili kupanua chemba ya sehemu hiyo ya moyo iliyo nyembamba. Kwa kawaida X-ray hutumiwa kuangalia na kuongoza harakati ya katheta katika mwili. Lakini timu ya wataalmu wa Afya wa London imegundua njia ya kutumia MRI badala ya X-ray, na upasuaji wa kijana huyo mdogo unaonekana kuwa ni mafanikio makubwa katika uwanja huo. Baada ya kumalizika opersheni hiyo, baadaye Jack alipotoka chumba cha upasuaji alikuwa akikimbia huko na huko na kujisikia vyema. Wataalamu wanasema kwamba, teknolojia hiyo ni mafanikio makubwa, na katika mustaqbali wanataraji wagonjwa wengi wengine watafaidika kwa kutumia MRI badala ya X-ray, na kuepuka kupigwa miale kwani MRI haiumii miale.

Sunday, January 10, 2010

Chai yaweza kuwazuia wanawake wasipate kensa ya kizazi


Kama wewe ni mwanamke na hupendi kunywa chai itabidi ifikirie tena suala hilo, kwani wanasayansi wamegundua katika uchunguzi wao wa hivi karibuni kwamba, miongoni mwa faida za chai ni kuzuia hatari ya kupatwa na kensa ya kizazi. Huko nyuma pia tafiti mbalimbali zilionyesha faida kemkem za chai. Uchunguzi huo mpya umeonyesha kuwa, chai ambayo ni kinywaji cha pili kunywewa na watu wengi zaidi duniani, inaweza kuzuia kensa ya kizazi (endometrial cancer). Wataalamu wanasema mada ya polyphenols inayopatikana kwa wingi kwenye chai, kwa muda mrefu imeonekana kwamba moja ya faida zake ni kusaidia kupunguza ukubwa wa tezi za saratani, na sasa imegundulika kuwa pia ina faida kwa kensa ya kizazi. Uchunguzi huo umechapishwa katika jarida la Uzazi na Magonjwa ya Wanawake la Marekani, na kueleza kwamba, chai ambayo ina anti oxidanti nyingi inaweza kupunguza uwezekano wa kupatwa na kensa ya kizazi, saratani ambayo ni ya nne kuwapata kwa wingi wanawake nchini Marekani. Hata hivyo wataalamu wamesema kuwa, utafiti zaidi unapaswa kufanywa ili kuthibitisha zaidi utafiti wao huo.

Thursday, January 7, 2010

Komamanga huweza kuzuia kensa ya matiti isitambae mwilini


Uchunguzi mpya umeonyesha kwamba, katika tunda la komamanga kuna kemikali zinazozuia kensa ya matiti isitambae. Uchunguzi huo uliochapishwa katika jarida la Utafiti wa Kuzuia Kensa umeoneysha kwamba, kemikali ziitwazo ellegitannins zinazopatikna kwa wingi kwenye komamanga, zinaweza kuzuia kimeng’enya (enzyme) aina ya aromatase, suala ambalo huzuia kukua kwa homoni ya estrogen inayopatikana katika kensa ya matiti. Shiuan Chen Kiongozi wa uchunguzi huo amesema kwamba, kemikali hizo kupunguza uzalishwaji wa estrogeni, na kusaidia kuzuia seli za kensa ya matiti zisizaliane, pamoaja na tezi la ugonjwa huo lisikue.
Aromatase, ni kimeng’enya ambacho hugeuza homini ya androgeni kuwa estrogeni, na kushambulia kimeng’enya hicho ndio lengo kuu la dawa za kupambana na kensa za matiti inazosababishwa na homoni ya estrogen.
Huko nyuma pia chunguzi zilionyesha kwamba tunda la komamanga lina faida kubwa kiafya hasa kwa kuwa na anti oxidanti nyingi na vitamini mbalimbali, ambazo hulifanya tunda hilo liweze kusaidia katika kupambana na magonjwa ya saratani, matatizo ya moyo na hata ugonjwa wa kusahau uzeeni au Alzheimer. Anti oxidanti huzuia radikali huru ambazo ni hatari sana kwa miili yetu. Uwezo huo humepekea mwili kukabilina na magonjwa mbalimbali hata ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe.
Kama huwezi kupata tunda la Komamanga sokoni, basi unaweza kutumia juisi ya komamanga na daima tutunze afya zetu!

Wednesday, January 6, 2010

Namna ya kujikinga na Ugonjwa wa Kifua Kikuu… sehemu ya mwisho



Kuna njia mbalimbali zakujikinga na ugonjwa wa Kifua kikuu au TB ambazo ni:
 Kujikinga na Kifua Kikuu kunaanzia kabla ya mtu kupatwa na ugonjwa huo kwa watu wa kaiwada, ambapo kinga ya kuulinda mwili na ugonjwa huo hutolewa kwa watoto wadogo baada ya kuzaliwa. Kinga hiyo ya Kifua kikuu huitwa BCG yenye maana ya ( Bacillus Calmette- Guerin (BCG).
 Kuwakinga watu wa familia za wale walio karibu na wanaouguwa ugonjwa wa Kifua Kikuu.
 Kuwakinga wale wenye vijidudu vya ugonjwa wa kifua kikuu mwilini mwao lakini bado dalili za ugonjwa huo hazijajitokeza.
 Kuwakinga wale waliokuwa katika hatari ya kupatwa ugonjwa wa Kifua Kikuu.
Dawa aina ya Isoniazid (INH) inaweza kutumika katika kuzuia Kifua Kikuu kwa wale waliokuwa na vijidudu vya Kifua Kikuu katika miili yao lakini bado dalili za ugonjwa huo hazijajitokeza. Huko nyuma dawa aina ya Rifampin ilikuwa ikitumika kuzuia TB lakini kwa wale ambao dawa ya Isoniazid haikuwafaa.
Ugonjwa wa Kifua Kikuu ni ugonjwa unaozuilika kwa kiasi kikubwa. Ili kuwazuia watu wasipate ugonjwa huo inapasa watu walioambukizwa ugonjwa huo wajulikane mapema, hasa wale wanaokabiliwa na hatari kubwa ya kuonyesha dalili ya ugonjwa huo katika siku za usoni. Dawa ya INH inatumiwa kwa kiasi kikubwa kuzuia watu wasipate ugonjwa wa TB ambao wanaishi karibu na wagonjwa wa Kifua Kikuu au wale wenye uhusiano na wagonjwa hao, au wale wenye vimelea vya Tubercle bacilli katika miili yao lakini bado hawajafikia katika hali ya kuwa na TB halisi. Dawa hiyo hupewa na kutumiwa kila siku kwa miezi 12 mfululizo.
Katika nchi zilizoendelea kama vile Marekani, watu wa makundi yafuatayo wanapaswa kupewa dawa za kujikinga, bila kujali umri wao, iwapo huko nyuma hawajawahi kutibiwa ugonjwa wa Kifua Kikuu.
1. Watu ambao wanaishi na kushirikiana na wale walioambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu. (zaidi ya hayo watoto, na vijana ambao kipimo cha PPD kimeonyesha kuwa hawana ugonjwa huo, lakini kwa miezi mitatu wamekuwa wakiishi au kuwa na wa karibu na wenye ugonjwa huo. Matibabu yanapaswa kuendelea hadi pale kipimo cha ngozi kitakapochukuliwa tena na majibu kuonyesha hawajaambukizwa ugonjwa huo.
2. Watu ambao kipimo cha ngozi cha Kifua kikuu kimeonyesha wana ugonjwa huo, pamoja na wale ambao picha yao ya X-ray inaonyesha wana ugonjwa wa TB ingawa bado hawajaonyesha dalili za ugonjwa huo. (Inactive TB).
3. Watu ambao kipimo cha ngozi cha kifua kikuu kimeonyesha wana ugonjwa huo lakini pia wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa magonjwa kama vile ya HIV, Kisukari au wale wanaotumia dawa aina ya Corticosteroid.
4. Waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi na wale wanaodaniwa kuwa wameambukizwa virusi vya HIV na ambao wakati wowote huko nyuma kipimo cha ngozi kiliwahi kuonyesha wameambukizwa ugonjwa huo, hata kama hawana dalili.
5. Wale wanaotumia madawa ya kulenya kwa njia ya kujitunga sindano, ambao vipimo vya ngozi vimeonyesha wameambukzwa ugonjwa huo, hata kama bado hawana dalili za ugonjwa huo.
Watu wafuatao pia wenye umri wa zaidi ya miaka 35, wanapaswa kupewa dawa za kuzuia kifua kikuu:
 Wale wanaoishi katika maeneo yenye maambukizo mengi ya TB.
 Watu ambao wanaishi katika mazingira magumu, wale ambao wana kipato cha chini na wanaishi katika maeneo yenye misongamano.
 Watu ambao wameishi kwa muda mrefu jela, majumba ya kulelea wazee na sehemu za watu wenye matatizo ya kiakili.
Inapaswa kujua kuwa:
o Wafanyakazi wa vitengo vya afya wambao mara kwa mara wanakutana na kuwashughulikiwa wagonjwa wa kifua kikuu wanapaswa kufanyiwa vipimo vya ngozi vya TB kila baada ya miezi 6.
o Wagonjwa wenye kifua kikuu wanapaswa kufundishwa kuziba midomo yao na pua pale wanapokohoa au kupiga chafya.
o Wagonjwa wenye Kifua Kikuu wanapaswa kutengwa na kuwekwa kwenye vyumba ambavyo hewa inabadilika kwa urahisi.
o Wazazi wahakikishe kuwa watoto wao wanapatiwa kinga ya kifua kikuu katika wakati unaotakiwa.
'Daima tuzitunze afya zetu'

Monday, January 4, 2010

Watu wengi hawafahamu hatari ya kuwa wanene hasa kwa kuwa na matumbo makubwa



!
Karibu watu 9 kati ya 10 hawaelewi hatari inayowakabili kwa kuwa wanene hasa sehemu za tumboni na katika nyonga. Uchunguzi uliofanywa kwa kuwashirikishwa watu 12,000 wa nchi za Ulaya, umeonyesha kwamba, wengi wao hawajui kwamba kuwa na wanene sehemu za tumbo na nyonga ni dalili ya kuwa na ongezeko la mafuta kwenye viungo mbalimbali tumboni. Mafuta hayo yanayojulikana kitaalamu kama 'visceral fat' yanauhusiana moja kwa moja na ugonjwa wa kisukari aina ya pili na magonjwa ya moyo. Wataalamu wanasema kuwa, watu hawajui kwamba mafuta yanayokusanyika ndani ya mwili na kuzunguka viungo mbalimbali mwilini, ambayo hatuyaoni kwa macho au kuyahisi, ni yenye hatari kubwa. Hatari ya mafuta hayo inaweza kuwa ni kutoa protini na homoni ambazo zinaweza kuharibu mishipa ya damu, kuingia katika ini na kuathiri jinsi mwili unavyovunja vunja sukari na mafuta. Watu wengi waliokuwa wanene wanajihisi tu kuwa tatizo lao ni jinsi wanavyoonekana au namna wanavyopendeza na wala sio tatizo la kiafya. Uchunguzi umeonyesha kuwa, mzunguko wa kiuno au nyonga, ni ishara nzuri ya kukutambulisha kiwango cha mafuta ya visceral uliyonayo, na jinsi mzunguko huo unavyokuwa mkubwa ndivyo mafuta hayo yanavyoongezeka. Suala hilo huonyesha kwa kiasi gani mtu anaweza kupatwa na ugonjwa wa kisukari kinachotokana na unene. Wakati mtu anapopunguza uzito mafuta hayo yanayozunguka kiuno na tumbo ni huyeyeyuka kwa rahisi, kuliko mafuta ambayo yako chini ya ngozi, na hata kupunguza uzito kwa kiasi kidogo kunapunguza mafuta hayo. Ni muhimu kujua kwamba, mafuta yanayozunguka tumbo yana hatari kubwa kw afya, na watu wanatakiwa wajitahidi kuwa na uzito unaotakiwa ili kutunza afya zao.

Marekani yaondoa rasmi sheria ya kuwazuia waathirika wa Ukimwi kuingia Marekani


Marekani imeondoa marufuku iliyodumu kwa muda wa miaka 22 ya kuwazuia wahamiaji walioathirika na virusi vya HIV/Aids kuingia nchini humo. Rais Barack Obama wa Marekani amesema kwamba sheria hiyo iliyoondolewa, haikuwa inaendana na mikakati ya Marekani ya kuongoza jitihadaza za kupambana na ugonjwa wa Ukimwi. Sheria hiyo mpya ambayo imeanza kutumiwa leo Jumatatu nchini Marekani, huku Washinton ikipanga kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa Ukimwi kwa mara ya kwanza ifikapo mwaka 2012. Itakumbukwa kwamba marufuku ya kuwazuia waathirika wa Ukimwi wasiingie Marekani iliwekwa mwishoni mwa mwaka 1980, baada ya ugonjwa huo kuanza kutambulika duniani. Marekani ilikuwa ni miongoni mwa nchi 12 ikiwepo Libya na Saudi Arabia ambazo zinazowazuia wageni walioambukizwa virusi vya Ukimwi kuingia katika nchi hizo.

Sunday, January 3, 2010

Gundua siri ya kulala fofofo


UKOSEFU wa usingizi ni tatizo linalowasumbua wengi maishani, na inakisiwa kuwa zaidi ya humusi ya watu wazima wamewahi kutatizwa na usingizi wakati mmoja maishani mwao.
Ukosefu wa usingizi hutatiza sana , hasa ikiwa utatokea usiku, na mwathiriwa kuhisi usingizi na uchovu mchana, wakati ambapo anafaa kuwa akifanya kazi.
Kuna baadhi ambao, licha ya kulala masaa mengi, miili yao huhisi kwamba haijapata usingizi wa kutosha. Hii mara nyingi hutokana na kutoweza kupata usingizi haraka, kuamka mapema sana au kuwa na usingizi unaotatizika, au usio na raha.
Hii mara nyingi hutokana na mfadhaiko, hamu au wasiwasi kuhusu jambo fulani, hisia pamoja na mazingira kwa mfano kelele, hali ya kitanda au hata watu walio karibu wakati wa kulala.
Kufanya kazi kwa zamu, kwa mfano wakati mwingine usiku na mwingine mchana huwa pia sababu ya matatizo ya usingizi kwa kuwa mwili hushindwa kuzoea. Kufanya kazi zaidi, kunywa pombe kupindukia au hata kunywa vinywaji vyenye viwango vya juu vya kemikali aina ya kafeine ambayo hupatikana kwenye kahawa kadhalika huweza kusababisha matatizo haya.
Matatizo ya mwili kwa mfano majeraha, tatizo la maumbile kama vile kusikia kelele ndani ya sikio tatizo ambalo hujulikana kitaalamu kama tinnitus aidha huweza kutatiza usingizi wa mwanadamu.
Ukiweza kutambua kwa ufasaha kiini cha matatizo yako ya usingizi, unaweza kutafuta suluhisho. Kwa mfano, ikiwa kitanda kiko katika hali mbaya, unaweza kutafuta kingine, au hata kununua godoro na blanketi mpya.
Kuwa na mtindo wa kulala kadhalika husaidia sana . Unafaa kuwa na masaa fulani ya kulala na kuamka ili mwili uzoee.
Ubongo utakuwa tayari kila wakati huo ukifika kupumzisha mwili, na baadaye kuuamsha katika muda ufaao.
Unaweza kualika usingizi kwa kutojishughulisha na mambo mengi wakati wa kulala unapokaribia, kuoga kwa maji moto kiasi au kusikiliza nyimbo tamu. Si ajabu kwamba mama anapotaka mtoto alale, humwimbia nyimbo tamu, na hii hufanikiwa na hata mtoto aliyekuwa akilia akiwa amejawa na hasira hatimaye hulala.
Jiepushe pia na unywaji wa pombe kupindukia, au kunywa vinywaji vyenye viwango vya juu vya kafeine. Ikiwa tatizo lako ni mfadhaiko, tafuta mtaalamu wa matatizo ya fikira au mshauri atakayekusaidia kutua mzigo wa fikira.

Saturday, January 2, 2010

Wanasayansi watengeneza mashine ambayo ni sawa na tumbo la mwanadamu


Wanasayansi wametengeneza mashine ambayo inafanya kazi kama tumbo la mwanadamu. Mashine hiyo imetengenezwa na watafiti wa Kitengo cha Uchunguzi wa Chakula cha Norwich. Mashine hiyo ina uwezo wa kufanya kila aina ya kazi zinazofanyika tumboni, na ina hali mbalimali za kibiokemikali zinazopatikana katika tumbo. Wanasayansi wametengeneza mashine hiyo ili iwasaidie katika uchunguzi wao kuhusiana na chakula katika tumbo la mwanadamu. Mashine hiyo imechukua miaka 10 kutengenezwa na itatumika katika majaribio ya dawa katika mfumo wa chakula. Waliotengeneza mashine hiyo wana matumaini kuwa, mashine hiyo itakuwa msaada mkubwa katika majaribio ya dawa ambayo ni vigumu kujaribishwa kwa mwanadamu kwenye viwanda vya kutengenezea madawa. Martin Stock msemaji wa Kiwanda cha Boioscience Ltd kilichotengeneza mashine tumbo hiyo amesema kuwa, kila mtu anafikiria kuwa tumbo ni kama mfuko ulijaa tu maji na vimeng'enya (enzymes), lakini si hivyo bali tumbo ni sehemu yenye viungo vingi tofauti tofauti, na mashine hiyo inashabihiana kikamilifu na tumbo la mwandamu.

Ujue ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB)….sehemu ya pili


Wadau wapenzi mnaofuatilia makala mbalimbali katika blogi ya Kona ya Afya, natumaini mlifaidika na sheemu ya kwanza iliyozungumzia ugonjwa wa Kifua Kikuu. Hii ni sehemu ya pili ambapo leo tunaangalia vipimo vinavyotumika kujua iwapo mtu ameambukiza kifua kifuu. Vipimo vinavyotumia sasa katika nchi nyingi hususan katika ulimwengu wa tatu ni ni kipimo cha picha ya kifua au x-ray, kipimo cha makohozi, kipimo cha ngozi au Mantoux test. Iwapo vipimo hivyo vitathibitisha kuwa mtu amemabukizwa kifua kikuu, mtu huyo atapaswa kutibiwa kikamilifu kwa kufuata ushauri wa daktari ili kuutokomeza ugonjwa huo. Wadau wapenzi baada ya kufahamu nini maana ya Tb, chanzo chake na dalili zake, sasa ni vyema tuelewe matibabu yake. Je, Kifua Kikuu kinaweza kutibika? Jibu ni ndiyo. Kuna dawa aina ya antibiotic ambazo ni tiba barabara ya kuitokomeza Tb lakini chini ya ushauri wa daktari. Itakumbukwa kuwa Shirika la Afya Duniani WHO limetoa mwongozo mpya wa kutibu ugonjwa wa kifua kikuu kwa kutumia dawa za mseto (fixed dose combination drugs au FDCs) ambazo hutumika sasa katika nchi nyingi za ulimwengu ili kupunguza muda wa matibabu kutoka miezi minane hadi sita. Jambo muhimu la kuzingatia katika utumiaji wa dawa hizo ni kuwa, ni vyema mgonja atumie dawa hizo kama alivyoshauriwa na mtaalamu wa afya na kumaliza dose yake aliyoandikiwa. Kwa hiyo kuna haja ya mgonjwa kuwa chini ya uangalizi maalumu ili kuruhusu ufanyaji kazi wa antibiotic na kuleta athari nzuri kwa mgonjwa. Pili kuna chanjo ya BCG. Hii ni chanjo ambayo hutolewa kwa mtoto mara baada ya kuzaliwa. Chanjo hii humlinda mtoto na kifua kikuu. Hata hivyo katika nchi nyingine chanjo hii hutolewa baadaye kwa watoto ambao wako katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu.
Hebu sasa na tunagalie ni chakula gani anachopaswa kula mgonjwa wa TB. Mgonjwa aliye na kifua kifuu anatakiwa kula mlokamili wenye mada za proteini, vitamini na cabohyadarate. Vyakula vya protini ni pamoja na mayai,maziwa,maharage na soya. Vyakula hivyo hujenga misuli na kuzalisha chembe za uhai. Vilevile husaidia mfumo wa kinga ya mwili kupata nguvu. Vile vile ni vyema mgonjwa wa TB apate vitamini zitokanazo na mafuta na mboga za majani. Vyakula hivyo huongeza nguvu na kukinga mwili wake khususan ngozi. Chakula aina ya carbohydrate ambayo inapatikana katika chakula cha nafaka mfano wa mahindi na ngano na vilevile sukari itokanayo na matunda navyo vina umuhimu mkubwa.
Hii ni kwa sababu vyakula hivyo huleta nguvu katika mwili wa mwanadamu. Vile vile bila kusahau maji safi na salama yanayohitajika mwilini. Makala hii itaendelea na msikose kuungana nami tena ili kujua namna ya kujikinga na kifua kikuu. Tutunze Afya zetu daima!